Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa sababu nilikuwa na mgogoro wa Kazimzumbwi kwa kweli yeye na Mheshimiwa Waziri Mkuu waliingilia kati. Nawashukuru sana Waheshimiwa hawa, kwani walifunga safari kutoka hapa mpaka Ukonga na wakahakikisha kwamba jambo hilo linajadiliwa kwa manufaa ya watu wa Ukonga. Kwa hiyo, nawashukuru sana, nawatakia kazi njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Waheshimiwa Mawaziri wapo humu. Hizi pongezi ambazo Mheshimiwa Lukuvi anapewa na wengine, nadhani Mawaziri wangefanya kazi kama hiyo tungekuwa hatuna mgogoro mkubwa. Kwa hiyo, ni muhimu wakajifunza mambo mazuri kama haya. Anapokea simu na Naibu wake, wanakusikiliza, wanakupa majibu, wanatembelea Majimbo; na kama jambo haliwezekani, anakwambia hili kwa mujibu wa sheria haliwezekani. Mheshimiwa Lukuvi nafikiri kwa sababu ya uzoefu wake, anaweza akatoa tuition kwa wenzake ili tukaenda vizuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, Mheshimiwa Lukuvi naomba anisaidie kumaliza migogoro maeneo yafuatayo Ukonga. Moja, kuna mgogoro wa UVIKIUTA, nyumba zimevunjwa zaidi ya mara tatu, anaufahamu vizuri. Tunahitaji watu wale wapate amani, wapate maelekezo ya kisheria waishi kwa amani katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mgogoro upo pale Pugu Kajiungeni. Ni eneo la wazi, hakuna eneo lingine, vijana walikuwa wanacheza mpira, akinamama wanafanya kazi zao; nyumba zilivunjwa usiku wa saa 9.00. Ofisi ya Mkoa tumeenda mara nyingi sana, lakini hatuna majibu mpaka leo. Kwa hiyo, tunaomba atusaidie tupate majibu katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Kipunguni haina Shule ya Sekondari, haina huduma za kijamii, ni kata mpya. Eneo pekee ambalo lilikuwa limebaki, limevamiwa na watu, hawana documents zozote zile, lakini majibu hayapatikani mpaka sasa. Kwa hiyo, tunaomba atusaidie pia, kupata majibu katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro mwingine mkubwa wa ardhi ni wananchi ambao walihamishwa kutoka eneo la Uwanja wa Ndege wakapelekwa maeneo ya Buyuni, Zavala na maeneo mengine kule. Wale watu wameondolewa kutoka hapa Uwanja wa Ndege Kipawa, kule hawakupewa ardhi, lakini bahati mbaya pia wakapewa maeneo ya watu. Kwa hiyo, kuna ugomvi kati ya watu ambao wametoka Kipawa na wale ambao ni wenyeji waliokutwa katika eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lukuvi kwa sababu yupo tayari, akutane na watu hao awasikilize, kwani ni kilio cha muda mrefu na kweli wana shida kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni bomoa bomoa. Eneo la Kata ya Pugu Station, Kata ya Ukonga na Kata ya Gongo la Mboto, maeneo yaliyobomolewa kupisha ujenzi wa reli kwa kiwango cha standard gauge; hatupingi, lakini wale watu wengine walikuwa na hati, wamechanganywa kule kule na hakuna fidia yoyote ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mambo kama haya wakiyafanya ni muhimu watu wafahamu sheria zinasema nini? Haki zao ni zipi? Wakati mwingine kutoa taarifa in advance ili kama kuna mtu ana-vacate, aweze ku-vacate ili asipoteze mali zake zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, neno la mwisho ni upimaji wa maeneo ya umma. Migogoro mingi iliyopo katika maeneo yetu hayapimwi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Lukuvi, achukue hatua mahususi kupima maeneo haya ili kuondoa migogoro kati ya wananchi na maeneo ya umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.