Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji katika hotuba hii iliyopo mbele yetu. Leo nilikuwa sitaki kuchangia habari za haya mambo ya Road License lakini imenibidi nichangie kidogo tu ili tuelewane vizuri tu siyo labda kwa kushindana au nini ila kueleweshana tu.

Mheshimiwa Spika, nafikiri kama Waziri wa Fedha angefuata yale mawazo yetu ambayo tulikuwa tunampa siku tano za nyuma basi ina maana kwamba angepandisha Sh.140/= kwenye bei ya mafuta, asingepandisha Sh.40/=. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hii ni kwa sababu Wabunge wengi tuliokuwa tunachangia humu, mimi sikupata nafasi lakini wengi walikuwa wanasema kwamba, Sh.50/= weka kwenye maji, Sh.50/= weka REA na Road License weka kwenye mafuta. Sasa leo kwa busara zake tu akaamua kuweka Sh.40/= tu peke yake ile Sh.100 akaiacha lakini bado na hii nayo tunamgeuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ndugu yangu hapa Mheshimiwa Kamala yeye ni Mwalimu, ameeleza vizuri sana na mimi sasa ni Mwalimu wa huko mtaani nitawaeleza kidogo. Kwa hesabu tu nyepesi, niwape hesabu nyepesi tu, Road License gari lenye CC2500 ilikuwa inalipiwa Sh.200,000/= kwa mwaka. Sasa tuchukue mfano tu mwenye gari hiyo, maana yake tuangalie kwanza hawa watu wa kawaida, kila siku akijaza lita 10 ya mafuta kwa mwezi atajaza lita 300. Akijaza lita 300 ukiweka mara ile Sh.40/= kwa mwezi analipa Sh.12,000/=, ukiweka ile Sh.12,000/= kwa mwaka analipa Sh.144,000/=. Kwa hiyo, hata hiyo Sh.200,000/= bado hajafika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapeni mfano mmoja, tunaposema kwamba usafiri utapanda sijui kilimo kitapanda, Mungu ananisaidia mimi ni mkulima na msafirishaji, lazima ku-declare interest, bei ya EWURA ya mwezi huu tuliomaliza nao ilishusha dizeli kwa Sh.81/= na petroli kwa Sh.30/=, kwa mwezi huu wa Tano tuliomaliza. Mwezi huu bei iliyotangazwa juzi, dizeli imepanda Sh.43/= na petroli imepanda Sh.25/=. Kwa hiyo, hata ukiweka na hii Sh.40/= hatujafika bei ya mwezi wa Nne na bado hizo nauli zipo pale pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mtu jana alizungumza, nataka nizungumze kweli, bei ya mabasi iliyotolewa na SUMATRA imetolewa miaka mitano iliyopita lakini mpaka leo hakuna basi limefikisha ile bei waliyopangiwa na SUMATRA, hakuna. Dar es Salaam – Arusha ni Sh.33,000/= lakini watu wanaenda kwa Sh.25,000/=; Dodoma – Dar es Salaam ni Sh.24,000/= watu wanaenda kwa Sh.17,000/= mpaka Sh.20,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niseme hii kodi, hata Wabunge wengine wapo upande wa CCM na wengine wapo upande mwingine, walikuwa wanasema iingie kwenye maji, tumetoa Road License na gharama za Road License zilikuwemo kwa wasafirishaji hata msingepandisha mafuta walikuwa wanalipa Road License, kwa hiyo gharama ilikuwa ipo pale pale tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, gharama hii ya Road License ibaki kama Road License kwenye mipango yake ya Serikali. Kama kuna mpango mwingine wa kupandisha maji basi tuweke tena Sh.50/= nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusiingize hii huko kwamba tuitoe kwenye mipango yake ya Serikali, sijui ifanye hiki na kile kwa sababu hata usipopandisha mafuta, ukiacha Road License si ni pesa msafirishaji ataingiza tu ile.

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumze tu ili watu walielewe hili suala vizuri, hii ni nchi yetu. Kule China watu walikuwa wanavaa chunlai siyo kwamba walikuwa wanapenda, leo wanavaa bluu watu wote kesho kijani, walikuwa wanafunga mikanda ili wafike mahali wanapohitaji. Kwa hiyo, twendeni tufunge mikanda tufike mahali tunapotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine huyu Ndugu yangu Mheshimiwa Mpango leo nampa shikamoo. Mara ya kwanza humu tulikuwa tunakujadilijadili, tukaona huyu jamaa mpole sana kwa sauti lakini mbona kama haelewielewi, hataki ushauri.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa hivi kwenye Bunge hili tumegundua kwamba katika watu wanaopenda ushauri Mheshimiwa Mpango naye mmojawapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niseme kwa nini nimempa shikamoo. Ukiangalia taarifa ukurasa wa 54…

TAARIFA....

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Taarifa yake naipokea kwa sababu ni rafiki yangu huyu najua ananichangamsha tu, hakuna hata matatizo lakini najua nilishamwambia kwamba ni mkulima na mfugaji, ni rafiki yangu Waitara hakuna matatizo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa nini nilikuwa nasema Mheshimiwa Mpango shikamoo, amerudi pale pale kwenye vile viwanda vya Mwalimu Nyerere. Hii ni kwa sababu ukiangalia ukurasa wa 54, kipengele cha tatu, amezungumzia kupunguza ushuru wa vile viwanda vitakavyoletwa kwa ajili ya kuunganisha matrekta, boti na magari. Ametoa ushuru huu wa Corporate Income Tax kutoka asilimia 30 mpaka 10. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nataka nitoe ushauri, mpaka leo hakuna mtu aliyefikia rekodi ya mzee wetu Mwalimu Nyerere. Wakati ameanzisha kile Kiwanda cha TAMCO pale Kibaha cha kuunganisha magari ya Scania, pamoja na kuwaambia wawekezaji waje lakini aliwapa masharti ya kununua bidhaa zinazotengenezwa Tanzania ili kuunganisha yale magari.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, rejeta zote zilizokuwa zinatumika kwenye magari yote yaliyokuwa yanaunganishwa Tanzania zilikuwa zinatoka kwenye Kiwanda cha Serikali kinaitwa Afro Cooling, betri zote zilikuwa zinatoka kwenye Kiwanda cha Serikali kinaitwa YUWASA, wiring zote zilizokuwa zinafanyika kwenye magari zilikuwa zinatoka East African Cable, matairi yote yalikuwa yanatoka General Tyre, spring zote zilikuwa zinatoka Tasia Spring na muffler zote zilikuwa zinatoka Tanzania kwenye kiwanda cha Serikali. Sasa hapo ndiyo unaongeza ajira kwa sababu bila kufufua viwanda kama General Tyre, Afro Cooling na viwanda vyote nilivyovitaja na vingine viko vingi tu bado kuna tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ulikuwa ukiangalia ile gari ilikuwa inatengenezwa na Watanzania kwa asilimia zaidi ya 18. Kwa hiyo, ile gari ili ifanyiwe assemble hapa hivi viwanda vingine vyote vilikuwa vinafanya kazi na vinatoa ajira nyingi sana kwa Watanzania. Kwa hiyo, naomba kwenye huu ukurasa wa 54 hapa basi aweke hayo masharti ya kwamba mwekezaji yeyote atakayekuja kuunganisha magari hapa Tanzania basi lazima atumie bidhaa za Tanzania. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha ajitahidi juu chini ahakikishe hivi viwanda vinafufuka kama General Tyre, Afro Cooling… (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo namwomba Mheshiiwa Waziri afufue hivi viwanda ili hii dhana yake iende vizuri.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nashukuru sana.