Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa pongezi kwako na Waheshimiwa wote kwa kuchaguliwa kuingia kwenye Bunge la Kumi na Moja. Kipekee nampongeza Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejaliwa kuwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa nami nampongeza sana. Nimeisoma hotuba yake nzuri na nimekubaliana naye, lakini naomba ufafanuzi kwa mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezeshaji wananchi kiuchumi. Kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, ukurasa wa 14 na 15, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi imeelezwa vizuri sana, naomba kunukuu:-
“Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kuwadhamini wajasiriamali wenye miradi inayokidhi vigezo kwenye taasisi za fedha ili wapate mikopo yenye masharti nafuu”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naomba ufafanuzi wa kina kwani Tanzania ni kubwa na wajasiriamali ni wengi sana na hivyo si rahisi kama maandiko yalivyokaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rahisi kusema kuliko kutenda, hivi Waziri Mkuu anavyosema Serikali itaendelea kuwadhamini wajasiriamali anaweza kuwaeleza Watanzania ni lini dhamana hiyo ilitolewa na ni akina nani walifaidika? Endapo anazungumzia mabilioni ya JK, naomba kutofautiana naye kabisa kwani fedha zile zimetoweka na mzunguko sasa umekwama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na nia nzuri ya Serikali, naomba wananchi wapatiwe miradi zaidi ya fedha. Katika Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwawezesha wajasiriamali na wakulima wa Kilimanjaro mradi wa kopa ng’ombe ambao uliweza kuwapatia lishe bora, nyumba za kisasa, ada za watoto shuleni na hatimaye maisha bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aya ya 23 inasema, nanukuu:-
“Serikali imehamasisha uanzishaji na usajili wa vikundi vya kiuchumi kama vile Vyama vya Ushirika vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) na Benki za Jamii Vijijini (VICOBA).
Serikali pia imesimamia uanzishwaji wa Taasisi mwamvuli ya kusimamia VICOBA inayoitwa VICOBA FETA. Takwimu zilizotolewa Februari, 2016 na Taasisi hiyo zinaonesha kuwa, kuna vikundi 100,000 vya VICOBA vyenye wanachama milioni 2.2 na mtaji wa shilingi trilioni 1.2. Ni jambo la kujivunia kwamba asilimia 79 ya wanachama wa VICOBA ni wanawake”. Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na taarifa njema alizotupa Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu ushirika wa SACCOS na VICOBA, naomba atufafanulie ni jinsi gani wanawake hao watapatiwa mafunzo ya ushirika. Mpaka ninavyozungumza, jukumu kubwa limekuwa kwa Wabunge. Naomba nichukue nafasi hii nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu atufafanulie jinsi ya kuwapatia mafunzo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ule ukurasa wa 16, aya ya 24, hotuba imeonesha wazi hali ya Vyama vya Ushirika, SACCOS zinazokidhi vigezo vya usajili nchini imepungua kutoka 5,559 mwaka 2013 hadi 3,856 mwaka 2015. Huu ni upungufu wa asilimia 30.6 sawasawa na 31%. Huu ni upungufu mkubwa na tatizo ni kwamba, Serikali haitoi kipaumbele kwa ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naomba kufafanua, Novemba 2006, Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Magufuli alitangaza Baraza la Mawaziri na ndipo umma wa Tanzania ulipozisikia Wizara zilizopo. Wengi mpaka sasa wanajiuliza hivi Wizara ya Ushirika iko wapi? Endapo ni idara, je, iko kwenye Wizara gani? Pendekezo ni kwamba, ipelekwe kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara. Kwenye Awamu ya Nne, Wizara hiyo ilikuwa kwenye Kilimo na ilijulikana kama Wizara ya Kilimo na Ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.