Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri walio katika Wizara yake kwa kutuletea bajeti ili tuweze kuijadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hii imegusa kila eneo lakini yapo baadhi ya mambo ambayo nataka nipatiwe ufafanuzi:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu watu wenye ulemavu; niipongeze Serikali katika ukurasa wa 21 inasema inathamini mchango mkubwa wa watu wenye ulemavu katika maendeleo na kwamba wana haki sawa ya kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Hata hivyo, bado watu wengi wenye ulemavu wanapata mateso sababu Serikali haijaweza kutunga sheria kuhakikisha watu wanaomiliki vyombo vya usafiri wanahakikisha miundombinu inakuwa rafiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walemavu wengi wamekuwa wakipata mateso makubwa sana hasa wale wenye baiskeli kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine wanapokuwa wanasafiri umbali mrefu. Bado majengo mengi sana hayajaweza kuwa na miundombinu rafiki ya kumfanya mtu mwenye ulemavu aweze kuyatumia kama vile shule, hospitali, vituo vya afya hata ofisi zetu za Serikali, mtu mwenye ulemavu anapotaka huduma katika majengo hayo imekuwa ni mateso kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua ni lini Serikali itaweka sheria kuhakikisha zinalinda haki ya mtu mwenye ulemavu. Pia bado wetu wenye ulemavu wengi na hasa wale wasio na uwezo wa kupata baiskeli wapo nyumbani hawapati hata haki ya kusoma. Nashauri Serikali ihakikishe kila mwenye ulemavu anapatiwa baiskeli bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilianzisha program ya kuwasaidia watu wenye ulemavu katika mkoa wangu, niliamua kuwathamini, kuwajali na kuwasaidia pale walipo, naelewa changamoto nyingi sana ambazo Serikali yetu inatakiwa kuzitatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu ya bure; niendelee kuipongeza Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kutoa elimu bila malipo nchini, imesisitiza kila mzazi kupeleka mtoto shule na asiyepeleka mtoto hatua kali itachukuliwa dhidi ya mzazi/mlezi huyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali imeweka mkakati gani kuhakikisha hawa watoto wa mitaani au watoto wanaojulikana kama ombaomba nao wanapata hiyo haki ya kusoma? Ni nani anayewajibika ili watoto hawa wasome? Swali hili huwa najiuliza kila siku lakini huwa nakosa jibu, ningependa kujua mkakati wa Serikali kuhusiana na hilo.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa ushauri au pendekezo langu kwa Serikali, kwa kuwa kuna shule za watu binafsi na shule nyingi zimekuwa zikitoza fedha nyingi lakini nazo zimekuwa zikitozwa kodi na Serikali, kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa kuwapeleka hawa watoto katika shule hizo ili zile shule zinazokubali kuwachukua na kuwasomesha hawa watoto wa mtaani shule hizo zipunguziwe kodi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madeni ya wazabuni, wazabuni wa nchi hii bado wana mateso makubwa sana pamoja na kuwa walijitahidi kutoa huduma kwa Serikali yetu, kuna baadhi ya wazabuni ambao toka awamu zilizopita wamekuwa wakifuatilia malipo yao bila mafanikio. Serikali itambue kwamba wazabuni hawa wengi wao ni wale waliochukua mikopo benki na kuna wazabuni ambao wamesababishiwa kutaka kuuziwa dhamana zao walizoweka rehani ili wapatiwe mikopo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itambue kuwa wazabuni hawa pia wanadaiwa na kodi ya mapato, kwa sababu sheria inasema ukishatoa invoice kwa mzabuni wako unatakiwa ulipe kodi, sasa wanalipa kutoka wapi wakati bado hawajalipwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kuhakiki madeni ya wazabuni bado hatma ya malipo haijajulikana. Ningependa kujua Serikali hii ya Awamu ya Tano imejipanga vipi kuhakikisha wazabuni wanalipwa kwa wakati ili kumwondolea adha ambayo mzabuni amekuwa akiipata na imesababisha wazabuni wengi kufilisika na kufunga biashara zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali wa kutoa milioni hamsini kila kijiji; naendelea kutoa pongezi zangu kwa Serikali na Rais wa Awamu hii ya Tano kwa kuwa na mpango wa kupeleka milioni 50 kila kijiji. Sasa napenda kujua, Serikali imejipangaje kutoa elimu ya kuwatayarisha walengwa ili kuhakikisha pesa hizi zitakapoanza kutolewa zinawafikia walengwa na zinawasaidia, pia kuweza kurudishwa ili ziweze kuwa na mzunguko, kwa kuwa ukimpatia mlengwa akazirudisha zitasaidia walengwa wengi kufikiwa. Tuna rundo kubwa sana la akinamama ambao wameweza kuwa na uthubutu wa kufanya biashara, lakini hawana mitaji, sasa hili jambo litakuwa ndiyo suluhisho ya mambo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira zisizo rasmi; napenda kujua ni lini Serikali itarasimisha ajira zisizo rasmi? Kwa mfano, Mkoa wetu wa Iringa ni Mkoa ambao vijana wengi wamekuwa wakipata ajira ya kufanya kazi za ndani (house girl au house boy), pia tumekuwa na mkataba wa Kimataifa na nchi yetu kuridhia, bado ajira hii haijarasimishwa imekuwa ikisababisha vijana wengi kufanyiwa vitendo vya kikatili, kunyanyaswa, kubakwa, kupata mimba zisizotarajiwa na kuambukizwa UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua ni lini ajira hii itarasimishwa ili vijana wetu waweze kutendewa haki na hata kujiunga katika Mifuko ya Jamii, kuwekewa bima ya afya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mauaji ya vikongwe; haya mauaji ya vikongwe hasa Mikoa ya Kanda ya Ziwa yamekuwa ni tishio na mauaji haya yamedumu kwa muda mrefu sana. Ningependa kujua Serikali imejipanga vipi kukomesha ukatili huu wanaofanyiwa vikongwe kwa kushirikishwa na imani za kishirikiana? Je, toka mauaji haya yameanza kufanyika ni vikongwe wangapi wameuawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kumaliza miradi ya zamani. Ningependa kujua mpango wa Serikali kuhakikisha inamaliza miradi iliyochukua muda mrefu kukamilika. Kwa mfano, katika Halmashauri yetu upo mradi wa machinjio, mradi huu umechukua muda mrefu sana kukamilika. Ni imani yangu kuwa mradi huu ukikamilika Manispaa yetu itakuwa na chanzo kizuri sana cha mapato na pia Halmashauri itaongeza ajira kwa vijana wetu, hivyo ningeshauri Serikali ifanye tathmini ya vile vyanzo ambavyo vinaweza kutuongezea mapato na miradi yake ipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji; niendelee kuipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza Program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma ya maji safi, salama na ya kutosha. Imani yangu ni kuwa, kama program hiyo itakamilika, nia ya Serikali kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani itatimia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Iringa hauna tatizo la maji, bali tatizo kubwa ni usambazaji wa maji. Kwa mfano, Wilaya ya Kilolo ina mito mingi, Serikali inashindwaje kutoa maji kutoka kwenye Mto Lukosi, Ruaha na Mtitu? Nina imani kabisa kama Serikali ingesambaza maji kupitia vyanzo vya mito hii, ingeweza kutumia gharama nafuu sana ya uhakika kuliko kuchimba visima visivyokuwa na tafiti za kutosha na kusababisha pesa nyingi kutumika katika tafiti badala ya kutumia vyanzo vya mito, kwa sababu maji yanapokosekana ni mwanamke ndiye anayeteseka. Tunaomba ile ahadi ya kumtua mama ndoo kichwani ikamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma muhimu katika Wilaya mpya; kuna Wilaya ambazo zimeanzishwa muda mrefu sana, lakini bado hazijapatiwa huduma muhimu. Kwa mfano, Wilaya ya Kilolo ilipata hadhi ya kuwa Wilaya toka mwaka 2002, mpaka leo hii Serikali haijaweza kujenga Hospitali ya Wilaya, Makao Makuu ya Polisi, Mahakama ya Wilaya, pia barabara inayounganisha Makao Makuu na Wilaya mpaka leo hakuna lami pamoja na Halmashauri kuweka jitihada ya kutenga maeneo kwa ajili ya huduma hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina wasiwasi hata hizi ahadi za Serikali za kujenga Wilaya mpya kama zitatekelezeka, ningependa kujua mpango wa Serikali wa kuhakikisha hizi Wilaya zilizoanzishwa muda mrefu utekelezaji wake upo vipi, ukamilishaji wa hizo huduma katika Makao Makuu ya Wilaya, kwa sababu wananchi wamekuwa wakipata shida sana kuzifuata hizo huduma na hasa kutokana na changamoto za miundombinu ya barabara zetu za vijiji zilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.