Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. CECILIA D. PARESO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza naunga mkono maoni yaliyotolewa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani hapa Bungeni na nafikiri Serikali ni vizuri mkayapitia, mkasoma na mkayachukua kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani iliingia kwa mbwembwe nyingi ikijiita ni Serikali ya ‘Hapa Kazi tu.’ Lakini Serikali hii ya ‘Hapa Kazi Tu’ pia kupitia hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa 11 inasema ili kuboresha demokrasia hapa nchini hatuna budi kujenga jamii inayoheshimu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Wameandika hivi kwenye vitabu lakini sisi Wabunge na wananchi ni mashahidi kwamba hii Serikali ya hapa kazi ndio Serikali ambayo inavunja katiba, inavunja sheria, haifuati taratibu na haifuati misingi ya utawala bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivi? Sababu zipo nyingi lakini kutaja tu kwa uchache hoja mojawapo tu, leo tunawadhibiti na kuwanyamazisha wananchi na vijana mbalimbali ambao wanatoa maoni yao kwa namna yoyote katika nchi hii. Tunajenga vijana wawe waoga kwenye nchi yao, tunawaziba midomo vijana na wananchi wasitoe maoni yao wakati katiba ya nchi imetoa uhuru huu kwa wananchi kutoa maoni yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunavinyima vyama vya siasa visifanye mikutano wakati katiba na sheria zinaruhusu; na uhai wa vyama vya siasa, chama chochote cha siasa ni kufanya mikutano ya hadhara, ni kukutana na wanachama wake. Uhai wa wa vyama vya siasa ni kuongeza wanachama kwa sababu hawa wanachama; ni kama ilivyo makanisa kwenye vyama vya siasa, leo mtu yupo chama hiki na kesho
yupo chama hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji kuendelea kuimarisha vyama vyetu kwa kuongeza wanachama, tunaongeza wanachama kwa kupitia mikutano ya hadhara; lakini Serikali leo inapiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, inavunja katiba ya nchi iliyojiwekea, inavunja sheria. Sasa ndio tunajiuliza hii ndio hapa kazi kweli ya kuvunja katiba na kuvunja sheria? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini leo watu wanatekwa, wananchi hawana amani; kwenye mitandao sasa hivi ukisoma wananchi wanasema hata nikienda mahali naaga naenda sehemu fulani kwa sababu sijui kama nitarudi salama au nitatekwa. Tumeshuhudia hapa kuna watu wametekwa wamepotea, hawajulikani walipo, hakuna kauli ya Serikali; hatujasikia kauli nzito inatolewa na Serikali, tunajiuliza kama Serikali imekaa kimya je, ndiyo inayohusika na hili jambo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kama na ninyi mngekuwa mnaliona jambo hili kweli linatishia amani ya wananchi mngetoa kauli, hamtoi kauli watu wanatekwa, watu hawajui wanapotelea wapi; hatujui kama kina Ben Sanane haijulikani kama ni wazima au wameshauwawa, haijulikani walipo. Hamuwezi mkajiita hapa kazi tu kwa kufanya hivi vitu; au inawezekana mnajiita hapa kazi kwa kufanya hivyo vitu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Serikali hii kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa ilitakiwa ilee hivi vyama vya siasa. Leo mnashabikia ugomvi wa ndani ya Chama cha wananchi (CUF); Serikali imechukua upande ina-support upande mmoja na kuacha upande mwingine. Wakati wanachama wa chama hicho wanawatambua viongozi ikiwemo Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF kama ndio Katibu Mkuu wao,
lakini Msajili wa Vyama vya Siasa badala ya kulea chama hiki na kuhakikisha mgogoro uliopo unatatulika wamechukua upande na wanashabikia upande ule ambao wanaharibu Chama cha Wananchi CUF. Sasa hii ndio hiyo inayoitwa ‘Hapa Kazi Tu’. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Devotha ameeleza hapa asubuhi, hakuna tena ile hadhi ya Ubunge; Mbunge unaonekana si kitu na hasa upande wa upinzani wakati wowote unaweza kuvamiwa nyumbani kwako. Yaani Mbunge ni mtu ambaye anaweza akapotea kwenye nchi hii? Mbunge kama anatakiwa polisi akipewa taarifa ya kwenda kituoni hivi atapotea? Kwa nini tunamchulia Mbunge kama ni mtu ambaye anaweza kupotea? Kwa nini polisi wanatumia madaraka yao vibaya kuwaita Wabunge na kuwataka wakati wowote na kutumia silaha nzito utafikiri Mbunge ni jambazi sugu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima Wabunge tutetee hadhi yetu na ni lazima Wabunge tusimame tutetee hadhi ya mhimili wa Bunge; tukisimama hata mhimili wa Serikali nao utaweza kuona kwamba Bunge lina hadhi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, madai ya katiba mpya nadhani yapo pale pale, tunahitaji katiba mpya. Rasimu ya katiba mpya ilitengenezwa kwa fedha nyingi za walipa kodi, mmeiweka kapuni, mmeificha na hatusikii tena Serikali ya Awamu ya Tano mkizungumzia suala la katiba mpya.
Watanzania wanahitaji katiba mpya; tunahitaji katiba mpya na tunaitaka katiba mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mifuko ya Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi. Kumekuwa na mifuko mingi sana, kuna hizo asilimia kumi ambazo zinatengwa kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri. Kumekuwa kuna mifuko mingine kupitia Wizara mbalimbali, ya Vijana, ya Fedha na vitu kama hivyo. Kwa nini isifike mahali sasa mifuko hii ikaunganishwa kuliko kuwa na mifuko mingi ambayo inatoa fedha kidogo ambayo mwisho wa siku hata ukipima ufanisi wa hizo fedha haupo kabisa? Kwa nini tusiwe na mfuko mmoja wa pamoja ambao utatoa mikopo kwa vijana, akinamama na makundi mbalimbali ili kuwawezesha kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu ni kuunganisha hii mifuko na kuufanya mfuko mmoja ili iweze kwenda kutoa mikopo kwa wananchi wetu na kuwaimarisha kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/2017 ambayo tunaimalizia mwezi Juni. Bajeti tuliyoipitisha ilikuwa ni ya shilingi trilioni 29.5 lakini mpaka kufikia Februari fedha za maendeleo zilizotolewa kwa Halmashauri na Wizara ni asilimia 35 tu. Sasa asilimia 35 tumebakiza miezi kama miwili kwenda kumaliza mwaka wa fedha; kutakuwa na muujiza gani wa kwenda kukamilisha hizi fedha za maendeleo?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sababu ambazo zinaelezwa na Serikali, kwamba kwa nini wameshindwa kufikisha hiyo wanasema kuna fedha za wafadhili nyingine zimechelewa na nyingine hazijatolewa. Wakati tunapitisha bajeti hapa mwaka jana tulieleza athari ya MCC na wafadhili wengine kujitoa, mkasimama mkatetea sana hoja hii mkasema nyie mnaweza kujitegemea, mapato yenu ni mazuri na leo hizi ndio athari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine tulikuwa tunaona hizi taarifa Serikali ya Awamu ya Tano mnasema mnakusanya karibu Shilingi trilioni 1.2 kila mwezi. Serikali ya Awamu ya Nne iliyopita ilikuwa inakusanya kati ya bilioni 800 mpaka 900 kila mwezi. Kwa hiyo, ninyi mmejigamba kwamba mnakusanya mapato zaidi kila mwezi halafu siku hizi hata hatuoni hizo taarifa za TRA tena; mnajigamba kwamba mnakusanya vizuri kuliko Serikali iliyopita, lakini mnakusanya zinakwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri zetu zipo taabani hakuna fedha za maendeleo; wenyewe mnasema mpaka Februari fedha zilizokwenda ni asilimia tano tu, zingine zinaenda wapi? Mnakusanya zinakwenda wapi? Mtafikiaje kutekeleza bajeti hii ya Shilingi trilioni 29 wakati fedha zenyewe hazijakwenda?
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine inayotolewa kwamba wananchi hawana uelewa wa walipa kodi, mashine za EFD; ni hoja dhaifu sana ambazo zinatolewa na Serikali. Nadhani mnapaswa kutafakari na kutumia taarifa za wataalam ili muweze kufikia haya malengo ambayo
yanatakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti inayokuja ya mwaka 2017/2018, mnasema mna bajeti ya Shilingi trilioni 31.6; mimi naomba Watanzania muwashangae kama ambavyo mimi naishangaa hii Serikali. Hii ambayo tunamaliza sasa hivi ni trilioni 29 wakati fedha za maendeleo imefika asilimia 35 halafu hiyo projection ya 2017/2018 ni Shilingi trilioni 31, hivi kuna muujiza? Kuna Yesu atashuka awaletee fedha nyie mkatekeleze hii bajeti? Kwa kweli inashangaza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka Serikali ituambie mnaenda kufanya mabadiliko gani katika ukusanyaji wa kodi au katika kuimarisha kodi ili hiyo bajeti ya trilioni 31 iweze kufikiwa? Mtupe majibu sahihi. Hata hivyo, kama haifikiwi kama ambavyo hii ya sasa hivi tunamaliza
haitafikiwa kwa nini msije na bajeti halisi hata kama itakuwa na kiwango kidogo ambayo inaweza kutekelezeka? Kwa nini mnawafurahisha Watanzania kwa namba kubwa wakati utekelezaji wake unakuwa ni sifuri? Kwa hiyo, tunaomba tuambiwe ni kwa namna gani mnaenda kufanikiwa na bajeti hii. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana