Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Riziki Shahari Mngwali

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nianze kwa kumshukuru zaidi Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na uzima na afya na kutuchangia sisi kuwa miongoni mwa waja wake ambao leo wameweza kuendelea na shughuli zao ambazo wamejipangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianzie hapo ambapo Mheshimiwa Mtolea ameishia; na hili; mimi bahati niko kwenye Kamati ya Katiba na Sheria; tulilizungumza na tulisema pia kwenye Kikao cha Kamati, kwamba kuna taasisi za Serikali ambazo ziko chini ya ofisi nyingine kubwa za Serikali, utendaji wao kazi unakuwa ni mbaya na mbaya kiasi cha kuweza kuhataraisha hata usalama wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yanayofanywa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa yana hatari kwa sababu, kwanza yanahatarisha hata muungano wetu kwa sababu wanachezea chama ambacho kina nguvu sana upande mmoja wa muungano na chama ambacho kwa sababu
yake watu wengi wa upande huo wa muungano waliteseka, walikufa na wengine bado wana vilema vya kudumu mpaka hivi sasa. Anachezea Chama cha Wananchi – CUF, taasisi ambayo imeundwa kwa miaka mingi, watu wamejitolea nafsi zao na kila kitu chao kwa ajili ya taasisi hii. Hii ni taasisi kubwa ambayo watu hao hawatakubali kuona inaharibiwa namna hii na watakapofikishwa mwisho, kile ambacho watakifanya kitakuwa na hatari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kusema hapa, kwamba hata namna Serikali inavyofanya kazi inatujengea uhasama na inatuvunjia udugu kati ya pande mbili za muungano, kwa sababu upande mmoja unatumia kama ndio torturing centre au camp ya upande mwingine. Kwa sababu zilitolewa kauli kwenye Bunge hili au na baadhi ya viongozi wa siasa wa juu kabisa wakasema wanaofanya makosa upande mmoja wa muungano waletwe upande mwingine ambako watashughulikiwa ipasavyo. Hii ni hatari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kinachoniumiza zaidi ni ile kuona kwamba hizi taasisi ni subsidiaries tu, yaani ni taasisi ndogo, kama nilivyosema mwanzo, zinasimamiwa na taasisi nyingine, lakini Ofisi ya Waziri Mkuu binafsi sioni inafanya nini kukemea ofisi hii ambayo iko chini yake. Msajili wa vyama vya siasa anavuruga, lakini katika majukumu makubwa ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni kujenga mahusiano mema kati ya
Serikali na vyama vya siasa. Hebu tupate maelezo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, wanalifanyaje hili wakati wanaona wazi Ofisi ya Msajili wa Vyama inavuruga vyama vya siasa, inahatarisha au inaharibu mahusiano mema kati ya Serikali na vyama vya siasa? Tupate maelezo ya kina na hasa katika hili linaloendelea ndani Chama cha Wananchi – CUF.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niongeze zaidi kwenye hili itaeleweka zaidi, kwamba, hizi taasisi ambazo ziko chini zinapoachiwa namna hii ndio tunaona hata ufisadi. Tumeambiwa hapa, kwenye ripoti nyingi tu, ya mkaguzi na hata taarifa zinazotolewa na Wizara husika, kwamba kwa
mfano mashirika yetu ya umma mengi hayafanyi kazi vizuri au yanafanya kazi katika namna ambayo, zile bodi zenyewe zinashindwa kusimamia mashirika, lakini Wizara mama pia, zinashindwa kusimamia mashirika! Vinginevyo tusingekuwa tunaona taarifa hizi zinazoitwa ma-scandle sijui ya NSSF na wengine au taasisi kama hizi security funds kuwekeza kwenye miradi ambayo haina tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, pamoja na kwamba, taasisi hizo zina bodi zao, lakini pia hizi zinakuwa chini ya Wizara mama. Ofisi ya Waziri Mkuu ni mojawapo inasimamia NSSF, lakini katika mambo ambayo yalikuwa yamesemwa hapa ya kasoro kiutendaji ni hivyo. Sasa
tunajiuliza hivi inakuwaje kwamba, yule anayekabidhiwa ulezi hatazamwi tena yule mtoto anamlea vipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, haya yote yanatokea mpaka tukafikia hapo Bodi inawezekana zimeshindwa kufanya kazi, lakini Wizara mama ndio zimeshindwa zaidi kwa sababu, zimeshindwa kuchukua hatua kabla ya kufikia uharibifu mbaya. Nasema tena kwa msisitizo, suala hili linalofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa Ofisi ya Waziri Mkuu iwajibike ipasavyo na itupe maelezo ya kina.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine litakuwa ni masuala haya ya ujumla tu, namna gani vijana wa nchi hii wanavyokosa uhakika wa maisha yao na tuna wizara kama hii, lakini wakati mwingine mimi nikasema labda haya maneno yamekuwa mengi kwenye hii Wizara. Ofisi ya Waziri
Mkuu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira, Watu Wenye Ulemavu, yote haya yako mahali pamoja na sasa hivi naona mwanangu Mheshimiwa Mavunde kabaki peke yake Msaidizi wa Waziri, sasa sijui haya mambo yanakwendaje? Vijana wa nchi hii wanatakiwa kuhakikishiwa usalama wao, wanatakiwa kuhakikishiwa heshima yao, wanatakiwa kuhakikishiwa kweli hiyo tunayoita hawa ndio Taifa la kesho au Taifa in the making, basi kweli wawe hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitisho wanavyopata vijana wetu sasa hivi vya kutekwa, vya kupotezwa, kwa kweli vinasikitisha. Binafsi niliwahi kuwa karibu na ndugu Ben Saanane, mwanangu Ben Saanane, katika kama siku tatu hivi. Kwa hiyo, kila linapotajwa jina lake hapa mimi naleta picha mama yake Ben, najiweka mimi kwenye nafasi ya mama yake Ben, anafanya nini mwanamke yule sasa hivi? Hebu wanawake wa Bunge hili, tuungane kumdai Ben kwa ajili tu ya mama yake Ben na si kwa sababu nyingine yoyote. Hebu Serikali itwambie kijana huyu na vijana wengine hawa wanaokamatwa na kurushwarushwa kila wakati wanafanyiwa nini na wategemee nini kutoka kwenye nchi yao hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuelezwe vijana wetu na hasa Ben Saanane na nawaomba tena wanawake wa Bunge hili tumsemee mama yake Ben. Kila jina hili likitajwa mimi naamini wanawake ambao tumepitia labor ward, tunarudishwa kwenye machungu yale, kwa hiyo hili lifanyiwe
kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, taasisi nyingine ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni hii Kamisheni ya Usuluhishi wa Migogoro. Nitatafuta ile kesi mahsusi nitampa mtendaji yule kwa sababu aliniomba, lakini kuna taarifa hizi za jumla pia ambazo nilikuwa naomba sana wazifanyie kazi. Kwamba utendaji wa taasisi hii unaonekana kama vile hausaidii sana upande wa Serikali, kwamba kesi zinazopelekwa kule hazishughulikiwi vile ambavyo tungetarajia. Kwa hiyo, Serikali inabeba mzigo zaidi wa kulipa gharama na fidia kwa ajili ya wale ambao wanakwenda mbele ya Kamisheni hii kwa ajili ya kutatuliwa migogoro yao. Kwa hiyo, hilo naomba pia Serikali itupe maelezo juu ya namna gani hii taasisi nayo inatusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa niizungumzie Tume ya Uchaguzi. Kama taasisi nyingine zilizo chini ya Ofisi hii na yenyewe nayo ina mazonge yake mengi. Tunashuhudia amani ya nchi hii inahatarishwa sana na ujumla wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, kwa maana ya hizi taasisi zake ndogondogo zilizoko humu. Tume yetu ya Uchaguzi lazima iwe na maelekezo, iwe kwenye nafasi inayostahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nathubutu kusema kwamba, uchaguzi wa kuchagua Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, pia umevurugwa sana na Tume ya Uchaguzi, kwa sababu msimamizi wa uchaguzi ule alikuwa ametwambia kwamba yeye pia alikuwa anataka kupata taarifa zaidi za uthibitisho kwamba, nani ndiye, nani siye kutoka Ofisi ya NEC. Inavyoelekea NEC ikampa maelezo kwamba kutoka Chama cha Wananchi – CUF watu wanne wote wanafaa waje hapa na wagombee na tuliwaona mbele hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napata wasiwasi kwenye taasisi muhimu kama hizi ambazo tunazikabidhi majukumu muhimu kama haya ya kuendesha nchi hii yanavurugwa, lakini kama nilivyosema tena, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi inayolea haitoi kauli wala haioni kama inaguswa na matatizo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla basi, kama itakuwa kupitishwa bajeti, tunasema ile value for money iwe pia kwenye huduma. Je, tunapitisha bajeti kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kwa huduma hizi inazotoa? Nini inafanya mpaka kweli ituhakikishie sisi kwamba, inastahili kupata pesa hizi kwa ajili ya hizi taasisi zake zifanye kazi wakati huduma yenyewe inayotolewa mimi ninaiita ni chini ya kiwango?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.