Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii niweze kuchangia. kwanza kabisa, naunga mkono ripoti za Kamati zote mbili lakini nitajielekeza sana kwenye suala la elimu kama ambavyo tunajua elimu ya Tanzania iko ICU.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda kushauri baadhi ya maeneo ambayo Serikali inatakiwa iyafanyie kazi ili walau tuweze kuwa na elimu iliyo bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Dunia ilishauri ili Taifa liweze kuwa na elimu bora walau tuweze kuwekeza 5% ya Pato la Taifa. Ukiangalia nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wenzetu wamewekeza vya kutosha. Kwa mfano, Kenya wamewekeza 6% ya pato la Taifa, Rwanda wamewekeza 5%, Uganda wamewekeza 4%, Burundi wamewekeza 3% lakini sisi Tanzania tumewekeza 1% tu ya Pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutashikana uchawi hapa, Wakuu wa Mikoa watawafukuza walimu kama tulivyosikia Mtwara, wanasiasa wataingilia, watawaghadhibu walimu lakini uhalisia ni kwamba hatujawekeza vya kutosha kwenye elimu ya Watanzania. Kama Taifa lazima tuwekeze vya kutosha. Kamati hapa imesema tunatenga fedha lakini haziendi.
Kwa hiyo, naomba kabisa Waheshimiwa Wabunge tuazimie na kwenye bajeti ya 2017/2018 tuhakikishe walau tunatenga 3% ya Pato la Taifa kwenye elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kushauri Rais aone kwamba ni wakati muafaka sasa wa kuunda tume ya kuweza kuchunguza hali ya elimu nchini ili waje na mbadala wa nini kifanyike kuweza kufufua elimu yetu. Pia ni wakati sasa Waziri aweze kuteua Wajumbe wa Baraza la Kumshauri kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1978 na marekebisho yake ya mwaka 1995 ambao watakuwa wanamshauri Waziri kitaalamu maana tumekuwa tukishuhudia sasa hivi Mawaziri wanatoka tu na matamko. Kwa hiyo, tunaomba kabisa aunde lile Baraza liweze kumshauri kitaalam ni vipi tuweze kusonga mbele katika elimu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuwathamini walimu, mimi ni mwalimu. Walimu wasipokuwa na motisha hatuwezi kuwa na elimu bora. Imeelezwa hapa kwa mujibu wa takwimu za CWT ni zaidi ya shilingi trilioni 1.06 walimu wanadai. Wale ambao wamerekebishiwa mishahara ni walimu 5,000, walimu 80,000 bado hawajarekebishiwa mishahara wanadai zaidi ya shilingi bilioni 300, kuna wale walimu ambao wamestaafu takriban 6,000 wanadai zaidi ya shilingi bilioni 480 na kuna wanaodai madeni ya likizo ambayo hata bado hayajaboreshwa. Malengo ya BRN walisema walimu waweze kulipwa madeni yao ndani ya siku 90, sasa ni kwa nini Serikali inachukua muda mrefu sana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni kuhusu utekelezaji wa Sera ya Elimu kwa Wote (Universal Secondary Education). Kwa maoni yangu nashauri sera hii tusiitekeleze sasa hivi kwa sababu Serikali haijajiandaa. Kwa mfano, ukisema elimu ya msingi iishie darasa la sita na waendelee kwenda sekondari kwa wote, tumejenga sekondari zipi za kuweza ku-absorb hawa watoto wanaotoka shule ya msingi na kuendelea moja kwa moja, bado hatujajiandaa! Ni dhahiri sasa tuweze kujiandaa kwanza kama nchi, kwa baadaye ndiyo tuweze kutekeleza hii Sera ya Elimu kwa Wote.
Kwa hiyo, iendelee watoto kujiandikisha shule wakiwa na miaka saba na elimu ya msingi iendelee kuwa darasa la saba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni wanasiasa kuingilia masuala ya kitaalam ya walimu. Utakuta Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa anajaziwa mafuta eti anaenda kukagua shule wakati huo huo wakaguzi ambao ni wataalam wanakagua kwa 30% tu na wanasema hawana fedha za kuweza kuwazungusha kukagua shule. Sasa hawa Wakuu wa Wilaya na Mikoa wengine hata hawana utaalamu huo, wako busy wanajaziwa mafuta kuzunguka kukagua shule. Tusiingilie kabisa kwenye masuala ya kitaalamu tupeleke fedha kwa wakaguzi waweze kukagua na kutoa mapendekezo ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni kwenye afya kuhusu Taifa la vijana kuteketea na viroba. Kamati hapa imesema na mimi Jimboni kwangu kabisa waliniambia nilete Hoja Binafsi. Hivi viroba na sasa hivi hali imekuwa ngumu vijana asubuhi tu na mmewakataza wasiende kwenye bar mpaka saa kumi, kwa hiyo, wenyewe wakiamka tu asubuhi na pikipiki zao wamekamatwa na polisi na wengine kazi ngumu ngumu wanakunywa viroba vile. Viroba kwanza havina standard! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni kwangu nilivyokuwa nimekwenda baada ya hii likizo fupi tumezika vijana zaidi ya wanne na wananchi wamenituma kama Bunge tuazimie viroba vifutwe Tanzania, visizalishwe wala visiingizwe Tanzania.
Kwa hiyo, naunga mkono kabisa mapendekezo ya Kamati kuhusiana na viroba viweze kupotea kabisa vinginevyo tunateketeza Taifa letu, vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa wanateketea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine na cha mwisho ni kuhusu dawa za kulevya, zimezungumzwa kwa upana wake. Kama Taifa tujiulize ni kwa nini tumekuwa tukiimba, hatutekelezi. Kabla ya mwaka 2010 hata sijawa Mbunge tunaona kuna ma-champions walikuwa humu wakizungumzia dawa za kulevya na wengine wakataja kabisa, Marehemu Amina alitaja baadhi ya watu hapa. Tukaja Bunge la Kumi wengine tukawa Wabunge, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, Mheshimiwa Bulaya, Mheshimiwa Jenista, Mheshimiwa Rais Kikwete akasema ana orodha….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.