Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kunipa nafasi hii niwe mchangiaji wa pili kwenye hoja ambazo zimeletwa na wenyeviti wa Kamati. Kamati hizi mbili zimefanya kazi nzuri sana na wenyeviti mmetuletea taarifa ambazo zipo kamili, nawashukuru sana na nawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kwa kutoa mifano kama miwili hivi au mitatu. La kwanza kuna mkoa hapa nchini ambao miaka ya 70 nyani walikuwa wengi sana mkoani huko na walikuwa wanashambulia sana mahindi kiasi cha kuleta njaa kwa wananchi. Wananchi wa Mkoa huo wakaamua sasa kwamba nyani ni kitoweo, wakaanza kula nyani; wanakamata nyani wanakula, nyani wakatoweka kabisa na chakula chao kwa miaka iliyofuata kikawa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa pili kuna mkoa mwingine miaka hiyo hiyo ya 70 ilivamiwa sana na nzige; wananchi wa mkoa huo wakaamua kwamba nzige ni chakula wakawa wanakamata sana wanakaanga, wanakula; nzige wakatoweka. Maana yangu ni kwamba kukitokea maovu zipo njia nyingi za kuyashambulia ili yaishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano madawa ya kulevya ni ovu, yanaharibu wananchi na society; kwa hiyo, inaweza kutumia njia zozote kushambulia mpaka ziishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wizi ni dhambi; mwenye mamlaka ya kukamata mwizi ni polisi; sasa mtu akija shambani kwako anaiba mahindi unaogopa kukamata kwa sababu sio kazi yako kumkamata unasema ni kazi ya polisi utavuna mabua. Nadhani tutumie njia zote ili kuhakikisha kwamba maovu kama madawa ya kulevya yanatoweka nchini kwetu. Anakamata nani ni suala lingine, nani anayekamata ni kwenye vyombo vinavyohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka baada ya hapo niongelee masuala mawili tu machache ambayo Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ameweka mezani. Nianze na Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Wiliam Mkapa ambayo ipo hapa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali za rufaa hapa nchini zipo tano au sita; Muhimbili, Bugando, KCMC, Mbeya na Benjamin Wiliam Mkapa. Hiyo hospitali ya Benjamin Wiliam Mkapa ni kama Jakaya Kikwete Heart Institute; ina vifaa vya kisasa kweli kweli lakini watumishi hakuna. Ile hospitali ilikuwa na madaktari wanajitolea; vijana kutoka vyuoni wanajitolea wako pale kama saba au nane, wamejitolea kwa zaidi ya mwaka mmoja; wanasubiri Serikali itakaporuhusu ajira waweze kufikiriwa nao, sio kulazimisha Serikali kuwaajiri bali waweze kufikiriwa kuajiriwa. Mkurugenzi wa hospitali hiyo baada ya vijana kutumika pale amewaondoa, halafu baada ya miezi miwili baada ya kuwaondoa amewarudisha baadhi yao wengine amewaacha huko mitaani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wenyeviti wa Kamati mlishughulikie suala hili, naona kama si haki hata kama Serikali imesitisha ajira lakini hawa vijana wamejitolea kuokoa maisha ya wananchi; na hawasemi kwamba utakapokuwa tayari kuajiri waajiriwe wao, hapana; wanajitolea tu na uwape posho kidogo, naomba Wenyeviti mlichukue hilo na mlishughulikie ili muweze kuishauri Serikali vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye hospitali hiyo hiyo kama nilivyosema ina vifaa vya kisasa kweli kweli, sasa hapo mimi huwa naenda kutibiwa; kuna mashine ya MRI (Magnetic Reasoning Imaging) ya kisasa kweli kweli, haijafungwa bado ipo pale imekaa tu na mtu anayetaka kipimo cha namna hiyo inabidi umpeleke Muhimbili au kwingine lakini mashine iko hapa, kwa nini haifungwi? Tunahitaji lazima Mheshimiwa Rais atoe amri ya kufunga hiyo mashine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko mashine ya CT Scan ya kisasa kwelikweli, haijafungwa; iko mashine ya X- Ray, sasa hivi wanatumia mobile mashine ya X-Ray; iko mashine ambayo ni fixed, kubwa, ya kisasa kweli haijafungwa; tunahitaji nani aje atuambie tufunge hizo mashine? Mheshimiwa Mwenyekiti na Kamati yake naomba sana walishughulikie suala hili, waishauri Serikali iweze kufunga vifaa hivi na kutoa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye Hospitali ya Muhimbili, kama alivyosema Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii; Taasisi ya Jakaya Kikwete inafanya kazi nzuri sana, imepunguza Watanzania kwenda kutibiwa nje; unafanya vipimo na unatibiwa hapa hapa, naipongeza sana Serikali kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge mwenzangu aliyetangulia, tuiangalie taasisi hiyo, ipewe pesa ya kutosha ili lengo lake la kupunguza kabisa na kuweka sifuri ya Watanzania kwenda kutibiwa nje litimie. Kwa hiyo, namwomba Mwenyekiti wa Kamati waliangalie vizuri hilo na kuweza kuishauri Serikali; hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa hapo hapo, kuna Mturuki ambaye ametoa fedha kwa Muhimbili; amejenga maabara pale Muhimbili, Maabara ya Hermatology ya kupima kwa ndani sana vipimo vya mwili na damu mpaka kwenye details za vinasaba. Ameijenga maabara ile, iko pale, ame-train Watanzania sita au saba wa kuweza kui-manage hiyo maabara ili Serikali, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali nyingine ziachane na kupeleka sampuli Nairobi, Afrika Kusini, Uingereza na Marekani ambako tunatumia fedha nyingi sana. Hiyo maabara ipo tayari na naambiwa Kamati wamepita hapo na kuna vifaa vingine amevituma vipo njiani vinakuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Hospitali ya Muhimbili haipeleki hizo sampuli kwenye maabara hiyo ambayo ipo mlangoni hapo, bado inapeleka Afrika Kusini, Uingereza na Marekani, kwa nini? Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati naomba hilo alishughulikie aishauri Serikali vizuri. Maabara iko pale, mtu wa Mungu ameijengea Tanzania; tuitumie hiyo ili iwe kama ilivyo Taasisi ya Jakaya Kikwete kupunguza kupeleka fedha zetu nje ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii, naomba kuunga mkono hoja za Kamati zote mbili.