Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Edward Franz Mwalongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Awali ya yote niwapongeze sana Wenyeviti wa Kamati zote mbili jinsi walivyowasilisha taarifa zao kwa umahiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita sana na Taarifa ya Tawala za Mikoa (TAMISEMI). Kwanza kabisa liko tatizo kubwa sana ambalo nafikiri ni vizuri tukaishauri Serikali ikaona jinsi ya kufanya. Tunalo tatizo kubwa sana la watendaji katika vijiji na watendaji katika kata. Maeneo mengi watendaji hawa ndiyo wanasimamia maendeleo, watendaji hawa ndio wanaosimamia usalama wa wananchi kule vijijini, lakini hakuna watendaji kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine utakuta mwanakijiji mmoja wamemteua pale ndiye angalau awe anasaidia kazi za utendaji halafu wanakijiji wale ndiyo wanachanga angalau kumsaidia hela ya sabuni yule mtendaji wanayemsaidia. Kwa mfano, katika Jimbo langu la Njombe Mjini, Kijiji cha Idunda, ni kijana wa pale kijijini ndiyo amekuwa kama Mtendaji na ni muda mrefu kijiji hakina Mtendaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tatizo linalojitokeza ni nini? Wananchi wachange kwa ajili ya maendeleo yao, lakini wachange tena kwa ajili ya kumwezesha Mtendaji waliyemweka kwa muda sasa, vitu hivi vinaleta shida sana. Pamoja na ufinyu wa bajeti ambao Serikali inakuwa ikilalamika mara kwa mara, huu ni wajibu wake kuhakikisha kwamba Watendaji wanapatikana na Watendaji hawa ndio watakaosaidia kusimamia maendeleo kule vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watendaji wa Kata hakuna, kila Kijiji, kila Kata utaona Mtendaji anakaimu, anakaimu, anakaimu. Wanakaimu kwa miaka na Mtendaji akishakuwa Kaimu anakuwa ni Mtendaji anayekaimu Kata na wakati huo huo ni Mtendaji wa Kijiji fulani. Kwa hiyo, unaona kabisa pale kwenye Kata panakuwa hakuna Mtendaji ambaye anasimamia maendeleo katika ile kata. Hivyo naiomba Serikali iangalie kwa namna gani; pamoja na ugumu wote wa tatizo kubwa la ajira na tatizo la ufinyu wa bajeti; wapatikane watendaji; watendaji ni muhimu sana katika vijiji vyetu; ili kusudi waweze kusimamia maendeleo kwenye vijiji vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti naomba ku-declare, mimi ni mmiliki wa shule na katika suala la elimu kwanza kabisa nipongeze sana Mkoa wa Njombe na Halmashauri yangu ya Mji wa Njombe Mjini kwa kufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ziko changamoto nyingi kwenye sekta ya elimu ambayo sasa ni vizuri sana TAMISEMI wakajipanga vizuri na wakaangalia namna gani watasaidia. Wananchi wanajitahidi, wanajenga madarasa, wanaandaa thamani za madarasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini liko tatizo la Walimu, na kinachofanyika kule mashuleni ni kwamba, kwa kuwa Walimu ni wachache, yako madarasa ya awali katika kila shule ya msingi. Utaona utawala wa shule unaiambia Kamati ya Shule kwamba darasa hili la awali halina Mwalimu, kwa hiyo Kamati ya Shule inafanya utaratibu wa kuratibu ni kwa namna gani itapata Mwalimu; hivyo Kamati ya Shule inaajiri Mwalimu kwa ajili ya darasa la awali; wakati mwongozo unasema hakuna Mwalimu wa darasa la awali na kwamba Walimu wote wataajiriwa na Serikali na watalipwa na Serikali. Matokeo yake sasa hali hiyo inatia dosari nia nzuri ya Serikali ya kutoa elimu bila malipo pale ambapo sasa wazazi wanaanza kuchangia kwa ajili ya Mwalimu wa darasa la awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana, Serikali iangalie hilo na kama kunahitaji maelekezo, basi itoe maelekezo kwamba Mwalimu wa darasa la awali awe ni Mwalimu mwenye cheti na aliyeajiriwa na Serikali. Kama Kamati ya Shule itaona kuna umuhimu wa kuajiri Mwalimu basi iajiri Mwalimu kwa ajili ya madarasa mengine lakini si kwa darasa la awali; kwa sababu darasa lile sasa linaonekana kwamba ni darasa hafifu au darasa la hali ya chini sana ndiyo maana wanaajiri yeyote tu kule kijijini aendelee kufundisha darasa la awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika madarasa haya ya awali, liko tatizo lingine ambalo sasa linaanza kujitokeza. Mwongozo unasema kwenye sera kwamba watoto wakifika miaka minne na kuendelea wakasome madarasa ya awali katika maeneo ambako shule za msingi zipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta kwamba Shule nyingine ziko zaidi ya kilometa sita kutoka Makazi ya wananchi na wananchi wa vitongoji hivyo wamejenga madarasa mazuri sana yanasimamiwa na Serikali zao za Vijiji lakini watawala wa Idara ya Elimu wanazuia sasa watoto wasisome katika yale madarasa ya awali wapelekwe katika madarasa yaliyoko karibu na shule ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia umri wa yule mtoto ana miaka minne, atembee kilomita sita kwenda mahali ambako iko shule ya msingi, atembee kilomita sita kurudi. Huyu mtoto lazima atachukia shule lakini vilevile ni hatari kwake. Hayuko mtoto mdogo mwenye umri huu ambaye anaweza akatembea kwenda shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri ni kwamba; katika yale madarasa ambayo Serikali za Mitaa zimejenga au Serikali za Vijiji zimejenga na yako vizuri, Serikali iyasimamie yale madarasa ifuatilie kwa utaratibu mzuri ili kusudi watoto wale wasome kule kule wanakoishi na waweze kupata elimu kule kule wanakoishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika masuala haya ya utawala huko vijijini, liko tatizo la posho na mkono wa ahsante kwa Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Mitaa. Bila kuwa na Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Mitaa hatuwezi kabisa kufanya chochote kama Serikali. Ni vizuri Serikali sasa ikaagiza rasmi kwamba kila Mwenyekiti wa Mtaa posho yake ni kiasi gani; maana ile posho sasa inakuwa ni ya kufikirika tu; inafikirika tu kwamba leo Halmashauri ina kiasi gani cha fedha basi apewe; haina basi anaambiwa leo Halmashauri haina kitu lakini ukifikiria kazi anayoifanya Mwenyekiti wa Kijiji ama Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sasa Serikali ikatoa mwongozo rasmi kwamba, watendaji hawa, viongozi hawa waliochaguliwa na wananchi katika maeneo yale wanastahiki nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ulimwengu wa sasa hayuko mtu ana uwezo wa kufanya kazi bila malipo. Hebu tuingiwe hata na huruma tu Serikali tuone kwamba watendaji hawa, Wenyeviti wa Mitaa na Wenyeviti wa Serikali za Vijiji wana kazi kubwa wanayoifanya, wanaamshwa usiku, wanasuluhisha mambo mbalimbali kule vijijini, wanasimamia maendeleo, tunakwenda kule tunafurahia majengo yamejengwa vizuri lakini wao wenyewe hawana kipato chochote na wala hawapewi mkono wa ahsante wanapomaliza ile kazi yao ya kutumikia wananchi baada ya miaka mitano ikipita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la uwezeshaji wa vijana na akinamama. Tumeweka hii asilimia 10 lakini ukijaribu kuangalia asilimia 10 hii imekuwa bado haitoshelezi kuwawezesha hawa wananchi. Tuiombe Serikali sasa, ile fedha milioni 50 ambayo ilisema itaitoa, mchakato huu umekwenda muda mrefu mno na mchakato unapokwenda muda mrefu unakosa maana iliyokusudiwa matokeo yake unazalisha hadithi nyingine na kuona kwamba wananchi hawatatekelezewa ile ahadi. Hebu tuombe huu mchakato uende haraka iwezekanavyo ili kusudi fedha hiyo ipatikane na wananchi hawa wafanye maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Halmashauri zinafanya jitihada nyingi sana katika kuhakikisha kwamba wananchi wanapata ile asilimia 10, lakini asilimia hii 10 ni ndogo mno. Wenyewe tunajua kabisa hali ya Halmashauri zetu zilivyo hivyo tuone kabisa kwamba kama hii milioni 50 itapatikana itasaidia sasa kupunguza ile kiu ya wananchi kufanya maendeleo na kuwapa hamasa zaidi ili waweze kujikimu katika maisha yao ya kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimalizie na suala la TASAF; Naipongeza sana TASAF kwa jitihada zote walizofanya, sana sana. Wanatusaidia sana, wamepunguza kiwango cha uhaba wa fedha kwa wananchi, lakini nafikiri waende mbele zaidi. Wafikirie sasa kwa fedha ile kidogo wanayowapa wawape malengo, kwamba ile ile fedha kidogo wananchi wale wajaribu kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine wawape time frame, kwamba fedha hii watapewa mpaka lini; kwa sababu kuna watu sasa wameshajisahau kabisa wanajua fedha ile sasa wao mpaka siku watakapokufa ndipo itakapokoma. Ni vizuri sasa wananchi wale wakaandaliwa, wakaambiwa fedha hii wanapewa mpaka lini na ikabuniwa miradi midogo midogo ya mazingira wanayotoka hawa wananchi ili waweze kuwasaidia, kwa sababu wote tunaamini kwamba hayuko mtu mwenye uwezo wa kumpa mtu fedha siku zote za maisha yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naipongeza sana TASAF na uongozi wake wote pamoja na Wizara inayosimamia kwa usimamizi mzuri. Tuombe sana wajitahidi sasa wabuni miradi midogo midogo, washirikiane na Mabaraza ya Madiwani kuona kwamba namna gani sasa fedha ile hata kama ni kidogo inaweza ikasaidia kuwawezesha wananchi wale ili kuwa na vitu endelevu kusudi kesho kama TASAF inakoma kutoa hiyo fedha wananchi wasijikute kama wameachwa jangwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana.