Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi uliyonipa kuchangia. Naomba moja kwa moja niende kwenye hoja. Kwanza naanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kutimiza wajibu wake kwa kuivunja Bodi ya Korosho na sasa hivi tunaona wakulima na wananchi wa Mtwara wakiwa wanafurahi kwa sababu korosho yetu imefikia kuuzwa kwa sh. 3,800. Hata hivyo, Mheshimiwa Mpango pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo sijaona vema katika mpango wenu juu ya maendelezo au mwendelezo wa viwanda tulivyonavyo Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulisema toka mwanzo kwamba Mtwara hatuhitaji viwanda vipya kabisa, tunahitaji tu maboresho kwenye viwanda vyetu vya korosho na tunataka kufanya sasa tathmini ya vile viwanda kwa sababu majengo tulikuwa nayo, lakini yaliuzwa kwa watu ambao hawajulikani au wanajulikana kwa bei chee kabisa na wanawatumia kufanyia shughuli nyingine hasa zaidi wamegeuza kuwa maghala badala ya kufanya sehemu za kuzalisha korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa tathmini ifanyike, mpitie pamoja na mikataba waliyouzia maghala yale ikiwezekana sasa mle ndani viwekwe viwanda vidogovidogo na wazalishaji waendelee kubangua korosho zao kama ambavyo inafanyika kwenye kiwanda kwa Mheshimiwa Nape katika Jimbo la Mtama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakumbuka miaka ya 80, Tanzania ilikopa shilingi bilioni 20 kutoka kwa Wajapan pamoja na Serikali ya Italia, sasa tunataka hizi pesa kweli zilete manufaa kwa wananchi. Pamoja na manufaa ya wananchi wanayoyapata kutoka kwenye korosho, sasa hivi pamekuwa kidogo na ucheleweshaji wa malipo. Tunaomba na hili Waziri wa Kilimo alifuatilie tuone hawa wananchi wanalipwa kwa wakati kwa sababu sasa hivi ni mnada wa tatu kufanyika lakini bado wananchi hawajapata posho zao kwa uhakika na hawajui watamalizia lini kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Waziri wa Kilimo pamoja na mazuri yote yanayofanyika, kuna hii karatasi ipo hapa mbele yangu. Kuna Kampuni moja inaitwa HAMAS iko kule Mtwara, hawa watu wali-supply sulphur kwa ajili ya wakulima wa korosho mwaka jana na mwaka juzi, matokeo yake waliishia kufikishana Mahakamani na kampuni hii ililipwa shilingi milioni 953.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naileta kwenu kwa sababu sisi wananchi wa Mtwara tusingependa Kampuni hii tena ikapewa tenda ya ku-supply sulphur kwa sababu wanaleta ujanja ujanja na mwishoni wanapeleka Mahakamani wanaishia kulipwa pesa ambayo hawajaifanyia kazi. Nitaomba nafasi na Waziri Mkuu ikiwezekana tulijadili jambo hili kwa kina kwa sababu kuna taarifa za kutosha, achilia mbali hii karatasi niliyoshika hapa mbele yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri cha Mpango kwenye ukurasa wa 22, tumeongelea pale ndani kwamba kuna samaki wanaoingizwa nchini wanaagizwa kutoka nje. Tungependa sasa kufahamu kwa nini viwanda vyetu au maziwa yetu yasitumike watu wale wakawezeshwa wakaanza kuzalisha samaki hapa nchini baada ya kuamua wao kuvua na tunaleta sisi samaki kutoka nje. Kwa hiyo, kwa vyovyote lazima sasa tuamue tuwawezeshe watu wetu wao wajitosheleze kwanza soko la ndani, kama tuna soko la kutosha kabisa la ndani kwa nini sasa tuanze kuagiza samaki kutoka nje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye ukurasa wa 34 inaonesha pale ndani kuna tafiti mbalimbali zimefanyika za masuala ya kilimo. Mimi bado nirudi tena kwa wakulima wa korosho, niseme kuna tafiti nyingi kweli zimefanyika na Serikali imewekeza pesa nyingi sana pale ndani ikiwemo utafiti wa mabibo ambao unaonyesha una asilimia mara tano zaidi kutoa vitamin ā€˜Cā€™ tofauti ilivyokuwa tunda la chungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunataka sasa zile tafiti zianze kufanyiwa kazi, tusiendelee tu kukaa na mavitabu tukaanza tena kuwekeza kwenye pesa kwa ajili ya tafiti, twende tukawasaidie wale wakulima wa korosho kwa sababu kwa kufanya hizi tafiti vile viwanda vikianza kutengeneza basi kutaongeza mapato kwa wakulima wa korosho kwa sababu, sasa hivi hata bibo tunatamani lianze kununuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa badala ya kuendeleza kufanya taafiti mbalimbali, tafiti ambazo tayari zilishafanyika kutoka kwenye korosho, basi zitekelezwe ili kuwaongezea wakulima kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye ukurasa wa 38, tunakuta pale ndani Mheshimiwa Waziri wanasema tunataka kuwa-encourage investors waje kuwekeza nchini kwenye masuala ya viwanda. Naomba niongelee kwa masikitiko sana Kiwanda cha Dangote. Dangote walipokuja kuweka kiwanda Mtwara walisema kwamba watapewa umeme wa kutumia gesi ili waweze kuzalisha kwa gharama nafuu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshukuru kidogo bei ya cement imeshuka katika maeneo yetu imefikia shilingi 11,000, Mwekezaji huyu ana matatizo makubwa sana, mpaka sasa hivi hajapelekewa gesi pale kiwandani, amelazimishwa akanunue makaa ya mawe kutoka Mchuchuma na utafiti unaonesha kwamba gharama za kutoa makaa wa mawe Mchuchuma zimeongezeka kwa asilimia 20 zaidi tofauti na ambavyo angeweza kuleta makaa ya mawe au ambavyo alikuwa analeta kutoka South Africa. Kwa hiyo, tumsaidie yule Mwekezaji aendelee kuzalisha cement katika eneo lile ili simenti iweze kushuka, tuachane sasa na biashara ya zamani ya biashara ya matope wananchi watumie tofali za cement kujenga nyumba bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba sasa hivi bandari ya Mtwara ndiyo iwe bandari kuu itakayotumika kusafirisha mazao yetu ikiwemo pamoja na korosho. Tulipata pale taarifa wakati fulani kwamba Dangote na tunafahamu Dangote wanaleta cement Dar es Salaam kwa kutumia barabara. Barabara ile tumelalamikia kwa miaka 54 iliyopita ni miaka mitatu, minne iliyopita ndiyo barabara ya Mtwara imejengwa, sasa badala ya kusafirisha cement ya Dangote kwa kutumia bandari ya Mtwara bado cement inakuja Dar es Salaam kwa kutumia barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile ikiharibika Serikali hii haitaweza tena kujenga barabara, tunaomba tafadhali utaratibu ufanyike cement ya Dangote isafirishwe kwa kutumia Bandari ya Mtwara na siyo kupeleka kwa barabara, barabara itumike kwa matumizi mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu hizi kampuni zinazosafirisha cement ni Kampuni za wakubwa wanasingizia kuna kipande fulani cha barabara panaitwa Mikindani kwamba tuta lile litaharibika, kuharibu tuta dogo la kilometa 10 ni nafuu zaidi kuliko kuharibu barabara nzima ya kilometa 300 hadi 400 kufika Dar es Salaam, mtaturudisha kule tulikotutoa siku za mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona sasa hivi katika maeneo mengi ya Kusini kuna uchimbaji wa madini unafanyika katika maeneo madogo madogo (small scale). Tunataka kupata taarifa sahihi kule kunakochimbwa madini ni nini kinapatikana, madini gani yapo tuwaeleze wananchi wa Mtwara ili waweze sasa wao kuangalia nafasi ya kutumia fursa walizonazo katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani walikuwa wanasema Mikoa ya Kusini iko nyuma hasa zaidi Mtwara na Lindi, sasa hivi fursa tunazo za kutosha, tunachoomba tu sasa kutengenezewa mazingira wezeshi tuweze kufanya shughuli zetu wenyewe za kujizalishia kipato badala ya kila kitu tulichonacho ninyi mnataka kukiondoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikuona sababu za msingi za kutengeneza ule mtambo wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi badala ule mtambo ungetengenezwa kule kwetu, ungeweza kutoa ajira kwa vijana wetu, kidogo tunachokipata mkiache tukitumie baadaye kinachobaki mkipeleke kwa wengine nao wakakitumie. Tulikuwa nyuma kwa muda mrefu sana, tunaomba sasa resources zilizoko Mtwara zitumike kwa ajili ya maendeleo ya watu wa Mtwara na kwa Taifa zima kwa ujumla ili vijana wetu waweze kupata ajira ya kutosha katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuendelee bado katika lile jambo ambalo tulisema pale awali. Mtwara pia tunategemea sana uvuvi. Tuna eneo kubwa ambalo linaweza kufanyika shughuli za uvuvi. Tuiombe Serikali sasa iamue wazi kutuwekea hata kiwanda sasa cha uvuvi. Kama nilivyosema majengo ya kuweka hivi vitu tunayo lakini watu waliyageuza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda aamue sasa mara moja aka-review mikataba iliyowapa watu uendeshaji wa maghala kule Mtwara badala ya kufanya viwanda na wanaendelea kuhifadhia mazao wakijipatia pesa kwa sababu si kitu ambacho walikubaliana. Tunataka sasa viwanda vile vianze uzalishaji wa korosho ili kuongeza tija kwenye mazao ya korosho na wakulima waweze kupata kipato cha kutosha pamoja na kuongeza mzunguko wa pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipatia, nitakapopata tena wakati nitatoa maelezo zaidi. Ahsante.