Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami siko mbali na Waheshimiwa Wabunge wengine. Cha kwanza naomba nikupe pongezi wewe kwa umahiri wako wa hali ya juu. Mheshimiwa Tulia ninachokuomba wewe tulia, hawa tuachie sisi; sisi tutawatuliza. (Kicheko)
Waheshimiwa Wabunge, naomba niwaambie kitu kimoja; hawa Wabunge wa Upinzani siyo kwamba wanamchukia Mheshimiwa Tulia na siyo kwamba hawamtaki, wanampenda na wanamwamini. Mkitaka mliamini hilo, mwaangalie asubuhi, wanakuja hapa, anawaombea dua, wanaenda kufanya uhalifu mtaani. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie Watanzania kupitia Bunge hili, wanachofanya Wabunge wa Upinzani wakitoka hapa, wengi wanashinda kwenye jackpot, kwenye betting station, kwenye bars, usiku kucha, wakija hapa wanaombewa dua, wanaenda tena kufanya uhalifu. Naomba niwaambie, Wabunge wa Upinzani wakati Serikali ya Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete (Mstaafu), walisema Rais yule ni dhaifu. Alipoanza Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli, wakasema Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete (Mstaafu), hachomoki.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niwaulize, kati ya Mheshimiwa Jakaya Kikwete na wao nani hachomoki? Wakienda mtaani wanakutana na IGP Mangu, mzee wa Tii Sheria Bila Shuruti, hawachomoki; wakienda Serikalini wanakutana na JPM akisaidiwa na Mheshimiwa Samia Suluhu, hawachomoki; wakija Bungeni wanakutana na Mheshimiwa Tulia, umetulia kwenye kiti chako, hawachomoki; wakija kwa Wabunge, wanakutana na Mlinga, hawachomoki! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la pili, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mpango kwa kazi yake nzuri anayofanya. Kuna methali isemayo kuwa mgema akisifiwa, tembo hulitia maji. Mheshimiwa Mpango amepanga kote amemaliza, sasa akaamua kutupanga na sisi Wabunge. Mheshimiwa Mpango, mimi sikatai kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo cha Waheshimiwa Wabunge, ila masikitiko yangu ni kuwa Mheshimiwa Waziri Mpango umefikiria, umefika mwisho ukaamua utugeuze na Waheshimiwa Wabunge kama source of income. Hilo halikubaliki! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mipango hii ya Mheshimiwa Mpango, tukiliruhusu hili mwakani atasema tuuze magari yote ya Serikali, tutumie baiskeli na pikipiki; mwaka unaofuata atasema Ikulu tupangishe, Rais akaishi Mbagala. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mipango hii, hatuwezi tukakubali, inatakiwa kitendo cha kuwapa misamaha ya kodi viongozi wa Tanzania ilikuwa kama chachu; ilikuwa tuanze viongozi tuwasamehe kodi, tuje wafanyakazi tuwasamehe kodi. Tafuta vyanzo vingine, lakini siyo hili. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mpango amesema katika bajeti yake tukate makato kwenye miamala ya transaction za simu; jamani Mheshimiwa Mpango, kwa sababu huijui adha ya wapiga kura, hizi Tigo-Pesa na M-Pesa, wanatumia wananchi wa kawaida kabisa ambao wameshindwa kumudu gharama za Benki. Kwa sababu ungewahi kuwa hata Mwenyekiti wa TUGHE, ungejua mpiga kura maana yake nini. Makampuni ya simu haya hatujayatoza kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge mtakubaliana nami, nenda kaangalie transaction za Tigo, Vodacom kwa kiwango kile kile cha pesa, gharama zinatofautiana. Ndiyo ujue hawa watu hawalipi kodi. Miamala ya internet hailipiwi kodi; mpaka leo hii Tanzania hatuna mfumo rasmi wa ukusanyaji kodi katika makampuni ya simu. Wafanyakazi ndiyo wanakandamizwa. Mfanyakazi kabla hajaingiziwa hela yake kwenye akaunti ameshakatwa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Wizara ya Fedha mnakaa mnakubaliana na mmiliki wa kampuni ya simu, ulipe kodi kiasi gani; hatuendi hivyo. Inatakiwa muweke mfumo maalum wa makampuni ya simu yawe yanalipa kodi, kulingana na sisi tunavyotumia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie kwamba Waziri anafahamu, TRA ndiyo wanaokula pesa za makampuni ya simu, TCRA ndiyo wanaokula fedha za makampuni ya simu; hawa hawalipi kodi. Mnakula nao, mna kazi ya kuwakandamiza Watanzania wadogo, wananchi wa Tanzania leo hii tutawaambia nini tutakaporudi huko? Wafanyakazi wetu kwa mfano Walimu, wanafanya kazi ngumu sana katika nchi hii. Napendekeza kwa upande wa Walimu, kile Chama cha Walimu, tuwaondolee kwa sababu kile inawanyonya na hiyo iwe option, Walimu wanapoanza kazi kujiunga ili kuwapunguzia mzigo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Walimu hawa tuwaondolee malipo ya NHIF. Serikali iwalipie asilimia 100 ili tuwapunguzie mzigo Walimu. Walimu wa Ulanga kule, Mwalimu anaenda kituo cha kazi hajawahi kufika kijijini, hakuna nyumba, hakuna umeme, makato ni makubwa katika mshahara wake, kwa nini asijiburudishe na wanafunzi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye tozo za watalii, ndiyo maana nasema Mheshimiwa Mpango, umekuja na mipango ambayo haitekelezeki. Umeongeza VAT kwa watalii, unategemea hawa watalii watakuja? Si wataenda sehemu nyingine? Kwani tembo tunao sisi tu? Hata nchi nyingine wanao tembo.
Mheshimiwa Naibu Spika, amekuja kwenye tozo za magari; naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, hivi anapoandika jina pale Profesa Maji Marefu, inaigharimu nini Serikali mpaka aongeze kwenda milioni 10? Kwa nini asishushe iwe shilingi milioni mbili? Sisi haitugharimu chochote, tunachotaka ni mapato, pale huongezi mapato; wale watu wataacha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja suala la tatu, unapoongelea kuinua maisha ya wananchi wa Tanzania ni pamoja na wananchi wa ulanga.

TAARIFA ....

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naifuta hiyo kauli, lakini sikudhamiria kama walivyofikiria. Nawaomba radhi Walimu wote, sikudhamiria kama walivyofikiria, nimetoa mfano.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapoongelea kuinua kipato cha wananchi wa Tanzania ni pamoja na wananchi wa Ulanga. Barabara kutoka kivukoni mpaka Mahenge haipitiki. Ulanga tunalima ndizi; karibu kila familia inalima ndizi, barabara ile mngetuwekea lami, tungekuwa tunauza ndizi Mjini. Kila familia ingeweza kuongeza kipato chao. Ulanga tunalima mpunga lakini barabara haipitiki, hatuwezi kutoka kuuza mpunga mjini. Robo ya mpunga wa Tanzania unatoka Ulanga, lakini leo hii hatuwezi kuleta mpunga mjini kwa sababu ya gharama kubwa za usafirishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea viwanda, tunaongelea umeme. Ilagua leo hii hakuna umeme tunashindwa kutengeneza viwanda vidogo vidogo, mtuwekee umeme ili tutengeneze viwanda vidogo vidogo ili tuongeze mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea kuinua kipato cha Mtanzania ni pamoja na mawasiliano ya wananchi wa Ulanga. Wananchi wa Ulanga leo hii hawana mawasiliano ya simu, ukizingatia hata watu wa Ilagua, mtu anatembea kilomita 20 kwenda kumpa taarifa, badala angetumia muda ule kuzalisha mali ili Serikali ipate kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea kuinua kipato cha Mtanzania ni pamoja na huduma za afya. Wananchi wanatumia muda mwingi kwa ajili ya kusotea kupata huduma za afya. Wananchi wangu wa Lupilo hawapati huduma za afya nzuri, kwa hiyo, wanatumia muda mwingi kutembea kwenda mbali kupata huduma za afya, badala muda huo wangeutumia kuzalisha ili Serikali ipate kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la mwisho, nataka kumwambia Mheshimiwa Waziri ameongelea suala la Wabunge kuwa sawa na wafanyakazi wengine. Waheshimiwa Wabunge tumeingia NHIF, nilishasema katika Bunge lako hili, kwa nini sisi Wabunge tumeingia, Mashirika ya Umma hayaingii NHIF, nataka nimwambie leo hii Mheshimiwa Waziri, baadhi ya makampuni ya private insurance walinifuata, wakaniambia dogo, unapiga mayowe mno Bungeni, badala uongee herufi kubwa tukupooze unaenda kupiga makelele. Naomba niwaambie kupitia Bunge lako hili, kwanza mimi bado mdogo, siwezi kuongea herufi kubwa. Suala la pili hawawezi kunipooza mpaka wawapooze Watanzania na umaskini walionao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hawa waingie NHIF ili kuongeza kipato cha Serikali. Mashirika mengi kama PSPF, PPF, NSSF,TANESCO, LPF, NMB, TCRA, NHC hawataki kwenda NHIF kwa sababu kuna yale makampuni ya private insurance wana hisa mle; na kama hawajaingiza majina yao, wameingiza majina ya wake zao; na kama hawajaingiza majina ya wake zao wameingiza majina ya watoto wao ili tusiwagundue. Mheshimiwa Mpango, naomba ulisimamie hili ili haya Mashirika yote ya Umma yaingie NHIF. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo yangu ni hayo machache, sina mengine.