Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Salum Mwinyi Rehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kujikita zaidi kwenye suala zima la kilimo. Bajeti haikumtazama mkulima, haikutazama kilimo kwa ujumla wake. Mimi kilichonisikitisha zaidi, bajeti ya mwaka uliopita pembejeo zilitengewa karibu zaidi ya shilingi bilioni 50, lakini mwaka huu ambao tunajiandaa kuwa Tanzania ya viwanda pembejeo haikuzidi shilingi bilioni 20. Sasa tunaposema kwamba tuna lengo la kuongeza uzalishaji au kupata mazao kwa ajili ya viwanda, mazao haya yatapatikana vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia tathmini ya pembejeo zilizotoka miaka iliyopita siyo zaidi ya asilimia 10 kwa wale wasambazaji wa pembejeo, wakulima walikuwa wanapata pembejeo hizo katika maeneo yao. Hali hii mwaka huu tunaitazama kwa jicho gani? Obvious, uzalishaji utashuka. Hakuna njia ya mkato, uzalishaji utashuka kwa sababu hakuna pembejeo ambazo zitatosha kwa ajili ya kuwafanya wakulima hao waweze kuzalisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili litaathiri maeneo mengi, litaathiri kwanza wazalishaji wenyewe, litaathiri zile Taasisi na Mamlaka tulizoweka kwa ajili ya kununua mazao katika maeneo yao mbalimbali na hasa kwa zile taasisi ambazo tumeziweka zinunue chakula kwa ajili ya chakula cha akiba na kile cha ruzuku, hakutakuwa na chakula cha kutosha kwa hali inavyokwenda. Vilevile athari nyingine iliyojitokeza hapa ni kufungua milango kwa private sector au waleta pembejeo binafsi kuweza kuleta hizi pembejeo na kuziuza kwa bei ya juu sana kwa sababu ndiyo mahali pekee panapopatikana hizi pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niliona kwenye ripoti au taarifa ya Kamati ya Bajeti na tulilipeleka kama Wajumbe wa Kamati ya Kilimo suala hili liongezewe fedha na lipewe msukumo maalum ili kuwafanya wananchi wa nchi hii waweze kuzalisha kwa uhakika na ile surplus itakayopatikana iweze kupelekwa kwenye hivyo viwanda ambavyo tunataka tuvianzishe. Wasiwasi wangu, mpango mzima wa kuanzisha viwanda katika maeneo haya hasa kwa kutumia raw materials za kilimo utaweza kuathirika na vinginevyo usiweze kufanyika kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kuzungumza kwenye suala zima la kilimo cha umwagiliaji maji. Bado Serikali hapa haijawa na kipaumbele. Tanzania hii ya leo iliyokuwa imeathirika na mazingira na hali ya hewa katika maeneo mbalimbali vyazo vingi vya maji vimepotea, hata yale unayochimba sasa hivi unayochimba katika urefu mkubwa sana kwenda chini, water table imeshuka. Njia pekee ya kulima ni kutumia umwagiliaji. Scheme zetu zilizokuweko nyingi zimechoka zimetengenezwa zamani na zile zinazotengenezwa sasa hivi speed ya utengenezaji wa hizo scheme mpaka kuwafanya wakulima waweze kulima kwa kutegemea maji ni ndogo, lakini fedha vilevile zilizotengwa kwa ajili ya masuala mazima ya umwagiliaji maji ni kidogo sana. Sasa nina wasiwasi nia ya kweli ya dhati ya Serikali ya kuhakikisha kwamba wakulima hawa wana uhakika wa kulima iko wapi.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba Waziri wa Fedha aangalie sana, tuwe na mpango maalum wa kuhakikisha kwamba tunaongeza maeneo ya umwagiliaji angalau asilimia kumi kila mwaka ili tuwe na uhakika wa uzalishaji wa mazao mbalimbali na kuweza kuwafanya wakulima wetu wawe na uhakika wa uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine katika hilo ni suala zima la utafiti. Nchi yoyote katika eneo ambalo linatakiwa liwe na kipaumbele utafiti ni eneo mojawapo kwa sababu ndipo mahali ambapo unapata hizo facts. Nina-declare interest kwamba na mimi niluwa mtafiti kwa zaidi ya miaka nane, ninajua machungu, adha na taabu za utafiti kama hakuna fedha zinazotikawa. Leo hakuna msukumo wa fedha ambazo zinakwenda kwa watafiti moja kwa moja wakati watafiti wale tayari wameshaanza kazi kubwa ya miaka mitatu, miaka minne kutafiti aina mbalimbali, aidha, mbegu, au maradhi mbalimbali au dawa au ufumbuzi wa tatizo ambalo limekabili katika eneo fulani. Leo hii kama hakuna fedha ambazo zinapelekwa katika maeneo haya ya utafiti kwa kweli tunaanzisha kitu ambacho kitawavunja moyo watafiti na hatutakuwa na maendeleo thabiti kwa sababu hatutakuwa na uhakika wa kile ambacho tunakifanya, tutakuwa tunakwenda kwa kubahatisha. Niombe sana kuwepo na msukumo maalum katika eneo hili la utafiti na zipelekwe fedha ili hawa watafiti wengine wamalize research zao na wengine waweze kuanzisha zile research ambazo zitaleta manufaa na mwelekeo mpya wa Tanzania hii ya viwanda tunayokwenda nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti uko katika kila eneo, hata hivyo viwanda ambavyo tunataka kuvifanyia kazi au kuvianzisha lazima kuwe na tafiti za kutosha kuona kwamba zinaweza zikafanya kazi vipi. Kuna material au kuna malighafi za kutosha za aina gani na ubora wa hizo malighafi ambazo zitatumika katika hivyo viwanda tulivyokuwa navyo. Niombe sana tuziangalie taasisi zetu za elimu ya juu, lakini tuangalie Taasisi za Utafiti ili ziwe na kazi na kuleta mabadiliko ya kweli hapa nchini. (Makofi)
Nizungumzie eneo lingine ambalo nimeona bado mkazo wake siyo mkubwa. Tuna mifugo mingi Tanzania, lakini bado eneo hili halijawa productive kwa nchi yaani zile revenue hazijaonesha kwamba kweli inaisaidia hii nchi kupunguza umaskini na kuwaongezea kipato, siyo kwa wananchi wenyewe lakini siyo kwa Serikali vilevile. Eneo hili linahitaji tafiti, lakini inahitaji kutiliwa mkazo ili tuweze kuwa na mifugo iliyo bora na kuwa na ufugaji wa kisasa zaidi. Bado mifugo yetu tunaendelea kuendeleza ufugaji ule tunauita indigenous ufugaji wa kizamani sana, kiasi kwamba mifugo yetu inakosa bei lakini inakosa vilevile kustahimili mazingira yaliyokuwepo hivi sasa matokeo yake ng’ombe, mbuzi na wanyama wengine wanakufa kwa wingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitishwa na kitu kimoja ambacho Serikali inapoteza pesa nyingi sana. Utafiti tulioufanya kuna ng’ombe wengi wanavushwa kimagendo hasa katika mpaka wa Arusha kwenda Kenya. Wakenya wanatarajia kupokea ng’ombe 2,000 karibu kila wiki kutoka Tanzania, lakini ng’ombe wale wakishachinjwa na kufanyiwa process nyinginezo miguu na zile kwato tunaletewa Tanzania kwa ajili ya viwanda au kwa ajili ya ku-pack na kupeleka katika maeneo ambayo watu wanaweza kuifanyia bidhaa. Sasa tunajiuliza…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuunga hoja.