Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nichukue fursa hii kukushukuru, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo kwa uwasilishaji wake mzuri, lakini kwa kazi yake. Hakuna ubishi kwamba mzee huyu kwa kweli ana-fit kwenye nafasi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na umeme; katika Jimbo langu la Singida Mjini ninavyo vijiji 13 na mitaa 13 ambayo haina umeme. Katika taarifa yake Mheshimiwa Waziri, imeonesha wazi kwamba kutakuwa na KV 400 zinapita Singida kwenda Shinyanga, lakini pia kwenda Namanga. Nimuombe sana tusiwe watazamaji, lakini tusiwe watu wa kupisha mradi unapita unaenda kwa wengine na sisi tuwe sehemu ya mradi. Naomba Mheshimiwa Waziri utushirikishe na ikiwezekana sasa vijiji vyangu vyote hivi nilivyovitaja na mitaa viweze kupatiwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeguswa kidogo na suala la vinasaba. Kabla sijaendelea na mimi nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuweka vinasaba ambavyo vimetusaidia kwa kiasi kikubwa sana; vimepunguza uchakachuaji wa mafuta kwa asilimia kubwa na kama haitoshi vimedhibiti mafuta ya magendo (smagling product). Vinasaba hivi vimedhibiti pia on transit product. Yale mafuta yanayopita hapa kwenda nchi za jirani vimedhibiti, lakini pia hata yale mafuta ambayo yanasamehewa kodi, vinasaba hivi vimetusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama haitoshi vimeongeza makusanyo ya kodi na vimeleta ushindani kwa wafanyabiashara wa mafuta nchini. Nikuombe sana na niwaombe Waheshimiwa Wabunge na wananchi tufike mahali tuiunge mkono Serikali, tuwe waadilifu na kama haitoshi kwa wale wafanyakazi wetu ambao tunawatuma kwenda kubeba mafuta haya sasa wawe makini na kazi hii kwa sababu Serikali kwa kweli ina mkono mrefu na nikuombe Mheshimiwa uifanye kazi yako vizuri, nakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie suala la madini. Kwa kweli, kwa Mkoa wangu wa Singida tunayo madini mengi sana na ya kutosha, lakini hali tuliyonayo pale haifanani na yale madini tuliyonayo pale. Nataka niiombe Serikali sasa iwaangalie wale wachimbaji wadogo waweze kupewa fedha na kama haitoshi, wachimbaji wadogo wale waweze kupewa elimu, kwa maana sasa waendane na teknolojia ya uchimbaji ya sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tatizo ninaloliona pale, naliona tatizo kubwa moja, GST. Mamlaka ya GST siyaoni, GST wanavyoonekana kwa sasa kazi yao haina meno. GST wakati umefika sasa wafanane kama EWURA kwa sababu, na wao nao ni wakala, wapewe hatimiliki. Sasa hivi makampuni yote tunayoyaona makampuni makubwa ndio ambayo yanafanya utafiti na wakishamaliza utafiti ule hawako tayari kutupa hali halisi ya madini tuliyonayo pale kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejionea, nitoe mfano wa Shanta Company Limited pale Singida walitoa eneo la Mwintiri kwa wachimbaji wadogo, lakini eneo lile wachimbaji wadogo wameshindwa kuliendeleza kwa sababu hawana utafiti, hawajapewa ramani nzima ya eneo lile lililopo pale. Sasa kwa hali hii ni lazima Serikali ije na mpango kama ni sheria, kama ni nini, ije tuweze kuisimamia. GST wapewe mamlaka wawe mawakala ambao wanaweza kusimamia raw data na sio watu wa kupewa processing data. Huu sio wakati wa processing data. Wawe ni watu ambao wana raw data na wawekezaji wote wanaokuja waanzie GST, hii inaweza kutusaidia sisi na wale wachimbaji wetu wadogo walioko kule wanaweza kupata mwelekeo wa kuchimba madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama ambavyo alitangulia msemaji mmoja tuko naye kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara alizungumzia namna ambavyo TANELEC, kiwanda ambacho sisi tuna hisa, kiwanda ambacho kimefika mahali sasa Serikali imekitelekeza. Mimi nizungumzie upande mdogo wa REA. REA waliwapa kazi Symbion, Symbion wamekwenda kuomba kutengenezewa transfoma TANELEC, hivi tunavyozungumza zimetengenezwa transfoma za zaidi ya shilingi bilioni mbili zimekaa pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia kama Kamati transfoma ambazo Symbion walizi-order ziko pale TANELEC, kwa hiyo, wametuingizia hasara Serikali. Nikuombe Mheshimiwa Waziri na kuna taarifa kwamba ulifika pale na ukatoa maagizo. Na sisi tukuombe ifike mahali sasa hawa watu wanaopewa tender, tender hizi lazima ziangalie kwanza viwanda vya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka wakati nachangia kwenye viwanda nilitoa ushauri kwamba kabla hatujaenda kwenye kutangaza tenda ya kuingiza viwanda vyetu kwenye tender ni lazima kwanza ikiwezekana 40% ibaki kwetu, 60% waende wakashindanishwe kwenye tender, hali hii itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia wenzetu wa Symbion wanaagiza transfoma kutoka India. Na nilitoa mfano siku ile wenzetu kule wanatoa ruzuku kwenye viwanda vya ndani 10% kwa kila kiwanda. Uzalishaji unakuwa mwingi kwa hiyo, wanatafuta sehemu ya dumping, sasa sisi hatuwezi kuendelea kuwa dumping place. Niombe sana na sisi sasa tufike mahali tuone umuhimu wa viwanda vyetu vya ndani, hali hii itatusaidia kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa nchi yenye viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Singida Mjini tumejaaliwa kuwa na chanzo cha umeme ambacho ni upepo na mpaka sasa sioni juhudi za Serikali kuhakikisha kwamba rasilimali hiyo ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia tunaweza kuitumia ipasavyo, sioni. Maana tunakoelekea tunaelekea kwenda ku-misuse rasilimali ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niuone mpango wa Serikali wa kuhakikisha rasilimali ile iliyojitokeza kwenye eneo letu la Singida Mjini ya umeme wa upepo, Serikali inakuja na mpango wa kuwekeza ama kutafuta wawekezaji. Na kwa bahati nzuri tayari walishajitokeza wawekezaji, kwa bahati mbaya sijajua wameishia wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako Wind East African Company walijitokeza, lakini kama haitoshi wako Power Pull nao walijitokeza. Sasa niiombe Serikali, kama wawekezaji walijitokeza na wameonesha nia, kama kuna mahali tunaweza kuwa-support basi tuwa-support waje wawekeze umeme pale Singida. Tunajua umuhimu wa umeme kwenye maeneo yetu, sisi tumejaaliwa hilo na maeneo yetu tuna uzalishaji mkubwa sana. Tunauhitaji umeme huu kwa kasi kubwa, utatusaidia kuinua uchumi wetu hasa kwa maeneo yale ya Kisasida ambayo tayari pale tuna uzalishaji na ndio tuna kilimo cha umwagiliaji cha mboga mboga.
Mheshimiwa Waziri nikuombe sana ifike mahali, sisi ndugu zetu wa Singida Mjini pale tunakutakia kila la heri, tunakuomba ufike ili uweze kutuwezesha na sisi kuweza kuupata huu umeme na uchumi wetu uweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya na mimi nimalizie kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kweli kumteua baba huyu ametusaidia sana sisi. Ameionesha dhamira ya dhati ya nchi yenye viwanda kwamba inawezekana kwa sababu tayari tuna uwezo wa kupata umeme kwa kila eneo. Baada ya kusema haya, naunga mkono hoja.