Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Samweli Xaday Hhayuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hanang'

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na jioni ya leo naanza kuchangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniruzuku uhai, afya njema na nguvu ili niweze kuchangia kwa niaba ya wananchi wenzangu wa Jimbo la Hanang.

Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kwamba tarehe 3 Desemba, 2023 Jimbo la Hanang tulipata changamoto kubwa sana ya maporomoko ya Mlima Hanang na kwenye hayo maporomoko madhara mengi yalitokea. Narudia tena kuishukuru Serikali kwa kazi kubwa ambayo ilifanyika. Mji wa Hanang ambao ni Makao Makuu ya Wilaya pale Katesh palijaa tope ambalo kwa kweli tungetakiwa tutoe sisi wenyewe ingetuchukua labda miaka mitatu ili tuweze kulimaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa angalau wananchi wanapita kwa sababu Serikali yetu sikivu ya Chama Cha Mapinduzi chini ya usimamizi makini wa Dkt. Samia Suluhu Hassan waliacha kila kitu ili kuhakikisha kwamba wanatusaidia na kwa sasa mambo mengi yanaenda sawasawa. Mambo mengi yalifanyika ili angalau zile huduma za msingi ziweze kurudi kwenye hali ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kipindi kile kila mtu alikuwa amechanganyikiwa. Tumepoteza ndugu zetu 89, wengi waliathirika lakini na biashara za watu ziliathirika. Miundombinu mingi ambayo tulikuwa tumeitengeneza kwa gharama kubwa yote ilienda na yale maporomoko. Tunasema tunaishukuru sana Serikali kwa nguvu ambayo iliitoa, tulishinda usiku na mchana na Mheshimiwa Jenista Mhagama na timu nzima ya Serikali, tunasema ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi nyingi zimekwishafanyika. Madhara yale ni makubwa sana, ukiangalia kwa miundombinu ambayo iliathirika, kwa maana ya barabara, mpaka sasa Barabara ya kutoka Endasak – Gitting – Gendabi - Dawar hiyo haipitiki kabisa. Ukishuka upande wa mjini barabara zote za mjini maeneo mengine ni maporomoko makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna fedha tulizoziomba kwa upande wa barabara. Upande wa miundombinu ya maji, mlima Hanang ndicho chanzo kikuu cha maji kwa Wilaya ya Hanang. Tuna kata karibu saba, tunaanza Kata yenyewe ya Gendabi, Kata ya Dawar, Gitting, Measkron, unakuja Kata ya Nangwa. Ukija kwenye mamlaka yote ya mji, Kata ya Katesh, Kata ya Ganana, Kata ya Dumbeta na Kata ya Jorodom wote hao miundombinu ya maji iliathirika, tulijaribu kurudishia kwa kipindi kile kwa dharura.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatamani na sisi turudi kwenye hali ya kawaida ya maendeleo ambayo tuliyatamani na ile Hanang ambayo ni ya maziwa na asali ili tuweze kuirudia. Kuna fedha ambazo tuliziomba, tunaomba zile fedha zitoke kwa wakati ili miundombinu hiyo yote iweze kurudishwa kwenye hali yake ya kawaida ili Hanang iweze kwenda sawasawa na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu, fedha kwenye upande wa maji na upande wa miundombinu ya barabara zitoke kwa wakati ili kazi ile iweze kukamilika na sisi tuweze kurudi kwenye hali ya kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kipindi kile kuna biashara ambazo ziliathirika moja kwa moja kwa sababu lilipigwa eneo la soko ambalo lilikuwa linategemewa na wananchi wote wa Mji wa Katesh. Kwa sasa tunaishukuru sana Serikali, imejenga soko kwa ajili ya kurudishia. Hata hivyo lile soko liko pembeni kidogo ilhali wananchi wameshazoea kuishi mazingira ya mjini. Kuna changamoto ya kukubali yale mazingira kwamba sasa tukitoka kule nani atatufuata, kwa sababu utaratibu wa binadamu pale ambapo umezoea kila siku kwenda ndiyo akili yako muda wote iko pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa ukitembea Mji wa Katesh kila sehemu kila mtu ametegesha sehemu ya kushikilia na wale wafanyabiashara wengi waliathirika. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Jenista Mhagama. Tuliwaita watu wa benki na taasisi za mikopo, tukaongea nao ili waangalie namna ambavyo wanaweza kuangalia kupata unafuu kwa wale wafanyabiashara kwa sababu athari zile ni kubwa na biashara nyingine zilikuwa ni ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee kuangalia namna ya kusaidia zile biashara zilizoathirika moja kwa moja. Tuwalee wale ili waweze kurudi kwenye hali yao ya kawaida, wale wanahitaji kulelewa. Tunafahamu kazi kubwa imefanyika, tunaomba, kwa sababu kweli changamoto ilikuwa ni kubwa, lakini ukiangalia biashara 713 zilizoathirika moja kwa moja kila mtu alikuwa na hali tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wale ambao wanaweza kujimudu baada ya kuwaombea zile nafuu ambazo tuliziomba na wakazipata, lakini kuna wale ambao hawana namna, hawa tuendelee kuwalea, tuendelee kuwawezesha ili kuhakikisha kwamba wanarudi kwenye hali yao ya kawaida ya maisha. Naomba kwenye eneo hili tuendelee kushirikiana, kuhakikisha kwamba wale wananchi wanaweza kurudi kwenye hali yao ya maisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kati ya sehemu kubwa ambayo Ofisi ya Waziri Mkuu inaifanyia kazi, ni kuwawezesha wananchi kwa kuhakikisha kwamba wanapata au wanachochea uchumi wa wananchi. Tumekuwa na utaratibu wetu wa kuwapa mikopo isiyokuwa na riba kupitia mapato ya ndani ya halmashauri zetu, ile 4:4:2. Kwa maana ya kwamba vijana wanapata asilimia nne (4), akinamama wanapata asilimia nne (4) na walemavu asilimia mbili (2). (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo hiyo ilitolewa kwa kipindi kirefu, lakini wananchi wengi walinufaika na walikuwa wakiitegemea. Ni kweli changamoto zilijitokeza kwamba fedha zile zilikuwa hazirudi. Tunachoomba sasa ile mikopo iliyosimama maana yake shughuli nyingi za wananchi za kiuchumi zilisimama. Ungefanyika utaratibu wa haraka kuhakikisha kwamba zile fedha zinaanza kutoka tena ili wananchi wetu waweze kufanya shughuli zao za kawaida ambazo wamezoea, za kilimo, biashara, uvuvi na ufugaji. Tukiendelea kushikilia hizo fedha maana yake tumeshikilia uchumi wa wananchi, tumeshikilia uchumi wa nchi yetu. Hizo fedha zianze kutoka mapema inavyowezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuangalia mahitaji makubwa ya kupeleka ile elimu ya vitendo kwa wananchi wetu Serikali iliridhia vyuo vya ufundi vijengwe kwenye maeneo mbalimbali ndani ya wilaya yetu. Kulikuwa na ujenzi wa vyuo vya ufundi kila wilaya. Ukipita pale Hanang ambako tulichagua eneo la Nangwa kwa ujenzi wa chuo cha ufundi, ukipita unasikitika kwa jinsi unavyoenda kwa kasi ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iwe inatoa fedha kwa wakati ili ujenzi ukamilike kwa vyuo vile ambavyo tumevilenga ili hatimaye tupate wataalam tunaowahitaji kwenye maeneo yetu. Imekuwa zaidi ya mwaka mmoja sasa hakuna hata sehemu moja kwenye ujenzi wa vyuo vya ufundi ambao unafanyika, nikitolea mfano eneo la Nangwa ambao haukufika hata hatua ya lintel.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali kwenye eneo hili iweke fedha za kutosha ili kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika kwa wakati. Ili hatimaye watoto wa Kitanzania wapate ujuzi unaohitajika kwenye eneo la kilimo, uvuvi, mifugo na hatimaye waweze kupambana na mazingira waliyonayo kutumia elimu ambayo itatokana na vyuo vyetu vya ufundi ili kutibu tatizo ambalo lipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi ya wafugaji yalianzisha shule maalum za watoto wa wafugaji. Kwa Jimbo la Hanang sisi tulikuwa na shule mbili maalum kwa ajili ya watoto wa wafugaji. Tulikuwa na shule ya Gendabi na shule ya Bassodesh ambazo zote ni shule za msingi za bweni. Shule hizi zilikuwa zinasaidia kwa sababu maisha yetu ya ufugaji kwa sasa bado hatujayaboresha kiasi cha kwamba tunaweza kutulia sehemu moja na watoto wetu wakapata elimu inayostahiki, tumekuwa na maisha ya kuhamahama. Ili kutibu tatizo hilo la wazazi kuhamahama, watoto walikuwa wanawekwa bweni ili wapate elimu kwa wakati bila kubughudhiwa na tabia ile ya kifugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali chini ya usimamizi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumepata ukarabati mzuri kwenye Shule Maalum ya watoto wa kifugaji ya Gendabi ambako angalau pakikamilishwa kabisa yale mazingira yangekuwa sawasawa. Ukienda Bassodesh kwa sasa hali ni tete, mabweni yamebomoka, madarasa yamebomoka na ile shule ni ya miaka mingi, wamesoma watu ambao mpaka sasa wameshastaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba tutengewe fedha ili kuhakikisha yale maeneo maalum tuliyoyatengea na yale ya uangalizi yaweze kupata fedha na kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanatengenezwa vizuri ili watoto ambao wana changamoto ya kupata elimu nao wapate elimu inayopaswa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumalizia kwa kutoa salamu kwa ndugu zangu wa Wizara ya Ujenzi. Kumekuwa na taratibu hizi za EPC+ F, taratibu hizi za design and build lakini taratibu hizi barabara zingine unaanza ule upembuzi wa awali na usanifu wa kina. Barabara ya Haydom- Mogitu imekuwa ya muda mrefu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, tukiendelea hivi hatutaelewana, barabara hii inapaswa kujengwa ni ahadi ya Marais watatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)