Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami kuchangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni Rais ambaye amejipambanua vizuri kwa Watanzania na ameonesha kiu ya kutibu matatizo ya Watanzania, mahali popote unapokwenda unapotaja mama kabla hujaendelea Watanzania wanamalizia vichwani Samia, ni kwa namna ambavyo Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameonesha nia, uthubutu na ari kubwa ya kutatua matatizo ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Watanzania wanampenda Mama Samia na Watanzania wa Ngara wanampenda sana Mama Samia kwa sababu Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha mapenzi makubwa kwa Watanzania hasa kupitia miradi mikubwa ya maendeleo anayoisukuma kwenye Jimbo la Ngara na maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaenda kwenye mchango wangu halisi, nisiruke bila kumpongeza sana Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Mawaziri wengine wote na Naibu Mawaziri waliopo kwenye hii ofisi ya Waziri Mkuu. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na hao wengine sijawataja Jenista Mhagama naye yuko mle mle na wengine hakika ni miongoni mwa viongozi ambao nchi hii wametafsiri vizuri matakwa na maono ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania, sasa viongozi hawa wakiongozwa na Mheshimiwa Majaliwa wanatekeleza vizuri Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na wanasimamia vizuri shughuli za Serikali. Hakika tunawapongeza sana, chukueni maua yenu live hapa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nielekeze mchango wangu kwanza kabisa kwenye eneo la kuwezesha wanafunzi wa elimu ya juu hapa nchini. Dhamira ya HESLB ilikuwa ni kuhakikisha Watanzania wengi wanaweza kusoma elimu ya vyuo vikuu na elimu ya vyuo vya kati, tunaipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo imeifanya ya kuhakikisha inatoa mikopo pamoja na kuongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu, lakini kuna kundi la Watanzania kama ambavyo ipo kwenye school dropout kwa maana ya ngazi za chini hivyo hivyo na vyuo vikuu sasa hivi kuna university dropout. Nataka nikwambie Mheshimiwa Naibu Spika na Bunge lako hivi tunavyozungumza Wabunge wengi wanafuatwa na wazazi pamoja na wanafunzi waliotoka vyuo vikuu wakienda kuombwa wasaidie kusomesha watu walioko vyuo vikuu, ukiuliza unaambiwa mtoto alikosa mkopo. Baada ya kukosa mkopo kuna wazazi wanaouza mifugo, mwenye ng’ombe anauza, mwenye kuezua nyumba anaezua na wenye kuuza viwanja wanauza. Kwa bahati mbaya wazazi wengi hawatoboi miaka mitatu au miaka minne, wengi wanaishia katikati. Matokeo yake unakuta mwananchi wa kijijini ameuza mali yake lakini watoto hawajamaliza vyuo vikuu, wanarudi nyumbani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba kwa dhati ya moyo wangu kabisa, Serikali wafanye uchunguzi wa haraka wawabaini wanafunzi ambao wame-drop vyuo vikuu, waende HESLB wawape mikopo hao watu ili warudi vyuo vikuu wamalizie. Lipo kundi kubwa mpaka jana mimi nyumbani kwangu wamekuja wazazi zaidi ya sita, wote watoto wameshindwa kumalizia vyuo vikuu kwa sababu wamekosa mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kero kubwa kwa Wabunge wengi kwa sababu wazazi wale wanahisi sisi Wabunge tuna mifuko tunaweza tukachukua fedha za kuweza kuwasaidia watoto wakamaliza vyuo vikuu. Sasa kundi hili naomba litafutwe, lihudumiwe kwa kuwa linajulikana. Mtu anaandika barua kwamba naacha kuendelea na chuo kwa sababu amekosa ada, anarudi nyumbani anakaa mwaka mzima, vyuo vikuu wanazo taarifa, Serikali ifanye mawasiliano, wachukue takwimu za hawa Watanzania, wasaidieni wapate mikopo waende wakamalizie vyuo vikuu. Naomba hili jambo mlipe kipaumbele kwa sababu watu wanalalamika na kuna kundi huko limeachwa. Naomba Watanzania hawa waweze kusaidiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili kwa sababu hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu inakuwa na mawanda mapana, naomba niongelee eneo la miundombinu hasa upande wa miundombinu ya barabara. Sisi ni miongoni mwa Watanzania ambao wamewahi kupewa ahadi sugu ya muda mrefu ya kujengwa kwa barabara kwa kiwango cha lami. Naibu Waziri hapa anaifahamu, ameshakwenda mpaka akawaahidi wananchi wa Rulenge. Hii ni Barabara ya kutoka Mrugarama kwenda mpaka Rulenge, kutoka Rulenge mpaka Tembo Nickel, kutoka Rulenge mpaka Kumbuga, Murusagamba na Nyakahura, barabara ina urefu wa kilometa 114.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya barabara hii kama haijengwi hata ule Mgodi wa Tembo Nickel hauwezi kufanya kazi. Watanzania wote wanafahamu ni kwa kiasi gani tunatarajia mgodi wa Tembo Nickel ulete fedha nyingi kwenye nchi lakini kwa bahati mbaya kama hakuna barabara ya lami ile nickel haiwezi kuchimbwa. Hivi tunavyozungumza kuna mitambo imeshindwa kupita kuelekea Tembo Nickel ili wawekezaji waendelee kuwekeza na kujenga ule mgodi kwa sababu hakuna barabara ya lami. Natambua juhudi nyingi ambazo tumeshazifanya, nakumbuka engagement ambazo nimeshazifanya na Wizara mbalimbali zinazohusika, nawaomba kwa unyenyekevu mkubwa kuhakikisha fedha yote imeingia kwenye bajeti hii. Sijawahi kukamata shilingi lakini kwa hili kwa sababu wananchi wangu wameahidiwa mwaka 1995, 2000, 2005, 2010, 2020 mpaka mimi naingia tumeahidi na Mawaziri wote wameahidi.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa unyenyekevu mkubwa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ninayotaka nimpe msemaji ni kwamba ile barabara ikijengwa kwenda kwenye machimbo hayo ya nickel itajenga barabara nyingi kutokana na faida ambayo itapatikana kwenye ile biashara ya nickel.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa taarifa hiyo.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, yaani ndugu yangu natamani wangekuwa wanaruhusu kuja Bungeni na soda ningekupatia pepsi, nimeipokea hiyo taarifa. Naomba barabara hii itendewe haki na bajeti iingie ili barabara hii isaidie barabara nyingine za Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine kwa upande wa miundombinu inasikitisha sana ni eneo la miundombinu ya umwagiliaji. Serikali ilifika Ngara Rulenge eneo la Vigombo na kuanza kujenga Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Vigombo zaidi ya miaka tisa iliyopita. Kwa bahati mbaya wale watu sijui hela waliitafunia barabarani wakati wanakuja kumalizia ujenzi, ile skimu ilitelekezwa mpaka leo, kwa miaka tisa iliyopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefanya engagement na Serikali nimewaomba, sasa naomba niwakumbushe sasa hivi haiwezekani mimi nikapiga kura ya ndiyo kama ile skimu ya Vigombo fedha yake haijaingizwa kwenye bajeti kwa sababu tumewadanganya na tumewaahidi wananchi vya kutosha, muda umefika wa kwenda kukamilisha skimu ya umwagiliaji ya Vigombo, naomba wahusika watenge fedha twende tuwapatie haki wananchi. Kwa bahati mbaya Wabunge wengi wanajua ile miradi haikuwa Ngara tu ilikuwa maeneo mengi, sijui nini kilitokea ilitelekezwa na wakati muafaka wa kwenda kukamilisha miradi hiyo umefika, naomba bajeti iingizwe ili twende tukakamilishe ujenzi wa miundombinu hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni eneo la kilimo. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu wananchi wa Jimbo la Ngara wamelima mazao mengi ikiwemo mazao ya mahindi. Hivi karibuni tumevuna zaidi ya metric ton laki moja na kwa bahati bei ya mahindi imeshuka kilo moja ya mahindi ni shilingi mia mbili. Nashukuru baada ya kupaza sauti Serikali imewatuma NFRA kwenda kufanya tathmini ili waanze kununua yale mahindi kwa bei elekezi ya Serikali, lakini tathmini ya nini wakati unakwenda sokoni unakuta mzigo wa mahindi umejaa, si uje na pesa anza kununua, pakiza kwenye fuso, lete Dodoma, tunza kwenye maghala ya Serikali? Siwaelewi kwa sababu mahindi yapo ya kutosha zaidi ya metric ton laki moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kwa unyenyekevu mkubwa ianze kununua. Utafiti wakati mahindi unayaona unatafiti nini, unataka ugundue kitu gani zaidi ya mahindi yaliyoko sokoni? Naiomba Serikali ianze kununua, wawatumie fedha wale maafisa wanaofanya utafiti huko Ngara waanze kununua mahindi hayo ili tuweze kuwaokoa wakulima ambao wanauza mahindi kwa bei ya chini. Eneo lingine...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)