Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja kwa sababu hotuba hii ya bajeti imekidhi mambo mengi ambayo tumekuwa tukiyatarajia Wabunge katika majimbo yetu, lakini imeonesha namna gani ya mambo yaliyotekelezwa katika sekta ya afya, elimu, barabara, maji na umeme, kwa hiyo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa kuweza kuyafanya yote haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote hayo yapo mambo machache ambayo yanahitaji marekebisho ya haraka ili tuweze kusonga mbele. Mara kadhaa toka tuanze Bunge hili nimekuwa nikipigia kelele suala la wananchi wa Rangitatu mpaka Kongowe kulipwa fidia zao, ni mwaka wa saba sasa wananchi wale wametathminiwa. Kama unavyojua sisi wananchi wa Dar es Salaam nyumba zetu ndiyo biashara zetu, ndiyo sehemu zinazotupatia riziki. Kwa hiyo nyumba sasa zimekuwa hazipangishiki na haziuziki, tumeendelea kupata ugumu wa maisha kutokana na kutokulipwa fidia zaidi ya miaka saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile sehemu inayotaka kulipwa fidia ni kwa ajili ya kujengwa barabara ile ambayo inatoka Rangitatu kwenda Kongowe. Wote mtakuwa mashahidi bahati nzuri Waziri Mkuu naye ndiyo njia yake ya kuingilia Dar es Salaam, barabara ile imekuwa na msongamano mkubwa kila mwaka tunaizungumzia. Nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri leo amenijibu kwamba barabara imepata kibali cha kutangazwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hoja yangu ya msingi tunatangaza barabara kujengwa, je, hawa watu ambao tumewaweka muda mrefu bila ya kulipwa fidia tunawafanyaje. Naomba sana Serikali itupe majibu lini watu hawa watalipwa fidia na lini barabara hii itaanza kujengwa ili tuondoe sintofahamu ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara katika barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo nataka kuliongelea ni suala zima la alama za X nyekundu zinazowekwa katika maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Dar es Salaam. Katika Jimbo langu Barabara yote inayotoka Rangitatu - Charambe kwenda mpaka Maji Matitu – Chamanzi mpaka Msongola kupitia Mbande pande zote mbili imewekewa X, sasa tunajiuliza hawa wenzetu wa TANROADS wanaweka X kwa sababu gani. Bahati nzuri sisi wengine tumezaliwa Dar es Salaam, maeneo tunayokaa ndiyo tuliyozaliwa. Tunafahamu historia ya maeneo yale, maeneo yale yalikuwa ni Vijiji vya Ujamaa ambapo wazawa wa pale walitoa ardhi zile kwa ajili ya kuwapa makazi ndugu zao waliokuja katika maeneo yale lakini kwa masharti watakapokata mti basi mti ule ulipwe fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kijiji kile kukua Serikali tunaishukuru iliamua kututengenezea barabara na mwaka 1994 Serikali kupitia Kampuni ya ADUCO iliamua kuboresha barabara ile, barabara ile ilijengwa kwa upana wa mita saba na nusu kwa pande zote mbili kwa maana ya mita 15. Wakati inajengwa miti ya wazee wetu ililipwa fidia na ikapisha ujenzi wa barabara ile mpaka sasa tunapita kwa amani.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2007 Sheria ya Barabara Namba 13 ilitungwa. Katika sheria ile inaelezea barabara itakuwa na mita 27.5 pande zote za barabara kutoka katikati ya barabara, hoja yetu tunayojiuliza, unatuwekea X je, barabara ile ilipandishwa hadhi mwaka gani na ilipandishwa hadhi kwa GN namba ngapi? Ili tuone kama kweli X zile zinazowekwa zinaendana na ile sheria ya mwaka 2007 iliyotungwa Sheria Namba 13.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli sheria ile wakati inatungwa hakuna aliyelipwa fidia na kama wapo waliolipwa fidia basi tuwaombe wenzetu wa TANROADS watuletee orodha ya watu waliolipwa fidia ili tupishe eneo lile kwa amani. Tumekuwa tukiwaomba mara kwa mara, lakini wameshindwa kufanya hivyo hatimaye Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa imesitisha zoezi lile la kubomoa, zoezi lile tunasema limesitishwa kwa mdomo, tunaomba tupewe maandishi kwamba zoezi hili limesitishwa kwa sababu moja, mbili na tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi tunayo maswali ya kujiuliza, moja, tunataka tujue GN namba ngapi na ya mwaka gani iliipandisha hadhi barabara ile ili tuweze kujua sasa kama sisi tuliokuwepo tulikuwepo kimakosa au tuko sawasawa. Jambo la pili ni wananchi wangapi walilipwa fidia baada ya GN ile kutoka, lakini jambo la tatu kwa nini Wizara ya Ardhi imetoa hati miliki katika maeneo yale pande zote mbili za barabara? Wananchi siyo tu wanamiliki leseni za makazi wanamiliki kwa hati miliki, tunaomba tupewe majibu hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tunataka tujue ni vigezo gani ambavyo TANROADS walitumia kulipa fidia watu waliokuwa barabarani wakati wanajenga stendi ya mwendokasi na hawa waliopo sasa hivi watakiwe kubomolewa bila kulipwa fidia. Mambo haya yameleta taharuki kubwa sana kwa wananchi kwa sababu ni zaidi ya kaya 100,000 zinaenda kuathirika katika barabara ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunajua Jimbo la Mbagala na Jimbo la ndugu yangu Jerry ndiyo yanaongoza kwa population kubwa hapa nchini, kwa hiyo mjue kitendo kilichofanywa na TANROADS kimeenda ku-disturb siasa za Dar es Salaam. Naomba sasa Serikali ije na kauli ambayo itawatoa hofu wananchi wa Mbagala Rangitatu, Charambe, Chamazi na Msongola.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nizungumzie suala la miundombinu ya barabara. Tunafahamu mvua zimenyesha na barabara zimeharibika kwa kweli katika Jimbo zima la Mbagala kama siyo Mkoa wote wa Dar es Salaam barabara zimeharibika sana, tunawaomba sana TANROADS na TARURA waje warekebishe barabara zile ili ziweze kupitika vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho tunazo mamlaka au taasisi mbili zinazojenga barabara hapa nchini. Tunao TANROADS na TARURA, ushirikiano wao hauko sawasawa kwa sababu wakati fulani TANROADS wanajenga barabara na wanaweka mifereji lakini maji wanaelekeza katika makazi ya watu na wanasema wananchi suala la maji yale kuyapeleka mtoni ni suala la TARURA, je wali-check bajeti za TARURA wakalinganisha na bajeti zao ili kuona barabara ile itajengwa na TARURA watapokea yale maji kuyapeleka mtoni?

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba sana watendaji wetu wa Serikali pale wanapotaka kufanya maamuzi ambayo yatawagusa wananchi moja kwa moja hasa suala la bomoa bomoa waangalie historia ya maeneo yale, sisi tunawafahamu, ukiangalia TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam wote wanaofanya kazi sasa hivi ni watu ambao wamekuja miaka ya 2000, wangeuliza historia kwa wenzao waliokuwepo nyuma wangepata hadhi ya barabara ile ilikuwaje ili sasa wakurupuke na mipango yao ya kuweka X.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)