Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Tecla Mohamedi Ungele

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ili nami nichangie hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunipatia zawadi hii ya uzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuleta ustawi na maendeleo ya jamii ya Watanzania. Nampongeza pia Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kazi kubwa ya kusimamia kazi za Serikali na pia kwa wasilisho zuri la bajeti na hotuba ya bajeti ya Wizara yake. Hotuba hiyo imesheheni mambo mengi ya sekta mbalimbali nchini zikiendelea kuleta maendeleo na kuchochea maendeleo. Pia nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Mawaziri wote katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zote zilizoko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, wanafanya kazi nzuri kwa maendeleo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu nauelekeza kwenye maeneo kadhaa. Hotuba ya Waziri Mkuu ina mambo mengi, lakini kutokana na muda, nitachangia maeneo machache tu. Kwanza, ni usafiri na usafirishaji. Tumeshuhudia miundombinu ikiboreshwa; barabara za mijini na vijijini na Watanzania wote ni mashahidi, lakini miundombinu hiyo imeharibiwa na mvua kubwa ya El-Nino. Tumeshuhudia maeneo mengine mawasiliano yalikatika. Kwa mfano kule Liwale, Barabara ya kutoka Nangurukuru kwenda Liwale na Barabara ya Masasi - Nachingwea kwenda Liwale, Barabara ya kutoka Nanganga kwenda Ruangwa, zote zilikatika na maeneo hayo yalikuwa hayana mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, mawasiliano ni muhimu sana katika ustawi wa jamii, kusafirisha mazao, kusafirisha watu na kadhalika na maendeleo yote tu yanategemea usafiri. Ombi langu, barabara hizi zijengwe kwa umakini mkubwa kweli na kwa kiwango cha lami; vile vile Masasi – Nachingwea – Liwale, Nangurukuru kwenda Liwale na Daraja lile la Nanganga ambayo inaunganisha Wilaya ya Masasi na kule Ruangwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia madaraja yajengwe kwa uimara mkubwa. Maeneo tuliyokuwa tumetegemea yawekwe makalvati, ndiyo hayo mvua hizi kubwa zimefika zikayavunja yale makalvati na kuyazoa kabisa, sasa hivi kumebaki wazi kabisa. Kwa hiyo, yatengenezwe madaraja makubwa na imara ya kupitisha maji katika maeneo mapana.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nachangia liko Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Kuna program hii ya kukuza ujuzi kwa vijana, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, vijana wamepata nafasi kwenda kusoma vyuo hivyo, tumeenda kule Rwazari kule Tabora Manispaa na kule St. Antony Manispaa ya Musoma na kwingineko, wanapata ujuzi wa ushonaji, useremala na mambo ya umeme na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu, kwanza idadi ya vijana iongezeke na ichukue maeneo mengi ya Tanzania, kwa sababu maeneo mengi yana vijana ambao hawana ujuzi, lakini pia kuna vijana ambao wako kwenye makundi maalum, nao wanahitaji ujuzi, kwani nao wana umuhimu na wana vipaji vikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu lingine, vijana hawa wapatiwe vifaa vya kufanyia kazi wakishamaliza masomo. Tunawafundisha ujuzi pale, wanapata ujuzi vizuri sana na wenyewe wanafurahi sana, tumewaona tulipokuwa tumeenda wakati wa ziara za Kamati. Wanafurahi sana kupata ile nafasi na wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iweke bajeti maalum ya kununua vifaa ili vijana wale wakishatoka kwenye mafunzo, wakisharudi majumbani kwao, basi kuwepo na mwendelezo wa kazi zile, wakajiajiri wenyewe na wakaendelee kufanya kazi ya kujipatia riziki, badala ya kutoka pale na ujuzi wao ambao hautakuwa na maana, kwa sababu wengine hawana uwezo wa kumudu kununua vifaa vya kufanyia shughuli zile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii na naunga mkono hoja. (Makofi)