Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye mjadala wetu huu wa bajeti yetu ya mwaka ujao. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais, Waziri wa Fedha na Waziri wetu mpya wa Mipango na crew nzima ya Wizara hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikifuatilia mijadala iliyokuwa ikiendelea hapa kati ya Waheshimiwa Mawaziri kwenye mjadala wa CAG na Waheshimiwa Wabunge, kitu kimoja kinanipa shida kidogo ni kwenye suala hili la Mikataba. Sitaki kuongelea mkataba wa DP World maana yake wenyewe umekwishamalizika, naongelea hii Mikataba mingine ambayo inasemwa kwamba Mikataba hii itakuwa ni siri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najaribu kujiuliza, ni kweli ndoa inakuwa siri lakini talaka na ugomvi wa talaka wa ndoa unakuwa wazi. Sasa ni kweli Mkataba unakuwa wa siri, huyu kesi ikianza kesi inafanyika hadharani na kila kitu kinaletwa wazi, sasa maana ya huu usiri ni nini hasa na nani alileta hii proposal ya Mkataba uwe siri? Aliuleta mwekezaji au ni Serikali ndio ilitoa huo muundo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili neno kwa sababu naona nusu ya mgogoro uliokuwepo hapa ni Suala la Mikataba na penalty zote na riba zote zinazolipwa ni kwa sababu mikataba yote inaonekana ni siri. Sasa kama mikataba ni siri basi na kesi ziwe siri. Leo tunamwona Profesa Mruma kesi inaendeshwa hadharani, lakini Mikataba ile ilikuwa siri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa labda Mheshimiwa Waziri wakati wa kufanya majumuisho, ajaribu kutueleza nini hasa kinachosababisha iwe siri. Maana yake ukitaka kwenda kuwekeza kwenye nchi yoyote duniani unapata data za kila aina ya uwekezaji ulioko pale, labda kama unataka special case ndio unakwenda sasa kuongea na Waziri au Baraza la Mawaziri au Kamati ile, ndio unasema bwana mimi kwa masharti yenu haya naona labda kipengele A, B, C, D naomba kirekebishwe lakini kama hakuna marekebisho mengine yoyote sioni sababu Mikataba yetu kuwa siri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango ni mzuri sana, lakini hofu yangu ni kwamba hauendi kwenye yale maisha kabisa ya kila siku ya wananchi. Wananchi wanachohitaji ni kile ambacho kinawagusa, leo sisi kwenye maeneo yetu ya Kanda ya Ziwa na maeneo ya Tabora kuna maeneo ya hifadhi ambazo hazina hata nyani, wala hazina tumbili, wala hazina kitu chochote lakini kuna dhahabu mle ndani na almasi na ziko labda kilomita saba, kwa nini Wizara ya Maliasili kama yenyewe inapenda miti, iruhusu watu wahamishe ile miti, ihamishiwe sehemu nyingine ili watu wachimbe dhahabu zile. Haiwezekani tukachorewa michoro na Wazungu, tukafa njaa eti pale pana dhahabu si ndio lakini wewe unakatazwa kwamba huwezi kuchimba kwa sababu kuna miti. Kwa nini miti ile isihamishwe?

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tabasamu.

TAARIFA

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Kishimba kwamba sheria zinazotumika kwanza hizo za hifadhi ni sheria za mwaka 47, Mjerumani, akaja tena Muingereza, halafu na sisi tukapata uhuru. Sasa kwa nini tusitumie sheria zetu za wakati ambapo tumepata uhuru? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jumanne Kishimba unaipokea hiyo taarifa?

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, yeah ninaipokea. Ndiyo maana nimesema ndugu zetu wasomi tuleteeni pia mawazo kabisa ambayo raia anaweza akakutana nayo mtaani kuliko huu ustaarabu mwingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana sana Mheshimiwa Waziri wa Afya kwenye suala la bima ya afya, lakini tunaiongea bima ya afya kwa maongezi rahisi kwa ajili ya maisha yetu sisi yalivyo ni mazuri. Jana, mtoto wa ndugu yangu kapata ajali kule Mwanza, amefika Sekou-Toure anaambiwa kupimwa kwenye scan anahitaji shilingi elfu sitini, mtandao hauendi, mpaka tunalia na Daktari kwamba bwana mpime pesa tutatuma, anakataa na mtu karibu anafariki. Bahati nzuri mtu amekimbia pale amekwenda kulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo napigiwa simu toka kijijini, uzuri Mheshimiwa Mwigulu Nchemba na Mheshimiwa Kitila ni watu wa Singida. Leo humu hata kwenye Mpango hawajasema nyoka au mbwa, je, wakimuuma mtu huwa ni ajali au yenyewe inaitwa nini? Maana yake ukifika umeumwa na nyoka unaambiwa ulipe shilingi elfu 60 na ukiongea na mtu anakwambia huyu alienda kuwachokoza nyoka kule shambani. Huyu mtu kazaliwa Dar es Salaam. Nafikiri wangeangalia kabisa suala la kwamba, je hawa watu tunaohudumia ni Watanzania wa aina ipi? Msisemee tu habari ya mbolea sijui habari ya nini, hapana, wasemee maisha yao kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukiwa una wezi, hata kama wamekuja wezi wa kuku, ukipiga simu au yowe zinakuja defender nne au tano za Polisi, lakini polisi wale watamkata huyu mtu au hakupatikana wataondoka, gharama ni karibu shilingi laki mbili. Leo mtu anaumwa amekwenda hospitali hana pesa, haya mtu wa msamaha amemsamehe kweli hakuna shida, lakini hakuna dawa pale hospitali, lakini pale pharmacy dawa zipo, anafanyaje kati ya hospitali na pharmacy. Huyu mtu atakufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha aeleze kwamba mtu kama hana pesa na wale hospitali hawana dawa, huyu mtu aende polisi aje na polisi mpaka pharmacy anywee dawa hapo. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo wananchi wanayohitaji, hizi blaa blaa zote, hakuna mwananchi anayehitaji. Tuweke kitu ambacho kiko practical wazi, kwamba mimi kama naumwa sina pesa, nafanya nini hasa? Kweli msamaha nimepata, lakini wale pale hospitali walionipa msamaha hawana dawa, kwa nini huyu mtu wa msamaha tusiondoke naye mpaka Polisi, Polisi wanidhamini ile dawa wapige picha WhatsApp waitume Wizarani, si wana mafungu ya maafa. Sasa hayo mafungu ya maafa huwa yanatumika namna gani au maafa maana yake nini? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake hiyo mifumo kama tumeirithi toka kwa wakoloni, matokeo yake inatutesa, inatutesa. Leo hii wanakusanya pesa kwenye njia ya M-Pesa, kwani kwenye M-Pesa pesa haramu huwa inarudishwa? Mtu akituma pesa ya uwizi au rushwa kwenye M-Pesa ina legality? Ameuza gongo si akutuma kwenye M-Pesa inapokelewa na ushuru wanakata. Sasa wanakataaje kumtibu mtu? Kama ni watakatishaji, basi mtakatishaji wa kwanza atakuwa Serikali. Maana si ndio Mheshimiwa Mwigulu, yeye ndiye anapokea pesa zote kwenye miamala, miamala imewahi kurudisha pesa, kwamba pesa hizi hatuzitaki kwa sababu ni haramu? Inapokea pesa zote na inachukua na ushuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najaribu kulieleza neno ambalo linawagusa wananchi. Sisi tunaowakilisha hayo yote wanayoongea wala hawana habari, wanachotaka ni kwamba huu uhuru tulioutafuta, nikiwa leo naumwa naweza kusimimamiwa na Mwenyekiti wa Kijiji nikatibiwa na Serikali ikatambua hilo? Ndicho wanachotaka na dhamana ikawa ni mimi mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kumalizia tu, sisi leo tuna matatizo sana kule kijijini, leo ukipata kesi unatakiwa udhaminiwe na mtu ambaye ni mwajiriwa wa Serikali, lakini unakataaje mtu wa ng’ombe, ana ng’ombe kunidhamini mimi. Je, mimi nina ng’ombe 200 unakataa kweli mimi nisimdhamini mtu kwenye kesi? Ng’ombe, sisi ndiyo tunatumia kuoa mke. Huwezi kwenda kuoa kwa kutumia friji wala TV, huyu mtumishi wa Serikali anamiliki TV na friji, unamkataliaje mwananchi mwenye ng’ombe kudhamini mtu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri Mwanasheria Mkuu wa Serikali yupo, hivi vitu vyote tumerithi ni vya mkoloni, waendelee kuwafanyia urahisi wananchi ili wananchi waanze kuona kwamba kweli sasa tuko na Mama. Mama Samia anataka vitu kama hivi ili wananchi wa-feel kweli kwamba wako huru hata. Kama hana maji ya kunywa na wanawakopesha wanakataaje kumkopesha mtu dawa? Kwa nini unakataa? Umeme unanikopesha, maji unanikopesha nitalipa mwisho wa mwezi, wewe unakataa kunikopesha dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mchango huo naendelea kumshukuru tu Mheshimiwa Rais hasa kwa suala hili la bima ya afya. Baada ya hapo nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)