Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Mpango huu wa Serikali.

Kwanza, nataka niwaeleze wananchi kwamba, Chama Cha Mapinduzi katika Ilani yake ya Uchaguzi wa mwaka 2025, Mheshimiwa Rais kama alivyojua yaani nafikiri kwenye maono yake akaona Mheshimiwa Kitila Mkumbo anafaa kuwepo hapo katika sehemu ya Mpango, ndiyo Mwandaaji. Ndiyo aliyeandaa hii Ilani ya Uchaguzi halafu leo ndiyo amewekwa kwenye mpango, baba ukitufelisha tumekwisha na wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, Chama Cha Mapinduzi ni chama cha kijamaa. Vilevile viongozi wake wote ni wajamaa lakini sisi tunafuata Sera za kikomunisti. Kwa hiyo, hauwezi kumtenganisha Mheshimiwa Rais na ukomunisti wa ujamaa. Hata hivyo, Mheshimiwa Rais ana dini na imani tena kwa mapenzi makubwa kwa wanachi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, sisi ambao tumemtanguliza Mheshimiwa Rais mbele na sisi tuko nyuma yake, sisi pia ni wajamaa lakini pia ni wakomunisti. Sasa, mimi hapa kama Tabasamu hauwezi ukanitenganisha na ukomunisti.

MHE. DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasam kuna taarifa. Mheshimiwa Dkt. Bashiru.

TAARIFA

MHE. DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, anachangia vizuri sana Mheshimiwa Tabasamu. Namuomba radhi ni mara ya pili nampa Taarifa katika maisha ya Bunge hili. Sisi ni wajamaa siyo wakomunisti, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasamu, unaipokea hiyo Taarifa?

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiunga mkono mimi mjamaa, sasa nikikataa kwamba siyo mjamaa, itakuwa ni hatari sana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba sisi wajamaa tunapekea sana miradi na huduma za wananchi kule kwa wananchi. Ndiyo maana ya Sera ya Chama Cha Mapinduzi. Ni kwenda kuwasaidia wananchi wake kule chini. Sasa, Mheshimiwa Profesa Kitila nakuamini kwa kuandika, wewe ni Profesa. Vilevile wewe ni Mwalimu wangu. Kwa hiyo, sina shaka na wewe. Kwa hiyo, siwezi ku-doubt mahali popote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndugu yangu ni kwamba, tuna vijana zaidi ya milioni 20 katika nchi hii, vijana wenye ajira ya kazi, wenye uhakika wa ajira rasmi hawazidi 300000 mpaka 600000. Sasa, huu Mpango wako uje na kuondoa tatizo la hawa vijana kukosa ajira. Lakini vijana wa Kitanzania hawana shida, wakitengenezewa mahala pa kufanya biashara na kufanyia kazi, wako tayari kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Rais mwaka 2022 alielekeza yajengwe masoko ya Machinga kuanzia kule kwenye ngazi za halmashauri mpaka ngazi za kata. Mheshimiwa Waziri, ninaimani wewe ni bingwa kabisa wa kuandika. Hivi ukitengeneza yale magulio yakapata nafasi wale vijana wakaanza kufanya biashara zao kule, mbona tungepunguza sehemu kubwa ya ajira?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Chama Cha Mapinduzi tulisema tuna ajira milioni 10. Ninaimani unaweza ukatengeneza ajira milioni 15. Sasa tunachokuomba, kwa mfano Sengerema inazungukwa na ziwa kwa asilimia karibu 72, asilimia kama 30 hivi ndiyo nchi kavu. Sasa, siyo Sengerema peke yake, Buchosa, ukichukua Geita vijijini, ukichukua Ukerewe, ukichukua Magu, Bunda mpaka Musoma moja kwa moja mpaka Tarime huko. Maeneo haya yote ukija ukachukua hiyo Kagera mpaka Chato, maeneo haya yote tunaweza tukafuga Samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wanaofuga Samaki na kuzalisha Tani za Samaki wanategemea maji yanayotiririka kutoka kwenye Ziwa Victoria kupitia Mto Nile. Sasa, tulikuwa tuna uwezo wa kupeleka vijana Misri au tuwachukue Wamisri waje huku tuwape vizimba wawekeze na tuwape kwa gharama nafuu kabisa ili watu wetu waje kujifunza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wamisri wakija, wafanyakazi wao watakuwa ni watanzania. Sasa, andikeni maandiko muwakaribishe wamisri tuje tufuge Samaki ndani ya Ziwa Victoria. Mheshimiwa Mkumbo, hili kwako siyo tatizo.

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Cherehani.

TAARIFA

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kumpa taarifa mzungumzaji kuwa, wenzetu Misri pia walitengeneza ziwa la kutengeneza na wanafuga samaki vizuri, pia linasaidia mambo mengi ikiwepo umeme. Kwa hiyo, sisi sasa hivi kipindi hiki cha masika maji ya mvua yanapotea, kwenye madaraja yetu maji yanapotea. Tunauwezo wa kutengeneza benki ya maji ya mvua katika kipindi hiki cha masika.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeikubali hiyo taarifa.

MWENYEKITI: Haya ahsante. Endelea Mheshimiwa Tabasam.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la ufugaji na uvuvi. Huko kwenye ufugaji tungeunda Mamlaka ya Uvuvi, Mamlaka ya Mifugo. Nasema kama tutafanya kama walivyofanya TARURA na TANROADS yaani maeneo yote ambayo yameundiwa authority yote yanafanya kazi vizuri sana. Tungekuwa tuna Mamlaka ya Mifugo ingesimamia Minada, ingesimamia zahanati kule za mifugo, ingesimamia mambo mengi, uzalishaji wa nyasi mambo yote mazuri yangefanyika kule, lakini kule kwenye Uvuvi pia tungesimamia mambo mengi makubwa tukazalisha. Tunakwama wapi katika Mpango kuweka suala la Mamlaka katika huu Mpango na Mamlaka ya Mifugo na Mamlaka ya Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la huduma za afya. Hapa kwenye Mpango mimi nimeona kwamba tumeboresha na tunapanga kuboresha huduma za afya, lakini kama hatutatafuta wawekezaji wakaja kuweka madawa kuweka viwanda vya kuzalisha dawa nchini, ni kwamba tu madawa peke yake, tunanunua dawa nje ya nchi asilimia 85, asilimia 15 ndio inayozalishwa nchini. Jamani hata syringe tu ya kuchoma sindano miaka sitini ya Uhuru hatuwezi kutengeneza Kiwanda cha syringe tu ya kumchoma binadamu, shilingi mia na yenyewe tunaagiza kutoka Korea, tunaagiza kutoka India.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hawa Wahindi kule kwao wana dawa za gharama nafuu, dawa zao ni za gharama nafuu sana, kwa nini tusiwafuate Wahindi wakaja kuweka viwanda hapa Tanzania, tukakubaliana wasilipe kodi lakini tupunguze nakisi ya kuagiza madawa nje ya nchi. Hili naliomba sana kwenye Mpango Mheshimiwa Profesa Mkumbo aliweke pale ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la mitambo ya maji, mitambo ya maji tumenunua mitambo ya maji mingi sana hii mitambo ya maji kweli kama ilivyokuwa inazungumzwa hapa na Mheshimiwa Monni, Mbunge wa Chemba kule, alizungumza akasema mitambo hii imesimama. Ninachotaka kumwambia Mheshimiwa Mkumbo hata mimi kwangu Sengerema hii mitambo ipo, nina visima 39 sijui vimechimbwa viwili tu, hii mitambo imesimama, imekosa mafuta. Ukiwauliza wanakuambia hakuna mafuta. Kama tumeweza kununua mitambo ya karibu bilioni 250, Serikali inaweza ikakosa mafuta?

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maneno siyo sahihi, tujue tatizo ni nini kwa sababu Serikali haiwezi kukosa Wazabuni wa kufanya kazi hii. Kwa hiyo, tunaomba kwamba aje na majibu mazuri tu. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kutuletea mitambo, Mheshimiwa Rais kununua hii mitambo alikuwa na nia njema sana katika nchi hii. Sasa tunawaomba tu, hii mitambo kwa nini isimame kwa sababu ya kukosa mafuta, ifanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho ni suala la Mkataba wa Bandari, Mkataba wa Bandari huu tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maono yake, lakini tuliomba hawa Dubai World pia wangepewa Gati la Mafuta kwa sababu kule ndio ingerekebisha ile mifumo ya uzalishaji wa mafuta, wakatujengea hub na matenki tumezungungukwa na zaidi ya nchi nane, wanategemea hapa kwetu. Sasa tunaomba sana, kwamba tungerekebisha mifumo ya ushushaji wa mafuta, angalau hata meli zenye metric tons 500,000 zishushe mafuta kwa muda mfupi na tupate storage, matokeo yake gharama za mafuta katika nchi hii zitapungua. Tunaliomba sana hilo Mheshimiwa Mkumbo aliweke katika mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii tunamwombea sana Mheshimiwa Rais apate maisha marefu sana, mpaka kijijini kwangu sasa hivi kuna watoto wanazaliwa wanaitwa Samia, inaonekana wananchi wamemkubali sana Mheshimiwa Rais katika jambo hilo. Ahsante sana. (Makofi)