Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii tena nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii aliyonipatia ya kuchangia katika Bunge hili leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kukubali mpango wa kuirejesha tena Tume ya Mipango. Kwa sababu huko nyuma ilikuwepo, ikaunganishwa na baadaye imerudishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulisema sana juu ya Tume ya Mipango kwamba, itakwenda ku-centralize mipango yetu na sasa itajulikana nani anatakiwa kufanya nini na wakati gani. Nawapongeza sana Mawaziri wote wawili, Waziri wa Mipango na Waziri wa Fedha. Waziri wa Mipango kwa kutuletea Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2024/2025 lakini Waziri wa Fedha kwa kutuletea mwongozo unaotuonesha ni nini kitakwenda kuingia kwenye Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Mkatibu Wakuu, Mtendaji Mkuu wa Tume ya Mipango na uwasilishaji mzuri uliofanyika kwenye Bunge hili. Pamoja na pongezi hizi, yako mambo mengi ambayo yamesemwa katika hotuba hii. Iko mipango mikubwa imeoneshwa kwenye hotuba hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kujikita kwenye Fungu namba 57 ukurasa wa 27 kinachosema kwamba, Mpango huu utathibitisha Maendeleo ya Kweli yanatokana na Mpango mzuri na nidhamu ya utekelezaji wa mipango hii. Kwa hiyo, kuna hoja ya Mipango na nidhamu ya utekelezaji na hapa ndipo kuna changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki nzima tumekuwa tunaongelea habari ya CAG, ni hoja tu ya nidhamu ya utekelezaji kwamba kuna mahali fulani kwenye nidhamu hatufanyi vizuri sana. Mipango tunayo lakini hatutekelezi vizuri kwa sababu nidhamu yetu iko chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kifungu namba 35 ukurasa wa 26, Waziri wa Mipango alitoa Mfano wa Ndugu yangu Lee, kiongozi wa Singapore. Anasema, uwepo wa Mfumo wa taasisi nzuri ni muhimu na inasaidia lakini muhimu zaidi ni kuwa na watu wazuri katika kuendesha mifumo na taasisi ya Serikali. Sasa, hoja yangu hapa pamoja na kwamba aliitoa kama quotation, hawa watu wazuri tunao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa tuliyonayo ni kwamba, tuna mifumo na taasisi nyingi za Serikali lakini na changamoto ya watu wazuri kama inavyoonekana hapa. tumekuwa tunafanya vetting kila mwaka kwa viongozi mbalimbali lakini baada ya muda tunajikuta kwenye tatizo kwamba, mtu mmoja anaonekana hajafanya vizuri na CAG anatuambia kwamba huyu hajafanya vizuri ameiba bilioni 18, huyu amesababisha loss ya kitu fulani. Kwa hiyo, watu wazuri hatuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu sasa, ni ombi langu kwamba, upande wa elimu watu wa elimu waingize elimu bora ya uraia na uzalendo. Maana inaonekana uzalendo ndani ya nchi hii ni tatizo. Kila anayepewa nafasi anafungua mdomo kwa ajili ya kula badala ya kufungua mikono ili atufanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sana hili. Tunapokwenda kwenye mipango yetu, watu wa elimu wahakikishe kwamba, mitaala hii ambayo inakuja hivi karibuni inaweza kutufanya kwenda hatua moja mbele kwenye elimu ya uraia na uzalendo ili huu wizi na vurugu zinazotokea hadi Wabunge wamefikia mahali fulani wanafikiria kuwaondoa watu kwenye uso wa dunia, maana yake wanyongwe. Kabla hatujakwenda huko tuwape elimu. Pia tukishawapatia elimu tunajua kuwa matokeo mazuri yatakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza sana, kiongozi aliyepewa responsibility matrix yake, amepewa nini anachotakiwa kufanya, amepewa KPI yake, vilevile amepewa milestone yake kwamba kama amepotea njia anaweza akajua huku ninakokwenda siko, aende huku. Unashangaa anachokifanya ni kitu ambacho hakuambiwa kwenye ile responsibility matrix yake. Tuna kitu cha kufanya maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa yale ambayo yametekelezwa katika mipango iliyopita. Tunaiona SGR ikiwa sasa inakwenda Lot one iko kwenye hatua nzuri na sasa tunakwenda karibu Lot Five huku. Vilevile, tuna habari ya umeme vijijini ambayo inaendelea kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana, ukiangalia umeme, mchangiaji aliyepita amethibitisha wazi. Nimewahi kufanya kazi viwandani, kama umeme wa kutosha haupo uchumi wetu wa viwanda utadorora kabisa. Hata kama tutaonekana tunapambana kwenye zile hatua nyingine, kama uchumi wa viwanda haujakaa vizuri kwa sababu ya umeme hatuwezi kutoboa. Tutafika mahali fulani tutashindwa tu. Gharama ya kutumia mafuta kuendesha viwanda inaomndoa kabisa ile net profit ya kiwanda, kwa hiyo, niwaombe sana kwenye hii habari ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye umeme utagundua kwamba, tuna umeme wa maji megawatt 574. Mpaka sasa tuna umeme wa gesi megawatt kama 1198 hivi, lakini tuna umeme wa mafuta kama megawatt 94.58. Tuna Tungamotaka megawatt 10.5, huu ambao uko gridi karibu megawatt 38, ukiangalia unaona karibu megawatt karibu 1.9 hii storage capacity.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa hivi ukienda kuangalia wanachozalisha watu wa umeme, ni asilimia 50 ya hiyo. Maana yake kwenye Mpango huu tunahitaji kuweka fedha ili hiyo mitambo iliyosimama ikafanye kazi, viwanda vyetu vitembee. Wanasema wameona kabisa maximum demand, yaani umeme wa juu unaotumika kwenye nchi hii kwa Mwezi Agosti, ni megawati 1800. Ukienda kwenye ukweli, tukiwasha migodi yote, tukawasha kwa wananchi wote ambao tumewawekea umeme tutahitaji karibu megawati 5000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaponhgeze kwamba Bwawa la Nyerere litaingia hivi karibuni. Lakini pamoja na kuingia kwa Bwawa la Nyerere, sisi tumesema malengo yetu tunahitaji megawati 10000 kwa ajili ya nchi hii kuanza kuyaona maendeleo. Niombe sana mipango yetu ya umeme iendelee kuwepo na hawa wapewe fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ripoti hii utagundua kwamba, mauzo yetu ya nje ya madini mwaka 2022 yalitoka dola bilioni 3.1 mpaka dola bilioni 3.4. Vilevile, ikaonekana kwenye mauzo ya nje, madini wamefanya vizuri kwa asilimia 56 kwenye mauzo yote ya nje. Kwa hiyo, nilitegemea hapa kwenye madini twende kuhakikisha kwamba tunaingiza fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko vision ya Mheshimiwa Waziri 2030, inayosema kwamba madini ni utajiri lakini vilevile inaonesha kwamba itatuletea ajira za kutosha. Hii vision aliyoisema inahitaji kuingiza utafiti GST unaoitwa High Resolution Airborne Geophysical Survey ambao haujafanyika kwenye nchi hii. Umefanyika kwa asilimia 16 tu. Kwa hiyo, tunategemea kwenda asilimia 50. Niwaombe sana kwenye hili kwamba, huu utafiti upewe fedha na hii ifanyike ili twende kwenye asilimia 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukajua kwenye asilimia 16 tumepata dola bilioni 3.4. Je, tukifanya asilimia 50? Kama tumekwishaona haya mafanikio, basi haya mafanikio tuyaongezee nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme, kule kwangu wanachimba madini. Maeneo yote yanayoleta haya madini, barabara zake ni mbovu. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri anayeshughulika na barabara (ujenzi wa miundombinu), katika nafasi hii tuliyonayo sasa ya kutoa mapendekezo kwenye hili, zile barabara zijengwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeisema sana barabara ya kutoka Geita kwenda Kahama, inapita kwenye migodi katika majimbo matatu. Hawa watu wanabeba Carbon, hawa watu wanabeba magogo, hawa watu wanabeba selenide, ili waongeze kwenda na kurudi kwa urahisi ni lazima watengenezewe barabara ili wazalishe mara tatu ya hiki ambacho leo tunakiona leo. Kama hatutafanya hivyo maana yake uzalishaji wetu hautapanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara inatoka pale kwangu Katoro kuelekea Jimbo la Bukombe, linapita kwenye migodi zaidi ya sita hadi saba. Niombe sana barabara hii itengenezwe. Haitengenezwi kwa ajili ya kuwafurahisha wale watu. Inatengenezwa ili iweze kuwafanya wale watu wafanye kazi zao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kilimo, mwaka 2022 tumetenga zaidi ya bilioni mia tisa tisini na kitu lakini tunaona kabisa sekta ya kilimo cha umwagiliaji imekwenda kutoka hekta 300 mpaka hekta 800. Lengo letu ilikuwa ni hekta milioni 1.2 bado kuna 400 bado hatujaifikia kwa miaka hii mitano. Niwaombe sana kwenye utekelezaji wa bajeti hii, kwenye mapendekezo yangu fedha ipatikane ya kuongeza kwenye eneo hili la umwagiliaji ambalo linaajiri watanzania wengi ili waweze kuchangia pato la Taifa kwa kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ninayotoka mimi kuna Ziwa Victoria lakini maji yake hayajatumika. Yakitumika ninaamini tutazalisha kuliko inavyoonekana leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii katika kilimo hiki hiki ambacho tunakiona kama ni cha mchezo mchezo, inaonekana tulizidi kwa asilimia 124. Kwa hiyo, tulizidi. Maana yake ni kwamba, tukiwawezesha zaidi tutapata hata asilimia 200. Kwa kuwa kilimo ni biashara sasa itatufanya hawa watu wetu watakula na tutauza mazao yetu nje. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana…

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ya uvuvi. Ndugu yangu Jirani hapa Mheshimiwa Mwijage asubuhi alisema kwamba, mpaka sasa uvuvi wa vizimba tuna metric tani 18000, wenzetu wa Uganda wana metric tani 120000. Egypt wana tani milioni moja kama na laki mbili. Nilikuwa nafanya hesabu ya kawaida tu. Leo tukiweka tukawa na metric tani milioni moja, tunauwezo wa kutengeneza trilioni tano kwa mwaka. Trilioni tano hii itakwenda kufanya kazi kubwa, tunaogopa nini kwenye potential kubwa ya uvuvi kuingiza fedha. Tunaogopa ni kwenye potential kubwa ya mifugo kuingiza fedha? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tumaini Magessa, muda wako ulikuwa umekwisha. Naomba tafadhali umalizie.

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)