Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika mpango huu, pia nichukue nafasi hii kupongeza kwa ajili ya mpango huu na nitakuwa na mambo machache ambayo naamini nitachangia na kupata ufafanuzi ili tuweze kwenda vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachangia mpango na hii ndiyo dira ya utendaji wa kazi katika nchi yetu, katika Wizara zote na Idara zote. Kama ambavyo mpango unasema tunaangalia dira ya maendeleo ya Taifa lakini pia tunaangalia mipango mingine iliyopangwa ya muda mrefu lakini tunaangalia mpango uliopita mwaka jana, tunaangalia na Ilani ya CCM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo nilitegemea kama ambavyo Kamati wameeleza kwamba kuna mapungufu ya jumla yaliyotokea kwenye Mpango, ni kitu cha muhimu sana ambacho Mheshimiwa Waziri akisimama atuambie. Tunakwenda kupitisha mpango huu lakini mapungufu yake ya jumla ni kwamba tumemaliza mpango ambao umeisha, hatujaambiwa katika Mpango ule ulioisha kuna ajira ngapi zilitengenezwa kutokana na ile miradi ya maendeleo. Sisi 2025 tunakwenda kwa wananchi waliotupa ridhaa ili tuwaambie yale maelekezo ya CCM tutengeneze ajira 8,000,000 mwaka huu tulitengeneza hizi, mwaka huu tulitengeneza hizi lakini mpango haujaeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda mpango huu una miradi ya maendeleo baadhi yake haijaelezwa bayana na sisi tunakwenda kupitisha kwamba uwe ni mpango wetu ambao unabeba miradi yetu ya maendeleo ambayo haijaelezwa bayana. Tunaomba miradi hiyo Mheshimiwa Waziri ukisimama tupate kwa ubayana wake. Pia hatujaelezwa kinagaubaga mafanikio tunayokwenda kuyapata kwenye huu mpango, akisimama atueleze mafanikio tunayokwenda kuyapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba nne mpango huu kama ambavyo upo sasa, kwa kuwa tumesema mipango yetu sasa hivi tunayopanga iendane na Sensa tuliyoifanya na kuimaliza mwaka jana. Haijatoka ile ripoti yote ya Sensa lakini anagalau tumepata baadhi ya ripoti. Sasa kama walivyosema mzungumzaji Mheshimiwa Mbunge aliyepita Mheshimiwa Ng’wasi tumetumia zaidi ya bilioni 400 kufanya Sensa, yale matokeo ya Sensa yanatakiwa kutusaidia kupanga mipango yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatamani kuona tumeambiwa kwenye Sensa work force ya nchi yetu ambayo tunaitegemea watu wenye umri kati ya miaka 15 – 64 ni asilimia 53.1. lakini ukiangalia katika hao watu asilimia 34.5 ni watu wenye umri kati ya miaka 15 – 35 ambao ni vijana tunabakiza work force ya 18% tu ndiyo wale ambao ni miaka 36 – 64.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, mpango huu ni namna gani umezingatia umri huo wa nguvukazi ya Taifa letu, kuwaweka mipango. Tunakwenda kukopa mkopo wa ndani, sijaelewa mkopo wa ndani ni vipi, tutakopa kwenye mabenki yetu au tunakwenda kukopa kwa wazabuni au tunakwenda kukopaje Waziri atatuambia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya dola 6,000 hizo sijui milioni elfu sita sijui, hlafu nje tunategemea kukopa hizo 2,200 na ngapi. Sasa katika huu mkopo ni namna gani hii workforce ya vijana miaka 15 – 34 tunakwenda kuitumia. Mheshimiwa Waziri umeongea vizuri sana kwenye ripoti yako, kwamba tunatakiwa tuwe na watu wa kutosha na tuwe na watu bora, watu wa kutosha kwa mujibu wa Sensa na ambao ni bora kwa ajili ya workforce hii ni hawa asilimia 34.5 wenye umri kati ya 15 mpaka 34.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoa walioko shule, milioni tano na kidogo, unabaki na watu karibu 16,000 ambao ni vijana. Hao wengi wao ni wale ambao wameajiriwa kwenye Machinga, boda boda, bajaji, kilimo na ufugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti inaeleza vizuri sana kwamba Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 62 kupitia NFRA na CPB kununua mazao ya wakulima. Nilitamani Waziri wa Kilimo angekuwa hapa, naye kama akipata fursa atuambie ni kwa nini fedha wamepewa za kutosha lakini bado kuna malalamiko kwamba wakulima hawajalipwa mazao yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Iringa wameuza mahindi NFRA na wameuza CPB lakini hawajalipwa fedha zao. Tatizo liko wapi? Kwa sababu hii ndiyo workforce ambayo tunaitegemea kwa mujibu wa sensa. Sasa ile mipango ambayo tumesema, kwa mfano, vijana, tuwe na programme kabisa ya kuchakachua kuona kwamba tuna programme gani? Tuache ile 4:4:2 peke yake, kwa sababu workforce kubwa ukiangalia kwenye Taarifa ya CAG, wanaopewa ile mikopo wengi ni akina mama, ndio waliopewa zaidi ya asilimia 50 lakini vijana wamepunjwa na watu wenye ulemavu wamepewa kidogo. Kwa hiyo, hii workforce bado tunai-neglect na kuiacha nje wakati hii ndio nguvu ya Taifa ambayo tunategemea ibadilishe uchumi wetu, tuwe na huo uchumi shindanishi ambao tumeuandika kwenye mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii nguvu ya kuchochea tunaiwekea mpango gani? Tuache ile kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu ilipewa shilingi bilioni moja ikakosa vijana wa kukopa, wakakopesha tu shilingi milioni 200 tu, shilingi milioni 800 sijui ikaenda wapi; tuwe na mpango madhubuti kabisa. Leo hii tunapoongelea hiyo workforce, vijana wengine, nimewatoa wale milioni tano ambao ni wale walioko sekondari, form one mpaka six, lakini tuna vijana wako vyuo vikuu. Hawa ni workforce ambao tunategemea baada ya miaka miwili, mitatu wana-mature wanaingia sokoni. Mpaka sasa hivi tunavyoongea, wako foleni wameandikiwa kupewa mikopo lakini hawajapewa na masomo hayajaanza tunaingia Novemba, Desemba, muhula unaisha. Bodi ya Mikopo hawajatoa. Hawa ndio watu tunaowaongelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namna gani mpango huu uta-accommodate hii workforce ya nchi yetu ili kutusaidia ku-push uchumi wetu? Hii mikopo tunayosema tunaomba ya ndani zaidi, nataka kujua, kwa sababu kama tutaendelea kuwa-drain watu wetu, wazabuni wetu na kuwakopa, ku-drain benki zetu, Serikali ikawekeza nguvu kubwa kukopa huko kwenye benki, halafu wakija sekta binafsi ambayo wewe kwenye mpango wako unasema tuna nia ya kuinua sekta binafsi, kuwaboreshea waweze kuwekeza na kuacha zile shughuli nyingine ambazo Serikali inafanya zinazoweza kufanywa na sekta binafsi, sasa Serikali tuki-drain kwa kwenda kukopa kule na kutowaachia wawekezaji binafsi hiyo fursa, bado tutakuwa tumechukua fedha mfuko huu, tumehamishia mfuko huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungetamani fedha kubwa na ajira nyingi zijengwe na sekta binafsi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, ukisimama naomba utuambie, hiyo ndio workforce tuliyonayo? Ndiyo mashine yetu, ndiyo kiwanda chetu cha kuzalisha na kuinua uchumi wetu. Hawa vijana tunawawekea mpango gani kabambe? Tukiachana na miundombinu, tunawawekea mpango gani kabambe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna mpango wa kusema, sasa katika hii fedha, sijui ni shilingi trilioni tatu au ngapi tutakayochukua, hatuna mpango wa kusema hizi shilingi bilioni 500, hebu sasa tukakopeshe kwenye sound organisation za vijana wetu wanaofanya biashara ndogo ndogo ili watulipe kodi, lakini uchumi utakuwa umefunguka, kama ambavyo tulikuwa tunasema mabilioni ya mama. Tulivyo-inject shilingi milioni 1.3, tayari nchi yote ilikuwa inatetemeka kwamba kuna mabilioni ya Mama Samia yameenea nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tutafute fedha ambayo tutakwenda ku-inject kwa vijana, Machinga. Tutafute namna ya ku-inject kwa bodaboda au bajaji tukaziweke biashara zao kuwa rasmi, wasimame kutoa ajira. Sasa hivi tuna vijana wengi wame-graduate wanafanya vizuri kwenye kilimo cha irrigation. Hata ukija kwangu Mkalama wamenitengenezea, kila mwezi nauza nyanya hapo kwa zaidi ya shilingi milioni mbili au tatu. Wametengeneza vijana wadogo tu wa kutoka SUA. Tukiwawezesha hawa katika kila wanachokifanya, tukakiboresha kuwe cha kisasa, tukawatafutia masoko na kuwa-connect kwenye masoko nje ya nchi, tunaondokana na umaskini kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, naomba ili tuendane na sensa sawasawa, utakaposimama uje utujibu haya, miradi hiyo ni miradi gani? Iwe bayana; ajira ngapi utakwenda kutengeneza? Mwaka jana ngapi tumezitengeneza? Manufaa gani tunakwenda kuyapata kupitia Mpango huu?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)