Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nami nianze na pongezi, kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha uanzishwaji wa Tume ya Mipango chini ya Ofisi yake. Pili, uwasilishwaji uliofanywa na Mawaziri; Waziri wa Mipango na Waziri wa Fedha, umekuwa mzuri na wenye weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapendekezo ya Mpango yaliyowasilishwa yamezingatia mambo mawili muhimu. Kwanza, yamezingatia hali ya uchumi wa dunia ambayo imeanza kuimarika kwa sasa hivi baada ya janga la UVIKO; vile vile, yamezingatia hali inayoridhisha ambayo tunaendelea nayo hapa nchini (hali ya ukuaji wa uchumi wa Taifa), ambayo imekuwa bora zaidi hata kuzidi baadhi ya mataifa jirani. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa hatua hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati anajiandaa kuwasililisha vipaumbele, Waziri amezungumzia pia mambo mawili makuu. Jambo la kwanza amezungumzia ni shabaha kuu, akasema shabaha kuu ni kuchochea uchumi jumuishi unaolenga kupunguza umaskini, kuzalisha ajira, kutengeneza utajiri na kuongeza mauzo ya bidhaa nje ambazo zimeongezewa thamani. Jambo la pili, akazungumzia msukumo ili kufikia mafanikio hayo yanayolengwa, kwamba msukumo utakuwa ni kuongeza tija ya uzalishaji, kuongeza thamani ya ambazo kabla hayajauzwa nje, ambayo hii ni kazi ya sekta binafsi. Hayo ni mambo mawili. Halafu jambo la tatu akasema ni kuongeza uwekezaji wa Serikali kwenye sekta za elimu, TEHAMA na huduma za jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina tatizo na shabaha, lakini nauona msukumo kama umezingatia supply side zaidi kuliko kuzingatia demand side. Tungeweza kujenga vizuri msukumo na hivyo kujenga msingi wa vipaumbele kwa kuangalia demand side. Kama tunalenga kuchochea uwekezaji, lazima tujiulize maswali kama matano hivi. Wawekezaji wanahitaji nini? Kwenye maeneo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nilijaribu kujiuliza kwa niaba ya Serikali; swali la kwanza, wawekezaji wanahitaji nini? Nikajipa majibu kama matano hivi. La kwanza, nikapata kwamba wawekezaji wanahitaji kuwe na gharama nafuu kwenye sekta ya usafiri na usafirishaji. Kusafirisha nini? Kusafirisha malighafi kutoka zinakozalishwa, kuja viwandani na baadaye kusafirisha bidhaa kutoka viwandani kwenda kwenye soko. Wanahitaji gharama nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama wanahitaji gharama nafuu, Serikali ijielekeze kuwekeza wapi? Lazima ijielekeze kuwekeza kwenye sekta za miundombinu zinazohudumia usafiri na usafirishaji. Kwa hiyo, hicho nikakipa kipaumbele cha kwanza. Lazima Serikali iendelee kuwekeza kwenye Barabara zinazopitika katika kipindi chote cha mwaka, lazima Serikali iendelee kuwekeza kwenye bandari na bandari zetu za Dar es Salaam, Bagamoyo, Tanga, Mtwara, Bandari za Maziwa kama Mwanza, Kigoma na kadhalika. Vile vile, viwanja vya ndege, madaraja makubwa, vivuko na mawasiliano (TEHAMA). Kwa hiyo, ni kipaumbele cha kwanza ni miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wawekezaji wanahitaji kuwe na gharama nafuu za uendeshaji wa mitambo inayotumika kwenye uzalishaji, usafiri na usafirishaji. Kwa hiyo, Serikali kama kipaumbele cha pili lazima iendelee kuwekeza kwenye sekta ya nishati. Vyanzo vya uzalishaji wa umeme, mitambo ya kupooza umeme na kuimarisha njia za usambazaji wa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kwenye hili ni kuimarisha uthibiti wa bidhaa za mafuta tangu zinapoagizwa kutoka nje mpaka zinaposambazwa hapa nchini. Vilevile, ni muhimu sana kuendeleza utafiti wa mafuta. Kwa hiyo, hivyo ni vipaumbele ndani ya vipaumbele. Tatu, kuendeleza miradi ya kuzalisha miradi ya kuzalisha na kusambaza gesi asilia. Kwa hiyo, kipaombele cha pili kilikuwa ni nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele cha tatu kutokana na swali, wawekezaji wanahitaji upatikanaji wa uhakika wa malighafi wanazohitaji viwandani muda wote wa mwaka. Viwanda vingi wawekezaji wana kilio, hasa viwanda vya kuzalisha mafuta hata alizet; unakuta supply ya alizeti inapatikana viwandani kwa muda wa miezi mitatu au minne. Kwa hiyo, viwanda vinakuwa vinasimama miezi saba, miezi nane havizalishi. Kwa hiyo, kunahitaji msukumo wa Serikali kuwekeza kuisaidia sekta ya kilimo kuzalisha zaidi malighafi viwandani. Sasa hii ingekuwa ni kipaumbele cha tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele cha nne, wawekezaji wanahitaji upatikanaji wa nguvu kazi nyingi na ya kutosha na ya gharama nafuu. Kuna baadhi ya viwanda hapa nchini vinalazimika lazima kuajiri watu kutoka nje kwa ajili ya viwanda vyao. Kwa mfano, viwanda vya sekta ya Ngozi na viwanda vya sekta ya maziwa. Ukienda VETA yoyote ile hakuna watalamu wanazalishwa pale. Hamna! Kwa hiyo, lazima sekta ya elimu, tunaipa maua yake kwa kuwekeza kwenye VETA kila mkoa, VETA kila wilaya lakini lazima waangalie mitaala, ni watu gani wanazalishwa ili waende wakatumike kwenye sekta za uzalishaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine, wawekezaji wanahitaji huduma za Serikali. Kwa hiyo, lazima Serikali iendelee kuwekeza kwenye huduma za afya ili wafanyakazi kwenye sekta wanakoajiriwa wawe na afya nzuri. Serikali lazima iendelee kuwekeza kwenye huduma za maji, ulinzi na usalama na huduma nyingine. Kwa hiyo, hicho kingekuwa kipaumbele cha tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili vipaumbele vyote hivyo vitekelezwe vizuri, lazima kama nchi kuwe na mfuatano (sequencing) ambao unazingatia mahitaji ya hali halisi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, najua hiyo ni kengele ya kwanza hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima Serikali izingatie mahitaji ya sasa. Nimejaribu sana kupitia mifano. Kwa mfano tuna shehena kubwa sana ya chuma kule Liganga imelala chini, hatujaanza hata kuitumia, lakini ni mwaka uliopita 2022 Serikali imewekeza kujenga foundry ya kuyeyusha chuma katika Kiwanda cha KMTC kule Moshi. Kwanza tu hata ujenzi wa KMTC kule Moshi na ujenzi wa Mang’ula yote yalikuwa ni makosa. Kama Mang’ula na KMTC ingejengwa kiwanda kimoja tu maeneo ya Iringa au Njombe, ina maana tungetoa chuma pale chini tukakiyeyusha tukatengeneza pulley kule kule kwenye eneo la kupatikana chuma badala ya chuma kipatikane Mchuchuma na Liganga halafu usafirishe kilomita 800 kwenda kuyeyusha kule KMTC ni uwekezaji ambao hauna tija katika nchi. Ni muhimu sana kuangalia mambo kama hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa pili, miaka ya 1970, Serikali ilianzisha Mashirika kama TIRDO, TEMDO na SIDO. Lengo kubwa lilikuwa ni kusaidia uendeshaji wa viwanda vya Serikali wakati huo ambavyo vyote tumeshaviuza. Hivi kwa nini haifanyiki tathmini ya mahitaji ya mashirika hayo? Je, katika mazingira ya sasa yatakuwaje na tija katika uchumi wa nchi? Sijaona kwenye mpango, lakini nilikuwa nafikiri kwamba kuna baadhi ya mashirika yanahitaji kuunganishwa na kuna baadhi ya Mashirika yanahitaji kujiunda upya. Kuna baadhi ya Mashirika yanahitaji kufa ili kuweza ku-fit kwenye mazingira ya sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa ujumla naunga mkono Mpango, isipokuwa tu maboresho hayo machache yafanyike. Sina matatizo na malengo ya ukuaji wa uchumi, ni mazuri, malengo ya Mpango ni mazuri, nguvo kumi za utekelezaji ni nzuri, tuboreshe mpangilio wa vipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)