Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Antipas Zeno Mgungusi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi. Nina masuala kadhaa hapa ya kuchangia, kwanza ni migogoro ya ardhi baina yetu wananchi wa Bonde la Kilombero na Wizara, lakini suala la biashara ya viumbepori hai ambayo imesitishwa, suala la kutaka Jeshi la Uhifadhi li-retain mapato yake, pia ukamilifu wa Jeshi la Uhifadhi na mwisho masuala ya wastaafu kama muda utaniruhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe shukrani kwa Serikali, hasa kwa Mheshimiwa Rais kwa kuunganisha barabara yetu ya Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Ruvuma kwa lami ambapo kwa sasa haipitiki. Tumetajwa kwenye mpango kupitia Mpango wa EPC + F. Natoa shukrani sana kwa hilo kwa niaba ya wenzangu wa Ruvuma na wa Malinyi, pia kuna suala la vifo vya wananchi na usumbufu kwenye mazao kutokana na tembo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipiga kelele na mwezi huu nadhani mlisikia wananchi watatu wa Malinyi walipoteza maisha kutokana na ajali ya tembo, lakini bahati nzuri Wizara imeridhia wametuweka kwenye mpango tutapata kituo cha kudumu cha Askari Wanyamapori kule Kilosa kwa Mpepo. Kwa hiyo, kwa hayo natoa shukrani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mhifadhi Mstaafu. Nimehudumu Wizara ya Maliasili na Utalii miaka kadhaa, nikahudumu katika Jeshi la Uhifadhi kama Afisa Askari miaka kadhaa, katika maisha yangu yote niliapa kwamba, sitakubali kushiriki kuharibu uhifadhi kwa sababu ya umashuhuri wa kisiasa, huu ndiyo msimamo wangu mpaka sasa hivi. Tofauti napishana na wenzangu jambo dogo tu, kwa maana ya wahifadhi wenzangu wa maliasili na wale mabwana Waheshimiwa Mawaziri Nane ambao walikuwa assigned ku-solve migogoro ya nchi hii. Shida yao kubwa ninayopishana nao ni approach, namna gani wana-enenda katika suala la ku-solve migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwangu katika Bonde la Kilombero kwa maana ya Wilaya ya Malinyi na majirani Mlimba, Ulanga na Kilombero tuna migogoro na Wizara kwa namna mbili. Kwanza kuna Kijiji kinaitwa Ngombo kule kwangu Malinyi, wananchi wanaishi pale tangu mwaka 1935, thelathini na kitu mpaka leo, lakini pia lile bonde limekuwa hifadhi mwaka 1952, iliwekwa GN. 107 na wakoloni tangu kipindi kile mpaka leo Wizara ime-maintain.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi hatuna tatizo. Nafahamu kulingana na uhifadhi eneo lolote likionekana ni nyeti kuna haja ya kuhifadhiwa, Serikali inaamua inafuata utaratibu na inakuwa hifadhi. Kama kuna wananchi, wanapisha, ndiyo utaratibu. Kwa hiyo, nilitarajia watu wa maliasili na Mawaziri Nane walipaswa kusema tunatambua Kijiji cha Ngombo ambacho kimesajiliwa na Serikali, wananchi wanaishi miaka hiyo kabla hata uhifadhi pale kuanza. Tunafikiria kuna haja ya watu kutolewa kwa sababu ya mradi wetu wa Stigler’s Gorge na vitu vya namna hiyo kama kuna haja. Wangetusikiliza, tusikilizane nao, pengine tusingeweza kubisha. Watu wa maliasili mara zote wamekuwa wakiimba hata wakijibu maswali yangu hapa walikuwa wanasema wananchi wamevamia kule Ngombo, wamefanya maisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nawauliza walivamia mwaka gani? Ukisema umevamia lazima uwe specific utaje mwaka gani wamevamia? Hawakuweza kutaja na mpaka kesho hawataweza kwa sababu wananchi wameanza kuishi kabla ya uhifadhi. Kwa hiyo, sisi hatuna shida sana na hilo, nilikuwa nasema suala la approach.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekubaliana Mawaziri Nane wamekuwa assigned, wakati tunawasubiri wao wafanye maamuzi ya mwisho kuhusu Kijiji chetu cha Ngombo, wananchi waendelee na Maisha, watakapoamua tutachukua kile ambacho Serikali itasema, lakini mpaka sasa maamuzi hayajatoka, wananchi kule tunalima kwa kubahatisha, Askari Wanyamapori wa TAWA kila mara wamekuwa wakiingia kufanya doria. Watu wanaishi kuna nyumba, kuna shule, kuna kila kitu, tunaendelea kuishi mpaka leo, wananchi zaidi ya Elfu Nne.

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa, Mheshimiwa Naibu Waziri.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa ambaye amemaliza kuzungumza sasa kwamba, ni kweli kuna Kamati ya Mawazi Nane ambao wamezunguka, lakini Kijiji cha Ngombo hakiko kwenye hifadhi ambayo watumishi wa TAWA wanasimamia mapori. Pori ambalo linasimamiwa na watumishi wa TAWA ni Pori la Kilombero. Kijiji cha Ngombo kiko mbali kidogo na Pori la Kilombero. Kwa hiyo, haya maamuzi siyo kwamba ni ya uhifadhi wa maliasili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa tu mzungumzaji kwamba, maamuzi ya Baraza la Mawaziri hayakuangalia pori hili kwamba linasimamiwa na watu wa Maliasili, isipokuwa vyanzo vya maji viliangaliwa kwenye eneo ambalo ni kijiko au bakuli ambalo eneo hilo Kijiji cha Ngombo kiko ndani yake. Tuliangalia hilo kwamba, eneo hili ni mahsusi kwa ajili ya mchango mkubwa wa maji ambayo yanatiririka kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Antipas.

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri Mary Masanja ninaheshimiana nae, ninajisikia vibaya kumsema vibaya kwa hiyo, ninamsitiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi Kijiji cha Ngombo hata ukichukua ramani mpaka leo wanakijadili kwenye Pori Tengefu la Kilombero kipo katikati ndiyo ukweli wake, kipo katikati. Kama hafahamu, nadhani anafahamu, wanaruka na ndege mara nyingi kipo katikati, aidha hakumbuki au pengine hafahamu au anajisahaulisha, sitaki kumsema vibaya. Namsitiri, naomba nisizungumze juu ya hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliomba na mimi niliomba Kijiji chetu cha Ngombo kulingana na unyeti wake kama kinataka kitolewe it is ok, pengine tunaweza tukaridhia, niliomba tupunguze hata ukubwa wa Kijiji tuko radhi tubki eneo letu la asili dogo, watu waendelee kuishi, watu wanaishi pale miaka mingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnamfahamu Waziri Juma Ngasongwa kazaliwa mwaka 1941 katika Kijiji cha Ngombo, kasoma shule ya msingi pale Ngombo, Shule ya Msingi ipo kabla ya mwaka 1950, wao wanasema wananchi tumevamia! Mzee wangu Mzee Zeno Mgungusi Mhifadhi, kazaliwa Ngombo, kasoma shule ya msingi pale kabla ya uhifadhi. Hawa wanaendelea kusema tumevamia, siyo sahihi! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi niliomba, sibishani na Serikali, nimeomba tuko radhi kupunguza ukubwa wa Kijiji sehemu nyingine iwe hifadhi, sehemu ndogo ibaki tuendelee kuishi. Kama mnafahamu kabila linaitwa Wandamba akina sisi, akina Joti, akina Ngasongwa, akina Beno Ndulu wote asili yatu ni Ngombo. Tuko radhi tupunguze ukubwa wa Kijiji libaki eneo dogo tuweze kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukisema tusifanye kilimo kikubwa cha matrekta na kadhalika tuko radhi, nilisema …

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Antipasi lakini bila maji vilevile hamtaweza kuishi.

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, naam.

NAIBU SPIKA: Bila maji hamtaweza kuishi. Maji alikuwa anazungumzia Mheshimiwa Waziri hifadhi, bila maji hamtaweza kuishi. Wewe endelea na mchango.

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, sawa, ninalifahamu hilo ndiyo maana nimetoa mapendekezo. Tulikuwa tunaomba tuko radhi kupunguza idadi ya mifugo hata kwa asilimia 90, tupunguze ukubwa wa Kijiji hata kwa asilimia ngapi, nilitoa maombi nilikuwa natarajia Serikali ikubali, lakini hata kama ikikataa sina tatizo, basi wafanye maamuzi kwa wakati. Kama wanasema hatusikilizi mawazo ya Mbunge tunataka watu watoe it is ok, waseme hata kesho, mimi kama Mbunge nitatoa ushirikiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wanashindwa kuamua kila siku tunaviziana, tunaviziana. Mpaka sasa hivi ninavyokuambia watu wamekamatwa kule wananyang’anywa mchele, wananyang’anywa mpunga, watu wanaishi mpaka leo. Toeni tamko kwamba watu waondoke, tunaondoka, sasa hamsemi. Kila siku mnasema Mawaziri Nane wanakuja kesho, Bunge lijalo, kesho, Mimi Mbunge nifanye nini? Tukisema mtaanza kusema Mbunge mkorofi anaonea Serikali, sasa mimi nitakuwa Mbunge wa namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatakiwa iwe serious, wafanye maamuzi, kama mnataka mtutoe basi isemwe hata kesho, mimi kama Mbunge sitabisha, nitawaambia watu wangu, tutatoa ushirikiano wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili mgogoro huo ni mpaka. Kuna mpaka wa mwaka 2012 wa hilo Bonde la Kilombero lote, Majimbo Manne ya uchaguzi. Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) ilisema ili bonde liwe salama mpaka ukae hapa na tukaweka mpaka 2012. Wananchi tumeshirikishwa, tumeridhia, hatuna shida, lakini 2017 ukaja mpaka mwingine kuja kuchomekwa, wamekuja watu wa maliasili wameweka beacon mpaka ambao mpaka leo hauna GN, lakini mpaka leo kuna watu wamewakamata wamepewa kesi za uhujumu uchumi, wapo ndani ya hifadhi, lakini kwenye mpaka ambao hauna GN.

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo nalo mimi silibishii, wakisema na huko tuache kulima tutaacha, nitawaambia watu wangu, lakini Serikali watamke wanapochelewa kufanya maamuzi maana yake wanatuweka sisi kwenye wakati mgumu. Mnataka sisi tunyamaze, sasa mimi nitakuwa Mbunge wa namna gani? Tukisema mnasema tunaionea Serikali, mnataka tufanyeje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siasa zetu zinakuwa ngumu, wenzetu Mawaziri Nane watusaidie. Ninajua muda mwingine tunagombana na watu wa maliasili, watu wa TAWA, TANAPA, wanaonewa, lakini nadhani asilimia kubwa ni wale Mawaziri Nane ndiyo tatizo. Huu ni mwaka wa Sita tangu Tume imeundwa! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kituko kingine hawa Mawaziri Nane hawajawahi kukanyaga Malinyi, hawajawahi kufika hata pale Mlimba, wanaruka na ndege tu juu Kilombero wanaondoka, hawajawahi kufika, lakini pamoja na hayo mimi sijali sana, fanyeni maamuzi sitabisha. Msitutafutie lawama tuonekane wajeuri naomba mfanye maamuzi tutazingatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo, suala la pili ni suala la Mheshimiwa Waziri wa Fedha anahangaika kutafuta vyanzo vipya vya mapato fedha zipo Maliasili. Kuna biashara ya viumbehai pori kwa maana ya wadudu, kusafirisha wadudu nje ya nchi, hawa panzi mnawajua, kumbikumbi, sijui vinyongana kadhalika. Biashara hii ilikuwa inafanyika tangu uhuru Mwalimu Nyerere anaifahamu, walikuwa wanafanya Wazungu, badaye Shirika la TAWICO likapewa kazi ya kusafirisha wadudu nje ya nchi. Mwalimu Nyerere akazuia akasema wazawa wafanye hii kazi mwaka 1967 mpaka leo Watanzania walikuwa wanafanya biashara ya kukamata wadudu wanapeleka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii ilizuia mwaka 2016, Machi 2017, Waziri Maghembe alitoa sitisho hawa wadudu wasipelekwe nje ya nchi tena, nadhani ilikuwa kwa miaka mitatu, lakini mpaka leo mwaka wa sita, wale wafanyabiashara walishalipia kila kitu, wamelipa leseni, wamelipa kodi, wametumia gharama zote, tangazo limetolewa ghafla la kusitisha na tangazo lenyewe nadhani halikuwa kisheria, wale wafanyabiashara wamepata hasara zaidi ya Bilioni 1.6 Serikali haijawarejeshea.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo wakisema waende hata Mahakamani ni kesi nyepesi, mnaitia hasara Serikali, kwa nini? Wanasheria huko maliasili wapo, mnashindwaje kuishauri Serikali ama wawalipe fidia, lakini wenyewe wanazungumza hawana haja sana ya fidia wanachotaka wafungue biashara iendelee?

Mheshimiwa Naibu Spika, pengine najua kuna hofu, wengine wanasema wadudu wetu wanasafirishwa nje ya nchi, kule Wazungu watawazalisha watakuwa wengi, wakiwa wengi wadudu Wazungu hawatakuja kutalii Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa wale wadudu hawakamatwi hifadhini wanakamatwa mitaani, pili mnafahamu Wizara ya Kilimo inatenga bajeti, dawa ya kuuwa wadudu…

NAIBU SPIKA: Ahsante, kengele ya pili hiyo. Malizia sekunde kumi, ahsante.

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, aah, umeniongezea.

NAIBU SPIKA: Eeh, sekunde kumi.

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, hawa wadudu bajeti wanatenga Wizara ya Kilimo kuua ndege kweleakwelea, kuuwa viwavidudu, wale sijui viwavi jeshi na kadhalika, ambao wanaathiri mashamba ya watu. Wale wadudu ni deal watu wanawahitaji, wanakamatwa mtaani wanapelekwa nje tunapata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hatupati fedha, tunatumia fedha kuwauwa wadudu ambao wanatakiwa kule Ulaya, kama kulikuwa na kutokuwa na uadilifu kwa wafanyabiashara au watendaji haipaswi kuwa kisingizio. Kwa hiyo, ninaomba Serikali ifungulie biashara ya viumbepori hai tuweze kupata fedha za kigeni tupate mapato. (Makofi)