Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Bahati Khamis Kombo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaali kunipa uzima na kuweza kusimama mbele ya Bunge letu kuweza kuchangia bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, niendelee kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha kwamba analeta maendeleo katika nchi yetu. Nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha pamoja na timu yao yote kwa kutuletea bajeti hii ambayo imemgusa kila Mtanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja katika Sekta ya Ujenzi na Uchukuzi. Pia niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Nitakwenda katika meli yetu ya MV Mwanza Hapa Kazi tu. Meli hii pamoja na changamoto zilizopo, tuwapongeze sana vijana wetu wazawa ambao wameshiriki katika ujenzi wa meli hii. Kwa kweli vijana hawa wamefanya kazi kubwa na ni vijana wa mfano. Naomba tu Serikali itakapomaliza meli hii, basi nao waweze kupatiwa ajira kwa wale ambao wanaweza kufanya kazi katika meli ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niende moja kwa moja katika Sekta ya Kilimo. Naomba nisome kidogo maelezo ya Mheshimiwa Waziri, ameeleza kwamba, Tanzania ni aibu kulia kwa shida ya ngano au mafuta ya kula, kwani tunayo fursa ya kulisha Afrika, Ulaya, Asia katika baadhi ya mazao. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuliona hili. Kama Tanzania kweli tunaweza, na tunaweza kwa kila upande. Hata kule Zanzibar kwa upande wa Pemba sasa hivi tunapata tender kubwa sana kwa ndizi zetu za mkono wa tembo au kwa jina jingine mkono mmoja. Hili ni soko kubwa na tunaiomba Serikali wale wakulima waweze kupatiwa mikopo ya uhakika. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni soko kubwa na tunaiomba Serikali wale wakulima waweze kupatiwa mikopo ya uhakika. Vilevile nije katika zao letu la alizeti, niiombe Serikali kupitia Mfuko wa TASAF kule Zanzibar, wananchi waweze kuelekezwa juu ya kilimo hiki cha alizeti, bado Zanzibar hatujawa na utaalam wa kulima alizeti. Kipindi ambacho Waziri wa Kilimo wa Tanzania Bara na Waziri wa Kilimo wa Zanzibar watapeana ushauri wa kusaidiana, basi naamini kwamba tatizo hili la mafuta litaondoka Tanzania nzima. Nije moja kwa moja katika sekta ya elimu, tunavyo vyuo vikuu vingi hapa Tanzania Bara, lakini kule Zanzibar tunakosa matawi yake. Tunaiomba Serikali vile vyuo ambavyo kule Zanzibar hatuna matawi yake basi tuweze kupatiwa matawi, ili wale wanafunzi ambao wanahitaji kuomba nafasi zile za kusoma wasipate ule usumbufu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naamini kwamba sekta ya elimu ya vyuo vikuu ni sekta ya Muungano, niiombe tu Serikali kwa upande wa Pemba, tuweze kujengewa chuo kimoja kikuu ili iwe urahisi kwa wananchi ambao wako kule kupata ile elimu. Pia, tutapata fursa nzuri ya watoto wetu ambao wako Mwanza, wako Kigoma kuja kusoma kule Pemba. Hii pia itasaidia na wao kuijua nchi yao lakini pia wataiona kwamba Pemba kweli inanukia marashi ya karafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)