Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa napenda nitoe shukrani zangu za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya. Bajeti ya mwaka 2021 Wabunge wengi sana alituvisha nguo katika Majimbo yetu. Miradi mingi ya maendeleo imefanyika na hilo halina ubishi kabisa, kila Mbunge aliyekuwa hapa katika Jimbo lake, basi kuna kikubwa ambacho amekipata kutokana na bajeti ya mwaka uliopita. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, napenda kumpongeza na kumshukuru Waziri wa Fedha kwa kazi kubwa anayoifanya na pia napenda kumpongeza Naibu wake Bwana Hassan Chande, Katibu Mkuu pamoja na viongozi wote wa Wizara, wamejitahidi sana. Bajeti ya mwaka huu ni bajeti ya mfano ambayo inakwenda kuwaweka Watanzania katika hali nzuri ya maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka niuelekeze mchango wangu katika Sekta ya Nishati. Nchi imefunguka, Serikali inataka mapato, lakini mpaka leo bado tuna tatizo kubwa sana katika nchi la Nishati ya umeme. Umeme wetu bado haukidhi vigezo au viwango katika uzalishaji ambao unahitajika katika nchi yetu. Kwa mfano, viwanda vingi sasa hivi vinazalisha lakini unapokatika umeme kunakuwa na tatizo, production ikisimama, mpaka itakapoanza upya ni hasara kubwa ambayo wanaipata wazalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanalipa umeme bei kubwa sana na matokeo yake wanashindwa kulipa kodi inayopaswa kwa Serikali. Kwa hiyo, naiomba Serikali katika Bajeti ya mwaka huu iangalie sana katika suala zima la nishati ya umeme ili kuboresha viwanda vyetu na hatimaye uzalishaji uweze kufanyika katika kiwango kinachotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kuipongeza Serikali ni suala la ongezeko la bajeti ya Kilimo. Serikali imefanya jambo kubwa sana, kutoka Shilingi bilioni 294 hadi kufikia Shilingi bilioni 954, siyo padogo! Ongezeko la karibuni Shilingi bilioni 660 ni hatua kubwa mno imepigwa. Naomba Serikali ihakikishe kwamba hii pesa ambayo wametengewa Wizara ya Kilimo, basi yote iende katika Wizara ya Kilimo ili tuweze kuwa na uzalishaji ulio bora wa chakula pamoja na bidhaa nyingine za kilimo ambazo zitakwenda katika viwanda vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumza ni suala la Bandari zetu. Kumekuwa na changamoto kubwa sana katika Bandari ya Dar es Salaam ambayo kwa sasa hivi imezidiwa. Ukisafiri kama unakwenda Zanzibar utakuta meli zimejazana kule mbele. Kama kilomita chache kutoka Bandarini pale, meli nyingi mno; zaidi ya meli 25 mpaka 30 utaziona zimetia nanga, zinasubiri kwenye kupakua mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la Bandari ya Bagamoyo ambayo kila siku inazungumziwa. Mheshimiwa Waziri katika bajeti yake aliizungumza katika ukurasa wa 47, namnukuu: “Serikali inaendelea na majadiliano na Wawekezaji watakaowekeza katika eneo maalum la uwekezaji la Bagamoyo, hususan katika miradi ya misingi mitatu; Bandari ya Kisasa (Modern Sea Port); sehemu maalum ya kusafirishia na kuhifadhia mizigo (Logistics Park); namba tatu, sehemu ya Mji wa Viwanda (Port Side Industry).

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri umuhimu wa hiyo Bandari unajulikana, kama tunakata Serikali iongeze kipato na ipate pesa, basi ichukue hatua za dharura na za makusudi kabisa kuhakikisha hii Bandari inajengwa haraka. Bandari hii itakapojengwa itaipunguzia mzigo Bandari ya Dar es Salaam na kuiingizia Serikali pesa nyingi za kutosha. Kwani mpaka sasa bado Bandari haifanyi kazi vya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi katika Bandari yangu ya Bagamoyo. Mheshimiwa Waziri, pale kwangu Bagamoyo kuna Bandari. Ile bandari inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa sana, lakini nilikuwa naomba sana hapa Bungeni kwamba pale Bagamoyo imefikia wakati sasa Serikali iangalie uwezekano wa kujenga gati la kupaki zile meli (boat) au majahazi yanayokuja kwa ajili ya kushusha mizigo. Bandari hii inaingiza Shilingi bilioni 27 kwa mwaka, Shilingi bilioni mbili kwa mwezi. Hii siyo hela ndogo. Miundombinu ya Bandari ile ya Bagamoyo imechoka, haiko vizuri, sehemu za kupaki meli hakuna. Kwa hiyo, kidogo kunakuwa na changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tuangalie kwa undani kabisa jinsi gani tunaweza tukairekebisha miundombinu ya Bandari ile ili iweze kuingiza pesa zaidi. Kwa sababu mpaka sasa sehemu kuba sana ya mapato inakwenda katika sehemu tofauti, yaani kuna mianya ya kutorosha mapato. Kuna bandari bubu nyingi, nyingi kule. Hii ni kwa sababu miundombinu ya pale siyo sahihi. Kama kungekuwa na miundombinu sahihi na tukaweka ulinzi katika sehemu za Bagamoyo, nafikiri Bandari hii ingeweza kutuingizia pesa nyingi. Hii Shilingi bilioni 27 kwa mwaka ingekuwa ime-double au ikawa zaidi ya hapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa sana niipongeze Serikali kwa kundoa ada katika elimu ya Kidato cha Tano. Kwa kweli Serikali ya Mama Samia naipongeze sana kwa jambo hili, wamefanya kazi kubwa sana na Mwenyezi Mungu atawalipa kwa hili kwa sababu wazazi wengi wamefurahia jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nataka kuzungumzia kidogo ni suala la utalii na hasa katika upande wa barabara. Pale kwangu Bagamoyo kuna barabara ambayo inaenda Pangani, Tanga, inatokea Makurunge. Ile barabara katika uchumi wa nchi ni muhimu sana, kwa sababu Mbuga ya Wanyama ya Saadan, watalii wote wanapita katika ile barabara. Ile barabara ikinyesha mvua kidogo haipitiki, kwa hiyo, ile Mbuga ya Wanyama ya Saadan ina-cease.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbuga ya Wanyama ya Saadan ni mbuga ambayo watalii wanaipenda. Kwa sababu ni mbuga ambayo unakaa Baharini unamwangalia twiga, unamwangali mnyama yoyote, ukiwa beach. Kwa hiyo, ni mbuga ambayo ni ya pekee kabisa. Tatizo kubwa ni miundombinu. Kwa hiyo hii barabara ya kutoka Makurunge kwenda Saadan ikianza kutengenezwa itahamasisha utalii, na hii Royal Tour ya Mama Samia, ambayo ameanzisha Rais wetu itakuwa na faida kubwa sana. Kwa hiyo, nawaomba mlizingatie hili, kama tunataka kukusanya mapato, tuangalie sehemu ambazo muhimu zitakazotuingizia mapato haraka zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bagamoyo ina vivutio vingi sana vya utalii. Bagamoyo ni sehemu ambayo ina utalii wa asili, utalii wa bahari. Kwa hiyo, narudi pale pale, itakapotengenezwa gati ya speed boat au gati ya kupaki vyombo vya majini, watalii wengi kutoka Zanzibar watakuja Bagamoyo na hivyo Serikali itaongeza kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)