Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Shabani Hamisi Taletale

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. HAMIS S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa nipende kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kile anachokifanya kwenye Jimbo letu la Morogoro Kusini Mashariki na Wilaya yetu ya Morogoro Vijijini kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii unatembea Morogoro Vijijini ukiona kwamba huduma za kiafya zinakuja, huduma za shule pamoja na maji zinakuja. Wiki iliyopita tumepata mradi wa maji wa Morong’anya wa bilioni 24 na vilevile tumepata mradi wa maji wa Mtambarani bilioni nne, nani kama Mama Samia! Mama Samia hajaishia hapo kulitendea haki Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki. Ninavyozungumza hapa ametuletea kituo cha afya kwenye Kata ya Kinole ambacho hatukutegemea kabisa. Na kutokana na zile fedha za UVIKO Mama Samia ametuletea kituo cha afya kwenye Kata ya Mkulazi. Kutoka Kata ya Mkulazi mpaka unakwenda Ngerengere ulikuwa unatembea kilometa 70.4 lakini Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameliona na amatutatulia hilo tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye hoja. Nimpongeze sana kaka yangu Mheshimiwa Waziri Mwigulu na mtani wetu. Kwenye huu mradi wetu wa SGR, ule mradi naamini unaanza mwezi wa kumi treni inatoka Dar es Salaam inakwenda Morogoro. Ni vituo vitano kutoka Dar es Salaam, kituo cha tano ni Ngerengere. Ngerengere ya sasa tofauti na Ngerengere ya zamani. Leo hii kama tunakwenda kupokea kituo cha mwendokasi maana yake mkazi wa Ngerengere anaweza akaenda Dar es Salaam kufanyakazi, akaenda Dodoma kufanyakazi Ngerengere inatanuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuombe kaka yangu Bashungwa, leo hii Ngerengere tuna kituo cha afya ambacho hakina mortuary. Leo hii kama kuna mtu anafariki asubuhi saa moja Ngerengere basi anatakiwa azikwe saa nne, la sivyo maiti itaharibika kwa sababu kituo cha afya hakina mortuary. Kituo hiki cha afya tumekirithi kwa wakoloni. Sasa nakuomba kaka yangu Mheshimiwa Bashungwa, najua hushindwi. Kama umenipa Kituo cha Afya Mkulazi, umenipa Kituo cha Afya Kinole naomba ukatupe Kituo cha Afya Ngerengere linawezekana kwako kaka yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, si tu mortuary leo hii tunasema Kituo cha Afya cha Ngerengere kina changamoto ya mama na mtoto. Kama leo hii mama anakwenda kujifungua kwenye Kituo cha Afya cha Ngerengere yaani hakuna pa kupumzika. Yaani huyu anajifungua huyu mwingine akae amsubirie. Mheshimiwa Bashungwa, nakuomba kaka yangu kwa heshima na taadhima kwa niaba ya Wanakusini Mashariki tunakuomba uitazame Ngerengere kwa ajili ya kile kituo cha afya. Tunaua watu na watu wanateseka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mji unakua lazima uwe na afya lakini vilevile lazima uwe na ulinzi uliotukuka. Kama tunakwenda kwenye Kata ya Ngerengere leo hii tuna kituo cha polisi cha kurithi pia, hatuna kituo cha polisi Kata ya Ngerengere, Kata ambayo tunakwenda kuwa na kituo kikubwa cha mwendokasi. Huu ni mtihani, na mtihani huu ninaamini kabisa wa kuutatua ni wewe Mheshimiwa Mwigulu. Ninakuomba kaka yangu, tunaomba utuletee fedha na sisi wana Ngerengere tupate kituo cha polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilimuona juzi kaka yangu akitamba kuhusu Yanga kuhusu nini lakini pia akazungumzia miradi mikubwa ya Serikali na pia akauzungumzia Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere; naomba nimuelekeze kaka yangu, Bwawa la Mwalimu Nyerere wakati unakwenda kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere lazima upite Bigwa Kisaki. Leo hii katika barabara zetu; tunakushukuru umetupa barabara ya Bigwa Kisaki kilometa 78, lakini haipo kwenye kipaumbele chako. Twende tukailinde Ilani yetu ya Chama Cha Mapundizi Mheshimiwa Mwigulu, twende tukawasaidie, na mje mtusaidie wana Morogoro Kusini Mashariki. Leo kama tunakwenda kulitazama Bwawa la Mwalimu Nyerere mnakwenda kwa kupitia helkopta, wageni wakija wanapanda ndege wanashuka; huu ni mtihani

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna njia ya Bigwa-Kisaki, kilometa 78, na pia kuna njia ya Ubena-Zomozi-Ngerengere-Mvuha. Tukitengeneza hizi njia tunaenda kufika kirahisi kwenye mradi wa kimkakati. Ninakuomba Mheshimiwa Mwigulu, kama unaamini mradi wa kimkakati ni Bwawa la Mwalimu Nyerere weka imani kwamba Bigwa-Kisaki ni njia ya kimkakati, iende ikatengenezwe; tusije tukasema tu tumetangaza kilometa 78 lakini hatuzioni. tunaomba tuione barabara yetu ya Bigwa Kisaki ni mtahani. Nakupongeza sana kwa vile ambavyo unatutazama, lakini nakuomba kwenye hili utupiganie.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi wiki iliyopita niliongea na ndugu yangu, kaka yangu, mtani wangu, Mheshimiwa Bashe; nikasema leo hii sisi wanakusini mashariki tunalima karafuu inawezekana tunachuana na Pemba. Lakini utaratibu wa kupata wateja, utaratibu wa kupata wanunuzi inakuwa ni shida kwa sababu ya barabara ya Bigwa Kisaki. Leo hii hapa Dodoma watu wanakula machungwa, Iringa wanakula machungwa kwa asilimia hamsini yanayotokea Morogoro Kusini Mashariki. Ninakuomba ulisimamie hili suala kwa sababu Kusini Mashariki …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa, mortuary hakuna wasaidie.

MHE. HAMIS S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)