Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuwa miongoni mwa wachangiaji katika Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kuipongeza Serikali ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri bajeti ya mwaka 2021/2022 ambayo Bunge lako Tukufu lilipitisha kwa Jimbo langu la Igalula imekwishafika kwa asilimia 100, hiyo niwapongeze sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya, zimebaki chenji tu kidogo za wahisani sasa sijajua zimekwama katika mlengo gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuipongeza Serikali leo tuko katika Bajeti Kuu ya 2022/2203 ambayo tutakwenda kuitekeleza kuanzia Julai Mosi, mwaka 2022, pamoja na pongezi nzuri lakini mimi nilikuwa kidogo katika Bajeti ya Waziri kuna mambo ambayo nilitaka tuyazungumzie kama wananchi na nchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza kwanza nikupongeze Mheshimiwa Waziri kwa kupunguza tozo ya miamala ya simu ambayo ilikuwa ni changamoto na ilieleta taharuki lakini Mheshimiwa Rais baada ya kusikia kilio cha Watanzania alipunguza hiyo tozo na baadae kwenye bajeti yako hii umeonyesha kuwa utapunguza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka tujue kama Watanzania kwa sababu tulipitisha tunaenda kukamilisha mwaka mmoja, tangu tumeanza kuchangia hizi tozo, trip ya kwanza ulikuja ukatuambia tumekusanya mabilioni ya fedha tukaona kwenye TV, lakini baadae tukaona kimya, sasa tunataka tujue haya makusanyo mpaka leo tulikusanya Shilingi ngapi ili tuwapongeze Watanzania ambao walivumilia maumivu na ninyi baadae mmekuja kuwaondolea kwa sababu ya hali ya kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili mimi nikupongeze pamoja na kuendelea kuwaona Watanzania na kuwapunguzia makali, mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri katika bajeti yako umejikita sana kuwapunguzia mzigo Watanzania lakini umeenda zaidi, ukasema baadhi ya milolongo iwezwe kupunguzwa ili wananchi waweze kupata fursa na tunu na maendeleo ya Serikali yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amesema vizuri wananchi wanasafiri umbali mrefu kwenda kufuata huduma, na hii umeiweka vizuri sana ukasema baadhi ya vitambulisho viweze kutambulika, lakini Mheshimiwa Waziri nikuombe kuna kundi kubwa sana la Machinga na Bodaboda na hapa umeliweka vizuri sana, bodaboda ndio wengi zaidi katika maeneo yetu ya vijijini, sasa mimi nashindwa kuelewa, anayeendesha lori leseni yake ni Shilingi 70,000 anayeendesha Kirikuu 70,000, bodaboda 70,000! mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri, hebu punguza hawa watu wa bodaboda ili wasikimbizane na Polisi iwe tu tozo Shilingi Elfu Ishirini utakuwa umewasaidia sana na wataacha kuwa wanawakimbia Polisi na kwenda kufuata huko leseni, kwa sababu unakuta mafunzo 80,000, leseni 70,000 kabla ajaanza kazi Laki Mbili imeisha sasa unakuwa umemsaidia au umemsababishia hasara kwa sababu hiyo hela ingeweza kuwasaidia wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite kwenye mambo mawili au matatu katika bajeti hii. Kwanza nikupongeze Mheshimiwa Waziri kwa kutambua Sekta ya Kilimo. Nimpongeze Waziri kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya. Mheshimiwa Rais amesema ili kuweza kulikomboa Taifa lazima tujikite kwenye sekta ya kilimo, bajeti tumeiona imeongezeka mara dufu katika sekta ya kilimo, kazi yetu sisi kama Wabunge kwenda kuwahimiza wananchi wetu kuweza kwenda kuitetea sekta hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2021 Mkoa wetu wa Tabora ulizindua kitabu ambacho walikuja Mawaziri wengi, kitabu hicho kilitangaza fursa mbalimbali zilizoko katika Mkoa wetu wa Tabora. Ninakumbuka Mheshimiwa Bashe leo ni Waziri wa Kilimo alikuwepo wakati huo akiwa Naibu Waziri alishiriki katika kongamano hilo la kufungua fursa, kitabu hicho kipo na kumbukumbu ya Serikali ipo. Waliomba Mkoa wa Tabora uweze kutengeneza block farm mbalimbali ili ziweze kusaidia wananchi katika sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuondoka tuliweza kukaa kama Halmashauri, wakapendekeza eneo la Kalangasi Kata ya Tura Jimbo la Igalula itengenezwe block farm ya korosho. Jambo la kushangaza tulipitia michakato yote ambayo ilikuwa utaratibu na kwa mujibu wa sheria na Baraza la Madiwani liliridhia kuwa Kalangasi sasa tutakwenda kutenga ekari 15,000 itakuwa block farm ambayo tutalima kilimo cha korosho, ajabu imeingia mdudu asiejulikana sasa imeanza kupigwa danadana block farm ile haijulikani kama ipo au haipo, wanataka waweke kilimo cha mizinga ya asali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Bashe unatoka Mkoa wa Tabora hebu naombeni mnitajie ni nani ametajirika kwa asali anayetoka Mkoa wa Tabora? Wananchi wetu wengi matajiri wanatajirika kwa nafaka za chakula, sasa tunakwenda kuweka kilimo cha asali, wananchi wa Kalangasi waliweka block farm ya korosho wameutunza msitu kwa muda mrefu sana. Mheshimiwa Jafo alikuja pale ziara akasema huu msitu muhimu sana. Sasa mimi nashindwa kuelewa, hivi Serikali huwa wanawasiliana?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo anataka block farm, Mheshimiwa wa Mazingira anasema huu msitu utunzwe kwa sababu ya mazingira, sasa mimi niiombe Serikali, wananchi wa Jimbo la Igalula Kata ya Tura, Kijiji cha Kalangasi wako tayari kushirikiana na Serikali kuweka block farm ya korosho, pia wako tayari kushirikiana na Serikali kwa kila hatua ili kuhakikisha mradi huu unaleta tija kupitia Halmashauri yetu na kupitia Taifa na kuingiza pato.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuomba Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo yuko hapa kupitia majibu ya Serikali, tunataka tujue tunapoondoka kwenda Majimboni tuondoke na kauli moja, kwa sababu wameshaanza TFS kwenda kupima eti lile eneo liwe la uhifadhi, wakati miaka yote tangu uhuru hawajawahi kwenda kule, wananchi wamehifadhi kwa kutumia gharama zao, leo wanaenda kupima kule nini? Nasi kama Wawakilishi wa Wananchi tunakataa na tunalaani wasisogee tena huko kwenda kupima eneo hilo, nadhani watakuwa wamenielewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufungua uchumi wa Mkoa wa Tabora tumepewa fedha nyingi za kujenga reli ya kisasa (standard gauge) ambayo katika Mkoa wa Tabora asilimia 70 ya reli kutoka Makutupora kwenda Tabora….

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa

T A A R I F A

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kumpa taarifa mnenaji kwamba mabadiliko ya tabianchi duniani yamekuwa ni mabaya sana na mvua zimekuwa zikipungua mwaka kwa mwaka. Kwa hiyo, kuna umuhimu wa Serikali kuendelea kutunza misitu, kwa hiyo nimeona kusema kwa kutumia neno kusema walaaniwe ni kosa, kwa sababu nchi inateketea na dunia inateketea kwa sababu ya mazingira. Ahsante sana.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Venant.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza hili neno walaaniwe sijalisema yeye ameongeza chumvi misitu Tanzania iko mingi.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa wewe sema tu unaipokea ama huipokei ni vitu viwili tu.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei taarifa kwa sababu mbalimbali.

NAIBU SPIKA: Endelea na mchango wako.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ninalolisema uhifadhi upo, misitu ipo waende wakahifadhi kule, wananchi hawa walihifadhi kwa miaka yote, sasa hivi wanakuja kufanya nini, kwa hiyo tunataka kilimo cha korosho usinipoteze kwenye mada yangu.