Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa inayofanyika nchini, ni kazi iliyotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kuipongeza Serikali kwa jitihada kubwa za utatuzi wa matatizo ya wananchi wetu katika majimbo tuliyotoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwanza kuzungumzia suala la kikokotoo. Hali ni ngumu sana kwa watumishi ambao wamestaafu hivi sasa. Nadhani tutazame jambo hili kwa sababu kwenye vijiji tulivyotoka wastaafu wengi wanapofika umri wa miaka sitini, hawana zaidi ya miaka sabini; wengi wao umri wao unaishia kwenye miaka sabini au sabini na kitu. Kiwango hiki cha kikokotoo tunachoonyesha sasa, kwao siyo rafiki kwa sababu mahitaji ni makubwa kulingana na afya yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nashauri Serikali, jambo hili kwa kuwa walikaa na viongozi wao na vyama hivyo na vikakubaliana, basi nao watoke hadharani walizungumze badala ya sisi tu kama Bunge kuhangaika kulizungumza na pengine tutapata tafsiri ya wazi kwa wananchi ili wananchi waweze kufurahia jambo hili na hasa wale wastaafu wetu. Unapofika miaka 60 kwa kweli wewe ni kambi ya matatizo mengi kwenye afya, lakini pia huduma nyingi zinahitajika, unarudi kwenye hali ile ya zamani kama mtoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nafikiri, kama inawezekana, eneo hili litazamwe upya kwa sababu wastaafu wengi wanatupigia simu wakizungumzia kwamba jambo hili kwao siyo rafiki, Serikali ilitazame kwa namna inavyoona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nije kwenye bajeti. Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Mawaziri bajeti zetu kila mwaka, mimi nina mwaka wa saba katika Ubunge. Inaonekana bajeti zetu ni nzuri wakati zikiwasilishwa, lakini kwenye utekelezaji tunashindwa kufanikisha kwa sehemu kubwa. Kwa hiyo, nafikiri kama ambavyo fedha za Mheshimiwa Rais zile za COVID 19 zilitoa taswira kubwa sana kwa wananchi na heshima kubwa sana kwa wananchi na ikagusa maeneo makubwa ya wananchi wetu, basi tutazame namna ambavyo na bajeti yetu inakuwa wazi na pia inagusa yale maeneo tuliyoazimia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekaa kwenye Bunge hili nikiangalia, kila mwaka inapokuja bajeti tunaifurahia sana, lakini baadaye kwenye utekelezaji maeneo mengi yanakwama. Ushauri wangu ni nini hapa? Ushauri wangu ni kuona viasharia vilivyokwaza mwaka wa kwanza, basi tuone namna ambayo mwaka huu kwenye makusanyo yetu tunaweka vile vipaumbele kwenye maeneo yaliyokwama, lakini pia kwa jinsi ambavyo inaweza ikatekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mchezo tunacheza huku Bungeni, huu wa kushika Shilingi na kurudisha. Mimi naona ni mchezo tu wa kushika Shilingi na kurudisha. Nimwambie Waziri wa Fedha na hata Mawaziri wengine wote, taarifa ya bajeti ya mwaka huu kwenye Jimbo langu la Mbulu Mji imeandika vitu vingi sana. Nina hofu kwamba haya yatatekelezeka? Kwa hiyo, kila Waziri nimwombe atusaidie. Nami nitoe tu tafsiri wazi kwamba mwakani mimi nashika Shilingi, wala siirudishi. Ninawa-alert kabisa Waheshimiwa Mawaziri, ikishindikana tafsiri ya wazi tuwe nayo kwa wananchi, kwa sababu hali ni mbaya ya jinsi ambavyo tunashika shilingi halafu tunarudisha; halafu mwaka mwingine tunakuja tunashika shilingi halafu tunarudisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za mpango wa barabara ile ya Karatu – Mbulu – Hdyom ni mwaka wa nne ikitembea kwenye vitabu vya bajeti, lakini inashindikana kutekelezwa kwa sababu hatuna fedha. Wananchi kule hawaamini hivyo, kwa sababu tayari tulishaweka nia yetu njema.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nafikiri hatamu hii ya mwaka huu, tender ilitangazwa na tayari toka mwezi Mei. Cha kushangaza kabisa, tunajua kwamba manunuzi yataishia mwezi wa Saba kwa ajili ya mchakato wa mkandarasi yule aliyewekwa kupeleka vifaa mwezi wa nane ili aanze kazi. Je, atakwenda, au ni maandalizi mazuri tu kwenye kitabu chetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nitakaposhika Shilingi wala siirudishi. Mawaziri wote ni marafiki zangu na huwa wanatekeleza mambo mengi, lakini kwa kuwa yanakwama na wananchi baadaye wanakuja na hoja ya kudai kwanini haikutekelezwa, basi ni wajibu wetu na sisi pia kuyakataa yale ambayo tunashika Shilingi halafu tunarudisha. Pengine utetezi wenu uwe wa wazi mbele ya wananchi na uweze kuleta taswira nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine, nizungumzie suala la vifaa vilivyoagizwa vya COVID 19. Tumesubiri magari ya ambulance toka madarasa yale yamejengwa, toka Mheshimiwa Rais ameleta fedha, mchakato wa manunuzi Serikalini siyo mzuri mimi nawaambia, kwa sababu tayari toka zile fedha zimekuja, majengo yamejengwa, miradi mingine imeshaanza kutoa huduma, lakini vifaatiba, magari yale ya ambulance na vifaa vingine, hata mitambo ile ya kuchimba maji, mpaka leo bado. Hali hii inaonesha nini? Inaonesha wananchi wanasubiri sana huduma, lakini sisi tunakuwa hatujafika kwa wakati unaostahili. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiri ifike mahali tuone utaratibu wa mchakato uangaliwe kwa namna ya pekee sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye eneo lingine la wahitimu wa vyuo vya kati. Kwa VETA nilikuwa nashauri kama itawezekana na vyuo hivi vya ufundi mlivyokarabati tutazame namna ambavyo wale vijana wanapomaliza masomo yao au kipindi kile cha mafunzo, basi hata Serikali ione namna ya kuwapa vifaa. Vijana hao wanaosoma kwenye vyuo vya ujuzi kuna changamoto kubwa sana. Kwa nini kuna changamoto? Familia wanazotoka hazina uwezo. Zinapowapeleka kwenye vyuo, baada ya kumaliza mafunzo, hata ile package moja tu ya vifaa, hakuna, yaani hawawezi kununua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa ajili ya kuondoa ada ya Kidato cha Tano na Sita. Nadhani mwakani mje basi na namna ya kuondoa pia karo kubwa sana kwenye vyuo vya vyeti kwenye afya na vyuo vya ufundi stadi na vyuo mbalimbali vya ujuzi. Mara nyingi wale wanafunzi wanapata gharama kubwa na familia zinazopeleka wale vijana wanatoka shule za kata na familia zao ni za kipato kidogo. Kwa hiyo, wanasoma kwa gharama kubwa. Ukienda kwenye vyuo hivi vya certificate, kama ni afya ama ni vyuo hivi vya ujuzi, chakula tu inaweza kuwa zaidi ya Shilingi milioni tatu kwa mwaka. Ukichanganya na gharama nyingine kwa familia ya kaya ambayo uchumi wake ni mdogo, wanashindwa kumudu na hatimaye wale wanafunzi wengi wanasoma kwenye mazingira magumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili ni la muhimu sana, hao vijana wa vyuo vya chini tuweze kuwaona, ni gharama gani wasaidiwe. Zamani Serikali ilikuwa inatoa chakula na kulikuwa na gharama ndogo kwenye familia zao kwa sababu sehemu nyingine Serikali inabeba. Tulipofuta, wameingia kwenye gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunategemea vijana wanaomaliza Chuo Kikuu, baada ya kuonekana ajira imekuwa ngumu sana, sehemu ile ya asilimia 10 ya mikopo inaweza kuwa sehemu nzuri sana katika kuwasaidia namna ambavyo ile 4:4:2...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)