Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Vincent Paul Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia bajeti kuu ya Serikali. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu, pamoja na timu nzima ya Wizara ya Fedha kwa kutuletea hii bajeti. Bajeti ni nzuri imegusa maeneo makubwa ya mwananchi kwa ajili ya maendeleo. Kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa sana anayoifanya ya kuliletea Taifa maendeleo, hasa wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia kwa kutoa ushauri upande wa vifaa vya ujenzi ambao bei imekuwa kubwa sana, ambapo kwa mwananchi wa kawaida kugharamia ujenzi wa nyumba kuweza kupata bati inakuwa ni tatizo kwa sababu wananchi wa Tanzania wengi wao vipato vyao ni duni. Kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri naomba unisikilize, kidogo, ukienda Uganda asilimia karibia 80 ule mji wa Kampala umeezekwa kwa vigae na vile vigae vinatengenezwa na wananchi wa kawaida kutumia tu udongo wanachanganya na simenti na baadhi ya mechanical.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi kama ikiweza kutoa elimu, utaalam kama wa Uganda wanavyofanya hata mwananchi wa kawaida ataweza kuezeka nyumba yake kwa kupitia vigae. Vigae ni mbadala wa bei ilivyo juu ya mabati na vifaa vya ujenzi, hasa kupitia VETA, majeshi yetu pamoja na magereza, hivi vyuo vya VETA tukiviwezesha tujenge na viwanda vya vigae, wanafunzi wanapopata utaalam wa utengenezaji wa vigae itamrahisishia mwananchi wa kawaida kwenda kupata huduma ya vigae na kuweza kuezeka nyumba yake kwa urahisi zaidi. Kwa sababu sasa hivi hata mabadiliko ya tabia nchi vijijini hata nyasi zenyewe za kuezekea nyumba hazipo kwa hiyo vigae ndio suluhu pekee hata nyumba za tembe wenzengu Wagogo wataezekea vigae Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije upande wa ranchi, hii ya Kongwa; kwenye bajeti yako ulielezea kuhusu Kongwa. Mheshimiwa Waziri ile ranchi ya Kongwa naomba uachane nayo kwa sababu mji wa Dodoma ni jiji; hadi sasa hivi kuna mahitaji makubwa sana ya nyama, hasa ukizingatia Kombe la Dunia. Ukiingia huko bei ya nyama sasa hivi ni tatizo. Sasa ranchi hii tukianza kuivuruga na kuibadilisha kuwa ya kilimo ilhali Jiji la Dodoma linakua, na mahitaji ya nyama pia; hata mnadani tunaenda kula nyama kule, tutakosa kula nyama za mnadani siku ya Jumamosi. Kwa sababu ile ranchi inasaidia, hata wafugaji wa kawaida wanaweza wakatumia kulisha wanyama kama ng’ombe katika hifadhi ya Kongwa. Tukiivuruga tutasababisha mahitaji ya nyama Jijini Dodoma kuwa ni ya shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo mengi zipo skimu nyingi sana Mkoa wa Rukwa zimetelekezwa, miundombinu ipo, lipo ziwa Tanganyika hakuna gharama ya miundombinu; kuliko kuanza sasa kuivuruga Ranchi ya Kongwa. Naungana na wabunge wote, hii Ranchi ya Kongwa isiguswe. Ikiwezekana iboreshwe, mitambo ya ngombe pamoja na madume; hapa tunalalamika wananchi wetu wanafuga mifugo ya kienyeji ambayo haina tija. Sasa ranchi ile inatakiwa irekebishwe, iboreshwe hawa wananchi wafugaji wapewe mbegu bora kutoka Ranchi ya Kongwa na rachi nyingine zote zinazomilikiwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuje kwenye gridi ya Taifa. Mkoa wa Rukwa tunatumia gridi ya taifa kutoka nchi Jirani, siwezi kuitaja jina. Kwa sasa hivi ninamshukuru Mungu kwenye bajeti yako umesema unatuunganisha Gridi ya Taifa kutokea Iringa. Hili jambo linatakiwa lipewe kipaumbele kwa sababu tupo kwenye ushindani wa kiuchumi. Tupo kwenye ushindani wa kiuchumi lakini umeme tunategemea nchi Jirani. Kwa hiyo hujuma (sabotage) ya aina yoyote ile ya kuweza kudhoofisha maendeleo ya Mkoa wa Rukwa ni rahisi.

Kwa hiyo, hii gridi ya Taifa mmesema mnaunganisha na Iringa fanyeni hili jambo liwe la kipaumbele, hii kazi ikamilike mapema kwa sababu tupo kwenye shindano la kiuchumi, kwa hiyo sabotage, umeme unaweza ukakata, watu viwanda vyao vikaharibika. Mambo ya kiuchumi na ushindani kuna sabotage nyingi, ni ushindani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye uchumi wa bluu, uchumi wa bluu hasa mikoa mitatu; Rukwa, Katavi na Kigoma, tunashukuru mmetupatia meli kwenye bajeti, imeingia baada ya Wabunge wa mikoa mitatu kupiga kelele, tumepata meli Ziwa Tanganyika. Kwa hilo jambo, tunasema ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja upande wa miundombinu. Miundombonu bado. Kuna baadhi ya mikoa jamani, tuongee ukweli, ilisahaulika katika nchi hii. Hii mikoa ya pembezoni ilisahaulika na ndiyo maeneo yenye uchumi. Miundombinu mpaka sasa hivi kwa mfano kwenye Jimbo langu la Nkasi Kusini kata nne ambazo barabara hizi za uchumi, siyo za uchumi tu, ni pamoja na ulinzi kwa ajili ya wananchi, kwa sababu wananchi kule hata wakipata tatizo la uharamia, askari hawezi kufika kule kwa sababu miundombinu haipo. Kwa hiyo, ndiyo fursa ya maharamia na majambazi na wahalifu kwa ajili ya ukosefu wa miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuombe, Mheshimiwa Mwigulu unapokuja wind-up, utuambie hizi barabara za kimkakati katika majimbo yale yaliyosahaulika nchi hii hasa Kigoma, Nkasi Kusini toka uhuru barabara, hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye soko la mahindi, tena mwaka huu ndiyo kuna changamoto kubwa sana. Soko la mahindi mkulima anahangaika huko pembejeo gharama; tunashukuru mmeweka ruzuku katika pembejeo, lakini mnapokuja kununua pamoja na kuweka ruzuku, kama ni NFRA, mje mkae na wakulima mjue gharama ya gunia moja huyu mkulima wa kawaida ameligharamia kwa Shilingi ngapi, ili muweke bei inayolingana na thamani ya gunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, NFRA wanaweza wakaja wakasema hili gunia tunanunua kwa shilingi 55,000 kwa mkulima, kumbe gharama hizo za gunia ni shilingi 120,000 mpaka shilingi 100,000. Kwa hiyo, unakuta huyu mkulima hamumsaidii, mnamdidimiza. Kwa hiyo, wakati wakununua bei za mahindi NFRA mfanye utafiti kujua gunia moja huyu mkulima wa kawaida ametumia gharama ya shilingi ngapi mnunue kulingana na thamani ya gunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja vyuo vya kati. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais amefuta ada Kidato cha Tano na cha Sita. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi anayoifanya. Vyuo vya kati ndiyo vinavyotengeneza utaalam na ajira. Hivi vyuo mafundi gereji wengi mtaani huko ni darasa la saba. Pia ni mafundi wazuri mno, ambao hawa wanapomaliza Darasa la saba wakiingia kwenye VETA hapa, naomba Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba ahakikishe kama Serikali aone namna ya kuweza kufuta ada kwenye vyuo vya kati, atasaidia kundi kubwa sana ambalo linachangamoto ya ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti yake ameisoma, upo ubadhirifu wa fedha za UVIKO. Mheshimiwa Rais anatafuta fedha, anahangaika huku na kule na ametuletea maendeleo makubwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbogo kengele ya pili.

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)