Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Rais wetu Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anaendelea kupambana kuhakikisha kwamba maendeleo ya wananchi wake yanaweza kusonga mbele. Vilevile niweze kumpongeza Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote kwa kutuletea bajeti ya wananchi; kwa maana ya kwamba imejielekeza jinsi gani inakwenda kushughulikia, kufufua uchumi na kuongeza uzalishaji ili maisha ya wananchi wetu yaweze kuboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, taifa lolote ili liweze kuongeza uzalishaji basi lazima taifa hilo wananchi wake wawe na afya njema; na bajeti hii imejielekeza kabisa kwa kuendelea kuonesha kwa vitendo jinsi gani Serikali inaendelea kuongeza miundombinu ya afya lakini jinsi gani inaendelea pia kuboresha ile iliyokuwepo ili kuhakikisha wananchi hawa wanapata afya njema. Tumeona jinsi ambavyo bajeti hii imenunua vifaa hasa kwa ajili ya uchunguzi mbalimbali. Tumeona imenunua CT scan 11 lakini imenunua MRI nne Digital X-ray 104, echo cardiography saba, lakini na vitu vya oxygen tumenunua PET scan kwa ajili ya Ocean Road. Hivi ni vifaa ambavyo vinakwenda kuongeza jinsi ya kutambua magonjwa kwa haraka ili wagonjwa hawa waweze kupata matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru Serikali kwasababu kipekee na sisi Mkoa wa Kigoma tumepata CT scan ambayo imewekwa pale Maweni kwa hivyo wananchi wetu watakwenda kufanyiwa uchunguzi wa CT scan pasipo kusafiri kwenda Mikoa ya mbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kidogo kuhusu PET scan ninaendelea kuipongeza Serikali kwasababu imeona ni jinsi gani iendelee kuwasaidia wagonjwa wenye magonjwa ambayo hayaambukizi, ikiwemo saratani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii PET scan ambayo imefungwa pale Ocean Road tunayotegemea ianze miezi miwili au mitatu ijayo imegharimu takribani bilioni kumi na nane hii inakwenda kuwasaidia wagonjwa wa kansa tuliokuwa nao nchini; na hii ni mashine ya pili kwa East Afrika. Wenzetu Kenya walitangulia na sisi tumepata sasa. Hii inakwenda kuwasaidia wagonjwa wa Kansa kugundua ugonjwa mapema kugundua extent ya ugonjwa, na pale unapompatia matibabu basi utajua basi kansa imekwisha au haijakwisha, tofauti na zamani ambapo ukishampa matibabu basi unabaki unasubiri na kuona, wait and see, nimempatia tiba, je atapata dalili tena. Kwa hiyo hii haipo tena na tumesema tukimgundua mgonjwa mapema na akapatiwa matibabu basi saratani inakwenda kupona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwasababu kwa bajeti hii basi imemjali mwanamke; kwasababu wote tunafahamu kansa inayoongoza hadi sasa ni kansa ya mlango wa kizazi ikifuatiwa na kansa ya matiti. Ambazo hizi zote zinakwenda kumuathiri mwanamke. Kwa hiyo Mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amejionesha kwa kitendo kwamba anawajali akinamama wa nchi hii, anajali afya zao ndiyo maana akaelekeza fedha zake kwenye kifaa hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niombe Serikali PET scan zinatakiwa katika hospitali zote za kanda ikiwemo KCMC, Bugando na Mbeya ili kusogeza hizi huduma. Niiombe Serikali, katika zile fedha ambazo tunakwenda kuziokoa kutoka kwenye kubana matumizi basi zifanya kazi hii ili wagonjwa PET scan. Wagonjwa hawa tena wapunguziwe mwendo na gharama ili wapate huduma hizi karibu. Hii iende sambamba na kuongeza linear accelerators; matibabu modern kwa ajili ya kansa, zipo mbili tu Ocean Road. Naomba Serikali iangalie tena upya na hospitali zote za kanda ziweze kusaidiwa linear accelerator ili wagonjwa wetu wapate matibabu hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kigezo hiki wagonjwa hawa wakishapata hii PET scan na linear accelerator basi hatuna hata sababu ya kuwapeleka tena wagonjwa nje ya nchi. Ni ukweli usiopingika kwamba wagonjwa wa kansa ni wengi hapa Tanzania. Tunapata wagonjwa wapya takribani 14,000 kwa mwaka; na hawa ni wale ambao wanakwenda kuziona hospitali, ambao ni asilimia 33 tu ya wagonjwa tuliokuwa nao kwenye jamii. Kwa hiyo unaweza ukaona takriban 42,000 wapo mtaani, wanaogundulika kila mwaka kati yao ni 33 percent wanakwenda hospitalini. Kwa hiyo tuendelee kuwajali wagonjwa hawa wenye magonjwa ambayo hayaambukizi kwa kuendelea kuwaboreshea kuwapatia mahitaji hayo. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kujenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda Magharibi pale Mkoani kwetu Kigoma. Limekuwa ni ombi la muda mrefu; tangu mwaka 2016; wananchi wa Mkoa wa Kigoma walishatoa eneo lakini wakaenda mbali zaidi wakatoa hadi michango, tunazo milioni 100 kwenye mfuko. Hii ni kwa kuonesha jinsi gani tunahitaji hii hospitali ya rufaa kanda ya magharibi. Niiombe Serikali basi iharakishe mchakato wakupeleka fedha Mkoani Kigoma ili Hospitali yetu ya Kanda Magharibi iweze kuanza ujenzi mapema. Hii itakwenda kumuondolea mwendo mwananchi wangu anayetoka Muhambwe ambaye alikuwa akitaka kwenda kupata matibabu kwenye hospitali za rufaa either aende Bugando ambapo anatembea takribani kilometa 367 au aje Dodoma anatembea takribani kilometa 800, au aende Dar es Salaam ambapo anatembea takribani kilometa 1261. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni mwendo mrefu sana. Kwa hiyo kwa kutuletea hiyo hospitali pale Kigoma tunaamini huduma zitakuwa karibu lakini wananchi watakwenda mwendo mfupi na gharama pia za nauli na matumizi zitapungua. Niishukuru tena Serikali, na niombe fedha zile zije kwa wakati kwasababu tumeshatenga eneo katika Kata yetu ya Machinjioni pale Kigoma Kitongoji cha Kichangachui; tunaomba fedha zifike kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kigoma tumebahatika kupata miundombinu hii ya afya; na tunafahamu kabisa uhaba wa watumishi upo nchi nzima lakini unatofautiana. Kwenye ikama ya Watumishi wa Afya wa Mkoa wa Kigoma tuna uhaba wa takribani asilimia 33; kwa maana ya kwamba; I mean asilimia 67, tuna 33. Hii asilimia 33 ndiyo inayoitegemea sasa, maana tunakwenda kufungua vituo vya afya vingine tunakwenda kufungua Hospitali ya Halmashauri ya Kakonko na tunakwenda kufungua Hospitali ya Halmashauri ya Kigoma DC. Hii hii asilimia 33 ndio inategemea igawanywe katika hizo hospitali, kwa maana ya kwamba basi watendaji watakuwa wachache sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali; tunafahamu imetoa kibali kwa ajili ya ajira, basi Mkoa wa Kigoma upewe kipaumbele kwasababu tuna uhaba mkubwa sana wa watumishi wa sekta ya afya. Nimalizie katika eneo hili kwa kukumbushia tena, nilichangia nilivyosimama mara ya mwisho hapa; nikumbushe tena bima ya afya kwa makundi maalum. Tunafahamu Serikali ina mpango wa kutoa bima ya afya kwa wote, lakini najua ni zoezi ambalo haliwezi kwenda kwa mkupuo. Basi tuanze na haya makundi maalum ambayo yanataabika sana nikimaanisha wazee, watoto na wajawazito.

Mheshimiwa Naibu Spika, …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante muda wako kengele ya pili.

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)