Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii, naomba nichangie mambo manne kama muda ukiniruhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwanza ni umuhimu wa bajeti umuhimu wa hotuba ya hali ya uchumi, ni hotuba muhimu sana kwa sababu ndiyo inayotuonesha uwezo wetu wa kiuchumi na uwezo wetu wa mapato ili tunapopanga matumizi tujue nguvu yetu iko wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ndiyo hotuba ambayo inatupa vipaumbele vya Kitaifa, changamoto tu ni kwamba Waziri wa Mipango ndiye huyo huyo ni Waziri wa Fedha, kawaida Waziri wa Fedha ana mambo mengi ndiyo maana kitabu chake ni kikubwa wakati ile hotuba ya mipango ni kidogo, kwa sababu ina concentrate na mambo machache. Waziri wa Fedha anataka ikiwezekana fedha zote za nje ziingie Serikalini, yaani fedha zote katika nchi hii awe nazo yeye na ikiwezekana mahitaji yote ayamalize leo, ndiyo maana utaona ikisomwa humu ndani kuna mambo mengi unasoma unakutana na kiswahili kitumike kwenye usaili, unaelewa ni jambo jema kubwa na tukalipigia na makofi ni jambo zuri, lakini yote hii ni kwa sababu Waziri wa Fedha ana mambo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, of course nilikuwa nasoma nikasema dhima yetu ya mpango wetu wa maendeleo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu, nadhani kisera ni muhimu kuwasisitiza watoto wa Kitanzania na Watanzania ili waweze kushindana, wajue vizuri Kiswahili, wajue vizuri Kiingereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshakubaliana hapa tena Waziri anafahamu, tumeshafungua soko la ajira free movement of labor, sasa watakapoenda kule Uganda kufanya interview watu wetu inabidi na wenyewe washindane kwa hiyo, hili ni muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na hiyo changamoto ushauri ni kwamba pengine Bunge hili linaweza likaishauri mamlaka lione umuhimu tena wa kutenganisha hizi sekta mbili, za mipango na fedha. Nadhani tulipoandaa ile dira yetu ya mwaka 2025 ukiisoma ndiyo maana aliyesaini pale, hakusaini Waziri wa Fedha wakati huo Mheshimiwa Daniel Yona alisaini Mheshimiwa Nassor Malocho aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango, nadhani hili kuna haja ya kulifikiria tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge letu tujielekeze wenyewe na kujishauri pengine kuna haja hii hotuba ya hali ya uchumi ikatolewa mapema kabla sekta hazijaanza kuwasilisha bajeti, ili sasa wanavyokuja kuwasilisha bajeti za kisekta tuone hizo sekta ambazo zinawasilishwa kama zinaendana na hali yetu ya uchumi na vipaumbele ambavyo tunavyo and then, siku hii saa kumi ije bajeti ya National Budget ndiyo tuipokee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni kodi. Katika eneo la kodi nataka nianze kwanza kuwapongeza wafanyakazi wa Tanzania wanaoiongoza nchi hii siyo kwenye utumishi tu, lakini pia kwenye suala la mapato. Ukisoma takwimu za TRA wafanyakazi wa Tanzania ndiyo wanaoongoza kulipa income taxes, wanawazidi business income tax, wanawazidi mpaka cooperation tax, yaani ile tunayosema large tax payers hawawafikii wafanyakazi wa Tanzania. Wafanyakazi wa nchi hii wanalipa, ukisoma zile takwimu 12.3 percent ya makusanyo yote ya TRA ni pay as you earn, wafanyakazi wa Tanzania ukisoma zile za juzi 2.2 trillion shillings kutoka kwa wafanyakazi. Wafanyakazi wa nchi hii waheshimiwe, wanafanyakazi kubwa, tunawashukuru sana kwa mchango ambao wanaoutoa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pongezi vilevile kwanza kwa Mkoa wa Dar es Salaam, ukisoma takwimu za TRA asilimia 79 ya makusanyo yote ya kodi yamekusanywa kupitia Dar es Salaam, Dar es Salaam is the largest tax collection center in the country. Tunazungumzia Trilioni 13.9 kati ya Trilioni 17.6 ahsanteni sana Mkoa wa Dar es Salaam. Pia ukiangalia kwa maana ya wananchi wanaolipa kodi, asilimia 11 ya kodi zote za nchi hii zinalipwa na Mikoa Mitatu ya kikodi kwa maana ya Ilala, Kinondoni na Temeke of course kwenye Kinondoni pia pale Ubungo ipo, usisahau Ubungo ipo ndani ya Kinondoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hawa tunaozungumzia Trilioni 1.996, Mikoa mingine yote ukijumlisha wanalipa kodi Trilioni 1.921. Kwa hiyo, makusanyo ya Mikoa Mitatu ya kikodi Dar es Salaam inazidi Mikoa yote ya Tanzania ukijumlisha. Wananchi wa Dar es Salaam shikamooni sana, tunawashukuru sana kwa kuchangia. Nataka niwaambie shukrani za Serikali ya CCM….

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Stella Manyanya.

T A A R I F A

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza namshukuru Profesa kwa mchango mzuri lakini naomba nimpe taarifa moja, sisi ambao tunatoka kwenye maeneo yasiyolipa kodi kiasi hicho siyo kwamba hatutaki, lakini uwekezaji mkubwa umefanyika kwenye maeneo hayo na lazima mlipe hizo kodi, ndiyo maana tunaomba sasa nchi, Serikali iangalie na maeneo mengine ili na sisi tuweze kuchangia kwa kiasi hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo unaipokea hiyo taarifa?

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siwezi kukataa taarifa ya Dada yangu naipokea tu hata kama siijui sana, hiyo naipokea haina matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, point yangu ni hapo hapo kwamba nataka nichukue nafasi hii kuwahakikishia wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam Serikali ya Chama cha Mapinduzi hii

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo Chief Whip anataka kuzungumza.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi ni shabiki wa kusikiliza michango ya Profesa, ili tuweke mambo sawasawa hapa, hizi trilioni 13.9 zilizokusanywa na Dar es Salaam, Da es Salaam siyo wazalishaji, wanaozalisha wapo Mikoani, ndiyo maana asilimia 90 ya magari yetu ya mizigo, yote yametizama Dar es Salaam, tukiziba hizi barabara Dar es Salaam mtakufa njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo wamezalisha Dodoma, wamezalisha Mikoa yote nilitaka kumpa taarifa tu hiyo ili Watanzania wengine wasije wakajiona hawa mchango kwa nchi yao.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo unaipokea taarifa?

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Taarifa yake haina shida naipokea, mambo ya kuzingatia ni mawili nimeweka takwimu mbili na naomba unitunzie muda wangu, takwimu mbili za msingi za kuzingatia. Dar es Salaam kama collection center ndiyo hiyo Trilioni 13.9, hizo maana yake Watanzania wote wamechangia, ikiwemo airport, ikiwemo bandari, ile ni bandari ya wananchi wote wa Tanzania, kwa hiyo, hiyo ni Watanzania wote mpaka wa Singida na Iramba wamechangia hilo halina shaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna takwimu ya pili ambayo ni shukrani kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni wananchi ambao wamechangia 1.996 trillion wananchi wa Ilala, Kinondoni na Temeke, hawa ndiyo nawalinganisha na wengine. Sawa hawa Mheshimiwa Waziri hawa watatu hawa, wamekusanya kuliko nchi nzima ukijumlisha, wanastahili shukrani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo, nataka niwahakikishie wananchi wa Dar es Salaam kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi zile ahadi zake za kujenga barabara za mitaani itatekeleza ili mkusanye zaidi fedha. Nataka niwaambie Tarehe 31 Mei mwaka 2022, Mawaziri watatu walikutana na Wabunge Wabunge wa Dar es Salaam wakiongozwa na Waziri wa Fedha Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, pamoja na Waziri wa Ujenzi na wametuhakikishia kwamba mradi wa DMDP upo, zile barabara zitajengwa na akitoa ahadi Mnyiramba huwa havunji, kwa hiyo hili litakwenda vizuri.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu, nataka nipongeze TRA kwa kazi nzuri. Sisi tumekaa hapa tunachangia vizuri kwa sababu kuna watu wamekusanya mapato tukalipwa ambavyo tunalipwa na utaratibu wetu ukakamilika, TRA ahsanteni sana. Pamoja na hayo wameshasema Waheshimiwa Wabunge hapa tunachangamoto kwa kweli, bado tunakusanya kidogo sana! Kwa hapa East Africa sisi ndiyo tuko chini, wote tumewazidi DRC tu ambao wamejiunga juzi, lakini mpaka Burundi wametuzidi hii ni changamoto. Tunakusanya only 4.5 percent ya walipa kodi Tanzania. 2.7 Million out of Six Billion, only 4.5 percent ya watu wote wanaolipa kodi. Kwa kweli ni jambo ambalo linasikitisha lazima tutoke hapo, tusonge mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri, bahati nzuri TRA wamewahi kufanya study, TRA ilikuwa na maboresho katika maeneo mawili, eneo la kwanza ilikuwa ni hili kuitoa TRA kuwa chombo cha utawala kwenda kuwa component tax ya TRA. Eneo la pili ilikuwa waende kwenye ku-improve efficiency na walikuwa na mambo kadhaa, moja kupunguza viwango vya kodi, kurahisisha ulipaji kodi, wakaja na mapendekezo mengi lakini moja ya pendekezo zuri sana ilikuwa ni kwamba tupunguze wigo wa VAT iwe kati ya asilimia 10 mpaka 20, halafu tupunguze utiriri wa kodi kwenye Local Government Authority, badala yake VAT inayokusanywa watakuwa wengi wakishaongezeka, Serikali Kuu ibaki na asilimia 75 halafu Local Government Authority ibaki na asilimia 25 ya VAT, hivyo tutakuwa tumesaidia sana kwa maana ya accumulation wa zile kodi ni za kwetu lakini pia kupunguza utitiri wa kodi katika maeneo ya Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu Dar es Salaam nimerudia tena hapo, nilishatoa hapa angalizo na nikasisitiza Majiji yote yana sifa Kumi, lakini kwa sababu ya muda nitaje mbili. Moja miundombinu nadhifu ya usafiri, hii ni muhimu na ninaipongeza Serikali kwa kujenga Daraja la Tanzanite, sasa Mheshimiwa Waziri tumejenga daraja lile zuri kwa mkopo halafu unakuja na tozo achana na hiyo biashara. Daraja la Tanzanite ni daraja zuri, lilijengwa kwa lengo la kupunguza foleni katika hii barabara ya Ali Hassan Mwinyi na ni daraja zuri, kwa hiyo usiharibu furaha ya Dar es Salaam kwa kuweka tozo, achana na hiyo biashara.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili kuna kitu kinaitwa 24 hours activity, Majiji yote yanakuwa na ‘K’ tatu, piga kazi masaa 24, kula maisha masaa 24, lipa kodi masaa 24, Mheshimiwa Waziri hawa watu ndiyo wanakulipa kodi, habari za kusema fungua biashara kuanzia Saa Sita, achana na hiyo kitu! Eti, Jumamosi unaambiwa kwamba msifungue biashara mpaka usafi ufanyike, mambo ya wapi hayo? Hayo mambo hayawezi kuwa katika Majiji Mheshimiwa Waziri, kwenye hotuba yako umesema sanaa na burudani ndiyo inayokuwa kwa kasi kiuchumi, sasa burudani makao makuu yake si Dar es Salaam? achia Dar es Salaam 24 hours. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni ushauri. Mheshimiwa Waziri umeongeza import duty kwenye cotton yarn, Tanzania bahati mbaya Waziri wa Kilimo hayupo, hapa tuna ginnery peke yake hatuna spinning ukiongeza cotton yarn itabidi ufunge viwanda vya A to Z utafunga NIDA, utafunga kama viwanda vitano hivi, kwa sababu hapa hatuna raw materials. Hili jambo tumelizungumza mwaka jana, ninaomba sana Kamati ya Bajeti na wewe Mheshimiwa Waziri mliangalie, kwa kuweka import duty 24 percent mpaka 35 percent hatutaweza kushindana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani cotton yarn viwanda viko vichache mno ambavyo vinazalisha vingi tuna-import, sisi shida yetu tunataka tupate agro-processing industry tusafirishe mazao ambayo yamechakatwa, kwa hiyo kuleta yarn hapa ni jambo jema naomba sana liangaliwe hili ili viwanda vyetu visije vikaathirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)