Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu katika hii Wizara. Nitaendelea Mheshimiwa Lucy alipoishia. Naomba niongelee suala la asilimia 10 ambalo na wenzangu wameongelea sana. Namwomba Waziri asiitoe hii asilimia 10 kwa sababu, kwa sababu inawasaidia sana akina mama, mfano Mkoa wetu wa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Dar es Salaam asilimia 90 ya watu wanaoishi Mkoa wa Dar es Salaam ni wafanyabiashara. Kama unavyojua, asilimia nne inaenda kwa akina mama, asilimia nne inaenda kwa vijana na asilimia mbili kwa walemavu. Asilimia nne inayoenda kwa vijana ni hawa vijana ambao wamemaliza vyuo na hawana kazi. Sasa tutakapowaondolea hii asilimia nne itakuwa kwamba tumewaumiza sana. Kuna vijana wengi ambao wanafaidika kutokana na hii asilimia nne ambayo wanaipata kutoka kwenye Manispaa zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wengi sana ambao wanaendesha familia zao ni kutokana na hii asilimia 10 ambayo inapatikana kwenye Manispaa zetu. Nami nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala pamoja na Afisa Maendeleo Francisca Makoye, wanafanya kazi kubwa kuangalia Wilaya ya Ilala akina mama wanapata fedha hii asilimia 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia tu katika Jimbo langu la Segerea, katika mwaka ambao umepita tu, watu ambao wamekopeshwa kutokana na hii asilimia 10 wamekopeshwa Shilingi bilioni 4.6 kwa mwaka mmoja. Kwa hiyo, tunaomba hii fedha isitolewe, inasaidia kuendesha maisha ya watu na pia inawatengenezea vijana ajira. Tuna vijana wengi ambao wamemaliza vyuo vikuu hawana ajira, na tumekuwa tukiwaomba kwamba mtu anayetafuta kazi, wakati anaendelea kutafuta kazi basi wajiunge vikundi waende kutafuta mikopo Manispaa. Mkisema kwamba muitoe hii asilimia 10 ikabaki hiyo ambayo mnaipeleka kwenye miundombinu, mtakuwa mmewaumiza sana vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuliongea ni suala la miundombinu hususan mradi wa DMDP. Tumeshakuja kwako Waziri Dkt. Mwigulu tukiongelea mradi wa DMDP. Mkoa wa Dar es Salaam tunataka huko mbele uwe ni Mji wa biashara. Haiwezekani tukawa na mkoa ambao ni wa kibiashara lakini miundombinu yake mibovu. Kila nikisimama hapa huwa naongelea suala la DMDP na miundombinu. Miundombinu ya Mkoa wa Dar es Salaam, ikinyesha mvua dakika 10, Dar es Salaam nzima inasimama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia, asilimia 70 ya mapato ya Tanzania yanapatikana Dar es Salaam. Sasa ni kwa nini Wizara ya Miundombinu pamoja na Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu huu mradi wa DMDP bado haujaanza? Ndiyo mradi ambao tunautegemea sana na ndiyo unaoweza kutuokoa. Haiwezekani Mji wa biashara ukaonekana una miundombinu mibovu. Hata sasa hivi ukishuka pale Segerea Kata ya Kipawa, kitu cha kwanza kuona ni barabara mbovu. Tunahitaji tupate wawekezaji kutoka nje. Tutapataje wawekezaji na barabara hizo mbovu? Tumekaa sana na Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu tukiomba huu mradi uanze, tukaambiwa kwamba huu mradi utaanza mwezi wa Tatu, leo tuko mwezi wa Sita. Ameongea pale mwana-Dar es Salaam mwenzangu, mpaka sasa hivi hatujui huu mradi unaanza lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mradi wa Mto Msimbazi. Mradi huu ilikuwa uanze mwezi wa Tatu mwaka huu 2022, wakasema tayari wameshapeleka Wakandarasi wako wanafanya designing na mambo mengine ya kitaalam, lakini mpaka sasa hivi hatujapata taarifa ni lini huu mradi wa Mto Msimbazi unaanza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua, Mkoa wa Dar es Salaam mvua inanyesha saa yoyote, na kutokana na miundombinu mibovu maji yanaenda kwenye nyumba za watu. Kwa hiyo, nilitaka nijue, ni lini mradi wa Mto Msimbazi utaanza? Kwa sababu kuna nyumba nyingi sana zimeondoka kutokana na huu Mto Msimbazi. Kama ninavyochangia siku zote, ni kwamba, Mto Msimbazi au maji yanayoingia kwenye nyumba za wananchi siyo kwa sababu wananchi wameufuata Mto Msimbazi, ni kutokana na miundombinu mibovu, na ule Mto kutokana na kutokufanyiwa matengenezo au marekebisho; ule mto umepanuka na mvua kidogo tu ikinyesha unaingia kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tulikuwa tunaomba, mliahidi mwaka 2021 kwamba mtaanza kujenga mwezi wa Tatu, umeshafika, na hakuna kinachoendelea. Mpaka sasa hivi sijajua ni kitu gani kinaendelea kutokana na huu Mto Msimbazi pamoja na mradi wa DMDP. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya masuala ya miundombinu ya Mkoa wa Dar es Salaam ni muhimu sana, kwa sababu sisi tunavyotoka hapa, tunaenda kuwaahidi wananchi kwamba kuna hiki kitatengenezwa na hiki kitatengenezwa, lakini tukirudi hapa, kinaendelea kitu kinaitwa mchakato; tukitoka mchakato, tunaingia process. Hivi vitu haviishi! Watu wanasema kwamba Dar es Salaam inajengwa sana barabara, nataka niwakumbushe, Dar es Salaam ndiyo inayokusanya mapato asilimia 70 ya hili Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutakapopata barabara nzuri, na wafanyabiashara wetu watakapofanya kazi vizuri, ndiyo na fedha zitakapopatikana ili kwenda kujenga sehemu nyingine. Kwa hiyo, tunaomba Dar es Salaam Mheshimiwa Waziri aiangalie kwa macho mawili, kwa sababu, ndiyo Mji wa wafanyabiashara. Kama nilivyosema, asilimia 90 ya wakazi wa Dar es Salaam ni wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililokuwa nataka kuongelea ni kuhusiana na fidia ya wananchi. Leo siongelei tu fidia ya Kata ya Kipawa, kuna fidia mbalimbali. Unapoenda kuchukua sehemu ya mtu ambaye alikuwa amejenga nyumba yake, ardhi yake, unaichukua, unakaa nayo kwa kipindi cha miaka 10 bila kumlipa yule mtu, unamletea umasikini. Tuna sehemu nyingi ambazo Serikali imechukua na imewaahidi wananchi itawalipa, mmeweka miundombinu yenu, wananchi wanashindwa kufanya kazi, inabaki wananchi wanaendelea kudai. Yaani wananchi wanatoka Dar es Salaam, wanakuja Dodoma. Sasa hii Serikali ni kuwatia umasikini wananchi. Tunaomba Mheshimiwa Waziri hii tabia muache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnataka kuchukua eneo la mtu, basi mpeni fedha ili yeye aondoke na ninyi mchukue ile sehemu. Kama mlivyofanya kwenye Kata ya Kipawa Airport, mpaka sasa hivi, tangu mwaka 1997 hamjawalipa wale wananchi. Halafu pia mkaenda mkaweka na jiwe lenu la msingi, yaani kuonesha kwamba ninyi mmeshaichukua ile ardhi kabla hamjawalipa wale wananchi. Wale watu wameendelea kuteseka. (Makofi)

Mheshi,iwa Mwenyekiti, sasa juzi nimeuliza swali, Mheshimiwa Waziri akasema kwamba wale wananchi wanafanyiwa tathmini upya. Nami nimefurahi kwa sababu wanafanyiwa tathmini upya, na wakasema kwamba wameshapeleka barua Jiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, last week nimekwenda Dar es Salaam, hakuna barua yoyote ambayo imekwenda Jiji. Kwa hiyo, ninachokiomba Mheshimiwa Waziri utakaposimama, nilikuwa naomba Waziri husika aweze kuniambia hiyo barua ya wananchi wa Kata ya Kipawa Mtaa wa Kipunguni imepelekwa wapi, ili hao wananchi waweze kujua wanaanza lini kulipwa? (Makofi)

(Hapa kengele iliia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni jambo la muhimu sana. Jambo lingine la kuongelea ni kuhusiana na wafanyabiashara wa Mkoa wa Dar es Salaam.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kamoli, kengele ya pili ilikuwa imeshalia.

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)