Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Lucy Thomas Mayenga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kutoa mchango wangu kwenye bajeti hii. Nisipoteze muda nitoe pongezi nyingi sana kwa Wizara hii, watendaji wote wa Wizara hii, Naibu Waziri, Katibu Mkuu lakini bila kumsahau Kamishna Mkuu wa TRA ambaye anapambana sana kuhakikisha kwamba Taifa letu linapata mapato kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niongee kwa kifupi, najua wapi nitamalizia muda wangu. Nataka nitoe ushauri mmoja, wenzetu wengi wamezungumza, Wabunge wengi wamezungumza kwamba katika nchi yetu kazi ambayo amekuwa akiifanya CAG ni kazi ambayo inakuja mwisho kabisa, na amekuwa akigundua udhaifu mkubwa. Sasa wengi wametoa mapendekezo, kwamba tathmini, evaluation pamoja na monitoring inaonekana kama kuna yaani haipo. Ninafahamu kwamba chini ya Wizara ya Fedha Kitengo hiki kipo lakini nazani pengine kutokana na mfumo imekuwa ngumu kuweza kusimamia hii miradi kiasi ambacho imekuwa ikisababisha CAG kuja kugundua madudu mengi sana kwenye miradi yetu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba kutoa pendekezo, pendekezo langu ni kwamba naomba, kwamba kazi ya CAG ipo kwenye ukaguzi, naomba kupendekeza Serikali na hasa Mheshimiwa Rais aunde Presidential Bureau ambayo itakuwa inafuatilia kuweza kufanya monitoring na evaluation ya miradi yetu yote hapa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu kwamba hii ikiwepo kwanza watu watakuwa na heshima kwa sababu najua kwa mfumo uliopo sasa hivi Viongozi mbalimbali Mikoani, Wilayani, sometimes hawana mkono wa moja kwa moja kwenye kusimamia miradi kwa sababu ya hali halisi iliyopo; kwamba ni eyes on, hands off. Kwa hiyo unaweza ukaona kuna hitilafu lakini kuweza kusema kwamba mradi huu una hitilafu inakuwa ni shida. Lakini hata Kamati mbalimbali za Bunge, zipo, inakuwa ngumu sana kuweza kwenda na kuweza kuona kwa sababu ni wanakwenda kipindi ambacho, kwa mfano kama tunapokuwa tuko Bungeni wanatembelea mradi lakini baada ya hapo unakuta kwamba mradi unakuwa unaendelea. Kwa hiyo inakuwa si rahisi; madudu yakiendelea kule monitoring yake inakuwa ngumu kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninaomba, kwamba hili suala la hiki Kifungu kwenye TCRA ambacho mlikuwa mnataka kuondoa, nilikuwa naomba kifungu hiki majukumu haya ya TCRA yaendelee kubaki ya kwao. Ninasema hivyo kwa sababu wengi wamesema kwamba ubora wa utendaji kazi wa TBS wanapopima ubora na ubora wa TBS ni vitu viwili tofuati. Na next time ningeshauri Wizara hii wakati wanataka kufanya vitu kama hivi wawe wawe wana-consult hizo Sekta mbalimbali. Kwa mfano Wizara ya Kilimo kuna vifungu, na huku TCRA na maeneo mengine. Kwa sababu vitu hivi mnaweza mkaleta siku nyingine ikaja ikaleta hitilafu kubwa sana kwa watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu Royal Tour. Mimi nilikuwa naomba kuzungumza jambo moja. Mheshimiwa Rais wetu, kipenzi chetu, Mama yetu anafanya kazi kubwa sana. Kila Mbunge anayesimama hapa anakubali kwamba kuna kazi kubwa sana ambayo inafanywa. Lakini nilikuwa naomba kutoa angalizo kubwa sana kwa Waheshimiwa wabunge. Ipo tabia imezuka kwa baadhi ya wabunge kuleta maneno mengi sana dhidi ya Rais na Serikali yake. Ninasema hivi kwa sababu kuna tabia ya watu, mtu anaweza akasimama, asilimia kubwa sana hapa Bungeni tunaiunga mkono Serikali na tunatambua mchango mkubwa ambao Mheshimiwa Rais wetu amekuwa akiufanya. Lakini bado wapo baadhi ya Wabunge wachache ambao wao wanaamua makusudi kabisa kuipotosha Serikali, kupotosha wananchi, lakini kwa lengo la kutaka Rais wetu aonekane dhaifu, hawezi kusimamia mambo na kwamba kuna upigaji. Kwa hiyo, maneno yamekuwa ni mengi sana katika Bunge letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba nitoe angalizo kwa Wabunge hawa. tabia hii iweze kWisha na ife mara moja na ninaomba niwaambie Wabunge wageni ambao mmekuja ambao hamjui mambo ya humu Bungeni, leo hii mnaweza mkaona baadhi ya Wabunge wanapita kunong’ona ooh, kuna upigaji hapa, Wizara hii hiki na hiki; lakini nataka niwaambie, ikifika mwaka 2024 hamtaamini kama ndiyo hao. Kwa sababu kila atakayesimama ataipongeza Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo limekuwa likizungumzwa sana hapa na kaka yangu Mheshimiwa Sanga, jana amezungumza kuhusu suala zima kwenye sekta ya mbolea. Mtu anasimama hapa anasema kwamba yapo maeneo (upotoshaji wa makusudi kabisa), Serikali inaweza ikapata mbolea kwa bei rahisi ya Dola 300 kwa tani. Ni kitu ambacho hakipo. Sasa huu upotoshaji maana yake inakuwa ni nini? Kwa sababu mambo haya yanavyoendelea namna hii, matokeo yake tunakwenda kupeleka wrong message kwa wananchi wetu. Wananchi wetu kule watakuwa wanaona Serikali inashindwa kusimamia na Serikali haiumizwi na matumizi makubwa ya fedha za Serikali. Jambo ambalo ni baya sana sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa naomba niwape moyo Waheshimiwa Mawaziri, hata Bunge lililopita, kuna Waziri alisimama hapa, Wizara ya Nishati sijui imefanya hivi, kila siku ukisimama unasikia. Kama ninyi mna mapendekezo mengine, kwa nini msiende huko Serikalini kusema? Kwa nini mmekuwa mnakaa mnaongea? Wako wengine, Mbunge akisimama hapa anaongea ovyo, unajua kabisa kwamba ana-criticize, unaona kabisa kwamba huyu yuko genuine, lakini wako wale wengine ambao unakuta wana mambo yao, hebu mshindwe na mlegee. Hatutaki kuona huo mchezo hapa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilikuwa naomba kusema, tumpe muda Rais wetu. Mama yetu huyu jamani amekaa kipindi kimoja, amefanya kazi nyingi sana, amefanya kazi kubwa sana. Watu wanasimama hapa, anasema, kwenye Jimbo langu sijui shule, kwenye Jimbo langu zahanati; lakini akitoka hapo anakwenda huko kunong’ona maneno ya ovyo maneno ya kipumbavu kabisa!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba lingine nimalizie kwenye suala zima la amani ya nchi yetu. Niwaambie Waheshimiwa Wabunge, sisi wanasiasa dunia nzima chokochoko nyingi machafuko na vita huwa vinaanzishwa na midomo yetu. Nasema hivyo kwa sababu wapo watu ambao wamepoteza maisha kwa sababu ya kauli moja ambayo ameongea mwanasiasa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu ambao wameingia kwenye machafuko makubwa, wanahamahama duniani kwa sababu ya maneno ambayo wameongea wanasiasa, lakini wanasiasa wenyewe na hasa wakubwa wanakuwa wako salama. Kwa nini nasema namna hiyo? Wako viongozi wa kisiasa ndani ya Bunge pamoja na nje ya Bunge.

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. LUCY T. MAYENGA: Sitaki taarifa na wewe!

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.

T A A R I F A

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima sana, natambua mchango mzuri wa dada yangu Mheshimiwa Lucy, lakini naomba nimpe taarifa kwamba Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumepitisha mara kadhaa matamko humu ndani ya kumuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya. Kwa hiyo, naomba nimpe taarifa kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais. Kama yupo Mbunge ambaye anaongea hayo maneno huko nje, tutakaa kwenye vikao huko, lakini Bunge hili tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais. (Makofi)

MWENYEKITI: Haya, Mheshimiwa Lucy Mayenga, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu kwanza nimwambie Mheshimiwa Mbunge aliyeongea, ameingia hapa Bungeni kwa mara ya kwanza. Bunge hili, sijasema Bunge lote.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lucy, useme kwanza unaipokea au huipokei?

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa hii na nimesema kwamba sio Wabunge wote, ni baadhi ya Wabunge. Nina ushahidi kama mtahitaji ushahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee. Machafuko mengi ambayo yamekuwa yakitokea maeneo mbalimbali katika hii nchi, ni kwa sababu ya kauli za viongozi. Sasa nilikuwa naiomba Serikali hiki kinachoendelea kwenye hili sakata la Loliondo na ngorongoro…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. LUCY J. MAYENGA: ….nilikuwa naomba Serikali iwe makini kuweza…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

MWENYEKITI: Sasa ni Kuhusu Utaratibu au ni Taarifa? Maana naona kuna wawili.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

MWENYEKITI: Kuhusu Utaratibu haya, Mheshimiwa Musukuma.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mzungumzaji, dada yangu Mheshimiwa Lucy Mayenga haya mambo anayozungumza ni makubwa sana. Maana Wabunge humu tuko wengi, tunawakilisha wananchi wanaompenda Mheshimiwa Rais. Sasa kusema kuna watu Wabunge wanafanya hivi, tunafanya hivi, na ushahidi anao, halafu Kiti hakiwezi kumuomba, kwa sababu hili Bunge liko live; sasa wakitajwa, na sisi Wabunge tuwajue ili tuwaogope, maana sisi wengine tunamthamini Rais wetu. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma ingawa hujataja kanuni ipi imevunjwa, lakini hilo analozungumza ni sahihi. Mheshimiwa Lucy naomba ujielekeze kwenye mchango na kama kuna watu wanafanya hivyo na una Ushahidi, basi inabidi upitie utaratibu ambao unafaa zaidi kuliko kuzungumza hadharani kama hivi, na Watanzania wanasikia, wakaona kwamba kuna Wabunge na ingewezekana labda wengi sana wanaharibu hayo mambo. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Wapo, wapo!

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lucy naomba uendelee.

MHE. LUCY J. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea. Message imefika, waifanyie kazi, ndiyo cha muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho nilikuwa nataka kusema kingine ni kuhusu suala zima la hiki kinachoendelea huko kuhusu mambo ya Loliondo na Ngorongoro. Wapo wanasiasa ambao wanaingilia hili suala, lakini wana maslahi. Naiomba Serikali isinyamaze kimya. Naomba Serikali i-deal na hawa wanasiasa ambao kwenye hili suala wana maslahi. Hatuwezi kunyamaziana na mambo ya ovyo yakawa yanaendelea kwenye hii nchi. Haiwezekani, kwa sababu jambo hili likiendelea, mambo haya yanayoendelea huko yatashindikana, na vitu vyote…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. LUCY J. MAYENGA: Ndio walewale, nilijua…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lucy kengele ilikuwa imelia ya mwisho.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. LUCY J. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Wafanyie kazi na mbadilike. (Makofi)