Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa nami ya kuchangia Bajeti ya Serikali. Nipende kuchukua fursa hii kwanza kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake uliotukuka na maono makubwa aliyonayo kwa ajili ya kuiendeleza Tanzania. Watanzania wote ni mashuhuda na wameona kupitia bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango. Mheshimiwa Rais wetu ametoa maelekezo na ameelekeza bajeti hii iende kusaidia watanzania wa hali ya chini, na ndiyo maana fedha nyingi imepelekwa kwenye sekta ya uzalishaji.


Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nichukue fursa hii kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Naibu Waziri wake na timu nzima ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa utumishi wao mzuri ambao umetukuka na kwa kuweza kupokea maono na maelekezo ya Mheshimiwa Rais na kuyatekeleza kwa kiwango cha hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Ngara walionichagua kwa imani kubwa sana waliyonayo juu yangu na kwa kunipa ushirikiano mkubwa hasa ninapokuwa natekeleza majukumu ya kibunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nielekeze mchango wangu kwenye eneo la kilimo. Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizojaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa na ardhi nzuri, maji pamoja na hali ya hewa inayosapoti kilimo cha kahawa. Matokeo yake, Tanzania ni nchi ya tatu Barani Afrika kwa kuweza kuzalisha kahawa bora ndani ya Bara la Afrika ikifuatiwa na nchi ya Ethiopia pamoja na Uganda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi ya 15 duniani kwa uzalishaji wa kahawa bora kwenye hii dunia. Wanaozalisha kahawa Tanzania ni kaya 450,000 za Watanzania ambazo zinazalisha kahawa asilimia 90 ya kahawa yote inayozalishwa nchini. Kati ya kaya 450,000, kaya 120,000 zinatoka Mkoa wa Kagera na Ngara ikiwemo. Tunazalisha metric ton 50,000 kwa wastani kwa mwaka na mwaka tunaofanya vizuri tunazalisha tani 68,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mazuri yote haya, eneo linalotumika kwa kilimo ni hekta za mraba 265,000. Ilitakiwa tutumie hata zaidi ya hekta milioni moja, lakini uzalishaji unaofanyika, unafanyika kwenye eneo dogo ambalo halileti tija kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko changamoto kwenye eneo la kahawa hasa kwenye utaratibu mpya wa mnada wa kahawa. Hapo nyuma changamoto ilikuwa ni kubwa sana kwenye soko la kahawa, lakini nashukuru Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo yaliyopokelewa vizuri na Waziri Mkuu na baadaye kuchagizwa na Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussen Bashe na kuleta utaratibu wa kuuza kahawa kwa njia ya mnada. Nashukuru sana kwa hatua kubwa waliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko changamoto zinatakiwa kufanyiwa kazi kwa haraka. Moja, kwenye mnada anajitokeza mnunuzi mmoja, matokeo yake anaanza kuringa na kuweka bei anayoitaka. Ngara tumeonja bei nzuri ya kuuza kahawa. Tumeuza kwa mara ya kwanza kilo moja Shilingi 3,740/=, hatuwezi kurudi nyuma kwa sababu bei ya soko la kahawa kwenye dunia iko juu. Nimeshawaeleza wananchi wote wa Jimbo la Ngara na wakulima wa kahawa, kama bei haitashuka kwenye soko la dunia, nasi hatuuzi kahawa yetu kwa bei ya chini, na msimamo ni huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwaomba Watanzania wajisimamie, kwa sababu wanapoenda kwenye mnada anatokea mnunuzi mmoja anaweka bei wasiyoitaka. Kahawa siyo nyanya wala vitunguu waka biringani zinazoona. Kahawa zina uwezo wa kukaa muda mrefu, hatuuzi kama mnunuzi hatafika bei. Napenda kuwaomba Watanzania waweze kujisimamia katika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango amwezeshe Mheshimiwa Bashe ili aweze kuboresha miundombinu na utaratibu mzima wa kufanya mnada. Kwanza, wakati wa mnada internet imekatika zaidi ya mara mbili, matokeo yake wakulima wanashinda pale, wanashindwa kufanya biashara. Ni aibu mtandao kukatika wakati watu wanasubiria kuuza bidhaa zao wapate fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naomba lifanyiwe kazi ni kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa kwa kuhakikisha vijana wanawezeshwa kuanzisha mashamba mapya kwa sababu mashamba mengi yamezeeka, ni ya muda mrefu, yamepandwa na wazee. Sasa vijana hawana ardhi ya kutosha na mashamba ya kulima. Tuwawezeshe vijana kupata mashamba ili waweze kuanzisha mashamba mapya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nielekee kwenye eneo la miundombinu. Nimeshaeleza, Jimbo la Ngara ni jimbo ambalo liko mpakani na ni jimbo la kimkakati. Jimbo la Ngara linapakana na Rwanda na Burundi na ukitoka Ngara kwenda DRC Kongo ni karibu sana. Nimeshaeleza kwamba Ngara hitaji letu kubwa ni miundombinu ya barabara za lami za kisasa. Kuna kipande cha lami kutoka Nyakahula mpaka Rusumo kilomita 92, kama hakitatengenezwa wafanyabiashara wa Rwanda na Burundi watahama kutumia Bandari ya Dar es Salaam, wataenda kutumia Beira, Mozambique na watakwenda kutumia Mombasa, Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naomba sana Wizara ya Fedha na Mipango, tutumie utaratibu ule wa EPC+F (Engineering, Procurement, Construction plus Financing) ili tuweze kupata Wakandarasi waje kujenga barabara hiyo. Pia kuna barabara ya kutoka Mrugarama kwenda Rulenge mpaka Kwemubuga kilomita 75. Barabara hii imeahidiwa mfululizo kwa ziadi ya kipindi cha miaka mitano, na Marais wamekuwa wakija na kuahidi. Naomba barabara hii ipatiwe fedha kupitia utaratibu huo wa EPC+F iweze kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara inatoka Mzani inakwenda Kumbuga mpaka Murusagamba kilomita 34. Barabara hiyo inaiunganisha Tanzania na Burundi. Naomba sana Wizara ya Fedha na Mipango toeni fedha kwa Wizara ya Ujenzi ili barabara hii iweze kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna kipande kidogo cha kilomita 32 kutoka Rulenge kwenda mpaka Tembo Nickel. Naomba tena kipande hicho kiweze kujengwa kwa utaratibu huo wa EPC+F. Wizara ya Fedha tunaomba muidhinishe term sheet zinazoletwa na wawekezaji ili waweze kuleta fedha na waweze kujenga barabara hizi kwa utaratibu wa EPC+F. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Ngara hitaji letu lingine kubwa ni reli ya kisasa ya SGR kutoka Isaka kwenda Rusumo mpaka Rwanda. Nimeona kwenye mpango wa muda mrefu Serikali imeshatusikia na imeweka. Sasa nawaomba Wizara ya Fedha na Mipango waanze sasa kutafakari, kufanya feasibility study, kufanya design na kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga kipande hiki cha reli kutoka Isaka mpaka Rusomo Irala kuelekea mpaka Rwanda ili kurahisisha biashara mpakani katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende pia kwenye upande wa afya. Serikali imefanya kazi kubwa sana kuhakikisha kwamba inajenga vituo vya kutolea huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini. Nami kwenye Jimbo la Ngara hivi karibuni nimeweza kukamilisha ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya mbalimbali kikiwemo Kituo cha Rusumo, Kigina, Kabulanzimili pamoja na Kihinga. Vituo hivi vya kutolea huduma za afya, havina vitendanishi, havina vifaa tiba, havina watumishi na matokeo yake popo na mende ndiyo wanaotumia hivyo vituo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara ya Fedha na Mipango, toeni fedha TAMISEMI waweze kuleta watumishi. Toeni fedha waweze kununua vitendanishi na vifaa tiba ili vituo hivi viweze kufanya kazi. Pia tuleteeni watumishi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ridhaa yako naomba dakika moja tu nimalizie eneo la mwisho la kikokotoo kwa sababu eneo hili limeleta kelele sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kikokotoo kwa sasa linaleta pressure kubwa sana kwa watumishi wote nchini hasa wale wanaokaribia kustaafu. Watumishi wote Tanzania wana taarifa kwamba mwaka 2023 ndiyo mwisho wa kuahirishwa matumizi ya kikokotoo kilichokuwa kimeletwa na kikapandisha joto hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kila mtumishi ambaye umri wake umekaribia kustaafu wala hasubirii. Muda wake umefika wa kustaafu kwa hiyari, haraka haraka anamtafuta Mbunge, anawasilisha nyaraka zake, anastaafu kukimbia kikokotoo cha mwaka 2023. Naomba kikokotoo hicho ki-rest in peace huko huko ambako kilipelekwa, kisirudi tena kwa sababu mpaka sasa kinaleta joto kubwa na pressure kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja.