Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninapenda sana kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa mara nyingine tena, kwa namna ambavyo aliweza kuunda Wizara ya wanawake, jinsi na watu ambao hawajiwezi, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Nimesimama hapa kuomba kuongezewa fedha kwenye asilimia 10. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Kaka yangu, ‘Kalumbu’ ulikuwepo nilipochangia hapa kwamba ninaomba sana ile asilimia 10 niliyoiweka kwa ajili ya kusaidia, asilimia Nne wanawake, asilimia Nne vijana na asilimia Mbili watu wenye ulemavu. Niliomba sana kwa dhati ya moyo wangu, kwamba wanawake wana majukumu mazito sana. Majukumu mazito kwa maana ipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wewe naamini ni shahidi, mtoto akizaliwa wa kike kitu cha kwanza unamuita mama, umekuja, unamfurahia unamuita mama. Tayari ameshajiunganisha kwenye majukumu, nilitegemea hapa ombi langu la kuongezewa asilimia nyingine badala ya asilimia 10 waweke 15 ambapo asilimia tisa iende kwa wanawake kulingana na majukumu yao, kwenye asilimia hizo ni kwa sababu wanawake hao ndiyo hao hao wajasiriamali, ndiyo hao hao machinga, ndio haohao ambao wanatunza familia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri anavyokuja hapa kuhitimisha alichukulie uzito sana suala la wanawake. Wanawake wana majukumu mazito. Vijana hapa ambapo wanakuwa wanapata hiyo mikopo, akipata tatizo wa kwanza kuhangaika ni mwanamke ambaye ni ama mama yake au dada yake, lakini hatamwambia kwamba naomba fedha ya kukuuguza hospitali, hatamwambia hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa kilio cha Wabunge wote amekisikia, kuhusu kutokuondoa asilimia tano kwenye asilimia 10. Naomba iongezeke, badala ya asilimia 10 iongezeke iwe asilimia 15, Tisa kwa wanawake, Tatu kwa vijana, Tatu kwa watu wenye ulemavu kulingana na majukumu waliyonayo wanawake. Hata mabinti hawa niliomba kwamba mpaka sasa hivi kwa sababu ni wanawake wameshaunganishwa huko, wanakopa fedha kupitia Mfuko huo wa Wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitashukuru sana endapo hapa Mheshimiwa Waziri atalisemea hili, kwamba amebadilisha msemo wake ule wa kuondoa hata asilimia tano, bali ataongeza asilimia nyingine tano ili asilimia tisa iende kwa wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wa Tanzania hasa wanawake wa Mkoa wa Mbeya Wilaya za Kyela, Rungwe, Mbarali, Chunya, Mbeya Mjini na Mbeya Vijijini, wanawake wajane wa Taifa hili wanasumbuliwa sana. Ninaomba sana kwenye hili Serikali iwaone wanawake. Wanapokuja kuhitimisha ninatamani kama inawezekana ile sheria ya kusema mama anapofiwa na mume anasumbuliwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema hapa juzi, imenipasa nirudie kwa sababu baada ya mchango ule nilipotoka nje hapa kumbe kulikuwa na wageni wengi sana wanawake na kati ya wale wengi sana walikuwa ni wajane. Walijitokeza wanawake kuja kunisalimia na kunishukuru sana juzi nilivyowasemea wanawake wajane wa Tanzania hii. Mama mmoja nilipata uchungu sana, kati ya wale wanawake waliokuja kunishukuru, wanawake Wanne walikuwa na kesi Mahakamani za kudhulumiwa zao. Mmoja akaniambia, Mheshimiwa naomba samahani namba yako ya simu, mimi mume wangu nimeishi nae miaka 16 lakini amefariki, kesi ninayo Mahakamani. Baada ya kufariki anakuja Baba yake mdogo anasema mimi hii nyumba lazima iwe mali yangu niimiliki kwa sababu mume wako mimi ndiye liyemtafutia kazi! Ni uonevu wa hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali ichukulie kwa uzito kilio cha wanawake Tanzania nzima, hasa Mkoa wa Mbeya. Wanawake wengi sana hata kabla ya nafasi hii mimi kuwa Mbunge, walikuwa wakija kulia getini kwangu wakiniomba msaada, nilikuwa nikiwasaidia ili wapate haki zao waweze kusaidia watoto wao na familia zao. Nitashukuru sana kama nimeeleweka juu ya hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili jambo la TCRA. Kwenye Nchi yetu ya Tanzania tumeendelea sana kwa mawasiliano. Sasa hivi mfanyabiashara anakuwa yuko Mbeya, ameingia mteja dukani anahitaji kifaa yeye hana, anapiga simu dukani, anapiga simu Dar es Salaam anakipiga picha anauliza kama kifaa hicho kipo. Ni ndani ya dakika moja jawabu limepatikana na anaweza kukiuza kifaa kile. Mtu anasafiri anaweza akawa yuko Uturuki, anapiga picha vitu ambavyo amevikuta, mali mpya kule Uturuki, anauliza huku maduka ya Dar es Salaam; Je, nikileta hivi ili tuweze kuuza, je tutauza? Ndani ya dakika moja jibu vinapatikana, lete kwa wingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi vifungu wanavyosema viondolewe kwenye TCRA, hivyo vifungu vitaturudisha nyuma, mawasiliano yatapotea, yataisha, tutarudi nyuma. Ishu ya kidigitali hii itakuwa ni historia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake tumeingia kwenye mfumo wa kidigitali lakini matokeo yake tunaambiwa kwamba hivi vifungu viondolewe; TCRA watakuwepo kama nani, watakuwa wanafanya shughuli gani? Tutakuwa tumewaondolea kufanya kazi watu wa TCRA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui mlikaa na TCRA lini na wapi mkafikia mwafaka wa haya, lakini kwa vifungu vya sheria jinsi ambavyo tumevichanganua haitawezekana TCRA ikafanya kazi kwa ufanisi endapo vifungu hivi vitaondolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano sasa hivi kwa jinsi ambavyo yamekuwa yametuletea, wakati fulani unaweza ukawa una mawazo yako, una mambo mengi kichwani kulingana na hali ya maisha, lakini wakati mwingine unaona kwamba hebu nishike hii simu nijaribu kupata furaha yangu. Ukishika simu utacheka wakati umekasirika, utapata furaha pale, utapunguza stress, utapunguza maradhi, utatoa sumu ya mawazo kwenye mwili wako kwa kucheka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunakotaka kwenda, tukitoa vifungu hivi vya TCRA, vifungu vya sheria, tunakwenda kupoteana. Tutarudi kulekule, ukitaka kufungua mtandao ndiyo ukae baada ya siku moja, mbili au tatu, hatupendi Watanzania turudi nyuma, tunahitaji tusonge mbele kwa ajili ya maendelea ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, kulikuwa na kilio kikubwa sana cha wazabuni ambao ni ma-supplier Serikalini, wengine walikuwa wanadai madeni ya hata miaka 20 iliyopita, lakini Mheshimiwa Rais, Mama Samia, baada ya kuliona hili alituma fedha na baadhi yao walipunguziwa mzigo, nadhani yuko kwenye mchakato, ataendelea nalo hili. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa haya anayoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya Watumishi wa Serikali ni wazembe, wanatengeneza madeni wao wenyewe kwa uzembe wao. Baadhi yao wanafanya kazi nzuri, baadhi yao ni wazembe wanaiangusha Serikali. Fedha zinakuwepo kwenye akaunti, wanaagiza vifaa kwa supplier, akishaagiza fedha zipo lakini anafanya uzembe wa kumlipa supplier, mwisho wa siku zile fedha unaingia mwaka mpya wa Serikali zinavutwa zinakwenda Hazina, kuja kurudi ni ndoto. Hilo linakuwa linaunda madeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan nilimsikia hapa akisema Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu, alieleza kwamba wameacha utaratibu kuanzia sasa hakutakuwa na kurudishwa fedha. Fedha zilizoingizwa kwenye Halmashauri zetu, zilizoingizwa Serikalini kwa ajili ya kazi, zitabaki huko bila kurudi kule Hazina. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu ameondoa kilio cha wafanyabiashara walio wengi ndani ya hii nchi. (Makofi)