Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ELIMU, UTAMADUNI NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuja kuhitimisha Hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo iliyowekwa Mezani mapema leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuwashukuru wachangiaji wote wa hoja hii na wachangiaji wa hoja hii kwa siku ya leo walikuwa wachangiaji 16. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Adolf Mkenda, kwa kufafanua hoja mbalimbali ambazo zimeulizwa na Waheshimiwa Wabunge, hali hii itarahisisha sana kuacha mambo mengi ambayo tayari yameshafafanuliwa. Vivyo hivyo, namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro, kwa ufafanuzi alioutoa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kusema, kupanga ni kuchagua; kama Taifa na kwa kunukuu maelezo au maneno aliyoyasema Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo asubuhi ya leo kwamba ili kupata Taifa lililoelimika, lenye maendeleo endelevu, msingi wake mkubwa ni kuwa na elimu bora. Elimu bora ni ile ambayo inazingatia ubunifu, inazingatia uvumbuzi, inazingatia utayari wa Taifa kutengeneza wasomi ambao ni creative na ni innovative. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema Kamati inapokea mchango wa Mheshimiwa Sospeter Muhongo na iko tayari kutoa maazimio ambayo yatatolewa baadaye, lakini kwa hapa nasema maneno machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mitaala mipya ya elimu, sera na mitaala ya elimu, mabadiliko haya tuna Imani yatazingatia ubunifu, uvumbuzi, yataipa nguvu COSTECH kuendeleza kufanya tafiti na kubaini bunifu zote nchini kwa lengo la kuweka msingi bora kwa ajili ya kuimarisha maendeleo endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanya hayo, ni vyema Serikali ikaona umuhimu wa kuwekeza katika elimu. Kuwekeza kwa maana ya miundombinu, kuwekeza kwa maana ya walimu, kuwekeza kwa maana ya mambo mbalimbali ambayo yanagusa ukuaji wa sekta ya elimu hususani katika kuboresha sekta hii na mwisho wa siku kupata matokeo ambayo yatalisaidia Taifa kusonga mbele kimaendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya elimu, sayansi na teknolojia, yamezungumziwa hususani mambo saba makubwa; la kwanza ni lile ambalo nimeeleza la Mabadiliko ya Sera na Mitaala, lakini suala la ajira ya walimu, elimu ya watu wazima, elimu maalum, bajeti ya miradi ya Wizara kwa ujumla, bajeti ya elimu ya juu na elimu ya kati na VETA kwa maana ya Mamlaka ya Vyuo vya Ufundi na katika eneo hili yamezungumziwa zaidi masuala ya vifaa, walimu na mitaji mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nasema Kamati inaunga mkono mawazo na michango iliyotolewa na Waheshmiwa Wabunge wote 16 juu ya maeneo haya saba katika eneo hilo la Elimu, Sayansi na Teknolojia na Kamati itatoa Maazimio hivi punde. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la Utamaduni, Sanaa na Michezo; mambo makubwa matatu yamezungumziwa na Waheshimiwa Wabunge na tunawapongeza wote ambao wamechangia katika hoja ya Kamati. Sitaweza kuwataja wote, lakini nawashukuru wote ambao wameweka msisitizo katika suala la ukomo wa bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, wote ambao wameweka Hoja katika Sports Betting asilimia tano ya fedha inayotoka kwenye Gaming Board au Bodi ya Michezo kubahatisha lakini wote ambao pia wamechangia na kutoa msisitizo katika ujenzi wa viwanja vya michezo na miundombinu ya michezo kwa ujumla. Hapa napo niseme, kama Taifa, Taifa lolote ambalo linataka kupiga hatua ya maendeleo kwa haraka, ni lazima kuwekeza katika soft power au nguvu laini na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ndiyo soft power ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, soft power ikifeli, Taifa lolote linalazimika kwenda kwenye hard power kwa maana ya…, ikishindwa kutumia nguvu laini, itakwenda kutumia nguvu ngumu. Nguvu ngumu ni nguvu ya kutumia mabomu, mitutu ya bunduki na kadhalika.

Sasa ili tusiende huko, ni vyema Serikali ikatoa fedha zinazohitajika katika kukuza sekta ya michezo, utamaduni na sanaa ili kuwezesha Wizara hii kutekeleza miradi yote ambayo inategemewa kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, naomba sasa kujikita moja kwa moja kwenye Maazimio ya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufinyu wa bajeti ya Sekta ya Elimu;

Kwa kuwa, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo sehemu kubwa ya bajeti yake ni kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu inakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa Bajeti;

Na kwa kuwa, hali hiyo inakwamisha dhamira ya kuimarisha na kuendeleza kujielimisha na kuongeza tija katika maendeleo ya Taifa.

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba: -

(a) Serikali iendelee kuongeza fedha zinazotengwa kwa ajili ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; na

(b) Hazina ijitahidi kutoa fedha za Wizara hii kwa wakati kama ambavyo imeidhinishwa na Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa walimu wa amali nchini;

Kwa kuwa, licha ya Serikali kuanza kutekeleza Mtaala Mpya wa Elimu, na kusisitiza mafunzo ya amali, lakini taarifa zimeonesha kuwa kuna upungufu mkubwa wa walimu wa amali;

Na kwa kuwa, kutokuwa na walimu wa amali kwa idadi inayohitajika ni jambo linaloathiri madhumuni ya mitaama mipya na kwamba inaathiri manufaa ya elimu wanayopatiwa wanafunzi;

Kwa hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba: -

(a) Serikali iongeze fedha na uwezo wa Vyuo vya Ualimu kuandaa walimu wa amali;

(b) Na hivyo vyuo vya ualimu nchini viweke mkazo katika mafunzo yanayoendana na mitaala mipya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa walimu nchini; kwa kuwa, taarifa ya Serikali imeonesha changamoto ya Sekta ya Elimu ikiwemo: -

(i) Upungufu wa walimu wenye ujuzi unaostahili hususan katika masomo ya Hisabati, Fizikia na masomo mengine ya sayansi;

(ii) Upungufu wa miundombinu na vifaa vya elimu; na

(iii) Uchache na uduni wa zana za kufundishia na kujifunzia.

Na kwa kuwa, hali hiyo inaathiri ubora wa elimu nchini, na kwamba inachangia ufaulu usioridhisha wenye madhara kwa hazina na wataalamu wa Taifa.

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali iandae mkakati wa kuongeza ajira kwenye sekta yenye mahitaji yanayowezesha utekelezaji bora wa mitaala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufanisi mbovu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu;

Kwa kuwa, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inayotegemea kuweka mifumo ya taratibu kupata idadi kubwa ya wananchi walioelimika inakabiliwa na changamoto za ufinyu wa bajeti kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya wanaostahili, kutokupata marejesho ya mikopo ya wanaonufaika na wanaweza kurejesha kupata bodi kuweza kuweka mkazo katika jambo hili ipasavyo.

Na kwa kuwa, mambo hayo yamebainishwa na bodi kushindwa kutekeleza azma yake na kusababisha idadi kubwa ya watanzania wanaostahili kupata mikopo wanufaika wa mikopo hiyo.

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba,

(a) Serikali iongeze bajeti ya Bodi ya Mikopo kwa ajili ya kuongeza idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu wanaopata mikopo.

(b) Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu iongeze juhudi ya utoaji wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu na ulazima wa wanafunzi wanaopata mikopo kurejesha fedha hizo kama sheria inavyoelekeza.

(c) Serikali kwa kutumia balozi iandae taratibu madhubuti ya kufatilia wanufaika wa mikopo ya bodi walioko nje ya nchi ili kuweza kurahisisha urejeshwaji wa mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sheria, kanuni na taratibu za Bodi ya Mikopo kuendana na wakati;

Kwa kuwa, sheria, kanuni na taratibu zinazotumika na Bodi ya Mikopo zimekuwepo kabla ya bodi kuanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya kati na kwamba haziendani na masharti ambayo yanahitajika kwa sasa.

Na kwa kuwa, hali ya sheria na taratibu kupitwa na wakati haitoi mwongozo stahiki kwa sasa na hali inayoweza kuathiri ufanisi.

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali ifanye mapitio ya sheria, kanuni na taratibu ili kuzihaisha kulingana na mahitaji ya sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchakavu wa miundombinu na upungufu wa wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma;

Kwa kuwa, taarifa za Serikali zimeonesha kuwa Chuo Kikuu cha Dodoma kinakabiliwa na uchakavu wa miundombinu ikiwemo miundombinu ya maji; upungufu wa wahadhiri, uhaba wa mabweni kutokana na badhi ya majengo yake kutumika kama Ofisi za Serikali.

Na kwa kuwa, mambo haya yanakwamisha madhumuni ya chuo katika kutoa elimu bora.

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba;

i. Serikali iwezeshe Chuo Kikuu cha Dodoma kuajiri wahadhiri kulingana na uhitaji;

ii. Serikali iongeze jitihada na kuwa na mkakati wa dhamira wa kutatua changamoto ya maji katika Chuo Kikuu cha Dodoma; na

iii. Serikali iongeze kasi ya kukamilisha majengo ya ofisi kwenye Mji wa Serikali ili kuacha kutumia majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa vyuo vya mafunzo ya ufundi usioendana na mahitaji ya wanafunzi na vitendea kazi;

Kwa kuwa, Serikali imefanya kazi nzuri ya ujenzi wa vyuo vya ufundi kwa maana ya VETA, lakini haijatatua changamoto za idadi ndogo ya wakufunzi, upungufu wa vitendea kazi na ukosefu wa zana za kufundishia na kujifunzia.

Na kwa kuwa, changamoto hizo zinahitajika zisipotatuliwa tija wa ujenzi wa vyuo hivyo itakosekana.

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba;

(a) Serikali iwezeshe upatikanaji wa fedha na ununuzi wa vitendea kazi na uandaaji wa zana za kufundishia na kujifunzia; na

(b) Serikali iweze kuajiri wakufunzi wa mafunzo ya ufundi kulingana na mahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufinyu wa bajeti kwa ajili ya uendeshaji wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima;

Kwa kuwa, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima imebainika kukabiliwa na ufinyu wa bajeti.

Na kwa kuwa, ufinyu wa bajeti unaathiri uwezo wa taasisi kuendelea kutoa elimu nje ya mfumo rasmi wa elimu bila malipo na kwamba athari hiyo imekwamisha nia ya kuwezesha wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito na kadhalika.

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali itenge bajeti kwa ajili ya elimu inayotolewa nje ya mfumo rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya uendeshaji wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia;

Kwa kuwa, Taasisi za Serikali zinasababisha ufinyu wa bajeti ya COSTECH, hususan eneo la utafiti.

Na kwa kuwa, ufinyu huu wa bajeti unaathiri mwelekeo wa COSTECH, kuwezesha nchi kujielekeza katika sayansi ya teknolojia na ubunifu kwa maendeleo ya haraka ya kiuchumi na kijamii.

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba Serikali iendeee kuongeza bajeti inayotengwa kwa ajili ya COSTECH kila mwaka na COSTECH ijiimarishe kuratibu bunifu zote vyuoni na katika jamii kwa lengo la kukuza vipaji na kuleta tija inayotegemewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mradi wa EASTRIP;

Kwa kuwa, utekelezaji wa mradi huu umeripotiwa kuwa wa kusuasua.

Na kwa kuwa, hali hiyo inatokana na tofauti ya mifumo ya kifedha kati ya Benki ya Dunia na Tanzania, taratibu za manunuzi nchini zinasababisha tofauti ya bajeti inayotekelezwa na bei halisi ya vifaa vya ujenzi kuchelewa kukamilika kwa miradi.

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba;

(a) Serikali itatue changamoto na tofauti za mifumo ya kifedha ya Benki ya Dunia na Tanzania pamoja na kushughulikia taratibu za ununuzi unavyostahili; na

(b) Serikali iongeze mkazo katika utekelezaji wa Miradi ya EASTRIP ili kuwezesha wanafunzi wengi hususan wanawake kujiunga na vyuo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maazimio kuhusu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo; kukosekana kwa fedha ya miradi ya maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge:-

Kwa kuwa, taarifa za Serikali zimeshakuwa; Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo haipokei fedha za miradi ya maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge.

Na kwa kuwa, kukosekana kwa fedha hizo zilizoidhinishwa na Bunge ni jambo linalikwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopitishiwa fedha.

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba, fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Wizara hii kwa mwaka wa fedha 2023/2024 zitolewe ipasavyo na kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali iongeze bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa viwanja vya mpira vyenye hadhi inayokubalika kimataifa:-

Kwa kuwa, Tanzania imefuzu kuwa mwenyeji wa michuano ya AFCON kwa mwaka 2027 lakini haina viwanja vyenye hadhi inayokubalika.

Na kwa kuwa, hatua ya Serikali zilizoanza kwa lengo la kujenga viwanja vya mpira vya Dodoma, Arusha haziridhishi, kutakuwa na ugumu kuendelea kuwa mwenyeji wa michuano ya AFCON, uchumi wetu utapoteza fursa muhimu kutokana na michuano hiyo kutokufanyika Tanzania kama viwanja havitapatikana, na itaathiri heshima na hadhi ya Taifa letu katika masuala ya michezo.

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba;

(a) Serikali itoe fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa viwanja hivyo; na

(b) Serikali ijipange kuwa na usimamizi madhubuti wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo ili kuwa na ujenzi wenye thamani halisi ya fedha (value for money). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali isiyoridhisha ya Uwanja wa Benjamin Mkapa:-

Kwa kuwa, uchambuzi wa taarifa na hali halisi umeonesha kuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa unakabiliwa na changamoto za uchakavu wa eneo la kuchezea mpira (pitch); changamoto ya kutumika kupita kiasi na mfumo wa makusanyo kutokuruhusu viwanja kubaki na sehemu ya makusanyo.

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba;
(a) Fedha zinazotengwa kwa ajili ya ukarabati na uendeshaji wa miundombinu ya viwanja, uwanja huo wa Benjamin Mkapa zipatikane kwa wakati;

(b) Serikali iweke utaratibu wa sehemu ya makusanyo kubaki kwa uwanja (retention); na

(c) Serikali iandae mkakati wa kuboresha viwanja vingine ili kupunguza matumizi ya Uwanja wa Benjamin Mkapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sera na Sheria ya Baraza la Michezo kutoendana na hali halisi:-

Kwa kuwa, uchambuzi umebainisha kwamba, Sera na Sheria ya Baraza la Michezo haziendani na hali halisi licha ya kuwa michezo inachangia takribani asilimia 19 katika Pato la Taifa.

Na kwa kuwa, hali hiyo inayotokana na sheria kuwa zoefu tangu 1976 wakati wa mtizamo tofauti wa kiuchumia inakosesha uzingatiaji wa mchango wake katika Taifa.

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali ianze mchakato wa kuboresha sera na sheria inayohusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa fedha na watumishi wa Baraza la Kiswahili Tanzania:-

Kwa kuwa, Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) linategemea kuwa na mfumo madhubuti wa kusimamia na kukuza maendeleo ya Kiswahili Kitaifa, Kikanda na Kimataifa lakini inakabiliwa na ukosefu wa fedha za kutosha, inakabiliwa na upungufu wa walimu au wakalimani wa lugha mbalimbali.

Na kwa kuwa, hali hiyo ina kasi ndogo ya kubidhahisha Kiswahili na juhudi ndogo za BAKITA kuelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili na fursa ya kiuchumi kutokana na lugha ya Kiswahili.

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba;

(a) Serikali iwezeshe BAKITA kuajiri wataalamu wa lugha ya Kiswahili wenye ujuzi wa lugha nyingine ili kuongeza kasi ya ukuaji wa lugha sanifu ya Kiswahili;

(b) Serikali izingatie ahadi iliyotolewa kwenye Ilani ya CCM aya ya 283(d) kuhusu kuimarishwa kwa mila, desturi, utamaduni na kujenga Taifa lililobora na kuiwezesha BAKITA kuongeza wigo wa kuelimisha umma; na

(c) Serikali iwezeshe BAKITA kufanya tafiti katika nchi ambapo Kiswahili kinabidhaishwa ili kubaini fursa manufaa na namna ya kuwezesha kukistawisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwango duni vya filamu Tanzania:-

Kwa kuwa, Bodi ya Filamu Tanzania yenye dhamira ya kuweka mazingira bora na wezeshi kwa utoaji wa Tasnia ya Filami haijaweza kufanikisha ubora wa filamu Tanzania, kushawishi wasanii kuongeza upeo wao kuhusu filamu na Sanaa Tanzania. Kutoa msukumo kwa wasanii kuwa na script au maandiko yenye ufasaha wa lugha.

Na kwa kuwa, mambo haya yanasabisha mchango hafifu wa tasnia ya elimu katika biashara ya kimataifa na uchumi hasa kwa wasanii na ustawi wa watu wa Tanzania.

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba;

(a) Bodi ya Filamu ifatilie uzingatiaji na uhalisi wa filamu na kutoa msukumo stahiki kwa wasanii; na

(b) Bodi ya Filamu ihakikishe kuwa kuna mwongozo wa wasanii wanaoandaa andiko la filamu (script) ili kuzingatia ufasaha wa lugha na mvuto katika soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Samia Scholarship:-

Kwa kuwa, Mama Samia amefanya jambo jema la kutoa fedha maalum kwa ajili ya motisha kwa vijana kujikita katika masomo ya sayansi.

Na kwa kuwa, hali hii imeonesha uhitaji mkubwa kwa jamii kuhitaji hii sponsorship ya Mama Samia.

Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia;

(a) Kumpongeza Mama Samia kwa jambo hili jema kwa jamii ya Tanzania;

(b) Kuhimiza Serikali kuongeza fedha za mfuko huu ili wanufaika waweze kuongezeka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na michango mingi iliyochangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi kuhusu Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (Gaming Board of Tanzania), naomba kuongeza Azimio ili Bunge liweze kuazimia azimio hilo lisomeke kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (Tanzania Gaming Board):-

Kwa kuwa, Serikali ilipitishia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupokea asilimia tano ya mapato yatokanayo na kubashiri matokeo ya michezo (sports betting) inayosimamiwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha.

Na kwa kuwa, Wizara haipokei fedha hizo kwa mtiririko unaoeleweka na hivyo kuathiri utekelezaji wa shughuli za michezo.

Kwa hiyo basi, Bunge liazimie kwamba:-

(a) Serikali ipeleke fedha kwa wakati kama ambavyo inapeleka fedha za OC kila mwezi;

(b) Bunge liazimie kwamba, Serikali ianze mchakato wa kuihamisha Gaming Board kutoka Wizara ya Fedha na kwenda Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kuongeza ufanisi wa michezo ya kubahatisha, lakini vilevile kuongeza tija na kukuza mapato ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako sasa lipokee Taarifa ya Kamati na likubali maoni na mapendekezo yote ya Kamati kama yalivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

(Hoja ilitolewa iamuliwe)

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki. (Makofi)