Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Hassan Zidadu Kungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nami kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye hutuwezesha kutupa uhai na kusimama kwenye Bunge hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kwanza kabisa niwapongeze Wenyeviti wote wa Kamati mbili pamoja na Makamu Wenyeviti. Pia nitachangia upande wa elimu kidogo na baadaye nitamalizia upande wa michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kama kuna watu ambao wamefanya miujiza katika nchi hii, basi ni walimu. Kwa sababu tunafahamu kabisa walimu tunao kwa 40% lakini wamefanikisha ufaulu kwa zaidi ya 80%. Sasa nini nakusudia kusema hapa? Ninachokusudia kusema ni kwamba, laiti kama tungekuwa na walimu wa kutosha, tafsiri yake tungekwenda kupata ufaulu kwa zaidi ya 100%. Kwa hiyo, pamoja na changamoto nyingi za kielimu zinazopatikana, jambo la kwanza la kufanyiwa kazi kwa asilimia kubwa au kwa umakini mkubwa ni kuhakikisha idadi ya walimu inaongezeka, inakuwa ile ambayo inastahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, idadi ya walimu inapaswa kwenda sambamba na miundombinu ya elimu. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka imara ama kwa kuimarisha miundombinu ya elimu nchini, lakini walimu ni wachache sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakupa mfano, ziko baadhi ya shule unakuta ina madarasa saba lakini walimu ni watatu. Mfano kule Jimboni kwangu mimi kwenye Shule ya Msingi ya Mindu na Shule ya Msingi Nampungu; shule hizi zina madarasa saba saba lakini walimu ni watatu watatu. Sasa nini kinakwenda kutokea pale? Wanafunzi wanaokwenda kusoma, je, watapata elimu bora kama madarasa ni saba walimu ni watatu? Tujaribu kuona. Kwa hiyo, najaribu kuishauri Wizara, itakapotokea ama Mheshimiwa Rais atakapotoa ajira basi naomba tuweke kipaumbele kwenye zile shule ambazo zina uhaba wa walimu ili kuweza kuwasaidia wanafunzi wale wapate elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye upande wa vyuo, nakipongeza sana ama naipongeza Wizara kwa kuamua Chuo cha Kilimo (SUA) kwa kuweza kusogeza huduma ile ya kilimo ama elimu ya kilimo karibu na wananchi. Kwa upande wangu mimi Tunduru tunalo tawi la Chuo cha Kilimo (SUA) na Chuo kile kilianza muda mrefu sana. Yaani kilianza muda mrefu kabla ya Tawi la Chuo cha SUA Katavi. Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu kama wananisikiliza, hebu twende tukawasaidie watu wa Tunduru, kwa sababu Halmashauri ya Tunduru ilitenga takribani ekari 300 kwa ajili ya Tawi lile la SUA. Tumeweka majengo ya kutosha karibia asilimia 65, vifaa vipo, majengo yapo, kinachotokea majengo yale yanakwenda kuharibika bila ya kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hebu afikirie Tawi lile la Chuo cha SUA kikafunguliwe na badala ya kama kilivyo hivi sasa kinafanya kwa siku 14 tu kama practice kwa wanafunzi ambao wanatoka maeneo mengine, tunaomba utuangalie Tunduru Tawi lile la SUA liende likafanye kazi na hatimaye tupate elimu ya kilimo. Kwa maana tunatambua kwamba kila kitu kwa sasa ni elimu. Tunaomba elimu ya kilimo isogezwe Tunduru kwa kwenda kufungua tawi lile la Chuo cha SUA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda upande wa michezo. Michezo zamani ilikuwa ni burudani pekee, lakini kwa sasa michezo ni ajira, michezo ni burudani, michezo ni afya na michezo ni uchumi. Wenzangu wamezungumza sana, tunakwenda 2027 sisi kwa kushirikiana na nchi jirani tutakuwa wenyeji wa AFCON, lakini ili tuweze kuwa wenyeji wa AFCON, tafsiri yake ni lazima tuwe tumekamilisha miundombinu ya michezo kwa maana ya kukamilisha vile viwanja vitatu ambavyo tunapaswa kuvijenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sikosei tarehe 24 Desemba CAF wanakuja kukagua miundombinu ile ambayo sisi itatufanya kuwa wenyeji, lakini hadi dakika hii bado hatujaanza ujenzi wa viwanja vile vitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini mashaka yangu? Mashaka yangu ni kwamba utafika muda wa CAF kuja kukagua, sisi hatujakamilisha ama hatujafikia hata asilimia 50 ya ujenzi wa viwanja vile. Kitakachokwenda kutokea, tunakwenda kutia aibu kama Taifa kwa sababu tutakwenda kunyang’anywa wenyeji. Wenzetu Morocco waliomba ambao tayari wana viwanja. Sisi tumeomba tunataka kujenga viwanja, lakini mpaka leo jitihada zile za makusudi bado naziona kama ziko nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, Serikali iliangalie na ichukulie kwa umakini mkubwa sana na ikiwezekana kama zitaanza kazi za ujenzi huo, basi zifanyike usiku na mchana ili kuendana na muda kwa sababu tumebakiza muda mchache sana ili kuweza kuthibitishwa kuwa wenyeji. Sasa naomba tukamilishe angalau hata kwa asilimia 70 au 60 ili tuweze kuwa wenyeji wa michuano hiyo ya AFCON. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miundombinu hiyo ya michezo, nataka nizungumzie Timu ya Taifa. Timu ya Taifa inapaswa tuiangalie mara mbili. Hatuwezi kuwa wenyeji wa AFCON halafu tukawa na Timu ya Taifa ambayo siyo Madhubuti. Lazima Timu ya Taifa letu iwe madhubuti. Tumeona mfano wenzetu kule Ivory Coast wamefanya vizuri, wamekwenda sawa sawa wamekuwa wenyeji lakini na timu yao imefanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini nataka kuzungumza hapa? Ninachotaka kusema ni kwamba kwenye nchi yetu ni lazima tuingize kitu kinachoitwa uraia pacha. Tunao wachezaji wengi sana wanaocheza nje ya nchi na ni wachezaji wazuri kabisa ambao wangeweza kufanikiwa kuja kwenye Timu yetu ya Taifa, maana yake wangekuja kuiimarisha Timu ya Taifa. Sasa wanashindwa kuja kuiimarisha Timu ya Taifa kwa sababu nchi yetu hairuhusu uraia pacha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, timu nyingi tulizocheza nazo kule, zilizoshiriki AFCON ya hii iliyokwisha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umeisha, malizia.

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie sekunde kama moja au tatu au nne au tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri Cape Verde, yaani katika ile Timu ya Cape Verde waliocheza ambao wametoka nchi angalau kidogo haina upeo mkubwa wa mpira ni wachezaji wawili tu ambao nakumbuka kama alikuwa ni Inonga na Baka, ambao wametokea Tanzania, lakini wengine wote wanacheza Europe na maeneo mengine. Kwa mfano vile Morocco, Tunisia, Algeria, Cameroon, Congo, South Africa, hawa wote wanatumia mfumo wa uraia pacha na timu zao zile zilizoshiriki AFCON…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umeisha, nashukuru sana.

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)