Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii. Mimi nitachangia Kamati ya Elimu, Utamaduni na Michezo. Kwa kipindi cha miaka hii miwili mitatu, ni wazi kwa kila mtu kwamba tasnia hii imeitendea haki Tanzania. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kuishukuru Serikali, lakini na sisi Bunge tujishukuru. Unajua inabidi wakati mwingine ujishukuru, lakini kipekee nawashukuru Wajumbe wa Kamati na Mwenyekiti, kwa kusimamia kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niko hapa kushukuru, na anayeshukuru anaomba. Siyo siri na sioni aibu kuomba. Katika haya mengi ninayoyazungumza, maamuzi ya Serikali na Mheshimiwa Rais, mmefanya jambo moja jema, yaani elimu mmeipeleka kwao. Uamuzi wa kujenga Chuo Kikuu Bukoba au Kagera ni kuipeleka elimu kwao, ni jambo zuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja nataka kuzungumza, nimepitia Taarifa ya Kamati kuhusu vyuo vikuu vyote. Kuna upungufu wa watumishi, na unaponiambia upungufu wa watumishi chuo kikuu, ni Wahadhiri. Hili jambo lisikae likatokea. Ni kama kujenga hospitali nzuri wasiwepo waganga na wauguzi. Haupaswi kuwa na chuo kikuu ambacho hakina wataalam. Hili jambo linapaswa lijulikane mapema kwamba huyu atastaafu au kuna programu mpya tuweze kutengeneza hawa watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali bila daktari siyo hospitali, ni majengo tu. Kwa hiyo, hizi mnazoziita changamoto, mimi sikubaliani kama ni changamoto au tuseme ni uzembe. Tuseme ni uzembe, haya mambo yarekebishwe kusudi tuweze kuwa na chuo kikuu, na niwaeleze, watu wengi wangependa kuja kusoma hapa. Kama nilivyosema, kwa kuweka Chuo Kikuu Kagera, Bukoba ina maana watu wa maziwa makuu watakuwa wanakuja kusoma sehemu ile. Pamoja na kutoa elimu, tutaweza kupata utalii wa kielimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu VETA, VETA imefanya kazi nzuri, naweza kuwa ugomvi binafsi na Kamati na Waziri kwamba kila wanapokuja Kagera kukagua VETA hawaji kwenye VETA ya kwetu. VETA sio ile ya Bukoba tu, kwa hiyo mnapokuja kukagua Bukoba muende na Karagwe kuna VETA mtembelee VETA zote mje na Kamachumu kuna VETA ili kusudi muweze kuona tunakwama wapi. Mimi nina VETA huenda majengo hayatoshi, Karagwe kuna VETA huenda kuna mapungufu, ninyi ndiyo mnaojua. Mje mtukague ili kusudi mjue mapungufu ukienda ugenini lazima uende na zawadi yoyote, mtuletee zawadi yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu kuhusu VETA, mitaala yenu isiwe ya mchakato, iwe situational. Leo soko linataka mafundi wa pikipiki, leo soko linataka mafundi wa simu. Kwa nini leo msilete Wachina VETA wakafundisha vijana wetu namna ya kuunda simu, kutengeneza simu na kutengeneza pikipiki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini VETA watu leo wanakula kwa nini msilete VETA wataalamu wa food processing na vinywaji mkatengeneza vinywaji vyenye ubora ili watu wakaburudika na wakala maisha? Kwa hiyo, msitengeneze mchakato mirefu ya mitaala (situational au radical change). Tunataka VETA ya namna hiyo, msiwe mnapenda muda mrefu. Kuna mahitaji vijana wanajifunza. Kwa sababu unampeleka mtoto shule na unamuaminisha atapata kazi by the time anamaliza, kwa sababu ni mtaala wa kimchakato anakuta hiyo fursa imeondoka, tuwe situational, tuwe situational, tuwe situational kwenye hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kuishukuru TEA (Mamlaka ya Elimu). Mlifika kwetu Kisiwa cha Bumbire mkatujengea nyumba nne za walimu, nawashukuru sana. Lakini mlituahidi kutujengea mabweni, kule ni kisiwani, watoto wanakaa kisiwani. Najua maombi yako mezani, muwasaidie vijana wale wanapata shida, mamba ni wa kwao, mawimbi ni ya kwao. Nimesema leo nimekuja kushukuru, kwa hiyo watu wa TEA tafadhali, mnapoangalia yale yanayobaki muweze kutuzungumzia na sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nizungumzie mitaala mipya. Mitaala mipya inalenga kumuelimisha mtoto na ina wadau watano. Linalonipa shida, mimi ni muumini wa mitaala mipya kwa madhumuni yake, linalonipa shida ni kwamba, hawa wadau watano hawana uelewa, muwajengee uelewa ili wajue wanakwenda wapi. Kama mtu anaingia kwenye mitaala hii ajue anapofika mwisho wa safari anaweza kujiajiri au kuajiriwa, asifikirie kuajiriwa tu, alijue hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunapozungumza kwa mfano wadau wote ni pamoja na Serikali, na kwa shule za msingi unaizungumzia TAMISEMI. Kwa mfano mimi katika wilaya yangu tunapokwenda kwenye mitaala mipya nina upungufu wa vyumba vya madarasa kwa shule za msingi karibu 2000. Tunakwenda vipi? Kwa hiyo, ninakuwa na hofu ambayo wataalam wanasema Mwijage unakuwa na hofu isiyokuwa na maana. Lakini mimi nina upungufu wa vyumba 2000, watoto nitawasomeshaje kwenye mtaala wa namna hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna watu wengine kwamba labda tunataka kulipua. Tuwaeleze kwa namna gani hatutaki kulipua na kwa namna gani tunataka kufanya vitu vya namna hiyo. Lakini wengine wana upungufu wa walimu, tuwaeleze kwamba, tuna mpango wa kuwaandaa walimu na wameelewa vipi. Hoja ni kuelewa, na mpiganaji yeyote anayejua kwa nini anakwenda kupigana, atapigana vipi na nguvu ya adui, vita ataishinda kabla haijaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kutokuwa na uelewa wa pamoja kwa sisi hawa wadau watano ambaye ni mwanafunzi, mzazi, jamii, mwalimu, shule na Serikali, wote watano wakiwa na uelewa wa pamoja ninaimani tutaweza kuisimamia hii mitaala mipya, ukweli mimi leo asubuhi nilikimbilia kwa Mkuu wa shule, nilikuwa na wasiwasi na mitaala hii na nikawa nimejipanga kwamba, hapana nakwenda kukataa ili tubadilishe; lakini nilipokaa kwa Mwenyekiti hapa mwanangu akanieleza Baba hakuna hofu, usiwe na hofu, yale uliyokubali mwanzoni ulikuwa sawa, hii mitaala muwaeleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mimi naweza kutiwa hofu na umahili wangu huu, sasa wengine kule watakuwa na hofu kubwa, lakini tuiombe Serikali iongeze bajeti kama ilivyoelezwa, lakini bajeti iende na mipango isiwe ya ujumla. Kuna watu wa pembezoni tuna hali ngumu, mtu una shule zenye upungufu wa madarasa 2000 huwezi kulingana na mtu ambaye mwingine madarasa yanakaa yamefungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, niipongeze Serikali na nimpongeze Mheshimiwa Rais, zawadi aliyotutumia ya bilioni 3.8 tumeipokea na tunasubiri maua yake muda ukifika. (Makofi)