Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. kwanza, nashukuru na ninaunga mkono mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati mbili na kazi nzuri za Wizara hizo pamoja na kazi nzuri zinazofanywa na Serikali yetu chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita zaidi kwenye elimu. Nianze na pendekezo ambalo Mwenyekiti amelitoa kuhusu COSTECH, naomba nirudi kwa kusisitiza. Nadhani leo naiongea mara ya nne au ya tano, COSTECH kama tunataka kufanikiwa, inalazimika ibadilike iwe foundation ambayo itashughulikia science, technology na innovation. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zote ambazo zimefanikiwa duniani zina science foundation hazina commissions. Kwa mchango wangu, nataka niwarudishe nyuma. Sitapenda kurudia malalamiko na mapungufu ambayo tunayo kwa Sekta ya Elimu. Nadhani hayo tunayafahamu tunaweza tukaongea ndani ya dakika tano; lakini niwapeleke kwenye dunia ya sasa inakokwenda kwenye upande wa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudisha nyuma kidogo mfumo wa shule ulianzia wapi. Maana yake tunalalamika shule zetu hazifanyi vizuri, shule za kwanza kabisa zimeanzia huko Misri. Ilikuwa miaka 2061 mpaka 2010 kabla ya kuzaliwa Kristo BC. Huo ndiyo mfumo wa kwanza wa elimu lakini shule ambayo ni ya zamani kabisa duniani kote iko China. Hii ilianzishwa miaka 143 mpaka 141 BC, kabla ya Kristo, inaitwa Shishi High School. Bado ipo. Kwa hiyo, ndugu zangu hii ni kumbukumbuku kwamba, kwenye Sekta ya Elimu, tunayoyafanya tujue wengine wameyaanza siku nyingi sana. Sasa malengo ya mtu kwenda shule ni nini? Tukiyajua hayo malengo ya mwanafunzi Kwenda shule, ndiyo tunaweza tukarekebisha mitaala yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha kwanza kabisa, hizi shule huko Misri, China na duniani kote, mtu anakwenda shule akitegemea kupata maarifa (To acquire knowledge). Kitu cha pili kinachompeleka shule, ni kupata ujuzi (Skills acquisition). Sasa tunajiuliza shule zetu za Tanzania tuna hivyo vitu viwili? Maarifa na ujuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo langu kwa upande wa elimu, hivi viwili hivi kwa ngazi yoyote ile, awe mtu aliyemaliza darasa la nne, amalize darasa la sita, la nane mpaka chuo kikuu; kwa kiwango chake hichi anapaswa kuwa navyo hivyo vitu viwili. Sasa hapa kwetu vinakosekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekezo moja kwa upande wa elimu. Haiwezekani mitihani yetu iwe ya maswali ya kuchagua, hivyo vitu viwili hauwezi ukavipima hivyo. Kwa mfano, upande wa Hisabati, kwa waliofanya Hesabu duniani kote; lile jibu la mwisho la Hesabu lina asilimia 25. Asilimia 75, anayesahihisha anaangalia, je, huyu amechukua njia nzuri kufikia kwenye jibu? Sasa sisi tunaposahihisha A, B, C, D maana yake tunacheza na hiyo asilimia 25. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, baada ya kupata hivi vitu viwili, vinamwekea mtu msingi wa kuwa na udadisi (curiosity). Kitu cha nne, anakuwa mbunifu (innovative). Kwa hiyo, wanaoshughulika na mitaala hapa nchini, lazima tuzingatie hivyo vitu vine. Je, mitaala yetu itaongeza maarifa, ujuzi, udadisi na ubunifu wa mwanafunzi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya ndiyo ninapendekeza upande wa elimu wayafanye. Kwa sababu haya manne hayapo, ndiyo maana tunaona hata kwenye mitandao mtu anaweka tangazo alipwe fedha amfanyie mtu utafiti na alipwe fedha amwandikie mtu paper. Nilishangaa sana nilivyoona matangazo ya namna hiyo. Kwa miaka yangu yote ya kukaa kwenye academics sijawahi kukuta mtu anaandikiwa paper. Hiyo ni kwetu tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndugu zangu, baada ya hivi vitu vine, tuangalie dunia nyingine inakokwenda. Hivi vinne lazima tukiwa navyo, ndiyo tunaweza kuwa na vijana watakaoweza kushindana na vijana wengine dunia. Hii ajira tutakuwa tunaionea Serikali kila saa kulia ajira, ukweli ni kwamba, dunia ya sasa hivi ajira ni nyingi sana zinatafuta watu lakini ni watu wenye hivi vitu nne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikaona niangalie ni ajira zipi ambazo sasa hivi zinatakiwa kwa bidii sana duniani. Ninamuomba Mheshimiwa Almas Maige wa Kiswahili, alipita hapa nikamwambia ndugu yangu uje ujaribu kutafsiri. Sisi wengine tunatoka huko mikoani, Kiswahili chetu siyo kizuri sana. Hizi kazi, sijui hata Kiswahili chake. Kazi namba moja duniani inayotafutwa ni software developer, namba mbili ni data scientist, namba tatu ni information security analyst, namba nne ni ma-nurse wanao-practice. Unajua kipindi cha COVID walikufa wengi, sasa dunia inatafuta ma-nurse ambao ni competent; kazi namba tano ni management analyst na namba sita ni artificial intelligence specialist. Hizi ndiyo kazi sita duniani na kwa ushauri wangu sasa, ili tuzipate hizi kazi sita ni lazima tuwekeze kwenye science na technology. Ndiyo maana ninasema COSTECH lazima iwe foundation la sivyo hatutavuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote ukiyafanya unarudi kwenye uchumi. Unavyojadili elimu lazima ujadili na Uchumi. Sasa uchumi wa mwaka jana wa dunia, na utaona hizi kazi sita ambazo ni muhimu duniani nchi zenye uchumi mkubwa zote ndizo zinashugulika na hizi sita; kama haupo huku lazima uchumi wako utakuwa unadorola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana uchumi wa dunia ulikuwa wa jumla ya trilioni 105 (105 trillion USD dollars). Namba moja alikuwa Mmarekani, uchumi wake ulikuwa trillioni 26.9 sawasawa na asilimia 25.5 ya Uchumi wa Dunia, namba mbili alikuwa China trillioni 19.4 alikuwa na asilimia 18.4, akafuata Japan asilimia 4.2, akafuata Ujerumani asilimia 4.1 na wa tano India, kwa mara ya kwanza, amefika namba tano kwa uchumi wa dunia mwaka jana alikuwa na trillioni 3.7, ambayo ni sawasawa na asilimia 3.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nazidi kusisitiza, hata tukiwadharau wasomi labda tutabaki kwenye uchumi wetu huu. Lakini kama unataka uchumi ambao ni competitive duniani lazima usomeshe watu, na lazima uheshimu wasomi. lakini kama tupo kwenye primitive accumulation utatukana wasomi hawafai chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimechukua India ambayo ni ya tano mwaka jana kwa uchumi duniani nikaangalia ni maeneo gani ambayo India inayawekea mkazo. Yaani kijana wa India anakazana awe na elimu gani ili apate ajira ambazo ziko juu India. Angalia ile ya dunia, angalia na India. India wanaotafutwa namba moja ni data scientist, namba mbili block chain engineer, block chain ya kucheza na data, ndizo kampuni kubwa kama Amazon zinakuwa na data hizi. Ndiyo Amazon anataka ma-Engineers kama hawa block chain, kazi namba tatu India ni digital marketing. Ndiyo maana mnanunua vitu kwenye mitandao sasa hiviā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana, Mheshimiwa Professor.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia dakika moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tano ni machine engineering, sita artificial intelligence. Sasa kwa mfano Wachina; nimalizie na wewe ni mchumi, ni muhimu sana. Angalia India ilivyowekeza kwenye science na technology mwaka 2021, GDP yake ilikuwa dola trillioni 3.2, mwaka 2023, mwaka jana GDP ya 3.7, trillion ameongeza 0.5 trillion ndani ya miaka miwili. Na mwaka huu anategemea kuvuka zaidi ya trillioni nne za Kimarekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pendekezo langu kwa upande wa elimu lazima tuwekeze sana kwenye science na technology na tuheshimu tafiti, ahsante sana. (Makofi)