Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kidogo. Napenda tu kusema naipongeza sana Serikali ya Mama yetu Samia Suluhu kwa maendeleo yaliyopatikana katika kipindi chake cha miaka mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwangu Musoma Mjini karibu changamoto kama siyo zote, basi tunakaribia kuzimaliza. Kwa maana tulikuwa na tatizo la maji, lakini mpaka hivi leo ninavyozungumza mabomba ya mwisho yameshafika kwa ajili ya kumalizia maeneo machache ambayo yalikuwa yamebaki bila maji. Pia namshukuru sana kwa maana tulipata fedha za kutosha, tumeweza kujenga vyumba vizuri vya madarasa, vyumba vipya pamoja na Shule za Msingi na Sekondari. Kwa hiyo, namshukuru sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tumeendelea kupata fedha kwa ajili ya kujenga vituo vya afya pamoja na zahanati. Mpaka hivi tunavyozungumza nilikuwa na kero kubwa sana ya stendi, lakini mpaka leo tunavyozungumza, tayari ma-consultancy wako site kwa ajili ya ku-design stendi mpya ambayo itakuwa kwenye Kituo chetu cha Bweri. Hii ni sambamba na barabara za lami ambazo zina-cover barabara ya Mtende, barabara ya Shabani kuelekea kule kwenye Kwangwa Hospitali. Hii ni pamoja na Soko la Nyasho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kusema nini? Mambo mengi mazuri kabisa yanaweza kufanyika, lakini yakajitokeza mambo machache sana yakawafanya wananchi na watu wakasahau yale mazuri yote yaliyofanyika. Kwa mfano, kwenye shule zetu za msingi na shule za sekondari, ukienda unakuta kuna vyumba vizuri sana vya madarasa vimejengwa. Sambamba na hilo, viko vyumba ambavyo ni vya zamani na maboma ya zamani. Cha ajabu, utakuta kuna wanafunzi wanakaa kwenye darasa zuri, lakini wapo wanafunzi wanaokaa kwenye madarasa ya ovyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unapokuja kuniambia Serikali wanasema hebu iambieni halmashauri itenge fedha. Kwanza, leo halmashauri zetu nyingi zilisha-paralyze hazina hata mapato. Kwa hiyo, kwa namna yoyote ile, Serikali mlishasema kwamba hata wananchi sasa tuanze kuwapumzisha kwenye kutoa michango. Sasa, unajiuliza, hali hii tutaivumilia mpaka lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachotaka kusema, hebu sasa leo TAMISEMI watuambie wamejipangaje kumaliza vyumba vya madarasa ambavyo havijamalizika. Wamejipangaje kuhakikisha kwamba watoto wetu wote hakuna anayekaa chini? Sambamba na hilo, bado lipo tatizo kubwa la upungufu wa walimu. Unajua kuna hatua ambayo mwanafunzi akiipita ameipita. Leo unakuta kuna baadhi ya walimu especially wa sayansi unakuta shule nzima haina mwalimu wa physics, kemia na biology. Unakuta kwa vyovyote vile kwenye yale matokeo ya form four unakuta watoto wengi karibu nusu ya darasa wanapata division zero. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nadhani pamoja na mambo mazuri ambayo yamefanyika, lazima Serikali ijikite ihakikishe kwamba, kwenye haya madhaifu au huu upungufu uliopo, itenge fedha, vyumba vizuri vya madarasa viwepo, madawati yawepo, walimu wapatikane, watoto wetu wasome ili maisha yao yaendelee kuwa mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, hata kwenye vituo vya afya tunashukuru. Mfano, ukienda pale kwangu kuna Kituo cha Rwamlimi, Serikali imeleta fedha, tumejenga Kituo kizima cha Rwamlimi kimekamilika. Tofauti na hapo, jirani yake tu kuna Kituo cha Afya cha Bweri, kila siku mimi nikisema, hapo Mawaziri wanasema halmashauri itenge fedha. Sasa itatenga fedha mpaka lini? Nashauri tujipange tu tuweze kupeleka fedha ili vile vituo vyote vya afya view vizuri na viweze kutoa huduma nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni kati ya upungufu mkubwa ambao bado upo ambapo pamoja na mafanikio mengi makubwa yaliyofanyika, haya machache yanaendelea kutuchafua. Niwaambie kwamba huku tunakoenda safari hii ndugu zangu wa TAMISEMI, kusema kweli niwaambie kabisa, bahati nzuri tunaonana uso kwa uso. Safari hii rafiki zangu shilingi yenu naenda nayo. Kwa sababu haiwezekani huu upungufu uliopo uendelee kutuchafua wakati tukijipanga vizuri, wala siyo fedha nyingi zinatakiwa, tunaweza kuyamaliza na watu wetu wakaendelea kuishi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, liko jambo ambalo sasa aidha Wizara ya Afya ilitolee tamko au iamue. Sera yetu inasema hivi, mtoto chini ya miaka mitano atibiwe bure, mama mjamzito apate huduma za kujifungua bure. Naamini hata kule kwako hali kama hiyo ipo. Siku moja ilitokea nikaenda tu ghafla kwenye kituo kimoja cha afya nikakuta akinamama wanane wamejifungua, kila mmoja ametoa shilingi 120,000 shilingi 80,000 na kadhalika. Sasa ukimwuliza daktari, anasema Mheshimiwa Mbunge ni kwa sababu hatuna dawa, kwa hiyo, tunalazimika kuwa-charge fedha. Sasa tuna sababu gani ya kusema kwamba hizo huduma wanazipata bure, lakini wakati huo huo wakienda kule wanaweza kuwa charged?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, hata kuna siku moja ambayo nilienda kwenye mkutano, nikasema akina mama wanatibiwa bure, walinistahi tu kwa sababu mimi ni Mbunge wao, lakini ukiona akina mama wamevaa nguo za CCM wanaguna, ni kwa sababu hao wote wanalipia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaamua moja, aidha itoe hizo huduma bure kama ilivyosema na isimamie, na kama haiwezi, basi iwaambie wananchi kwamba wachangie ili wazoee na waone kama ni jambo la kawaida, kuliko kuwaahidi kitu ambacho tunadhani kwamba hatuna uwezo wa kutekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ambalo sielewi kwamba ni kwa nini limechukua muda mrefu na hata Serikali ilifikia mahali ikasema kwamba limeisha lakini halijaisha, ni mikopo kwa ajili ya akinamama, watu wenye ulemavu pamoja na vijana. Sasa, zile fedha tulifika mahali Mheshimiwa Rais akasema utaratibu wake hauendi vizuri, kwa hiyo, anasitisha ili Waziri mwenye dhamana apange utaratibu mzuri na hatimaye hizo fedha waweze kukopeshwa. Sasa leo nadhani ni mwaka wa pili, utaratibu kila siku tunaendelea kusema unapangwa, lakini haujakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yako, hata zile fedha ambazo tumewaambia kwamba zinaendelea kutengwa kule halmashauri, hivi wanatengaje fedha wakati kule Madiwani hawana posho?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimalizie tu kwamba hebu Serikali iweze kulimaliza hilo na iweze kuwaruhusu wale akina mama waweze kukopesheka na maisha yao yaweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)