Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa na mimi fursa niweze kuchangia katika hotuba hizi mbili za Wenyeviti wa Kamati muhimu za Kudumu za Bunge. Kwanza naanza kumpongeza Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mheshimiwa Mhagama, kwa kuwasililisha vizuri Hotuba ya Kamati lakini na ile ya TAMISEMI chini ya Mheshimiwa Dennis Londo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda kuchangia maeneo machache. La kwanza kabisa, naomba kuanza na hili la Maslahi na Posho za Waheshimiwa Madiwani pamoja na Viongozi wa Serikali za Mitaa. Ukifwatilia mjadala wa hapa leo kwenye hizi Kamati, hasa ya TAMISEMI, utasikia sauti za Waheshimiwa Wabunge wakilizungumzia jambo hili. Mimi kipekee, naipongeza sana Serikali, katika Awamu hii ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweza kuhakikisha kwamba Mheshimiwa Diwani anapata fedha yake, ile posho yake bila kukopwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Madiwani walikuwa wakikopwa posho zao lakini hivi sasa angalau wana uhakika wa kupatiwa fedha zile kwa sababu zinalipwa moja kwa moja na Serikali Kuu. Hii ni hatua kubwa na kwa mantiki hiyo, ninaiomba Serikali yangu ya CCM, iendelee kuwa sikivu na iendelee kumtazama mwananchi mnyonge hasa huyu Mheshimiwa Diwani pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji na Mtaa ambaye yeye ndiye ana-deal moja kwa moja na Miradi ile ambayo sisi tunaipitisha hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye ndiye anaishi na wananchi kila siku, changamoto zinazojitokeza kwenye jamii yetu yeye ndiye anahangaika nazo. Kwa mazingira hayo, ninarudi tena kuiomba Serikali yetu hii ya CCM ambayo ni sikivu sana, imsikie tena Diwani kilio chake cha kumwongezea ile posho inayompa ya shilingi 350,000 kwa mwezi. Posho ile ni ndogo, ukiangalia hata currency tu ya nchi sasa hivi, ukiangalia mfumuko wa bei, thamani ya shilingi hivi sasa, kwenye matumizi ya kawaida tu, shilingi 350,000 ni fedha ndogo sana haikidhi mahitaji ya mtu mzima ambaye tunasema ni kiongozi, tena anasimamia Wataalamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Diwani anamsimamia mtu ambaye ni graduate kwenye eneo lake lakini yeye analipwa shilingi 300,000. Hawezi kuwa na sauti, hawezi kuwa na confidence, anasimamia miradi ya mamilioni ya fedha lakini yeye analipwa shilingi 300,000, hawezi kuwa na confidence. Ndiyo unakuta hapo na yeye anaingia katikia ku-temper kuhakikisha na yeye anapata chochote kwenye miradi tunayoipeleka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, endapo ataongezewa kutoka hii shilingi 300,000, ifike hata basi shilingi milioni 1kama kule Zanzibar. Ikishindikana hiyo basi hata nusu yake, apate hata shilingi 700,000, aweze kukidhi, kumudu, kukidhi maisha yake ya kila siku. Naomba hili, Serikali yangu hii iweze kulichukua hili na kulitazama, huko tunakoelekea kwenye bajeti hii inayokuja hata ile nyingine, kabla ya kwenda kwenye uchaguzi unaokuja, angalau Mheshimiwa Diwani awe ameongezewa kiasi fulani kwenye posho yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo, naomba kuambatanisha na suala la ukubwa wa maeneo yetu ya utawala hasahasa kata na vijiji. Tunazo kata kubwa kwelikweli, ninayo Kata moja inaitwa Ughandi, ni kubwa inakaribia jimbo, ninayo Kata ya Mtinko, kubwa kwelikweli, nina Kata ya Makuro, Ngimo, mpaka kule kwa jirani zangu kule Mkalama kuna Kata inaitwa Mwangeza, kutoka mwanzo wa kata kwenda mwisho wa kata ni kilometa 70. Kata ya Ibaga, ni Kata kubwa yenye vijiji tisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, haya maeneo naomba sana Serikali yangu hii, itusikie, iende kuyagawa, tupelekeeni Watendaji wa kata, tupelekeeni Watendaji wa Vijiji ili tumuhudumie mwananchi. Kumfuata Mtendaji wa Kata kutoka kilometa 70, ni umbali mkubwa ukiangalia na hali za maisha za wananchi wetu. Naomba sana tulitazame hili jambo kwa ukaribu ili tuweze kuleta tija kwenye kazi tunazozifanya za kuwahudumia watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia upande mwingine wa Bajeti hizi tunazozipitisha hapa. Tunapitisha bajeti tunasema ziende zikatekeleze miradi ya maendeleo, lakini fedha haziendi kwa wakati kwa hiyo, utekelezaji wa miradi haufanyiki kwa wakati. Wakati mwingine, tunapitisha fedha lakini hakuna kabisa utekelezaji. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, tubadilishe utaratibu, fedha tunazopitisha hapa ziende kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaleta manung’uniko kwa wananchi mathalani hapa kwenye Bajeti hii iliyopita, nilitoa machozi hapa nikililia barabara yangu ile ya Singida – Ilongero Makao Makuu ya Halmashauri, mpaka hapa tunakwenda kwenye bajeti nyingine, fedha hazijaja. Hii inaleta hata mashaka kwa wananchi kule kwamba huenda tumedanganywa lakini kama fedha zingekuja kwa wakati, leo hii tungekuwa tunaifurahia Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana, Serikali ihakikishe fedha tunazozitenga hapa kama Waheshimiwa Wabunge, ziende kwa wakati zikatekeleze ile miradi ya maendeleo, kuna Kituo cha Afya pale Changimu, mpaka leo fedha hamna wakati tulishakubaliana fedha ziende. Kwa hiyo, niombe tunapopitisha vitu hapa, vitekelezeke kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la upungufu wa Watumishi kwenye maeneo yetu, kwenye Sekta ya Afya, Elimu, Utawala, Walimu. Tuna kilio kikubwa sana kwenye maeneo yetu kuhusu Upungufu wa Watumishi, niombe sana…

MWENYEKITI: Ahsante sana. Ahsante sana Mheshimiwa Abeid.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, huu muda ni mchache sana, ile programu ya Dr. Samia Legal Aid Campaign ambayo imepelekwa kule na Mheshimiwa Rais wetu kutoa msaada wa Kisheria kwa wananchi wetu kule masikini, ishuke iende mpaka kwenye vijiji, iongezewe manpower. Watumishi wale wanasheria wa Halmashauri waende mpaka kule kwa wananchi vijijini ili hii programu iwe na manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)