Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia mada iliyopo mezani. Awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetupa wasaa huu wa kuweza kupata fursa ya kujadili taarifa hii kwa manufaa ya Watanzania wote. Nachukua nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa pamoja na Serikali kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI nielezee tu kidogo kwamba Kamati ya TAMISEMI na TAMISEMI kwa ujumla pamoja na Utawala Bora kwa maana ya Utumishi na Utawala Bora ni Kamati muhimu sana pia ni Wizara muhimu sana kwa sababu inahudumia nchi nzima, nizungumzie tu kwamba jukumu hili la TAMISEMI limekuwa na mzigo mkubwa sana na mahitaji makubwa kama nchi, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali na Kamati yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na TARURA; Wakati tunaunda chombo hiki cha TARURA nilikuwepo Bungeni, kilikuwa chombo ambacho hatukukiamini kwamba kitafanya kazi kubwa sana kama kinavyofanya sasa kwenye majimbo yetu yote hapa nchini. TARURA ina kazi kubwa, tumeongeza mtandao wa barabara kwenda zaidi kwa wananchi na katika maeneo ambayo ni muhimu sana. Imekuwa kichocheo kikubwa sana kwenye shughuli za kijamii kwa maana ya miundombinu ya barabara ambayo TARURA inahudumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumshukuru Mungu kwa kutujaalia mvua mwaka huu, Mikoa kadhaa tumepata mvua kubwa sana ukiwemo Mkoa wa Manyara lakini hali ya barabara ni mbaya sana. Naungana na wenzangu wote, Serikali itakapokuja kutupa mrejesho, kwanza itupe kauli ya kupata zile fedha ambazo tayari tulishaomba kwenye bajeti iliyopita pamoja na nyongeza ya fedha shilingi bilioni zaidi ya 300 ili kuweza kurekebisha hali mbaya ya miundombinu iliyotokea kwenye Majimbo yetu, hasa mkoa wa Manyara umeathirika sana mtandao wa barabara kwa sababu mvua imenyesha zaidi ya miezi minne na hadi sasa inanyesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Watendaji na Watumishi unakuta wako wachache sana. Eneo hili litazamwe upya tuongezewe fedha, tunaiomba sana Serikali kwa sababu barabara tulizoongeza zinahitaji kufanyiwa matengenezo lakini nyingine zimeathirika na madaraja na miundombinu nyingine kwa ajili ya mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue tena nafasi hii kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati niongezee eneo la Madiwani, mimi ni Diwani nimetumikia miaka 10, baadae nimekuja sasa hivi ni miaka nane nikiwa Mbunge. Hali ya Madiwani wetu wetu ni mbaya sana kote nchini. Diwani ambaye alikuwa anapewa posho ya shilingi 65,000 mara mbili sasa hivi anapewa shilingi 80,000 kwa maana 40,000 mara mbili. Diwani aliyekuwa anapokea miaka 12 iliyopita 350,000 mpaka leo, hali hii inatisha sana na kwamba viongozi hawa kwa ngazi yao wamesahaulika sana. Tunaiomba Serikali itazame katika bajeti inayokuja ije na mpango mpya wa kuwaongezea fedha au wa kuwaongezea malipo ili kunusuru kada hizi ili tusiwe na tabaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wenyeviti wa Vijiji, mimi Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI, yaliletwa majibu mwaka huu kwa swali langu langu la msingi likijibu shilingi bilioni 220 zimetengwa kwa ajili ya kuwahudumia kundi hili la wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji kote nchini lakini hadi hivi tunavyoongea Halmashauri chache zenye uwezo ndizo zinazolipa wenyeviti wa vijiji na vitongoji na mitaa kwa ajili ya uwezo wao wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Halmashauri nchini hatuwezi kulipa hata ingekuwa miaka kumi, moja ni Halmashauri ya Mji wa Mbulu, mapato yake ni madogo. Hali hii ya ngazi au tabaka fulani inalipa wenyeviti wake na tabaka fulani haliwalipi inaweka tabaka na chuki kwa viongozi hao wa ngazi za chini. Yeyote ajae akija kule kwenye vijiji na kwenye ziara awe Rais, awe Waziri au awe nani Mwenyeviti wa Kijiji, Kitongoji na Mtaa wanahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zozote zinazotolewa iwe ni miradi ya maendeleo viongozi hao wameteseka wamefanya kazi kwa jinsi walivyoweza, tunasema ni kazi ya kujitolea lakini walau kwenye bajeti inayokuja Serikali yetu sikivu ije na utaratibu wa kuja walau na mpango wa kuwapa posho. Tumejitahidi mambo mengi sana makubwa hili nalo linawezekana panapokuwa na nia njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la walimu. Tunaipongeza sana Serikali tumejenga shule mpya nyingi sana nchini, shule mpya na madarasa. Moja kwa moja hali hii inachochea uhitaji wa walimu wapya na nyumba za walimu. Hili la walimu wapya tukilinganisha na ajira za miaka iliyopita kundi hili la walimu hatutapata watumishi kwa vyovyote vile na hawataweza kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira yao pia ni mabaya sana. Makazi ya walimu nchini, hali ni mbaya sana kundi hili la walimu, sote tiulioko hapa uwe mtu wa kusoma na kuandika na kuhesabu, uwe mtu wa PhD, uwe mtu wa taaluma gani na uwe na shahada mwalimu ndiye aliyekuwa tanuri lako na alikuwa tanuri letu. Naiomba sana Serikali iangalie eneo hili la nyumba za walimu pamoja na maslahi ikiwezekana na ruzuku ya ufundishaji iwepo. Pia, namna ambavyo nyumba zitajengwa na taasisi hizo zinazojenga kwa maana ya TBA, National Housing pia Watumishi Housing kwenye maeneo ambayo yana changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalimu anatoka kilomita tano mvua inanyesha anakwenda kufundisha, anarudi nyumbani kupata chai ya asubuhi, baadaye chakula cha mchana, baadaye kurudi shuleni na hatimaye kwenda, mshahara wake ukiufanyia mahesabu unaishia kwenye gharama za kutembea, kupata huduma pia na maeneo wanayoishi. Hali ya watumishi wetu hawa imekuwa mbaya sana na wao lazima tuwasemee Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza Mheshimiwa Rais, alipokuwa Mwanza aliwaunganisha na Waziri wa TAMISEMI akawaahidi ujenzi wa nyumba za Walimu nasi tujiongeze zaidi ya eneo hilo la ahadi ya Mheshimiwa Rais. Taasisi hizi tuzihamasishe kwa maana ya TBA, National Housing pia Watumishi Housing Cooperation kwa sababu hawa wana fursa ya kujenga jengo na kumkopesha mwalimu na akakatwa muda wote wa utumishi wake akagawiwa kwenye miezi nyumba hiyo mwisho wa siku ikawa ya kwake. Hilo linawezekana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tutazame hali ambayo wanakabiliana nayo wanayo madai mengi. Serikali itazame upya, tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ililipa madeni mengi, kwanza tuyazuie yasizalishwe mengi lakini pia yale yaliyokwisha kuwepo yaweze kufanyiwa kazi na kulipwa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mfumo wa ukusanyaji wa mapato ambao siyo mzuri. Serikali itazame upya, tumehama kwenye mfumo tumekuja kupata mashine za kukusanya fedha hizi POS. Hizi POS zimekuwa na tatizo la ukusanyaji wa mapato. Haiwezekani mashine zinatolewa na ofisi ya Mkurugenzi halafu kesho tunakuta nyingine ni fake haziingizi hela kwenye mfumo ama zinachezewa na watumishi bila hatua zinazochukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hii hali ya kuwahamisha hamisha watumishi ambao wana dosari zao Serikali iangalie upya kutokuwahamisha iwaondoe kabisa. Hii itasaidia watu kuwa na nidhamu katika kutumikia nafasi zao pia kwa namna ambavyo wanaweza wakawa waadilifu katika utumishi wao wa umma, pia kutokuongeza matatizo kwenye maeneo mengine ambayo yalikuwa yanafanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Utawala Bora, tunamshanga sana Mheshimiwa Makonda Katibu Mwenezi wa Itikadi anapofanya ziara. Yale mafuriko, mafaili, mabango na nyaraka zinazopelekwa kwenye ziara za Katibu wa Itikadi na Uenezi ni dhahiri kuwa ni picha ya wazi tuna kazi ya kutazama upya mfumo mzima wa Utawala Bora katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani kiongozi mkubwa anakuja mabango yanaletwa 1,000 kila anakoenda hawezi kufika mahali anakuta ni watu wengi wanajitokeza kutaka ufumbuzi wa matatizo yao.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili muhimu sana litazamwe upya kwa namna inayowezekana ili tuwezeze kufanyia kazi kama Serikali na wananchi wetu waweze kuona umuhimu wa Utawala Bora katika nchi yao na huduma bora lakini pia…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Issaay.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, mengine nitaandika kwa maandishi. (Makofi)