Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia kuwepo katika siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha halali na wala hapumziki akihakikisha ana nia nzuri ya kutaka kuleta maendeleo ya Tanzania. Wabunge wote tuungane tumsaidie Mheshimiwa Rais, kwenye mapungufu tuyaongee tusiyanyamazie. Tumefikia mahali ambapo unaona Mheshimiwa Rais anakimbia na anataka Tanzania iwe na maendeleo na mabadiliko makubwa yaonekane lakini anakwamishwa na makundi machache ambayo yamejificha wanataka kujiona wao wanafanya kazi lakini bado unaona kuna mapungufu makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza; ukikwaji wa Sheria za Manunuzi ni mojawapo ya hoja ngumu ambayo sasa hivi tunakwenda nayo kama mwiba wa nchi. Nikupe mfano, Mheshimiwa Rais alikwenda kutafuta fedha za mikopo katika upande wa Covid zikapelekwa halmashauri. Cha kusikitisha muda ule ule tu sementi ilipanda kutoka shilingi 14,000, shilingi 15,000 mpaka shilingi 30,000 baadhi ya mikoa. Bati zilipanda kutoka shilingi 15,000 mpaka shilingi 30,000, hali ya manunuzi ilikuwa ni mbovu, unajiuliza alipita mdudu gani mpaka kufikia katika mazingira yale. Maana yake kuwa watu wanangojea ahangaike kutafuta pesa wao watumie zile pesa kwa wanavyotaka, ukikwaji huu ni dosari kwa nchi yetu

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia mifumo, kila Wizara sasa hivi kuna mifumo ya kidijitali, mifumo hii haiongei. Kama mfumo hauongei maana yake bado tunaendelea kujikuta tunakwenda katika kianalogia badala ya kwenda kidigitali. Nikupe mfano, leo katika baadhi ya Wizara, wana uwezo wa kupata fedha za ndani za kutosha za kuifanya Wizara ile isiwe tegemezi tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, tulisema tutaanzisha vitambulisho vya wafanyabiashara ndogondogo, tukasema tutawafanyia nini? Walipe shilingi 20,000 ile Sh.20,000 ambayo wangetoa ukizidisha kwa wafanyabiashara ndogondogo iwe 30,000 tu, unaweza kupata shilingi trilioni sita. Naomba chukueni calculator zenu halafu mfanye hesabu hizi, lakini jiulizeni mfumo ule umekwenda wapi? Umeachwa. Tumerudia mfumo wa kila siku tunatoa Sh.1,000. Sh.1,000 kwa siku 30 inakuwa ni shilingi 30,000, 30,000 kwa mwaka mmoja mfanyabiashara ndogondogo analipa shilingi 360,000, hivyo tukiwa na wafanyabiashara ndogondogo wachache tu, nikupe mfano 7,500, tuna uwezo wa kukusanya zaidi ya shilingi trilioni 3.6.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tujiulize, sisi na usomi tuliokuwa nao, wasomi wanamsaidiaje Mheshimiwa Rais kutafuta hela za ndani zikafanya kazi, matokeo yake wanangoja ziingie pesa za OC wazitapakanye, wazitumie wanavyotaka wao, matokeo yake miradi mingi inakuwa imesimama. Siyo imesimama hivi hivi tu, ni mifumo tu haiongei. Baadhi ya watu kuisimamisha mifumo kutoongea ni kikwazo cha maendeleo ya uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali kama hii tusingekuwa tena tunakwenda kukopa, tunakopa nini wakati tuna hela yetu ya ndani? Shilingi bilioni 3.6 zikienda katika kukopesheka kwa wafanyabiashara ndogondogo tunakwenda kukopa tena hela za nje, tunazo hela zetu zinazokwenda katika mabenki, watu wangekopeshwa tusingekuwa hivi, lakini tumesimama hivi kwa ajili ya nini? Kwanza sisi si wabunifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi za jirani wanatupita kwa kila upande maana yake tuna uwekezaji, tuna maeneo mazuri, lakini kwa vile wenzetu ni wabunifu, wametupita vibaya sana, hapa Rwanda tu wanatupita. Sasa Mheshimiwa Rais anahangaika, Mheshimiwa Rais halali, nchi una uchumi mkubwa sana, nenda kwenye madini tupo sisi. Madini sasa hivi yamekuwa ni katika kila mkoa, leo Lindi ni kuchele madini tupu, lakini jiulize mifumo inaongea? Kama haiongei itakuwa tunacheza nini? Tunaimba lakini bado tunaifanya nchi kuwa imesimama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kushindwa kulipa madeni; wakandarasi, mimi wananijua wakandarasi kunishtakia mpaka najiuliza mimi sina uwezo, mkandarasi anajikuta toka mwaka 2013, alifanya kazi Serikalini anaambiwa tutakulipa mwakani, ikija mwakani, mwakani, mpaka sasa hivi wale watu wanadai mabilioni, billions of monies. Tunajiuliza hivi yeye huyu mtu alichukua mkopo benki, anauziwa majumba yake, mali zake zinakuwa confiscated. Je, tumefikia wapi? Hii ni dhuluma, dhuluma kubwa sana kwa makandarasi na wafanyabiashara ambao wamekopa wakafanya kazi kubwa lakini …

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Riziki kuna taarifa. Mheshimiwa Waziri.
TAARIFA

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mama yangu, Mheshimiwa Lulida kwa mchango mzuri, lakini ningependa kumhakikisha kwenye upande wa makandarasi, Serikali sasa hivi tuna mkakati mzuri. Kuanzia mwezi Agosti tumeanza kulipa makandarasi shilingi bilioni 70 kila mwezi. Kwenye shilingi bilioni hizi 70 tumeanza kuwapa vipaumbele wakandarasi wazawa, shilingi bilioni 50 kila mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelipa shilingi bilioni 50 mwezi Agosti, tumelipa bilioni 50 mwezi Septemba, tumelipa shilingi bilioni 50 mwezi Oktoba na bado kuna shilingi bilioni 17 kwa wakandarasi wazawa ambao wanadai mpaka tarehe 30 Juni, 2023, tutawalipa hizi shilingi bilioni 17 mwezi huu Novemba. Kwa hiyo, Mama yangu Mheshimiwa Lulida kwa upande wa Serikali tumejipanga vizuri lakini nimhakikishie hata makandarasi wa nje zile shilingi bilioni 70, kuna shilingi bilioni 20 ambayo tunawalipa kila mwezi na tukishamaliza wakandarasi wa ndani, basi tunaanza kuwalipa shilingi bilioni 70 wakandarasi wa nje, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Riziki umeipokea hiyo taarifa?

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza katika kijana msikivu, mnyenyekevu, hii ni mara ya pili nampongeza. Nakupongeza ndani ya moyo kuwa ni msikivu, lakini naanza na wewe, nina wafanyakazi wa TAZARA wamestaafu huu ni karibia mwaka wa 10 wametembea katika Kamati zote mpaka Wizara, mpaka Wizara ya Fedha nimekwenda nao hawajalipwa mpaka leo haki zao. Nina Wafanyakazi wa ATCL nao wamehangaika, wale mpaka wengine, kwa mfano TAZARA walikuwa watu 473 karibu wastaafu 73 wameshapoteza maisha yao, wamekufa kutokana na Mwenyezi Mungu kuwachukua, wao wanadai madai yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi wa ATCL, kwa vile umeshaniambia hivyo, nimetulia ila nakwambia nakuletea watu wangu, tena mimi nitakuwa mwakilishi wao. Kwa vile wananifuata mimi, wameona tunapeleka kwa Mama Lulida, hili nawaambia kabisa, waliko huko wananisikia, nakuja kwako wewe ili uweze kuwasaidia hawa watu kwa vile hali ya watu hawa ni ngumu hasa TAZARA, ATCL Makandarasi wananifuata. Nikupongeze sana, nilikuwa nataka kuongea mengi, lakini kutokana na hilo uliloniambia hapo kwa upande wako nimeacha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mawakala, tumefanya kazi nyingi sana kwa kupitia Mawakala, hawa Mawakala waliopewa kazi nyingi sana za kandarasi wamekuwa mwiba wa nchi. Makusanyo yanayopitia kwao hayafiki katika Serikali Kuu. Hivyo ningeomba kwa hawa Mawakala ambao tunaona kabisa, tunaona humu ndani, wewe umeshapewa kazi, lakini kwa nini unaukwepa mfumo, anau-by pass mfumo. Mfumo anauzima unakuwa haufanyi kazi, matokeo yake zile hela ambazo zilibidi ziingie Serikali Kuu zinaingia katika mikono ambayo siyo sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo nasema na hili nalo tulifanyie kazi. Nasema tena kwanza Mheshimiwa Waziri amenipoteza katika reli, hapa leo naondoka na furaha kubwa sana, yote yale niliyotaka kuzungumza leo nimeishia hapa. Nasema Mwenyezi Mungu awabariki tupate viongozi kama Mheshimiwa Innocent Bashungwa, anayetaka kusikiliza vilio vya Watanzania, yuko tayari kusikiliza kero za Watanzania. Waheshimiwa Mawaziri wajifunze kwa Mheshimiwa Bashungwa kutoka hapo migogoro mingine mingine itapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho, uwakala wa upimaji wa viwanja katika halmashauri imekuwa ni mwiba na hii inaonekana Wizara ya Kisekta haiko pamoja na halmashauri. Mtu wa halmashauri anapima kivyake na Wizara inafanya kazi yake, matokeo yake mfumo huu wa upimaji wa viwanja umesabisha migogoro Tanzania nzima. Ningeomba tukae chini tuangalie hii mifumo isiyoongea tutaisaidiaje. Kwa mfano, mfumo wa ardhi hauongei na wa halmashauri, lakini vilevile pesa za majengo ambazo zinatolewa katika baadhi ya taasisi ikiwa katika Wizara zingine kama Kazi …

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Riziki kuna taarifa nyingine kutoka kwa Mheshimiwa Jerry Silaa, Mheshimiwa Waziri.

TAARIFA

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mama Riziki Lulida, ni kweli kumekuwa na matatizo mengi kwenye upimaji wa ardhi kwenye maeneo mengi nchi nzima lakini hatua zimeanza kuchukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mosi, Serikali imesha-centralize utendaji kazi wa watumishi wa ardhi nchi nzima kwa ngazi ya wilaya, mikoa na Wizara ya Ardhi. Hivi ninavyozungumza tumeendelea kutoa maelekezo na kupitia Bunge lako Tukufu, watumishi wote wa ardhi wa ngazi za wilaya wazingatie taaluma zao wanapofanya kazi za ardhi; lakini maeneo mengi yenye mkwamo ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam ambapo zoezi la urasimishaji lilikuwa na mkwamo, tayari kupitia mradi wa Land Tenure Improvement Project (LTIP) tumeanza kuukwamua. Nilithibitishie Bunge lako kwamba kufikia Disemba 31 maeneo mengi matatizo haya yatakuwa yamekwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Riziki unaipokea hiyo taarifa?

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea hiyo taarifa na yeye vile vile nina msururu wa watu ambao nitakwenda nao kwake Mheshimiwa Silaa kwa heshima na taadhima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima alionionesha nakwenda kwake na ma-file ya watu ambao wanadai kihalali, wamenyang’anywa maeneo yao lakini bado kuna usumbufu mkubwa wanakutana nao. Vile vile na yeye ni Waziri wa pili nasema Mwenyezi Mungu ambariki. Tunataka Mawaziri wenye kusimamia, kuleta heshima kwa Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais anataka mambo kama haya, majibu ambayo hayana kando kando, majibu ambayo hayana ulinzi, kwenda kuwalinda watu ambao wanatufanyia vurugu, tunataka vitu vilivyonyooka. Mimi na Mheshimiwa Waziri tunataka twende kwenye rula, Mheshimiwa Innocent Bashungwa twende kwenye rula. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nasema nikushukuru sana na Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)