Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nami naomba kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutujali sana wana-Kinondoni. Tulikuwa na shida ya secondary schools mbili katika Kata ya Kinondoni ambayo imeshajengwa, ilibakia Kata ya Tandale nayo kwa sasa tumepata secondary school. Hivi tunavyozungumza, wananchi wanaopisha Mradi wa Bonde la Mto Msimbazi wameshaanza kulipwa fidia na wengine ambao walikuwa wameomba tathmini upya, wanafanyiwa tathmini. Hivyo, Serikali mambo ni bulibuli. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichobakia ni kwamba nilikuwa nimeomba high school na nilizungumza pia na Mheshimiwa Waziri Mkuu, mapendekezo hayo na maombi yangu nimeyapeleka Serikalini ili Kinondoni iweze kupata high school kwa maana ya form five na six.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nataka niangalie dhamira ya Serikali katika uwekezaji kwa umma. Hapa inanipeleka kuona kwamba Serikali inawekeza fedha nyingi kwa madhumuni ya kuimarisha sekta za kibiashara, sekta za utoaji huduma, na vile vile, kuchochea uchumi mpana ili hatimaye fedha ziweze kupatikana, zichangie katika Mfuko Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kustawisha Watanzania wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo unaiona kwenye dhamira ya Serikali, kwa sababu mwaka 2017/2018 uwekezaji katika sekta ya umma ulikuwa ni shilingi trilioni 55.76. Sasa katika kipindi cha miaka mitano, uwekezaji umekua na kufikia shilingi trilioni 73,37. Hii inaonesha dhamira ya Serikali. Sasa mtu yeyote anayewekeza, madhumuni yake ni kupata returns. Sasa hapa ndipo kwenye matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana TR, Bwana Nehemia Mchechu pamoja na timu yake, kwa kuleta mageuzi makubwa katika Ofisi ya TR, kiasi kwamba gawio limeweza kupanda na kufikia shilingi bilioni 850. Hii yote inaonesha seriousness ya Ofisi ya TR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna matatizo katika ulipaji wa ile asilimia 15. Nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, mimi nimewahi kubahatika kufanya kazi kama Mkurugenzi Mkuu wa Gambling Board of Tanzania, taasisi ambayo haikuwa imetakiwa ilipe gawio wala mchango, lakini iliweza kufanya kazi ya kutoa mchango kwa hiari mapema kabla ya sheria. Maana yake ni kwamba baada ya ujio wa sheria, matakwa ya kulipia asilimia 15 ni lazima yatekelezwe na hakuna option katika hiyo. Utaona taasisi nyingi mpaka sasa hivi zinategemea ruzuku, hata kama taasisi imekaa miaka 10 au 15, bado inategemea ruzuku. Hii inafanya watu wabweteke, wasifanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mwenyekiti wa LAAC alipokuwa anazungumza, anawataka halmashauri na taasisi za umma ziache fikra za kuendelea kupata ruzuku. Hili jambo ni lazima TR aelekezwe, afanye uchambuzi; awape muda wakuu wa taasisi wanaotegemea ruzuku, wafanye kazi, waondokane na tabia ya kutegemea ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utashangaa hao ambao wanategemea ruzuku, mwisho wa siku wana-post ziada. Sasa kama wewe ulikuwa unahitaji ruzuku, ziada unaipata kutoka wapi? Maana yake ni kwamba sisi tunataka zile fedha ambazo zingepelekwa kama ziada zibakie katika Mfuko Mkuu wa Serikali ili zisaidie katika maeneo mengine. Maana yake ni kwamba failure ya kuweza kutengeneza ziada, failure ya kushindwa kulipa asilimia 15, watu wawajibishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mifano ya taasisi mbili; moja DAWASA mwaka 2019/2020 walichangia lakini mwaka 2020/2021 hawakuchangia, mwaka 2021/2022 walichangia. TCCA mwaka 2019/2020 alichangia, 2020/2021 hakuchangia, 2021/2022 amechangia; na wengine wanachangia wakijisikia siyo kwa matakwa ya sheria, ila wakijisikia ndiyo wanatoa mchango, lakini siyo asilimia 15 kama sheria inavyotaka. Unaweza ukashangaa kuna taasisi moja ambayo ni Mamlaka ya Chai, katika kipindi cha miaka mitatu wamechangia shilingi milioni mbili, kama siyo mzaha ni nini? Taasisi ya Umma unachangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali shilingi milioni mbili, kwangu mimi naona ni mzaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, naomba kuwepo na utaratibu kwamba kila mahali ambapo Serikali imechangia, ni lazima watu walete malipo yanayotakiwa kwa mujibu wa sheria. Kushindwa kufanya vile, nashauri Bodi husika pamoja na Mamlaka zile za Menejimenti ziweze kuchukuliwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo kila Mbunge aliyesimama amelilalamikia. Jambo hili linahusiana na Ripoti ya LAAC, PAC na hata Ripoti yetu ya PIC, zote zinaongelea kwa uchungu kabisa jambo linalohusiana na matumizi mabaya ya fedha za Serikali, ubadhirifu na upotevu wa fedha, lakini mbona hatuoni hatua zikichukuliwa? Hapa nashauri Serikali ilete taarifa Bungeni kila baada ya kipindi fulani; kama ni miezi mitatu, watuletee taarifa ni nani amechukuliwa hatua za kinidhamu, nani amechukuliwa hatua za kisheria? Tusikae kimya kwa kuzungumza tu. Tukikaa kimya kwa kuzungumza, hawa jamaa wanaofanya mambo haya wanatusahaulisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize, ni nani mwenye biashara? Mfano binafsi, halafu mtu achukue zile fedha azitumie, wewe ubaki kulalamika, mimi sikubali. Mimi ukichukua fedha yangu, kama sikuwezi, hata kukuloga nakwenda zangu kwetu Tanga, kukupiga hata jini. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali inakaa tunaletewa Taarifa ya CAG, watu wanachukua pesa na ukienda huko mjini lifestyle yao ni nzuri, hawana kipato cha kutosha, pesa wanatoa wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Marekani wana theory yao moja inaitwa Follow the Money. Hakuna pesa ya Serikali inayopotea. Hela ya Serikali lazima ipitie katika muamala. Ndiyo maana mwaka 1997 kulikuwa na film inaitwa All the President’s Men walikuwa wanazungumzia hiyo theory kwamba fedha ya Serikali haipotei. Ukifanya investigations utawakamata. Fanyeni investigations muwakamate wanaoiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo michongo basi ifikie mwisho. Hivi tuibiwe mpaka kiasi gani halafu mwisho tukasirike ndiyo tuoneshe kukasirika? Mimi ningeomba Serikali iwe na ukali katika suala hili ili ile theory nyingine ya Deterrence Theory, mtu anapoadhibiwa na mwingine aone kwamba kumbe nikifanya hivi naweza nikaadhibiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiwe na huruma na wala tusiwabadilishe wafanyakazi kutoka mahali walipoharibu kuwapeleka mahali pengine. Hicho siyo jambo jema. Tunatoa picha ambayo siyo sahihi kwa watanzania. Anayeharibu aharibiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi jamani hamkumbuki, kwa wale ambao tunasoma Biblia Zaburi 119 hadi 195 anasema hivi “wana amani nyingi waipendayo sheria yako wala hawana la kuwakwaza”. Hawa watu wanatuikwaza sisi wanaoiba, wanamkwaza na Mungu, Mungu anakwazika katika hili ndiyo maana ukisoma Zaburi anasema hivyo. Kama wao hawatupatii amani sisi na sisi tusiwape amani, huo ndiyo utaratibu, Tit for tat. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unatuibia, unatufanya tunapoteza muda, tunapoteza fedha za watanzania kujadili mambo ambayo umeyasababisha wewe mwizi, halafu wewe tukupe amani, sisi unatupa tabu, unatukwaza. Huo utaratibu haupo. Ifike mahali tuseme jamani hawa wahusika wote kaeni pembeni. Tena hata mkiwapeleka TAKUKURU, tuletewe taarifa ili tujue nini kinaendelea kule, isibakie kama ni kichaka. (Makofi)

(Hapa Kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Ninaamini bado nina dakika tano, au nimemaliza?

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha lakini malizia kwa dakika moja tu.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka nimalizie kwa kusema naunga mkono hoja zote tatu lakini naomba ikubaliwe kwamba, Kila Taarifa ya Kamati inayokuja hapa ielezee ni hatua gani zinachukuliwa ili mapendekezo ya kutaka kuongelea ruzuku kwenye Taasisi za Umma iweze kukamilika na iachwe kabisa, kusiwe na ruzuku, watu wajitahidi kutengeneza fedha na kuiletea Serikali mapato. Siyo wao kupelekewa fedha. Nakushukuru. (Makofi)