Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Janejelly Ntate James

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa wasaa huu wa kuchangia. Kwanza, nianze kwa kusmhukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa afya njema na uhai. Pia, nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi alivyoboresha hizi Wizara hasa upande wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma, upande wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja taarifa za Kamati hizi mbili. Zote zimejishibisha na zote zimekuja na taarifa iliyokamili. Nianze na Menejimenti ya Utumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza sana kwa marekebisho mnayofanya kwenye utumishi wa umma. Hata hivyo, nina machache ya kuwashauri. Leo asubuhi mmeulizwa swali kuhusu safari ya watumishi wanawake wanaonyonyesha, ule mwongozo uko vizuri kabisa lakini Maafisa Utumishi wanachokwenda nacho wanaenda pale mwisho kwenye mwongozo kwa sababu inasemwa; “Endapo hakuna mtu wa kufanya kazi hiyo.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo “endapo” imewatesa watumishi wanawake wenye watoto wanaonyonyesha kwa kiasi kikubwa sana. Nishauri, kama “endapo” inaweza ikatoka kwenye huo mwongozo basi itoke, kwa sababu si kwamba inawatesa hawa watumishi wanawake tu inatesa na wale watoto, sasa ili mtu aweze kuendelea na hizo kazi, mwisho anamwachisha mtoto kunyonya kabla hajafika miaka miwili ili aendelee na hizo kazi. Niwaombe mkaliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limeletwa suala la njiti, ninawaomba ni wakati sasa wa kuleta sheria humu kwenye Bunge hili Tukufu ya kuwalinda wanawake hawa watumishi wanaojifungua njiti. Sheria hiyo basi iseme kwamba siku ambayo yule mtoto njiti anapokuwa amefikisha umri wa kuzaliwa, sasa ndiyo aanze kuhesabiwa likizo yake ya uzazi, lakini watumishi hawa wanahesabiwa likizo ya uzazi pale anapojifungua kumbe amejifungua mtoto njiti, mtoto yule huwezi kumwachia msaidizi nyumbani, niwaombe sasa ni wakati wa kuleta hiyo sheria ili kuwalinda hawa watumishi wenzetu wanaojifungua watoto njiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee madeni ya mishahra ya watumishi. Mheshimiwa Rais alifanya maksudi mazima, akatoa bajeti ya kulipa madeni ya watumishi, hata hivyo, leo hii bado kuna baadhi ya watumishi wanadai madeni ya mishahara tangu mwaka 2017. Sasa, sielewi utumishi mnatumia kigezo gani, madeni ya 2020, 2019 analipwa, unakuta mwingine wa 2017 hajalipwa. Yawezekana ni mitandao yenu kati ya Wizara ya Utumishi na Idara zinazojitegemea haisomani. Niwaombe mitandao yenu isomane ili watumishi hawa wapate haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende upande wa TAMISEMI. TAMISEMI mmesema ukweli kwamba utendaji kule chini umekuwa hauridhishi. Hata hivyo, nini kinafanya utendaji usiridhishe? Ni upunguaji wa watumishi walioko chini hasa upande wa Watendaji wetu wa Kata, Vijiji na Vitongoji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii baadhi ya Walimu, baadhi ya Maafisa Ugani ndiyo wamekuwa Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vitongoji na Serikali za Mitaa. Sasa, huyu hawezi akatoa huduma kama inavyotakiwa kwa sababu yeye hiyo siyo kazi yake. Niiombe Serikali sasa, ni wakati wa kuboresha watumishi wa Serikali za Mitaa hasa kwenye Utendaji wa Kata, Vitongoji na Vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachosikitisha hata maelekezo yanayotolewa na Bunge lako, bajeti inayopitishwa na Bunge lako, haitekelezwi ipasavyo kwenye Serikali za Mitaa. Bajeti ya Serikali ilipitishwa hapa kwamba, Watendaji wa Kata walipwe posho ya 100,000. Posho hiyo imekuwa kitendawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninao mtandao na Watendaji wa Kata, kuna wengine toka posho hiyo ipitishwe hawajawahi kulipwa. Wengine wanadai miezi 11, wengine wanadai miezi 12. Si vizuri kutaja hizo Halmashauri. Nimeshakaa na Waziri wa TAMISEMI, nimemueleza suala hilo, nimekaa na Naibu Waziri wa TAMISEMI, nimemueleza suala hilo, niiombe leo Serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI, itoe tamko kwa hizi posho za Watendaji wa Kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imefikia sehemu nyingine wanaambiwa mkakusanye ushuru wa matrekta msipofikia malengo hatuwalipi hiyo posho. Sisi hatukupitisha hiyo posho kwamba wanakwenda kufikia malengo, ni haki yao. Wengine wameambiwa hizo hela zitapitia kwenye akaunti za WDC! Hili ni jambo la kushangaza, haki ya Mtumishi anayo akaunti ya mshahara unamwambia hela yake ipitie WDC, ikishapitia WDC ataipata kwa uhakika? hawezi kuipata kwa uhakika.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watumishi wanaolipwa na own sources za Halmashauri, badala kuwa mishahara yamekuwa mateso. Kuna watumishi wengine wanakaa miezi mitatu mpaka minne hajalipwa ule mshahara. Hivi kweli tunategemea huyu atafanya kazi ipasavyo! Maana haki na wajibu vinaendana. Naiomba Serikali iangalie hawa watumishi wanaolipwa mishahara kupitia kwenye Halmashauri, wanateseka. Sasa mtoe azimio, mtoe maelekezo, kama Halmashauri haziwezi kulipa, basi ndio hawa wapate ajira za kudumu, walipwe na Serikali Kuu kama walivyo watumishi wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niongelee TARURA. TARURA tumewapa kazi kubwa sana, kwa hiyo, tuwaongezee bajeti, tuwaongezee rasilimali watu, tuwape mamlaka yaliyo makuu ya kuweza kufanya hizi kazi. Utashi wa kisiasa umeingia sana kwenye TARURA. TARURA wanaweza wakasema barabara hii ndiyo ingestahili kujengwa, lakini utashi wa kisiasa ukasema ijengwe barabara sehemu nyingine. Kwa hiyo, nao wanakuwa kwenye mchanganyiko wa kushindwa kuamua ni kipi wafanye na kipi waache. Naomba kama tumeamua TARURA ndiyo ihusike na barabara za Serikali za Mitaa, basi tuamue kuongeza bajeti ya kutosha ili barabara hizi ziweze kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri, Dar es Salaam siasa zake ni Barabara na miundombinu, lakini ukiangalia barabara zilizoko Dar es Salaam ni za kitaifa. Kwenye mitaa kule ni hatari, na tunategemea hizo barabara ndiyo zitusaidie kupata kura za wananchi. Kama tukichukua uthubutu wa kutengeneza barabara za Dar es Salaam tunaweza tukaongea mengine kwenye uchaguzi. Barabara zinatisha, hazipitiki. Nawaomba... (Makofi)

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Janejelly kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mabula.

TAARIFA

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa mchango mzuri wa Mheshimiwa Mbunge. Nataka tu nimpe taarifa kwamba umuhimu wa barabara zinazojengwa na TARURA siyo kwa Dar es Salaam peke yake, ni nchi nzima, kwa sababu ushindi wa CCM utatokana na kura zitakazopigwa nchi hii na barabara zina hali mbaya. TATURA inahitaji fedha nyingi zaidi kuliko sasa. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Janejelly, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea, lakini nawaomba Wabunge, tunapoongelea suala la Dar es Salaam kila Mbunge atuunge mkono, kwa sababu hakuna Mbunge ambaye hana makazi Dar es Salaam ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kabisa!

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapoongelea suala la Dar es Salaam mtuunge mkono, mkubali barabara za Dar es Salaam zitengenezwe. Mwache kutujia inbox. Inbox wanakuja na kusema ongeleeni barabara ile, ongeleeni barabara ile, hata kwa message, lakini sasa hapa tukiongea, wanaona kama tunajipendelea Dar es Salaam. Hatujipendelei, Dar es Salaam ndiyo kioo cha Taifa, Dar es Salaam ndiyo Mji Mkuu wa kibiashara, lazima barabara za Dar es Salaam zitengenezwe. (Makofi)

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Janejelly kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Lazaro Nyamoga.

TAARIFA

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tu kuweka kumbukumbu sawa, tupo Wabunge wengi ambao hatuna makazi Dar es Salaam, tunaishi majimboni, mmojawapo ni mimi. Naomba kutoa taarifa hiyo ili wananchi wasije wakaelewa tofauti na hilo. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Janejelly taarifa hiyo unaipokea?

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimu sana mdogo wangu huyu, lakini hiyo taarifa siwezi kuipokea, sijasema hawakai kwenye majimbo yao, lakini nimesema wana makazi Dar es Salaam. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee na mchango wangu. Naomba Barabara za Dar es Salaam ziangaliwe kwa umuhimu wa kipekee.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea haya, mnafanya utani, mnanipiga taarifa, lakini Dar es Salaam tuelewe ndiyo ina asilimia 15 ya kura za nchi hii, tunazozitegemea. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, alishapewa taarifa mbili zinatosha.

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoongea ninamaanisha. Ni lazima Dar es Salaam iangaliwe kwa jicho lingine, ni lazima Dar es Salaam barabara zitengenezwe. (Makofi

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha. (Makofi)