Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge kuhusu Wakala wa Kimataifa wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (International Renewable Energy Agency - IRENA) na Azimio la Bunge kuhusu mapendekezo ya kuridhia Mkataba wa Kuanzisha Taasisi ya Dawa ya Afrika wa Mwaka 2019 (Treaty for the Establishment of the African Medicine Agency - AMA)

Hon. Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge kuhusu Wakala wa Kimataifa wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (International Renewable Energy Agency - IRENA) na Azimio la Bunge kuhusu mapendekezo ya kuridhia Mkataba wa Kuanzisha Taasisi ya Dawa ya Afrika wa Mwaka 2019 (Treaty for the Establishment of the African Medicine Agency - AMA)

MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia katika mada ambazo zimewasilishwa siku ya leo. Na mimi nitajielekeza katika kuchangia wasilisho linalohusu Taasisi hii ya Dawa Afrika (African Medicene Agency).

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba naunga mkono azimio hili lipitishwe na Bunge lako tukufu. Dawa ni kitu muhimu sana katika tiba za binadamu lakini dawa vile vile ni siasa, dawa ni biashara. Na katika matumizi ya dawa kuna watu wana nia njema na wengine na nia isiyokuwa njema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu ambao wanatengeneza dawa bandia na watu ambao wanatengeneza dawa ambazo hazina ubora unaotakiwa. Kwa hiyo, Azimio hili linakwenda kuwezesha Nchi Wanachama kuweka mfumo mzuri wa kuweza kudhibiti bidhaa za tiba, kwa kuhakikisha kwamba dawa zinakuwa zina ubora, zenye ufanisi na usalama unaojitosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza sana Serikali ya Tanzania katika masuala ya udhibiti wa dawa tuko vizuri na Taasisi yetu ya TMDA inafanya vizuri sana. Hongera sana Mheshimiwa Waziri na timu yako, kwa usimamizi mzuri ambao unaufanya katika Wizara hii, ambao umepelekea Tanzania tunasifika katika masuala ya udhibiti wa dawa na vifaa tiba katika Bara la Afrika na dunia nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nini manufaa ya Mkataba huu? Kwanza, unakwenda kuboresha masuala ya mifumo ya udhibiti katika Bara letu la Afrika. Sambamba na hilo, litasaidia sana kuweka mfumo wa kuweza kubadilishana taarifa na kuweza kujengeana uwezo katika nchi zetu za Bara la Afrika. Pia sambamba na hilo, kila nchi ya Afrika ina mifumo yake ya udhibiti na usajili wa dawa. Azimio hilo litakwenda sasa kuweka mfumo mzuri wa kuweka viwango na vigezo ambavyo vitatumika katika Bara zima la Afrika. Hii itapelekea kuweka sasa mifumo ambayo inafanana na kuwavuta wale ambao wako chini na sisi ambao tuko katika viwango vya juu kwenda viwango vya juu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimetoka kusema hapa katika viwango vile vya kimataifa vina hatua nne. Sisi Tanzania tuko katika hatua ya tatu, ni jambo la kujivunia sana kama Watanzania. Naamini kwa kupitisha Azimio hili, litatusaidia hata sisi katika viwanda vyetu vya ndani, kupunguza mlolongo wa usajili na pale ambapo tutahitaji sasa bidhaa zetu kuzipeleka nje ya nchi, sasa hivi Tanzania tuna Viwanda vya Dawa takribani 18. Mfumo huu utasaidia sana bidhaa zetu kuweza kuuzwa nje ya nchi na kupunguza mlolongo wa usajili. Utaratibu uliopo sasa hivi ndani ya nchi yetu kila dawa tiba ni lazima isajiliwe na mlolongo wake haupungui miezi sita. Utaratibu huu utasaidia kuweka benchmarks nzuri ambazo naamini nazo zitasaidia sana katika udhibiti, vile vile katika suala la usajili wa dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nataka niweke angalizo moja. Sisi kama nchi tumefanya vizuri sana. Mifumo yetu iko vizuri sana katika suala zima la usajili na udhibiti wa dawa katika nchi yetu. Sasa ni muhimu sana wakati tunapitisha azimio hili, kuhakikisha kwamba taasisi yetu ya TMDA inaendelea kufanya majukumu yake ya kimsingi bila kuathirika na vipengele ambavyo vinaweza vikasababisha taasisi yetu na sisi kushuka chini, kwa sababu wote hatuko katika viwango vya pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini kwamba, kwa kupitisha azimio hili Taasisi yetu ya TMDA ndiyo itakuwa kinara cha kusaidia nchi nyingine za Afrika na wao waweze kufikia katika viwango vya juu vya udhibiti wa ubora wa dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuomba jambo moja. Hili nitaendelea kulisema, lipo nje hapa kidogo, lakini tunaongelea masuala ya udhibiti wa vyakula. Katika nchi nyingi duniani suala la udhibiti wa dawa linakwenda sambamba na udhibiti wa usalama wa chakula. Suala la usalama wa chakula ni suala la afya, siyo suala la viwanda wala la biashara. Usalama wa chakula linapotokea changamoto katika suala la usalama wa chakula, uwe ni mlipuko wa magonjwa ambao umesababishwa na chakula, Wizara inayoshughulika ni Wizara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tulihamishe hili jukumu kutoka Wizara ya Afya kwenda Wizara ya Viwanda na Biashara. Niwaombe sana, katika nchi nyingi mamlaka zinaitwa FDA (Food Drug Authorities), siyo Medical Authority. Kwa hiyo, niendelee kuiomba Serikali iende ikaliangalie suala hili, ikiwezekana suala la usalama wa chakula lirejeshwe chini ya TMDA ili sasa jukumu hili liweze kufanyika. Hili nalisema kwa sababu gani? Sasa hivi kuna uingizaji mwingi wa chakula na vyakula vingine havina ule ubora ambao unatakiwa. Najua kwamba TMDA…

MHE. ASKF. JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumpa taarifa tu anayezungumza. Ni kweli kabisa kwa sababu, genetic modified food au chakula ambacho kimetengenezwa ku-genetic, ni hiyo hiyo sayansi ya dawa. Kwa hiyo, ikiwa pamoja itarahisisha sana kulinda watu wetu. (Makofi)

MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima kwa kuunga mkono hoja yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu kwamba, pamoja na kukubali Bunge lako liweze kuliridhia Azimio hili, basi naliomba Bunge lako vile vile litafakari kurejesha majukumu ya usalama wa chakula chini ya Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)