Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetujalia kukutana hapa siku ya leo katika kujadili hoja hizi zote mbili. Pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kuniamni na kuniteua katika nafasi hii kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatu, nichukue nafasi hii kukupongeza sana kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Mabunge ya Ulimwengu. Hongera sana. Pia, kwa kuwa niliwahi kuwa Mjumbe wa Mabunge haya natambua ugumu wa kupata nafasi hiyo. Kwa hiyo, nikupongeze sana pamoja na timu uliyokuwa nayo huko kwenye kampeni za ushindi.


Mheshimiwa Spika, lazima nikiri Wabunge wamefanya kazi kubwa katika misingi ya Katiba Ibara ya 61, 62 kuhusu kuisimamia Serikali. Kwa kila Kiongozi wa kuchaguliwa na kwa viongozi sisi wa kuteuliwa, Wabunge wanatutaka tufanye kazi zaidi ya kumsaidia Mheshimiwa Rais na Waheshimiwa Mawaziri kila mmoja wetu katika eneo lake ameweza kutoa majibu ya hatua ambazo tumechukua. Naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge kama Waziri ninayehusika na masuala ya Utawala, Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan iko imara sana leo kuliko jana.

Mheshimiwa Spika, hata leo tukisema tunakwenda kwenye chaguzi zetu hizo za kesho tutashinda kwa kishindo kwelikweli. Katika maeneo mengi ambako tumepita kazi kubwa imefanyika, lakini lazima nikiri Kamati ya Kudumu ya Bunge ya LAAC imefanya kazi kubwa na kazi nzuri sana, Mheshimiwa CAG amefanya kazi kubwa na kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumekuwa na ushirikiano ya karibu sana Wizara ya TAMISEMI na lazima nikiri kwamba mtu wa kwanza kuzungumza nae baada ya uteuzi wangu tukiachana na hawa wengine ni Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, lazima tukiri taarifa hizi zinatusaidia kuboresha utendaji kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili tuweze kufanya vizuri lugha ya kila mmoja wetu kwenda kuwajibika hakuna lugha nyingine kwenda kufanya kazi tu. Hakuna lugha nyingine na umewasikia kila Mheshimiwa Waziri akisimama hapa anazungumza ni namna gani tumewajibika tumeenda kufanya kazi katika maeneo yetu. Hakuna lugha nyepesi wasaidizi wetu na mimi nimekwisha waambia hata wasaidizi wangu Naibu Mawaziri, huu ni wakati wa kazi kama tunataka kupata ushindi wa kishindo miezi kumi ijayo katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni lazima tufanye kazi hasa kwa kuzisoma taarifa hizi vizuri na kwenda kuzitendea haki kama ambavyo tumeshauriwa na Mwenyekiti wa Kamati pamoja na taarifa ya Mheshimiwa CAG. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TAMISEMI hatuna muhali, hatuna muhali hata kidogo, tunachukua hatua kama ambavyo Waheshimiwa Mawaziri wengine wamekuwa wakifanya na sisi tunachukua hatua.

Mheshimiwa Spika, yamezungumzwa hapa, taarifa ya utendaji usioridhisha kwenye baadhi ya Halmashauri tunachukua hatua, tunachukua kwelikweli na leo nitaendelea kuchukua hatua. Naomba nikuthibitishie utekelezaji wa taarifa hizi tumeendelea kutekeleza kwa kiwango cha hali ya juu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, tumechukua hatua, hata wakati fulani nilipokuwa nikiwaona Waheshimiwa Wabunge fulani wakizungumza hapa pengine wamesahau kwamba nimechukua hatua juzi tu katika maeneo yao. Mheshimiwa Kuchauka alizungumza, Mheshimiwa Mbunge wa Kigoma kule Ndugu yangu amezungumza lakini Mheshimiwa Kuchauka anafahamu hatua nilizochukua juzi tu hapa takribani kama mwezi mmoja tu uliopita tumewasimamisha kazi Watumishi ambao wameshiriki kwenye ubadhirifu wa fedha, lakini siyo kuwasimamisha tu…

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kuchauka.

TAARIFA

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nilichozungumza hapa nataka nimpe taarifa mzungumzaji anazungumza vizuri sana, mimi kwenye mchango wangu nilisema tatizo liko TAMISEMI, katika hao Saba aliowapunguza yeye juzi alipokuja, mimi nilishapeleka taarifa zao miaka miwili iliyopita, TAMISEMI wanalindana.

SPIKA: Sasa hiyo taarifa, Waheshimiwa Wabunge ukisema TAMISEMI wanalindana, Mheshimiwa Mchengerwa yumo ama hayumo, maana yeye anakuambia hapa kwamba kachukua hatua na wewe unakubali kwamba kachukua hatua lakini unachojaribu kusema ni kwamba hatua zimechelewa, sasa ukitumia, sema walikuwa labda, sema walikuwa wanalindana ili ndiyo tujue hizi hatua.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, walikuwa wanalindana na ndiyo maana nikasema nimetoa taarifa miaka miwili iliyopita.

SPIKA: Ahsante sana, sasa kusema wanalindana maana yake ni sasa wakati hatua zimechukuliwa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nilishawaripoti kwamba Fulani na Fulani wanatuharibia Halmashauri, hakuna kitu kilichoendelea mpaka alipokuja yeye, kwa hiyo tunaiambia Serikali kwa ujumla kwamba wanalindana.

SPIKA: Sawa, Mheshimiwa Kuchauka ukitumia lugha hiyo tena tutarudi kwenye Kanuni zetu hapa, ukisema walikuwa maana yake unakiri anachosema Waziri kwamba kachukua hatua, ukisema wanalindana maana yake ni sasa na hawajafanya chochote, wewe unataka kipi kati ya hicho?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, huko nyuma walikuwa wanalindana.

SPIKA: Haya ahsante sana. Mheshimiwa Waziri unaipokea taarifa hiyo?

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, wakati tunachukua hatua kule Liwale nilichukua hatua mbele yake yeye akiwa pale pale, si kwa sababu mimi na yeye tulikuwa tumezungumza, yeye ni shahidi lakini kwa sababu ya vyanzo tulivyo navyo ndani ya Ofisi ya Rais, nilichukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumechukua hatua kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kwa kuwasimamisha kazi na kutengua uteuzi wao na wengine kufikishwa Mahakamani, tumechukua hatua kwa waliokuwa Wakurugenzi wa Halmashauri ya Majiji, Jiji la Mbeya, Mwanza, Dar es Salaam, Arusha na wengine wako ndani.

Mheshimiwa Spika, tumechukua hatua katika Manispaa za Singida, Iringa, Mtwara na Sumbawanga na hata aliyekuwa Mkurugenzi wa Sumbawanga akahamishiwa kwingine tumemrejesha ili akajibu kesi iliyopo Mahakamani. Kwa hiyo, zile taarifa kwamba kuna watu wanahamishwa wanapelekwa sehemu zingine katika kipindi hiki chini ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mtumishi yeyote popote alipo, awe amehamishwa, awe amestaafu, atakayeshiriki kwenye ubadhirifu wa fedha za umma hatutasita kumchukulia hatua, popote alipo na huo ndio ujumbe ambao tumeutuma katika maeneo ambapo tumekwisha kuchukua hatua.

Mheshimiwa Spika, pia tumechukua hatua katika Halmashauri mbalimbali kule Monduli, Muheza, Korogwe, Masasi, Kilosa, Uvinza, Buhigwe, Busega, Sengerema, Buchosa na Mvomero. Hivi tunapozungumza wataalam wangu wako uwandani wanaendelea kufanya uchunguzi kwa taarifa ambazo tumeendelea kuzipokea kutoka TAMISEMI, kutoka kwa watoa taarifa mbalimbali, naomba nitoe taarifa kwamba TAMISEMI inaendelea na uchunguzi katika Halmashauri za Wilaya ya Kibaha ambayo imezungumzwa kwenye taarifa ya LAAC, tunaendelea na uchunguzi kule Kigoma, tunaendelea na uchunguzi Uvinza, tunaendelea na uchunguzi Ileje pamoja na Ifakara.

SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa Mchengerwa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ole-Sendeka

TAARIFA

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, Wasomi wanasema “mnyonge mnyongeni haki yake mpeni”. Ni kweli kwamba Mheshimiwa Mchengerwa hufuata nyayo za Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu wa sasa Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa katika kushughulikia mafisadi, natamani kama watu wote wangeungana na Mawaziri wako wengi tu waliochukua hatua, kwa kwenda kwa kasi hii ya muda mfupi uliokaa TAMISEMI tuna matumaini makubwa sana na ninahakika Waziri Mkuu amempata Msaidizi katika eneo hilo.

SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa unaipokea taarifa hiyo?

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nimepokea taarifa ya ndugu yangu na rafiki yangu. Tunaendelea kuchukua hatua hata kwa Wakuu wa Idara, naomba nitoe taarifa kwamba Wakuu wa Idara ya Vitengo vya Ununuzi na Ugavi 23 tumekwisha waondoa, Waweka Hazina 16 tumekwisha waondoa, Wakuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Sita na Wakaguzi wa Ndani Wawili waliondolewa nafasi zao.

Mheshimiwa Spika, Waganga Wakuu 10 wa Mikoa wameondolewa nafasi zao, Waganga wa Wilaya 46 wameondolewa nafasi zao na mwingine tumemuondoa hivi karibuni kule Mbogwe, tumemuondoa hivi karibuni. Kwa hiyo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan inachukua hatua madhubuti.

Mheshimiwa Spika, imezungumzwa kuhusu….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika moja Mheshimiwa malizia.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba nikiri Serikali ya Awamu ya Sita inafanya kazi kubwa sana, sana, sana na ni lazima panapotokea mafanikio makubwa ni lazima credit tumpe Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na kazi nzuri anayoifanya kwenye maeneo yetu. Hatutaki tumpe taabu Mheshimiwa Rais 2024/2025, na ili tuweze kufanikiwa tusimpe taabu ni lazima tufanye kazi kwa bidii hakuna lugha nyingine! Hakuna lugha nyingine.

Mheshimiwa Spika, wale wote ambao wametajwa kwenye ripoti naomba niseme maneo yafuatayo; ole wake kiongozi yeyote mzembe na mbadhirifu, ole wake! Kiongozi yeyote mzembe kwenye Wizara yangu na asiye na nidhamu nitakaye mkuta huko na wabadhirifu, nataka niwaambie siku zao zinahesabika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Waziri malizia mchango wako.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kumuelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI kuchukua hatua dhidi ya Mkurugenzi wa Igunga, aliyekuwa Mkurugenzi kule Kigoma Ndugu Athumani Francis Msabila, kumsimamisha kazi mara moja kwa sababu ya ushiriki wake wa fedha za mifumo akishirikiana na watendaji wa mifumo walioko TAMISEMI wawili walitajwa katika taarifa ya ripoti. Katibu Mkuu awasimaishe kazi mara moja na taarifa hizi za ripoti ya LAAC pamoja na hii ya CAG ni wakeup call kwa kila mmoja wetu kuwajibika kwenye eneo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutahakikisha tunawatendea haki Watanzania, Serikali inafanya kazi kubwa sana ni lazima tumtendee haki Mheshimiwa Rais, kwa sisi viongozi kufanya kazi kwa bidi, hakuna lugha nyingine ni lazima tufanya kazi kwa bidi kila mmoja wetu katika eneo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja ya Kamati ya LAAC pamoja na Kamati ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na ninakuomba uridhie majibu ya kila Mbunge kwa namna yalivyotolewa TAMISEMI tumekwishaandaa majibu ya kila hoja kwa namna ilivyotolewa na tutaiwasilisha kwenye Bunge lako Tukufu ili tuweze kuwakabidhi Waheshimiwa Wabunge kila mmoja aweze kuipata na kuisoma, na wasisite wakati wowote pale popote kunapotokea changamoto TAMISEMI tutakuwa nanyi leo na kesho kuhakikisha kwamba tunafanya kazi kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana naomba kuwasilisha. (Makofi)