Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mimi sina shaka yoyote ju ya dhamira ya Waheshimiwa Wabunge katika hoja ambazo wamezizungumza na concern yao hususani kwenye kudhibiti fedha za umma. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba dhamira yao hiyo hiyo ndiyo dhamira ambayo Serikali yao inayo chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nithibitishe kauli yangu hiyo kwa hoja zilizoguswa kuhusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika Ripoti ya CAG na Waheshimiwa Wabunge pamoja na Kamati. Hoja kubwa ambazo zimeguswa ni hoja mbili.

Mheshimiwa Spika, nitaomba nichukue nafasi hii kuweza kutoa ufafanuzi huo kwa utaratibu wa kujiuliza swali mwenyewe na kujijibu mwenyewe. Wakati nitakapojijibu inawezekana ikawa inatosha kuweza kutoa ufafanuzi.

Mheshimiwa Spika, swala langu la kwanza nilikuwa nataka kujiuliza ni kwamba je sasa hivi, katika kipindi hiki cha Serikali hii wizi, ubadhilifu, ufisadi, unazidi, umekuwa mkubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote au kinyume chake?

Mheshimiwa Spika, hoja za CAG ambazo zimegusa Wizara yangu mbili. Moja ni hoja ambayo inahusu mfuko wa tozo na tozo na nyingine inahusu mfuko wa kufa na kuzikana. Majawabu haya ni vizuri yakajibiwa kwa facts and figures. Nikichukua hayo maeneo mawili ni maeneo ambayo yamegusa tuhuma nzito na kubwa sana na yametikisa chombo chetu muhimu sana kinacholenga kulinda usalama wa raia na mali zao hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, kimetikisa heshima yake, kimetikisa heshima ya Taifa ya chombo hiki kikubwa. Sio jambo dogo hizi tuhuma na shutuma, lakini tuhuma na shutuma hizi hazijatokea kipindi hiki lakini zinarekebishwa kipindi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda tunaweza tukajiuliza kwamba kwanini tunafanikiwa maana mafanikio ni makubwa. Leo CAG inazungumza Ripoti kwa uwazi kama hivi, Bunge linazungumzwa kwa uwazi na uhuru wametuongoza vizuri kwa uwazi kabisa na uhuru wa hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, hakuna Mbunge ambae umeacha kumpa nafsi. Haya ni mafanikio makubwa ya kujadili. Uwazi huu na mafanikio haya yana sababu zake na kila maji yanaanzia kwenye mkondo na samaki huanzia kwenye kichwa hatuwezi kuacha kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mkuu wa Nchi Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwezo wake mkubwa wa uongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni ishara ya uwezo mkubwa wa Kiongozi na ndiyo maana leo Taasisi zote muhimu zinafanya kazi zake nzuri kwenye Bunge hili, mihimili yote inafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya mafanikio ni kwa sababu Amiri Jeshi Mkuu ameweza kutafsiri vision yake ya wapi anataka Taifa liende kwa kuwapa imani, kuwa-inspire, kuwa-motivate vyombo na watu wanaoitwa mamlaka sisi tusimamie. Leo hii hata mimi katika Wizara niliyopewa dhamana sisubiri kusukumwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siwezi nikaona jambo lolote, doa lolote linajitokeza na tukaweza kulifumbia macho. Swali la pili je taasisi hizo mlizoziorodhesha chache TAKUKURU, Jeshi la Polisi na mengineyo na viongozi wanatimiza wajibu wao? Ama Serikali inalea wezi, serikali inalea wezi?

Mheshimiwa Spika, jambo moja ni muhimu sana Waheshimiwa Wabunge wakajua kwamba hoja hizi mbili na mimi nasema haya wazi kabisa na kama ninachokisema hiki nachozungumza hapa nitakuwa nashindwa kukitetea hakina ukweli, nasema mbele ya Bunge hili na wananchi wa jimbo langu wananisikia mimi niko tayari kuacha siasa.

Mheshimiwa Spika, nikiacha siasa maana yake Uwaziri haupo, Ubunge haupo ntarudi kwenda kushika spana. Lakini ninachokwambia ni kwamba haya ambayo tunayazungumza leo haya hayakutokana na uvumbuzi wa CAG, yametokana na maamuzi ya Serikali ambayo tulimwandikia sisi barua kufanya ukaguzi huu wa matatizo ambayo yametokezea kipindi kirefu nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiyo ilielekeza ukaguzi huu. Nihakikishe kwamba kila hatua anayochukua ni stahiki. Nachukua fursa hii kumpongeza CAG kwa kazi nzuri uliyofanya, nipongeze Bunge lako Tukufu na Waheshimiwa Wabunge kwa kujadili vizuri Ripoti hii ya CAG. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie, kama ambavyo tumeanza kuchukua hatua, nitazieleza hatua gani, na hatua ambazo hazijachukuliwa zitaendelea kuchukuliwa kwa kuzingatia maoni yenu.

Mheshimiwa Spika, suala lingine la tatu ambalo nataka nilizungumze, hatua gani ambazo zimeshakuliwa dhidi ya wabadhirifu hao. Kwanza nataka nieleze kitu kimoja; CAG anafanana kidogo na polisi, sema yule anashiriki masuala ya jinai na yule anashiriki masuala ya kifedha. Polisi anapomkamata mhalifu anafanya uchunguzi, na akimaliza anapeleka kwa DPP, DPP, anaangalia uzito wa ushahidi uliokusanywa kama unajitosheleza kumpeleka mtuhumiwa mahakamani.

Mheshimiwa Spika, CAG anafanya uchunguzi wa kifedha kuangalia compliance ya matumizi ya fedha. Sasa leo hii tukisema mtu ambaye ametajwa, tena hajatajwa waziwazi katika Ripoti ya CAG aende jela hiyo sio misingi ya utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie, wale wote ambao wamethibitika bila shaka yoyote kuhusika wamechukuliwa hatua. Na nina orodha hapa, nina jedwali hili lina majina na hatua ambazo kila mmoja alizochukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda…

MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, watu ambao wamefikishwa mahakamani mpaka sasa hivi ni watu 18…

SPIKA: Mheshimiwa aliyesema taarifa.

MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Spika, huku taarifa.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, watu ambao wamefukuzwa kazi ni…

SPIKA: Mheshimiwa Masauni, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ravia.

TAARIFA

MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Waziri; Ni kweli kachukua hatua lakini kwa askari wadogo tu, wale wakubwa bado wanaendelea kula maisha. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Masauni, unaipokea taarifa hiyo?

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, siipokei kwa sababu inaonekana Mheshimiwa Mbunge, alikuwa anasinzia wakati nazungumza, hakunisikiliza.

SPIKA: Hapana, ngoja, Mheshimiwa Waziri, hebu mwombe radhi Mheshimiwa Mbunge na ufute hayo maneno.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nimefuta hayo maneno na nimemwomba radhi... (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, hizo ni tuhuma zote ya kwamba Mheshimiwa Mbunge alikuwa alisinzia. Anafuatilia mjadala ulioko hapa Bungeni. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Spika.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, namwomba radhi swahiba wangu, Mheshimiwa Mbunge wa Makunduchi, tuelewane. Namwomba radhi na ninafuta, nina hakika hajakasirika kwa sababu ni rafiki yangu sana na anaelewa tunataniana mengi tu. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, baada ya kumwomba radhi Mheshimiwa Mbunge na kufuta kauli hiyo, naomba niendelee.

SPIKA: Mheshimiwa Masauni, ngoja, Mheshimiwa Ravia, naona bado umesiama.

MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Spika, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Waziri kwamba, heshima ni kitu cha bure, lakini la pili ni kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC, ninachokiongea ninakijua kwa silimia mia. Kwa hiyo sijasinzia na ninachokiongea ninakielewa. Waliochukuliwa hatua ni wadogo na wakubwa bado wanaendelea kula maisha.

SPIKA: Haya, ahsante sana Mheshimiwa. Waheshimiwa Wabunge, nadhani kwa sababu Mheshimiwa Waziri wakati amesema ile sehemu yake ya mwanzo pengine kwa sababu ya zile kelele haikuwa imesikika, lakini mimi nilimwacha aendelee na mchango kwa sababu alishasema. Ameanza kwa kusema naomba radhi, huyu ni swahiba, kwa hiyo watu hawakusikia lile neno la naomba radhi nadhani ndiyo maana watu wameendelea na hizi kelele.

Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri ameomba radhi na amezungumza na hayo ya ziada, Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nilikuwa nimefikia kwenye takwimu za watu ambao wamechukuliwa hatua mbalimbali...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika moja, malizia mchango wako, kengele ya pili ilihsapigwa.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, katika takwimu hizi za watu, kama ningesema nitaje majina ingeonekana ni wakubwa kiasi gani kwa maana tafsiri ya ukubwa ni pana sana lakini nina orodha ya watu waliofikishwa mahakamani, waliofukuzwa kazi na waliosimamishwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu ambao inasemekana walitoroka, lakini miongoni mwao hivi sasa wameshaanza kupatikana...

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: ...kuna mmoja amepatikana juzi, kwa hiyo kuna hatua nyingi ambazo zimeshachukuliwa kwa yale mambo ambayo yameshathibitika na hatua nyingine za kuweza kupata uthibitisho iliwaweze kuchukuliwa hatua zinaendelea.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka nizungume kwa haraka haraka…

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, ahsante sana.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Ni kudhibiti mifumo, ni kwamba, Je…

SPIKA: Mheshimiwa Masauni, muda wako umekwisha kengele ilikuwa imeshagonga nikakupa muda wa ziada. (Makofi)