Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye bajeti ya Serikali. Nimepitia taarifa ya hali ya uchumi iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri na kwa kweli nataka niipongeze Serikali kwa dhati, imepigana kwa nguvu zote kuhakikisha uchumi wetu upo katika hali nzuri. Fedha yetu imeimarika, lakini vilevile tumepambana na mfumuko wa bei kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala zima la mfumuko wa bei na kuongezeka kwa pato la Taifa, Mheshimiwa Waziri ameongelea habari ya miradi yetu mikubwa tunayoendelea nayo. Kokote duniani construction industry inaleta matokeo makubwa zaidi katika kukua kwa pato la Taifa na hata ukipima GDP unaangalia na miradi ambayo inatekelezwa. Katika mchango wangu nataka nijikite kwenye namna gani viwanda vyetu vya ndani hasa viwanda vya simenti na niseme tu duniani kote Taifa ambalo linatumia simenti nyingi ni mataifa ambayo yana uchumi mkubwa. Katika Afrika Misri ndiyo inaongoza kwa matumizi makubwa ya simenti na hiyo vilevile hata GDP yao inaongezeka, lakini vilevile ni kipimo kwamba nchi hiyo ina uchumi mzuri.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo na sisi katika suala zima la simenti hapa nchini, ni jambo la muhimu na lazima twende nalo hivyo hivyo. Shida iliyopo kwa sasa simenti yetu na bei yake imekuwa inaongezeka kila wakati badala ya kushuka. Kikubwa zaidi kinachotokea ni kwamba, lipo tatizo la malighafi inayoenda kutengeneza simenti na bahati mbaya viwanda vingi ambavyo vinatengeneza simenti vinanunua materials yale ya kutengeneza simenti kwa wafanyabiashara wadogo. Hakuna kampuni kubwa mahsusi ambayo inalisha viwanda hivi, lakini kibaya zaidi ipo Tume ya Madini ambayo inatoa bei elekezi za malighafi hizi ambazo zinalisha viwanda hivi.

Mheshimiwa Spika, mwezi Aprili mpaka mwezi Juni, Tume ya Madini imetoa bei elekezi za materials hizi ambazo zinatumika kutengeneza simenti. Kwa mfano, gypsum inauzwa kuanzia Sh.38,000 mpaka Sh.100,000. Sasa uchuke gypsum kutoka Itigi uipeleke Tanga kwa ajili ya simenti, uipeleke Mtwara au uipeleke Dar es Salaam lakini bei ya tani moja kuisafirisha ni Sh.123, bei iliyopo sasa hivi katika transport. Kwa hiyo unakuta hakuna mtu ambaye anataka kuwekeza katika biashara hii.

Mheshimiwa Spika, naomba ku-declare interest nafanya kazi ya ku-supply feldspar katika kiwanda mojawapo kinachotengeneza tiles. Bei hiyo ambayo tunapangiwa na Tume ya Madini inatuumiza kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo huwezi ukaingiza mtaji wako mkubwa uwe na magari ya kusafirisha, kazi iliyofanyika wafanyabiashara weni wanadaka gari kwenye barabara hizi Msamvu pale, wanadaka gari maeneo mbalimbali, hakuna kampuni mahsusi. Kwa hiyo Waziri katika hotuba yake ukienda katika ukurasa wa 10 amegusia habari ya kuondoa mrabaha katika makaa ya mawe na anasema ni Sura 123 ya Sheria ya Madini, kwamba kupunguza kiwango cha mrabaha kutoka kwenye makaa mawe yanayotumika kama malighafi ya kuzalisha nishati viwandani kutoka 3% hadi 1%. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uzalishaji viwandani, kuchochea uwekezaji zaidi na kukuza ajira.

Mheshimiwa Spika, jambo hili ni jema, lakini naomba Serikali iondoe malighafi kwenye viwanda ambavyo vinazalisha simenti na kama hili nililosema kwenye tiles na watoe kodi tunayolipa ya VAT kwa sababu VAT tena inakuja kulipwa kwenye kiwanda baada ya kuuza zile bidhaa, lakini kufanya hivyo unachochea supply ya materials kwenye viwanda kuwa kubwa. Kufanya hivyo italeta ahueni kwa wafanyabiashara wanao-supply kule kwenye viwanda lakini vilevile na kupunguza bei ya simenti.

Mheshimiwa Spika, ukienda katika Sheria ya Madini, Sura 123, kwenye regulations za mwaka 2019 wameongelea habari ya kuondoa kodi kwenye baadhi ya madini, lakini kwa makusudi kabisa sheria inasema sheria hii haihusishi, that trading of building all industrial energy minerals shall not apply to these regulations. Kwa hiyo naiomba sana Serikali na Mheshimiwa Waziri aangalie jinsi ya kuondoa kodi kwenye malighafi hizi na kufanya hivyo kutachochea kwa kiasi kikubwa kwamba viwanda vyetu hasahasa vya ujenzi viweze kupata malighafi na hivyo kuweza kushusha bei ya simenti hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye suala lingine kuhusu Shirika la Bima la Taifa. Kama unavyojua biashara ya bima imekua hapa nchini, lakini na sisi tuna Shirika la Bima la Taifa. Bahati mbaya shirika hili bado linaendeshwa katika muktadha wa Kiserikali, nataka niishauri Serikali iajiri watu ambao wanaenda kufanya biashara ya bima, lakini vilevile walipe fedha shirika hili. Tunavyojua kwamba Serikali haiyawekei bima magari yake, lakini zipo taasisi ambazo zinafanya biashara nazo zipo exempted kwenye bima. Ninachotaka kusema ni kuwa, si kwamba hili Shirika la Bima la Taifa wapendelewe na Serikali, hapana lakini wawezeshwe ili waweze kufanya biashara kama kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kwenye suala la kubadilisha matumizi ya Ranch ya Kongwa sasa ianze kulima alizeti na unaweza kukuta si tu alizeti na watataka walime na mahindi na vitu vingine. Mimi napinga jambo hili kwa kiasi kikubwa. Nimesoma kwenye hotuba ya Waziri katika sehemu ya masuala ya mifugo kwenye importation ya product kutoka nje na Waziri alisema kwamba nyama yetu bado haina ubora, lakini kinachotuzuia ni kwamba hatujaamua kama Serikali kuwekeza katika suala zima la kutoa nyama zenye ubora.

Mheshimiwa Spika, Ranch ile ya Kongwa ina capacity kwa sasa ya kuwa na ng’ombe 11,400, lakini na hiyo tumetoa nusu tumewapa baadhi ya wananchi wanachunga mle, vijiji vinavyozunguka, lakini ukija katika capacity yake nzima ina uwezo wakuwa na ng’ombe 40,000 kwa wakati mmoja. Nataka niseme Serikali iliangalie jambo hili, yapo mapori mengi wasikimbilie kupeleka alizeti sehemu ambayo haihusiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)