Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Anton Albert Mwantona

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rungwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Spika, nami pia niungane na wenzangu kumshukuru Mungu kwa kutupatia afya, lakini pia nimshukuru Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Fedha, Naibu wake na watumishi wote wa Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kutoa shukrani za pekee, wananchi wangu wameniambia nije nitoe shukrani kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miradi inayotekelezwa katika Jimbo langu la Rungwe. Ni miradi mingi inatekelezwa, lakini kwa upekee sana naomba nitaje miradi michache kwa sababu ya muda ili wananchi wangu wasikie kwamba nimewafikishia salamu zao.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Rungwe pamoja na mimi mwenyewe tumefurahi sana hasa baada ya Serikali kusikia kilio chetu, Mbunge mimi wa Rungwe wa Kyela, lakini pia Wabunge wa Viti Maalum dada zangu pale wa Mbeya tulivyokuwa tunapigania Mradi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira. Serikali imeshapata mteja ambaye atanunua makaa ya mawe kutoka Kiwira tani 60 kila mwezi. Upatikanaji wa mteja huyo utatusaidia sana watu wa Rungwe, Kyela, Ileje kupata ajira lakini pia kupata uchumi katika maeneo yetu. Vijana wengi ambao wako katika maeneo yetu walikuwa hawana ajira, tunategemea kwamba baada mradi huu kuanza ajira nyingi zitapatikana katika maeneo yetu na vijana wengi wataajiriwa.

Mheshimiwa Spika, pia wameniambia nilete salamu na shukrani pekee kwa Mradi wa Maji katika Mji wetu wa Tukuyu kwa Wizara ya Maji, tumepewa juzi milioni 402 kufikia bilioni moja na milioni 102 ambapo mradi mzima una bilioni 4.5. Sasa hivi tutapata mabomba ya kutosheleza kutoka moja kwa moja katika chanzo mpaka Tukuyu Mjini. Kwa hiyo tuna uhakika sasa hivi maji yatapatikana ndani ya muda mfupi, hiyo ni shukrani ya pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatu, katika bajeti hii tumewekewa milioni 90 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu kwa barabara inayotoka Kimo kuelekea Iponjola, Ikuti mpaka Ileje. Wananchi pia wanashukuru sana kwamba hii barabara ni dalili njema, kwamba inaanza kujengwa barabara hii kwa kiwango cha lami kutoka pale Kimo – Iponjola - Ikuti mpaka Ileje, hiyo ni shukrani ya pekee pia kwa Serikali hii.

Mheshimiwa Spika, pia kwa upande wa TARURA tumepewa tayari milioni 880 kwa barabara ambayo ilikuwa ni sumbufu sana kutoka Kijiji cha Kata ya Malindo, Kijiji Kapugi, kuelekea Lienje mpaka Kihobo Juu kwenye Kata ya Ikuti. Hizo ni shukrani za pekee sana kwa Serikali hii kwamba ni sikivu lakini pia imewafikiria wananchi kutatua matatizo yao ambayo yapo katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, niongee kidogo kwenye bajeti hii ya 2022/2023, nikipongeza Serikali kuongeza bajeti kwenye upande wa kilimo. Ongezeko ni kubwa ambalo litaenda kufanya mapinduzi makubwa kwenye kilimo. Mwaka jana tumepata shida kubwa sana kwa wananchi, tulivyokuwa tunafanya mikutano katika maeneo mbalimbali ya wananchi wetu tulikuwa tunaulizwa sana kuhusu bei ya mbolea. Bei ya mbolea kwa wastani laki moja mpaka laki moja na arobaini na hiyo imepelekea mwaka huu kilimo kikawa kigumu, watu wachache ndio waliweza kulima na hivyo tunategemea mwaka huu mazao yatakuwa ni kidogo.

Mheshimiwa Spika, katika suala hili naomba niishauri Serikali kwamba, tudhibiti chakula hicho kidogo tulichokipata, tuhakikishe kwamba utoaji wa chakula chetu cha nje kinatoka katika hali ambayo ni nzuri tukizingatia hasa usalama wa chakula hapa nchini. Hilo nimeona niseme, lakini kwa mwaka huu sasa kwa sababu tumeweka ruzuku kwenye mbolea uwezekano mkubwa ni kwamba mbolea itashuka na wananchi wengi watalima na hivyo tutapata chakula kingi cha kutosha.

Mheshimiwa Spika, Rungwe ni wafugaji wakubwa sana wa ng’ombe wa kisasa, tunafanya zero grazing, tunafugia ng’ombe ndani katika mazizi kwa kuwaletea chakula ndani, lakini tatizo kubwa la Rungwe na maeneo mengine ambayo wanafanya utaratibu huo wa ufugaji ni kwamba bei ya maziwa ni ndogo kwa wafugaji wetu. Tunaomba Serikali iangalie kwa jinsi gani itaongeza thamani ya mazao ya maziwa, lakini pia kuongeza soko mazao ya maziwa katika maeneo yetu. Rungwe ukifuga ng’ombe, lazima utumie lita 100 kununua mfuko mmoja wa pumba, pumba wanauza shilingi 70, maziwa yanauzwa kwa Sh.600 mpaka Sh.650. Sasa ukiangalia, kwa kweli wananchi wanapata shida, wanafuga mifugo yao katika gharama za juu lakini bei za maziwa ziko chini, kwa hivyo inawakatisha tamaa wengi katika ufugaji wao.

Mheshimiwa Spika, niende katika Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani. Mheshimiwa Waziri amesema hapa kwamba Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kinaongezewa independence zaidi kwa kupewa vote yao, lakini pia kwamba wao watakuwa wanaripoti moja kwa moja kwa Internal Auditor General ili at least zile ripoti zao ziweze kwenda vizuri na zisiingiliwe na mtu yoyote, ni jambo jema. Hata hivyo, naomba tuangalie pia katika utaalam wa kihasibu kwa sababu Internal Auditor ni sehemu ya menejimenti ya taasisi husika.

Mheshimiwa Spika, hapo lazima tuangalie jinsi gani ya kutenganisha Internal Auditor Unit lakini na kule anakoenda kuripoti, tusije tukatengeneza ugomvi mkubwa zaidi, halafu mambo yakazidi kuwa mabaya, kwa sababu Internal Audit kazi yake kubwa ni kushauri hiyo taasisi ambayo ipo ili kuhakikisha kwamba internal control ya taasisi inakaa vizuri na hakuna matatizo yoyote ambayo yanaweza kutokea kama mambo ya wizi na kadhalika. Kwa hiyo tuweze kuangalia vizuri hapo, ni jambo jema kuanza kutenganisha hapo.

Mheshimiwa Spika, mwisho niongelee watumishi ambao Mheshimiwa Waziri amesema kama wakiondolewa kwenye madaraka yao, kama alikuwa ni Mkuu wa Taasisi, tuchukulie labda ni Mkurugenzi, akiondolewa kwenye nafasi yake anatakiwa aende akatumikie mshahara wake ule wa awali, kama alikuwa ni Mtendaji wa Kata akachukue mshahara wake wa Mtendaji Kata. Naona hili kwangu sikubaliani nalo.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali waangalie upya katika hili kwa sababu tutakuwa tunawaonea watu wengi sana, kwa sababu watu wengi ukiangalia kutokana na historia wanaondolewa katika sehemu zao za kazi bila kuzingatia utaratibu. Anaweza akaja Mkuu wa Mkoa, akaja Mkuu wa Wilaya akamsimamisha mtu kazi kwa muda miaka sita, miaka saba, lakini hapati haki zake, anakuja mtu mwingine anachukua nafasi yake anachukua ule mshahara, halafu unasema kwamba tunamrudisha kwenye mshahara wake wa kipindi cha nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tuzingatie sheria iliyopo, kama tunataka kuanzisha sheria nyingine ambayo itawafanya watu wapunguziwe mishahara yao, basi tuanze sasa hivi lakini ajira basi ziwe za mikataba kama ajira zingine, lakini si ajira zile ambazo mtu anapewa barua ya ajira inakuwa ni permanent and pensionable lakini wanamwambia kwamba arudi kwenye mshahara wa zamani, nafikiri tutakuwa tumewaonea na itakuwa sheria kandamizi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)